Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya kumi na
saba katika kipindi cha mwaka 2017 naenedelea kukushirikisha uchambuzi wa
vitabu nikiwa na lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia
kwa ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika
makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na
badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “The Right Hook” kutoka
kwa mwandishi Gary Vaynerchuk. Gary Vaynerchuk ni mwandishi wa
vitabu ambaye vitabu vyake vimefanya vyema kwenye soko kiasi ambacho amekuwa
muuzaji bora wa vitabu kwenye jarida la New
York Times. Mwandishi pia ni mjasiliamali ambaye amekuwa akifanya vyema
katika miradi yake mbalimbali na amewahi kuchaguliwa na jarida la Businessweek kwenye orodha ya watu 20
ambao kila mjasiliamali anapaswa kuwafuatilia.
Kwa
ujumla mwandishi wa kitabu hiki anatushirikisha namna ambavyo kila mmoja
anaweza kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujitangaza na hatimaye kupata
mafanikio makubwa sana. Kwa sasa tunaishi kwenye ulimwengu wenye kila aina ya
kelele za kwenye mitandao ya kijamii, wapo ambao wametumia mitandao hii
kutengeneza kipato zaidi na wapo ambao wanatumia mitandao hii kwa mambo yasiyo
na tija katika maisha yao.
Mwandishi
anatushirikisha kuwa mitandao hii inatakiwa kutumiwa kama asset (kitu
kinachokuongezea kipato) badala ya kutumiwa kama liability (kitu kinachochukua
fedha zako mfukoni). Ili ufanikiwe kutumia mitandao hii kwa faida zaidi ni
lazima ufahamu mbinu muhimu za namna ya kuwasilisha ujumbe wako kwenye mitandao
hii na hatimaye ujumbe wako uwafikia watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:
1. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kupata wateja kwa ajili ya biashara yako ni sawa na jinsi
bondia anavyopangilia ngumi zake dhidi ya mpinzani wake. Mchezo wa ngumi
umepangwa katika mzunguko wa kwanza hadi wa kumi na mbili. Katika mizunguko hii
yote ni lazima bondia awe na mpangilio wa ngumi dhidi ya mpinzani mwake na
hatimaye afanikiwe kupiga ngumo moja ya ushindi. Hivi ndivyo ilivyo hata kwenye
ulimwengu wa biashara ni lazima upangilie huduma zako kiasi ambacho wateja
watavutiwa kufanya biashara na wewe kila mara na kwa kufanya hivyo utafanikiwa
kukabiliana na wapinzani wako wa kibiashara.
2. Simu
janja (smart phone) yako unaitumia kufanyia nini sasa hivi? Haijalishi simu
yako unaitumia kusoma makala hii kwa sasa, haijalishi unatumia simu yako
kuwashirikisha watu picha zako, haijalishi simu yako unaitumia kuchati kwenye
instangram, facebook au whatsapp au simu yako unaitumia kwa ajili ya
mawasiliano; muhimu kuanzia sasa tambua kuwa unatembea na nyenzo muhimu ya
kujitangaza kwa watu wengi zaidi tena nyenzo yenye uwezo wa kuvuka mipaka ya
nchi, mabara na bahari kwa muda mfupi sana.
3. Mapinduzi
ya mitandao ya kijamii yamebadilisha mfumo mzima wa maisha ya jamii. Mitandao
hii kwa sasa inatumiwa na kila mtu kuanzia vijana hadi wazee na hivyo mitandao
hii imeteka asilimia kubwa ya jamii kiasi cha kubadilisha namna ambavyo watu
wanaingia au kuachana katika mahusiano, ukaribu wa wanafamilia au namna ambavyo
watu wanaingia kwenye ajira. Kutokana na ukweli huu kuna kila sababu ya kila
mmoja kutumia mindao hii kwa ajili ya kujitangaza na hatimaye kuongeza wateja wapya
kwenye biashara au huduma zako.
4. Mitandao
ya kijamii inaaendelea kuteka njia nyingine za matangazo ya biashara. Njia za
matangazo ambazo zimekuwepo toka zamani kama vile mfumo wa kutumia magazeti,
mfumo wa kutumia digitali kama vile televisheni vyote kwa pamoja vimetekwa na
mfumo wa mitandao ya kijamii. Kwa sasa ni rahisi sana kuwafikia walengwa wa
huduma au biashara zako kwa kutumia mitandao ya kijamii kuliko ilivyo kwenye
mfumo wowote ule wa matangazo. Mfano, ilichukua zaidi ya miaka 13 kwa watu
milioni 50 kutumia redio au television lakini kwa mtandao wa instangram
imechukua kipindi cha mwaka mmoja na nusu kufikia idadi hiyo ya watu. Hii
inadhihirisha namna ambavyo ni rahisi kufikia watu wengi kwa muda mfupi kwa
kutumia mitandao ya kijamii.
