Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya kumi na
nane katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu
nikiwa na lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe
kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika
makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na
badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Do More Great Work” kutoka
kwa mwandishi Michael Bungay Stanier. Michael Bungay Stanier ni mjasiliamali
na mwanzilishi wa Kampuni Box Of Crayons ambayo inafanya kazi zake katika
mataifa mengi duniani. Mwandishi huyu mwaka 2006 alichaguliwa kama kocha
(mhamasishaji wa mafanikio) mwenye mafanikio zaidi nchini Canada.
Michael Bungay Stanier anatumia
kitabu hiki kutufunulia umuhimu wa kufanya kazi zenye tija katika kufikia
mafanikio yetu na kuachana na kazi ambazo zimekuwa zikitumia muda wetu mwingi
huku zikiwa na tija au mchango mdogo katika kufikia ndoto za maisha yetu.
Mwandishi
anatushirikisha kuwa kwa ujumla kazi zote tunazofanya katika maisha
zinagawanyika katika makundi matatu ambayo ni (a) kazi mbaya – bad work (b)
kazi nzuri – good work (c) kazi kubwa – great work.
Mwandishi
anatushirikisha kuwa kundi la kwanza linajumuisha kazi ambazo zinapoteza muda,
nguvu, rasilimali na hata maisha ya muhusika. Kundi la pili linajumuisha kazi
ambazo mhusika anafanya mara kwa mara na muda mwingi anautumia katika kazi
hizi. Mara nyingi kazi za namna hii zinatokana na taaluma au uzoefu wetu na
hivyo ni kawaida muhusika kufanya kazi hii kwa kiwango cha hali ya juu hata
kama tija yake ni ndogo. Kundi la mwisho linahusisha kazi zote ambazo kila mtu
anatamani kufanya kwa maana ya kazi ambazo zinaleta mabadiliko katika maisha ya
mhusika. Na kazi hizi zina sifa ya kumfanya mhusika afikirie kwa mapana,
aifurahie kazi anayofanya na kila siku atamani kuendelea kufanya kazi pasipo
kusukumwa na mtu yeyote.
Mwandishi
anatushirikisha kuwa kila mmoja anapaswa afikirie kufanya kazi zenye sifa ya
kundi la mwisho kwa vile kazi hizi zinaleta tija kubwa kwa muhusika, zinamfanya
muhusika hasiridhike na hatua aliyonayo bali aendelee kupambana kwa ajili ya
kuongeza zaidi na hatimaye akabiliane na kila aina ya changamoto. Kazi hizi
ndizo zinatofautisha watu au taasisi katika jamii kutokana na ubunifu na
utimilifu wa kazi husika kati ya mtu mmoja na mwingine au taasisi moja na
nyingine.
Hata
hivyo watu wengi wameendelea kufanya kazi za kundi la pili kwa vile hawataki
kujisumbua sana hasa katika kufikiri, wanaogopa kubeba au kuchukua maamzi magumu
(risk), wanatafuta usalama wa kazi kuliko tija ya kazi husika na hawako tayari
kuangaika mara kwa mara kutafuta maarifa mapya. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba kazi za kundi la tatu zinabadilika mara kwa mara kutokana na muda, yaani
kazi ya maana unayofanya leo hii baada ya miaka mitano haitakuwa kazi ya maana
na badala yake itakuwa kwenye kundi la pili.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:
1. Mwandishi
anatushirikisha kuwa pamoja na kwamba kila mtu anatamani kufanya kazi kubwa tena
zenye tija (kundi la tatu) ni lazima tutambue kuwa kazi hizo zinatokana na kazi
zetu za kila siku. Kwa maana hii, hatupaswi kuacha kazi zetu za sasa na kuanza
kutafuta kazi zenye tija bali tunachotakiwa kufanya ni kufanya kazi zetu za
sasa kwa weledi, ubunifu na utimilifu ili kupitia kazi hizi tufanikiwe kuhamia
kwenye kundi la kazi za aina ya tatu. Hivyo tunatakiwa kutumia kazi zetu za
kila siku kufikia viwango vya mabadiliko makubwa katika kila sekta ya maisha yetu.
2. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kinachowasukuma watu kufanya kazi kubwa zenye tija ni ile
hali ya kutaka kufanya vitu kwa njia ya upekee au utofauti. Kwa maana hii ni lazima
kwanza mhusika atathimini hali ya kazi yake ya sasa na hatimaye afanye maamuzi
ya kuiboresha kazi hiyo au pengine atafute kazi nyingine ambayo ina tija zaidi. Hata
hivyo wengi wanatamani kufanya kazi kubwa zenye tija lakini ni wachache ambao
wapo tayari kujitoa kwa ajili ya kazi hizo.
