Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya kumi na
sita katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa
vitabu. Lengo kubwa la kufanya hivyo ni kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia kubadilisha kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujafanikiwa kujifunza kitu chochote
katika makala hizi za uchambuzi wa vitabu nakushauri husiendelee kupoteza muda
wako na badala yake ufanye mambo ambayo umeyazoea.
Kujiunga na mtandao wa fikra za
kitajiri BONYEZA HAPA na
ujaze fomu ili uendelee kunufaika na makala za mtandao wa fikra za kitajiri.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao huu moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “The Seven Principles
For Making Marriage Work” kutoka
kwa waandishi John M. Gottman akishirikiana na Nan Silver. John
M. Gottmann ni mwanasaikolojia na mtafiti wa masuala ya familia na ndoa.
Wawili hawa kwa pamoja wameshirikiana kuandika vitabu mbalimbali kwa ajili ya
kuboresha maisha ya ndoa na familia kwa ujumla.
Katika
kitabu hiki waandishi hawa wanatushirikisha kanuni saba ambazo wanandoa kwa
pamoja wanaweza kuzitumia kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza maisha ya ndoa ambayo
imejengwa kwenye msingi wa furaha.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:
1. Furaha
katika maisha ya ndoa haitokani na pesa, akili nyingi au umiliki wa rasilimali
za aina yoyote ile. Waandishi wa kitabu wanatushirikisha kuwa chanzo cha ndoa nyingi
kuishi maisha yasiyo ya furaha ni wanandoa husika kuishi maisha ya fikra hasi pamoja
na hisia mbaya zinazojengwa juu ya mwenza wake. Hivyo, ili ndoa iwe na maisha
yenye furaha ni lazima kwanza wanandoa waheshimiane, wanyenyekeane, waelewane
na kusikilizana katika maisha yao ya kila siku. Kwa maana hii msingi mkubwa wa
ndoa yenye mafanikio ni kila mmoja kuwa na hisia juu ya mweza wake na wala sio pesa au umiliki wa rasilimali.
2. Ndoa
ni sehemu ya kuongeza siku za kuishi. Waandishi wa kitabu hiki wanatushirikisha
kuwa utafiti unaonyesha kuwa wanandoa ambao wameishi pamoja kwa muda wa maisha yao
wanaishi kati ya miaka minne hadi nane ikilinganishwa na wale ambao
wametalikiana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ndoa zenye msongo wa mawazo na
kila aina ya misukosuko ni chanzo cha miili ya wanandoa kuwa na upungufu wa
kinga za mwili dhidi ya maradhi mbalimbali.
3. Mawasiliano
kati wenza au familia ni chanzo cha kutatua migogoro na maisha yenye furaha ndani
ya familia. Mawasiliano ni chanzo kikubwa cha mapenzi ya dhati kati ya mke/mme
na mwenza wake na wanandoa ambao hawana mawasiliano ya mara kwa mara si rahisi
kudumu kwa muda mrefu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mawasiliano ni chanzo
cha kusikilizana na kufahamu mahitaji ya mwenza wako ili kuboresha maisha ya
ndoa yako.
4. Urafiki
kati ya wanandoa unasaidia kukuza ndoa imara na yenye furaha. Waandishi wanatushirikisha
kuwa ni muhimu wenza katika ndoa kuishi maisha ya urafiki na katika urafiki huu
wenza hawa wanatakiwa kutambua mapungufu ya kila mmoja. Pia, kila mmoja
anatakiwa kufahamu vipaumbele vya mwenzake na kwa pamoja kila mmoja atumie
jitihada za kumridhisha mwenza wake ili atomize vipaumbele vyake. Hivyo, ni
muhimu wanandoa wakaishi maisha ya urafiki yenye kila aina ya vichocheo vya
mapenzi.
5. Chanzo
cha ndoa nyingi kuanguka ni kukosa unyenyekevu kati ya wenza. Waandishi wanatushirikisha
kuwa dhumuni kubwa la maisha ya ndoa ni wawili (mme na mke) kusaidiana kwa
ajili ya kila mmoja kufanikisha ndoto za mwenza wake. Katika maisha ya namna
hii wawili hawa wanatakiwa waishi maisha yenye kusudi moja kwa ajili ya
kufanikisha kukuza familia yao kwa misingi bora. Endapo wanandoa watakosa
misingi hii ni wazi kuwa ndoa yao itakuwa kwenye malumbano ya mara kwa mara
ambayo yatapelekea ndoa yao kupoteza mwelekeo.