5. Unapojitangaza
kwa kutumia mitandao ya kijamii hakikisha tangazo lako lina sifa za kuamsha
hisia za wateja unaowalenga. Katika ulimwengu huu wenye kila aina ya kelele za
mtandao mteja ana sekunde chache za kumshawishi aendelee kusoma ujumbe wako au
ahamie kwenye jumbe nyingine. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili kukabiliana
changamoto za namna hii ni muhimu kuhakikisha ujumbe wako unamshawishi mlengwa
wa biashara au huduma zako asome ujumbe wako lakini pia ashawishike kufanya
biashara na wewe.
6. Kila
mtandao wa kijamii una kanuni zake za namna ambavyo unaweza kuweka ujumbe wako
na ukaeleweka vizuri kwa walengwa wako. Mwandishi anatusirikisha kuwa mpangilio
wa ujumbe kwenye twitter ni tofauti na facebook au instangram. Ili kuteka
mitandao hii kwa ajili ya kutangaza huduma zako ni lazima ufahamu mitandao hii
kwa ufasaha namna ambavyo unaweza kucheza nayo wakati wa kuweka jumbe zako za
matangazo. Hii itakusaidia jumbe zako ziwe na mvuto kwa watumiaji wa mitandao
ya kijamii.
7. Unapoweka
ujumbe wako kwenye mtandao hakikisha ujumbe wako unakidhi mila na desturi za
walengwa wako. Mwandishi anatushirikisha kuwa kila jamii ina mila zake hivyo
kabla haujaweka ujumbe wako kwenye mtandao wa kijamii huna budi kujiuliza kama
ujumbe wako hauendani kinyume na tamaduni za walengwa wako. Hata hivyo
unatakiwa kuufanya ujumbe wako uwe na mvuto kwa mtu yeyote kuusoma na
ikiwezekana kila anayesoma awe na hamasa ya kuwashirikisha wenzake.
8. Hakikisha
ujumbe wako unabeba taswira/chapa ya utambulisho wa biashara au huduma zako
(brand). Mwandishi anatushirikisha kuwa ni muhimu kuhakikisha kila ujumbe
unaouweka kwenye mitandao ya kijamii uwe na sifa ya kumfanya msomaji kwa haraka
aweze kutambua chapa ya kampuni au biashara zako kwa ujumla. Kama ujumbe
unakidhi sifa hii ni rahisi kila anayesoma awe na shauku ya kufuatilia zaidi
huduma zinazotolewa na kampuni yako. Hii ni pamoja na kuhakikisha majibu yote utakayotoa
juu ya ujumbe husika pale unapojibu maoni (comments) ya watu waliosoma ujumbe huo
yawe na mtiririko wenye kubeba taswira ya biashara au huduma zako.
9. Hakikisha
ujumbe wako kwenye mitandao ya kijamii unabadilika kulingana na nyakati. Mwandishi
anatushirikisha kuwa watu wengi wanafanya makosa ya kuweka ujumbe uleule kuhusu
biashara au huduma zao kwa muda wa miaka mingi. Hapa tunafundishwa kuwa
mitandao ya kijamii inahusisha watu na hivyo ni lazima kufahamu kuwa watu hawa
wanabadilika mahitaji na mitazamo yao kulingana na umri. Kwa maana hii kama
mfanyabiashara ambaye unatafuta soko kupitia mitandao ya kijamii ni lazima uwe
unabadilisha jumbe zako mara kwa mara ili zikidhi mahitaji ya makundi tofauti
ya watu.
10. Unapoweka ujumbe wako kwenye mitandao
ya kijamii kama facebook kwanza kabisa lengo kubwa linapaswa kuwafikia watu
wengi na wala sio mauzo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri ujumbe wako
utakavyowafikia watu wengi ndivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuuza bidhaa au huduma
zako. Hivyo hakikisha ujumbe wako unakuwa na mandhari ya kuwavutia watumiaji wa
mitandao ya kijamii kwa kutumia ujumbe wa picha au maandishi.
11. Watu wengi wanafanya makosa ya kupost
jumbe za biashara zao pasipo kuwekeza kwenye elimu kwa wateja namna ambavyo
wanaweza kunufaika na bidhaa au huduma wanazozitoa. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ni vyema sana kuwekeza kwenye elimu ya kumfungua mteja mtarajiwa (mtumiaji
wa mitandao ya kijamii) ili kupitia elimu hiyo apate hamasa ya kufanya biashara
na wewe. Hapa unaweza kuwa unaandika makala au kuweka video za kuelimisha watu
juu ya namna bora ya kutumia bidhaa au huduma zako.