3. Kazi
kubwa (great work) zina sifa ya kuwa rahisi au ngumu kwa kutegemea nyakati.
Mwandishi anatushirikisha kuwa katika kufanya kazi kubwa kuna kipindi mambo
yatanyooka na utaona kuwa kila kitu kinaitikia wito wako japo pia kuna nyakati
ambazo utaona kila kitu kinakukimbia. Hivyo ni muhimu kujipanga kwa ajili ya
kukabiliana na nyakati ngumu kipindi unapokuwa kwenye nyakati za neema.
4. Kufanya
kazi kubwa zaidi inaweza kuwa sehemu ya maisha yako endapo utaweka mikakati ya
kubadilisha kila sekta ya maisha yako ili iendane na kusudi la maisha yako.
Hivyo ni wazi kuwa kazi kubwa sio lazima itazamwe kwa maana ya kipato
inachokuingizia bali kila mmoja anatakiwa kutathimini kazi yake kwa kuangalia
nini hasa kusudi la maisha yake hapa duniani. Kwa maana hii hatua ya kwanza
kabisa ya kufanya kazi kubwa yenye tija ni lazima kufahamu kwanza wewe ni nani
na kwa nini uliumbwa hivyo ulivyo kwa maana ya kutambua umuhimu wako katika
ulimwengu huu.
5. Kabla
ya kuanza safari ya kufanya kazi kubwa yenye tija ni lazima kwanza utambue ni
wapi unaelekea na wapi ulipo kwa sasa. Mwandishi anatumia mfano wa kwamba ukiwa
unasafiri kuelekea sehemu ambayo hujawahi kufika ni lazima utaweka maandalizi
kwa kutafuta taarifa muhimu juu ya sehemu hiyo ikiwa ni pamoja na umbali wake.
Ndivyo ilivyo hata kwenye kuianza safari ya kufanya kazi kubwa zenye tija,
kwanza kabisa ni lazima utambue ni nini hasa unahitaji kutokana na kazi yako.
Kwa maana ya kwamba ni nini matamanio ya maisha yako, nini hobi zako, ni vitu
vipi vinakupa furaha ya kweli au vitu vipi vinaipa roho yako furaha ya kweli.
6. Unapoanza
safari ya kufanya kazi kubwa zenye tija ni muhimu kwanza ujiulize maswali haya;
(i) Ni nini hasa utambulisho wangu katika jamii? Hapa unatakiwa ujiulize sifa
muhimu ulizonazo (ii) Je ni lipi lengo na mwelekeo wangu? Hapa jiulize ni vitu
gani unataka kuvikamilisha katika maisha yako na kwani nini unataka vitu hivyo.
(iii) Jiulize ni watu gani naweza kuambatana nao? Hakuna kazi ambayo utaifanya
peke yako ni lazima pawepo timu ambayo utashirikiana nayo. (iv) Je ni
changamoto zipi ambazo navutiwa kuzitatua? Kazi yoyote ni kutatua changamoto
hivyo fahamu ni sekta ipi unajisikia huru kutatua changamoto zilizopo. (v) Ni jinsi
gani naweza kujenga mtazamo/mazingira chanya juu ya kazi yangu?. (vi) Je
naitikia vipi kwenye vikwazo vilivyopo mbele yangu? (vii) Je ni nini furaha
yangu na (viii) Je ni jinsi gani naweza kuhimili vipindi vya mpito?.
7. Fanya
tathimini ya viwango vyako vya juu kabisa katika utendaji kazi ambavyo uliwahi
kufikia katika hisitoria yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika kufikia viwango
vya ufanyaji kazi kubwa zenye tija ni lazima kwanza uorodheshe ufanisi wako wa
hali ya juu ambao unajivunia kuwahi kufikia. Hapa unatakiwa utambue kuwa
ufanisi huu unatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine lakini pia unatofautiana
kati ya aina ya kazi au tukio. Unapokuwa kumbuka nyakati za ufanisi wako wa
hali juu inasaidia kujenga hamasa ya kwa nini husiendele kufanya vyema katika
kazi au malengo yako unayojiwekea. Hii ni kutokana na ukweli kwamba nyakati
hizo za ushindi zinakujengea picha ambayo inakufanya ujione kuwa wewe ni
mshindi na kalama ya ushindi ipo ndani mwako.
8. Kila
mtu ana asili ya ukubwa ndani mwake tokea uumbaji wake. Katika hili maandishi matakatifu
yanatuambia kuwa “husiogope kwa kuwa Mimi Bwana wako nalikufahamu ungali tumboni
mwa mama yako”. Huu ni urithi tosha wa kutufunulia kuwa kila mtu ana alama ya
ushindi ndani mwake na hivyo unaweza kufanikiwa katika kila ya aina ya kazi
ambayo umedhamiria kufanya endapo ataondoa hofu ambayo imemkwamisha kwa muda
mrefu. Hivyo kuanzia sasa kila mara jisemee kuwa naweza kufanya kazi yoyote
kubwa na yenye tija ya hali ya juu kwa kuwa ushindi upo ndani mwangu tangu siku
niliyoumbwa.