6. Tabia
za kukosoa, vitendo vinavyoambatana na lugha ya mwili, kujiona wewe hauna kosa
bali mwenye makosa ni mwenzi wako, kuongea kwa jazba, kuwa na kumbukumbuku za
matukio mabaya kati yenu na malalamiko ya kila wakati ni sababu kuu kati ya nyingi
zinazosababisha kuvunjika kwa ndoa nyingi. Waandishi wanatushirikisha kuwa ni
vyema kila mmoja katika maisha ya ndoa atambue wajibu wake na pale inapotokea
kuna kutoelewana ni lazima kila mmoja atambue ni wapi amekosea yeye kama yeye
kabla ya kumlaumu mwenzake.
7. Kwa
asili mwanaume ndo nguzo ya familia na utafiti unaonesha kuwa ukweli huu
unajidhihirisha kwa zaidi ya asilimia 85 za ndoa katika jamii nyingi. Hii inaonyesha
wazi kuwa mwanaume na mwanamke ni viumbe vyenye maumbile tofauti. Mfano,
wanawake wameumbwa kwa ajili ya kufanya kazi ambazo zinawezesha kupumzika kwa
muda mrefu hasa kwa mama anayenyonyesha ili kuruhusu homoni za maziwa ziwezeshe
maziwa kuzalishwa kwa wingi. Kwa upande wa mwanaume yeye kimaumbile anaweza
kufanya kazi kwa muda mrefu kwa kuzingatia maumbile ya misuli yake.
8. Katika
maisha ya ndoa ni lazima kila mmoja amfahamu mwenza wake kwa undani zaidi. Hii ni
kanuni ya kwanza ambayo waandishi wanatushirikisha kwa ajili ya kuboresha
familia zetu. Hapa tunashirikishwa kuwa kama unataka kuboresha familia yako ni
vyema kuhakikisha unafahamu mwenza wako anapendelea nini, mwenza wako
anakabiliwa na tatizo lipi, hofu zake, matukio muhimu katika historia ya mwenza
wako, anasongwa na mambo yapi kwa muda husika n.k. Baada ya kumfahamu mwenza
wako ndani na nje unatakiwa kutumia vitu hivyo kuamsha vichocheo vya mapenzi
kwa njia yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuwa na muda wa utani na kufurahi. Mfano,
unaweza kutumia nyimbo au filamu ambazo mwenza wako anapendelea na kuhakikisha unazitumia
kwa ajili ya kuamsha hisia zake za mapenzi.
9. Wanandoa
wanapopata mtoto inaweza kuwa mwanzo wa mafarakano wa familia husika. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba mara baada ya kupata mtoto wanandoa wanakuwa na
majukumu mapya ambayo mara nyingi yanapelekea mapenzi ya wawili hawa yaamie kwa
mtoto. Njia pekee ya kuendelea kupendana na kila mmoja kutimiza majukumu yake
kwa mwenza wake ni kuhakikisha wanandoa wanafahamiana kwa undani ili hata pale
mabadiliko yanapojitokeza kila mmoja atafute namna ya kurudi kwenye msitari.
10. Rutubisha hisia na matamanio yenu ndani
ya ndoa. Waandishi wanatushirikisha kuwa ni muhimu kwa wanandoa kuhakikisha
kila siku hisia zao zinakuwa hai hii ni pamoja na kukumbuka historia za enzi za
uchanga wa penzi lenu la dhati. Hata hivyo ni muhimu kila mwanandoa kuhakikisha
kila siku anatafuta njia za kumchangamsha mwenza wake ili muda wote wawili hawa
wawe kwenye furaha yenye chimbuko la kutoka rohoni.
11. Mtazamo chanya juu ya mwenza wako na
mahusiano yenu ni nyenzo muhimu ya kuepuka mambo mabaya ndani ya mahusiano. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba mtazamo chanya juu ya mwenza wako ni tiba ya
mafarakano ndani ya ndoa. Kadri unavyokuwa na mtazamo chanya juu ya familia na
mwenza wako ndivyo kila kukicha mwenza wako unamuona mpya. Hii ni pamoja na
kuhakikisha mnaishi maisha ya shukrani kwa kila tukio linalotokea kwenye maisha
yenu.