12. Chagua hadhira/walengwa wa ujumbe wako
kwenye mtandao wa facebook. Sio kila ujumbe unaoweka kwenye mtandao wa kijamii
uwafikie wafuasi (follower) wako wote kuna baadhi ya jumbe ambazo unapaswa
kuziweka katika namna ambayo zitasomwa na kundi linalolengwa na si vinginevyo. Mfano
kama lengo lako ni kuwafikia watu wa rika flani pekee unatakiwa ujifunze na namna
ya kuweka ujumbe wako ili ufike kwa kundi husika tu. Kufanya hivyo unakuwa na
uhakika kuwa ujumbe wako umeenda kwa
walengwa pekee jambo ambalo ni wazi kuwa hii inakuongezea nafasi ya ujumbe wako
ya kusomwa na walengwa.
13. Jumbe nyingi kwenye mitandao ya kijamii
ambazo hajalipiwa ni asilimia ndogo ya wafuasi wako wanaofikiwa na jumbe zako. mfano,
mtandao wa facebook kila unapoweka ujumbe ambao haujalipiwa ni asilimia 3 hadi
5 tu ya wafuasi wako wanaofikiwa na ujumbe wako. Mwandishi anatushirikisha kuwa
kama unataka ujumbe wako uwafikie wafuasi wako wengi huna budi kufikiria
kulipia.
14. Hakikisha ujumbe wako wa matangazo
unakuwa na sifa za kuvuta hisia za mtumiaji wa mtandao, husiwe na maneno mengi
kiasi cha kumchosha msomaji, kama ni kuna namba za mawasiliwano ziwekwe sehemu
ambayo ni ya wazi kwa msomaji, kama ni picha hakikisha inaonekana vyema na ina
logo/chapa ya kampuni yako. Kwa kifupi hizi ni kati ya sifa ambazo mwandishi
ametushirikisha kwa ajili ya kuzitumia paindi tunapotangaza bidhaa au huduma
zetu kwenye mtandao wa facebook.
15. Kwa kutumia mtando wa kijamii kama
Twitter ni rahisi kuwafikia wafuasi wapya tofauti na Facebook au Tumblr. Hii ni
kutokana na sera yake ambayo inawezesha tweet za watumiaji wa mtandao huu
kufikia watu nje ya wale ambao ni wafuasi wako.
16. Tumia mtandao wa Instangram kufikisha
ujumbe kwa kutumia picha ambazo zimewekewa ujumbe kwa kutumia sanaa ya hali ya
juu. Mwandishi anatushirikisha kuwa mfumo wa Instangram tofauti ni facebook ni
kwamba Instangram hairuhusu ujumbe wa maneneo mengi hivyo kama unahitaji
kuwafikia watumiaji wa mtandao huu ni lazima ujikite kwenye matumizi ya picha zilizowekewa
ujumbe wa maandishi kama ndoano halisi.
17. Kila kukicha dunia inakuwa kijiji hasa
katika karne hii ya 21 ambayo watu wa kila kona ya dunia kwa sasa wanaweza
kushirikisha yale wanayofanya, hobi zao au kila aina ya fursa. Swali ambalo
kila mmoja anapaswa kujiuliza ni kwa namna gani amejipanga kutumia fursa
mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujitangaza na hatimaye kutengeneza kipato.
18. Bidii ndiyo kiungo muhimu cha kukuwezesha
ufikie malengo yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa pamoja na nguvu za mitandao
ya kijamii katika kulifikia soko, daima kinachotofautisha kampuni moja na
nyingine ni bidiii inayowekezwa katika teknolojia ya kutumia mitandao ya
kijamii. Jambo la msingi hapa tunakiwa
kufahamu kuwa fursa zipo nyingi hasa za kutumia mitandao hii kuteka soko lakini
ni wajibu wetu kuwekeza kwa ajili ya kufahamu mitandao hii kwa undani zaidi.
19. Mchezo huu tofauti na michezo mingine
wenyewe hauna mwisho hivyo jitihada zako na ubunifu wa hali ya juu ndivyo daima
vitaendelea kukutofautisha na watumiaji wa mitandao hii. Mwandishi anatushirikisha
kuwa pamoja na kuweka jumbe nzuri kwenye mitandao ya kijamii ni lazima uweke
utaratibu wa kuwalinda wateja unaowapata kupitia mitandao hii. Njia bora ya
kuwalinda wafuasi wako ni kuendelea kutoa huduma bora zenye kutimiza hisia za
wafuasi wako katika mitandao hii.
20. Mwisho daima kumbuka kuwa kadri ujumbe
wako utavyokuwa mfupi na ndivyo utasomwa na watu wengi zaidi. Hii ni kutokana
na ukweli kwamba watu wengi hawana muda wa kupoteza kwa ujumbe ambao hadi
anafikia mwisho amesahau kile alichosoma mwanzo. Hivyo hakikisha tangazo lako
linakuwa fupi na lenye vitu vyote muhimu ambavyo vitamfanya mfuasi wako aweze kupata
bidhaa au huduma zako kwa urahisi.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki. Kupata
nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com