9. Ushindi
katika kazi yako au tukio lolote lile unaleta hali ya kujiamini ambako pia
uambatana na hali ya kujiona wewe ni wa thamani na una uwezo wa hali ya juu. Vitu
hivi si vigeni kwa mtu yeyote yule kutokana na ukweli kwamba kila mmoha
alishawahi kushinda pasipo kujali ushindi wako ulikuwa wa tukio au kazi ipi. Kwa
ujumla ni kwamba ushindi wowote ambao umepatikana kwa jitihada mahususi huwa
unamfanya muhusika ajione mwenye fahari juu ya nafsi yake.
10. Je unajitambua wewe ni nani? Mwandishi anatushirikisha
kuwa kamwe hauwezi kufikia anga za kufanya kazi kubwa zenye tija endapo haujui
kusudi la maisha yako hapa duniani. Hatua ya kwanza kabisa ni kutambua wewe ni
nani na kwani nini mpaka sasa unaishi ikilinganishwa na wale wengine ambao
pengine hawakufanikiwa kufikia umri wako. Kusudi la maisha yako ndo mwongozo
wako wa kutambua ni kazi ipi unatakiwa kuikamilisha ulimwenguni humu.
11. Tunajifunza kufanya kazi kubwa zenye
tija kutoka kwa waliofanikiwa kufikia viwango vya juu. Hapa mwandishi
anatushirikisha umuhimu wa kuwa na watu amabao ni ‘role model (mtu wa kuigwa)’’
wetu katika kufikia viwango vya ufanisi tunavyokusudia. Unaweza kuwa na role
models wengi kwa kutegemea kila sekta ya maisha yako unayotaka kuiboresha. Hata
hivyo, unatakakiwa kufahamu kuwa role model wako sio lazima awe mtu maharufu
kwani watu wa namna hiyo wanatuzunguka kila sehemu. Role model wako anaweza
kuwa baba au mama, padre/mchungaji, mwalimu au jirani yako kwa kutegemea sehemu
ya maisha yako unayotaka kuboresha.
12. Ni vitu vipi vinakusukuma kufanya kazi
yenye tija tofauti na unavyofanya kwa sasa? Mwandishi anatushirikisha kuwa kama
unaongozwa na sababu zenye uzito itakuwa rahisi kufikia kule unakokusudia na
kinyume chake ni kwamba kama haufahamu wapi unaelekea au unaongozwa na sababu
finyu haitakuwa rahisi kwako kufikia viwango vya mafanikio makubwa. Hivyo hapa
tunafundishwa umuhimu wa kujiuliza sababu za kwa nini tunaka kufanikiwa na
baada ya kupata majibu ya swali hili tunakiwa kutengeneza ramani ili itumike
kama mwongozo wa kuongoza hatua zetu.
13. Maisha ni kachumbari yenye mchanganyiko
wa vitu vingi kama vile mahusiano, pesa, mapenzi, dini, elimu, afya, jamii,
familia, ubunifu n.k. Katika mchanganyiko huu kila mmoja ana wajibu wa
kujiendeleza na kuboresha maisha yake katika kila sekta. Kwa kufanya hivyo
tunapata thamani halisi ya maisha yetu ambayo kimsingi inatokana na matendo
yetu ambayo pia ni ukamilisho wa kazi zetu za kila siku. Hivyo kazi zetu pia ni
ukamilisho wa wito wetu hapa duniani. Jambo la kujiuliza ni je unajua wito wako
ni upi? Hii ni kutokana na ukweli kwamba kama haujui wito wako utaishia kufanya
kazi ambazo sio wito wako na hatimaye utaishia kufanya kazi hizo kwa ufanisi
mdogo sana.
14. Ni vitu vipi vinakuwasha mwili na kukuambia
kuwa bado… bado…. bado…. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama hauna sababu za
kukusukuma zaidi ni rahisi kuangukiwa kwenye mtego wa kuridhika na hatimaye
kujikuta unafanya kazi za kawaida. Hivyo ni muhimu kila hatua ujione kuwa
safari bado ni ndefu, hii itakufanya uendelee kutatua changamoto nyingi zaidi
zenye viwango tofauti na hatimaye uzidi kufanikiwa katika kila sekta ya maisha
yako. MUHIMU kumbuka mafanikio sio pesa tu bali mafanikio ni kwenye kila sekta
ya maisha kama ambavyo tumeona hapo juu kuwa maisha ni kachumbari yenye kila
aina ya mchanganyiko wa viungo.