12. Ndoa nyingi zimevunjika kutokana na
kukosa muda wa wenza kuwa pamoja. Sehemu pekee ya kufahamu mahitaji ya mwenza
wako ni kuwa na muda wa pamoja ambao mnaweza kuongea pamoja. Utafiti unaonyesha
kuwa ndoa nyingi zimebomoka kwa vile wanandoa husika wamekosa vionjo vya penzi
ambavyo awali vilifanya penzi lao liwe hai muda wote. Ili kuepuka mtego huu ni
muhimu kwa wanandoa kutenga muda wa kusikilizana kwa ajili ya kukumbusha vitu
muhimu katika maisha yao na hivyo kuhuisha akaunti ya penzi lao.
13. Ukaribu wa wanandoa sio tu unasaidia
kuboresha uaminifu wa wanandoa bali pia ni chanzo cha kuamsha hisia za mapenzi.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri wanandoa wanavyokuwa karibu muda mwingi
ndivyo wanasaidiana majukumu ya kazi zao. Katika kusaidiana majukumu haya
ndivyo kila mmoja anaonyesha thamani yake kwa mwenzi wake.
14. Kukua kwa teknolojia ya habari na
mtandao kumepelekea wanandoa wengi kukosa utulivu wa akili pindi wanapokuwa
pamoja. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanandoa wengi wamemezwa na mitandao
ya kijamii hivyo pindi wanapokuwa pamoja kila mmoja yupo bize na simu yake
akiendelea na kuchati. Hali hii inaendelea kupoteza amani ndani ya ndoa nyingi
kwa vile kila mmoja hana muda wa kumsikiliza mwenza wake. Ili kuepukana na
hatari hii waandishi wanatushauri kuwa ni vyema kutenga muda wa kupitia
mitandao ya kijamii, emails na ujumbe mfupi wa simu. Hakikisha muda ambao
umeutenga kwa ajili ya mwenza wako au watoto wako hauna mwingiliano wa mambo
mengine.
15. Mwanaume hasitumie madaraka yake kama
nguzo ya familia kuhakikisha kuwa maamuzi ndani ya ndoa anafanya peke yake bali
ushirikiano uwe msingi wa maamuzi ya wanandoa. Kanuni hii ni kwa ajili ya
kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa yanamfurahisha kila mmoja ndani ya ndoa. Daima
epuka maamuzi ambayo yanamfa mwenza wako hasijisikie vizuri juu utekelezaji wa
maamuzi yako. Maamuzi endapo yanafanywa kwa kushirikiana yanapunguza migongano
kwa wanandoa na hivyo kuboresha urafiki wa wenza hawa.
16. Migogoro ndani ya ndoa inagawanyika
katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni ile migogoro ambayo inajitokeza mara
kwa mara ndani ya wenza. Katika kundi hili wanandoa mara nyingi wanaishi ndani
ya migogoro hii kipindi kirefu cha maisha yao. Mfano, katika ndoa ya Jane na
Smith; Jane anataka tendo la ndoa lifanyike mara kwa mara wakati Smith yupo
tayari hata mara moja kwa wiki. Pia, migogoro hii inahusisha majukumu ya kazi
kwa wenza ambayo yanapelekea kila mmoja kuona kuna upungufu kwa mwenzake katika
kutimiza majukumu yake ya ndoa.
Kundi
la pili la migogoro ni ile ambayo inasuruhishika (solvable problems). Migogoro ya
aina hii pamoja na kwamba inatatuliwa mara nyingi inawaachia makovu wanandoa. Mfano,
migogoro hii inaweza kuwa uaminifu kwa wanandoa au kutotimiza majukumu ya ndoa.
Migogoro hii hisipotatuliwa mara nyingi inageuka kuwa migogoro sawa na ile ya kundi
la kwanza.
17. Njia mojawapo ya kutatua migogoro kwa
wanandoa ni kupeana thamani ya kipekee kama ambavyo thamani anayopewa mgeni
ndani ya familia. Mfano, unaweza kutembelewa na mgeni ambaye kwa bahati mbaya
akaharibu kitu – hauwezi kumkemea mgeni kwamba kwa nini umeharibu kitu hiki? Badala
yake utasema hakuna shida hiyo itarekebishwa. Waandishi wanatushirikisha kuwa
ni muhimu kutumia kauli kama hizo kwa mwenza wako pale ambapo unaona amefanya
kitu kinyume na utaratibu.
18. Pia, wanandoa wanaweza kutatua migogoro
kwa kuhakikisha kuwa utatuzi wa migogoro unafanyika na wawili hawa kwa kutumia njia
laini ambazo hazimuumizi mwenza wake. Mara nyingi tumezoea kuona ugomvi kwa
wanandoa kama sehemu ya kutatua migogoro yao, waandishi wanatushirikisha kuwa
njia hiyo inapaswa kuepukwa kwani sio tu inasababisha hofu kwa mwenza bali
makovu yake ni ya muda mrefu na hivyo kusababisha maisha ya ndoa hisiyo na
furaha.
19. Baadhi ya migogoro kwa wanandoa ambayo
chimbuko lake ni matatizo ya kifedha kwa wanandoa ambayo pia utegemea mtazamo
wa wanandoa juu ya fedha. Waandishi wanatushirikisha kuwa migogoro ya namna hii
inaweza kutatuliwa kwa kuhakikisha wanandoa wanapanga kwa pamoja juu ya matumizi ya
fedha zao. Pia, ni muhimu kufanya kazi kama timu ili kufahamu majukumu ya kila
mmoja katika kufikia malengo ya kifedha kwa wanandoa.
20. Zaidi ya asilimia 67 kwa wanandoa
inaonyesha kuwa wanawake mara baada ya kupata mtoto wanakuwa na mabadiliko ya
ghafla kwenye kutimiza majukumu ya penzi kwa wenza wao. Hali hii inapelekea na
wanaume kubadilika mara baada ya kuona hali ya kutoridhishwa na wenza wao. Hali hii kwa wanawake inasababishwa mara nyingi na mabadiliko ya majukumu yao ambayo kwa
wakati huo wanakuwa na jukumu la kulea mtoto ambalo uambatana na kukosa muda wa
usingizi wa kutosha. Waandishi wanatushirikisha njia nyingi za kukabiliana na
hali hii kwa ajili ya kuboresha ndoa kama zilivyoainishwa hapa chini;
- Katika kipindi cha maandalizi ya kupata mtoto wanandoa wanapaswa kutumia muda mwingi kufikiria majukumu yao mapya na jinsi ya kukabiliana nayo kama timu moja;
- Baba awe sehemu ya kumuhudumia mtoto kwa kadri awezavyo kuliko kumuachia mama majukumu yote;
- Baba apate muda wa kucheza na mtoto kwa ajili ya kumpa mama muda wa kukabiliana na majukumu mengine;
- Kila mmoja hasisahau wajibu wake kwa mwenza wake; na
- Kama baba mpe mama muda wa kupumzika.
21. Kuridhishana kupitia tendo la ndoa ni
kiungo muhimu cha kuboresha maisha ya ndoa. Kutokana na tafiti zilizofanyika
zinaonesha kuwa kimaumbele wanaume wana hamu ya kufanya tendo la ndoa mara kwa
mara ikilinganishwa na wanawake. Tendo hili la ndoa linaboreshwa na matendo ya
kimahaba kwa wenza katika majukumu yao ya kila siku na hivyo ni vyema wanandoa
wakatenga nafasi ya kipekee sawa na majukumu yao mengine kwa ajili ya tendo la
ndoa. Waandishi wanatushirikisha njia zifuatazo kwa ajili ya kulifanya tendo la
ndoa liwe na thamani na la kimahaba kwa wanandoa;
- Kuwa na maana yenu ambayo ina uhusiano mkubwa kati ya mahaba na tendo la ndoa katika maisha yenu ya kila siku;
- Jifunze jinsi ya kuzungumzia tendo hili pasipo kusababisha kumtoa kwenye hamu mwenzio katika maisha yenu ya ndoa;
- Kuwa na muda wa kuchati/kuzungumza juu ya maisha yenu ya kimahaba. Mfano mnaweza kuwa na muda wa kukumbushana juu matendo yenu ya kimahaba yaliyopita; na
- Jifunze namna ya kuanzisha, kukubali au kukataa kufanya tendo la ndoa pasipo kumuumiza mwenzio.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki. Kupata
nakala ya kitabu hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com