15. Wengi wetu tunafanya kazi kwenye
taasisi au kampuni ambazo tumeajiriwa. Kama hatujaajiriwa basi tunaweza kuwa tumeajiri
watu katika kampuni zetu. Hivyo wote kwa pamoja tunafamu kuwa jukumu kubwa la
mwajiriwa ni kutimiza majukumu ya mwajiri wake kwani hiyo ndio njia pekee ya
yeye kuendelea kwenye kibarua chake. Hata hivyo pamoja na kutekeleza majukumu
ya mwajiri wetu tunafahamu kuwa ndani mwetu tunaweza kufanya vitu vikubwa zaidi
ya haya tunayotekeleza kwa mwajiri. Kazi kubwa iliyopo mbele yako ni
kuhakikisha kila siku unafanya kazi zaidi ya matakwa ya kazi yako. Hii itakusaidia
kutumia nguvu iliyopo ndani mwako ambayo hajatumiwa ipasavyo.
16. Jifunze kusema HAPANA au NDIYO
kulingana na swali unaloulizwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa sio kila swali
majibu yake ni ndiyo. Kabla ya kusema ndiyo ni lazima ujipe muda wa kutafakari
swali unaloulizwa na pale ambapo unaona kuwa unachoulizwa/kuombwa ni vigumu
kutekeleza tafuta namna ya kumjibu mhusika pasipo kuharibu uhusiano wake kwako.
Hivyo hivyo kwa jibu la hapana, sio kila utakachoambiwa hapana ni hapana kweli,
unatakiwa kutathimini jibu unalopewa kabla ya kuamua kusonga/kutosonga mbele.
17. Je upo tayari kufanya kazi kubwa yenye
tija? Mwandishi anatushirikisha kuwa haitoshi kusoma kitabu hiki na kuhamasika
bila kuanza kuchukua hatua halisia. Baada ya kusoma kitabu hiki hadi kufikia
hapa naamini kuwa umepata mwanga wa kugundua nu changamoto zipi ambazo pengine zimekukwamisha
kufikia uwezo wako wa juu katika utendaji kazi wako. Ni wajibu wako sasa kuamua
ni wapi uboreshe ili uachane na maisha yako ya awali na hatimaye uanze kuishi
msingi wa maisha mapya yenye kuongozwa na kauli mbiu ya kutumia uwezo wako wote
katika kufikia mafanikio unayokusudia.
18. Kila mmoja ana wazo la kimafanikio na
mawazo hayo yanatujia kila mara katika mfumo wa fikra zetu. Hata hivyo kwa kuwa
hatujiamini tumekuwa tunapoteza mawazo ya kifursa na hatimaye tunaendelea
kufanya vitu vya kawaida. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama tunahitaji kutoka
hapo tulipo kwa sasa ni lazima kwanza tujiamini kuwa tunaweza na mara moja
tuanze kufanyia kazi mawazo yetu. Unaweza kuorodhosha mawazo kadhaa uliyonayo
na ukayapa maksi kila mmoja kutoka na umuhimu na uwezekano wake kiutendaji na
hatimaye ukachagua wazo moja lenye maksi nyingi ili uanze kulitekeleza mara
moja.
19. Je una ujasiri kiasi gani wa kufanya
kazi kubwa zenye tija? Ili ni swali ambalo unatakiwa kujiuliza kabla ya kuanza
safari yako. Swali linatakiwa likupe nafasi ya ya kujitafakari kama kweli una
nia ya dhati ya kubadilika. Safari unayoianza ni safari ambayo inahitaji bidii
ya kweli na nidhamu binafsi ya hali ya juu. Hakuna mtu wa kuja kugongea kengele
kuwa umechelewa au muda umeisha. Wewe ndo mhusika mkuu katika kila tukio, yapo
matukio ambayo yatakuwa na nia ya kukukatisha tamaa kama haujasimama vizuri
unaweza kurudi nyuma kwa kasi kubwa. Hivyo unapoianza safari hii unatakiwa
ufahamu kuwa kuna milima na mabonde mbele yako na yote hayo yapo kwa ajili ya
kupima uimara wako katika kukabiliana nayo.
20. Ainisha msaada unaotaka kabla ya kuanza
safari yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa kabla ya kuanza safari yetu ya
kufanya kazi kubwa zenye tija ni lazima kwanza tuainishe msaada unaotakiwa. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba kazi hizi hatuwezi kufanya peke yetu ni lazima
tufanye kwa kushirikiana na jamii inayotuzunguka na hatimaye tufanikiwe kufikia
malengo yetu.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Food
of thought “In the long run,
we shape our lives, and we shape ourselves. The processs never ends until we
die. And the choices we make are ultimately our own responsibility”. (Eleanor
Roosevelt)
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com