Tunapoelekea kuumaliza mwaka 2016 na kuuanza mwaka 2017
ni matumaini yangu kuwa rafiki unaendelea vizuri. Ni jambo la heri na la kujivunia
kuona mpaka sasa tu wazima wa afya kwani wapo wengi ambao walitamani kufikia
siku kama ya leo lakini hawakufanikiwa. Hivyo mimi na wewe ni akina nani hasa
mpaka tumefanikiwa kufikia muda kama huu? Shukrani za pekee ni kwake muumba
kwani ndiye anaejua makusudi ya uwepo wetu hapa duniani.
Karibu tena katika makala yangu ya leo ambapo leo hii
nitakushirikisha kauli mbiu muhimu ambayo inatakiwa kuwa dira ya mafanikio yako
katika kipindi chote cha mwaka 2017. Kabla ya kufahamu kauli mbiu hii,
ningependa nikukumbushe kuwa nimekuwa nikijitahidi kuhakikisha kila makala
ninayoandika inakuwa na hamasa ya kukutaka wewe rafiki yangu uwe na mtazamo wa
kuona kuwa kila aina ya mafanikio unayoyataka yanaanzia ndani mwako na wala si
kwingineko. Kwa maana hii leo hii jinsi ulivyo ni matokeo ya mambo ambayo
umekuwa ukiyachagua katika maisha yako ya kila siku.
Miaka itakuja na kupita kama ambavyo majuzi tulisherekea
mwaka 2016 ndivyo ilivyo hata kesho tutasherekea mwaka 2017 hali kadhalika
2018. Jambo moja la kujiuliza kila tunaposherekea mwaka mpya ni je tupo kwenye
njia sahihi ya kuzielekea ndoto zetu? Bila kufanya hivyo tutaendelea kusherekea
sherehe za mwaka mpya enzi na enzi mpaka pale ambapo maisha yetu yatafikia
ukomo kwenye sayari hii huku tukizikwa na ndoto zetu.
Rafiki yangu leo hii unaposherekea mwaka mpya 2017
naomba nikupe kauli mbiu ambayo itakuwa mwongozo wako katika kipindi chote cha
mwaka 2017. Kauli mbiu hii si nyingine bali ni KUWAZA CHANYA (POSITIVE
THINKING) katika kila hali/tukio.
Nini
Maana ya Kauli Mbiu Hii?
Kuwaza Chanya maana yake ni kwamba unaifundisha akili (ubongo)
yako muda wote ifikilie katika hali ya uchanya pasipo kutoa nafasi kwa mawazo
hasi. Kwa maana hii ni kwamba kila tukio unalokutana nalo unatakiwa ufahamu
kuwa tukio hilo lina sura mbili (Chanya au Hasi) na hivyo wajibu wako mkubwa ni
kutafuta hali ya uchanya kwenye tukio husika.
Soma Zijue
Sheria Za Asili na Jinsi ya Kuzitumia Kufikia Mafanikio Makubwa Sana - Sehemu ya
Nne – Sheria
ya Asili ya Uwili Kinzani
Ukiwa unawaza katika hali chanya kamwe wewe haupaswi
kuwa mtu wa kunungunika, kulalamika, kukasirika, kuwa na hofu, kuwa mmbea, kuwa
na visingizio, kukata tamaa, kuhahirisha mambo n.k. bali unatakiwa matukio yote
unayokutana nayo unayachambua ili upate upande chanya wa hayo matukio. Mfano,
umepanga kukutana na mtu sehemu flani na umejitahidi ukafika muda ule ule
mliokubaliana lakini kwa bahati mbaya yeye amechelewa kufika kwa muda wa nusu
saa. Kwenye tukio kama hili unachoweza kufanya ni kuangalia kwa muda huo
unaomsubiria ni kitu gani unaweza kufanya ili akiendelea kuchelewa husipoteze
muda wako bure, unaweza ukasoma kitabu/makala kama unacho kwenye simu
(softcopy), unaweza ukasikiliza nyimbo ambazo huwa ukisikiliza zinakupa hamasa
au faraja au ukasikiliza sauti za vitabu vilivyosomwa (audio books).
Je
nini unatakiwa kufanya ili uwaze chanya muda wote?
Ili uwaze chanya kwenye kila aina ya tukio fanya mambo
yafuatayo;
Fikiri
kama mtoto. Watoto huwa wana mfumo wa mawazo ambao mtu
mzima ukifanikiwa kuuhishi mfumo huu kamwe hauwezi kuwa na mawazo hasi. Mfano,
watoto muda wote wana furaha, hawana hofu na matukio ya baadae au yaliyopita
(wanaishi maisha ya sasa), hawakati tamaa pale wanapokutana na jambo jipya na
hawafikirii kuhusu sheria zinasemaje. Kwa hali kama hii watoto wanawaza mambo
mema kwenye kila hali wanayokutana nayo kwani hawajui mabaya yaliyopo kwenye
ulimwengu huu.
Kama mtu mzima unaweza kuwaza kama mtoto pale ambapo
unafanya jambo jipya. Husifikirie kushindwa kwenye kila jambo unalofanya bali
fahamu ya kuwa una mfumo wa mawazo ambao unaweza kutekeleza kila jambo endapo
umetumiwa ipasavyo. Pia, tumia njia hivyo kujiepusha hofu ambayo imekuwa
ikuzuia kutekeleza malengo yako.
Tumia
lugha ya mwili (Body language). Mwaka 2017 hakikisha kuwa
mwonekano wako wa nje unaonyesha kile unachokiwaza ndani mwako. Mara nyingi kwenye
jamii inayotuzunguka tumezoea kusikia kauli kama kijana yule anaonekana kuwa na
tabia nzuri, yule mzee huwa ana busara sana… Unaweza ukajua mawazo ya mtu hata
kabla hajaongea ila kwa kuangalia mwonekano wake wa nje. Hivyo ndivyo na wewe
unatakiwa uwe kama kweli unawaza chanya ili jamii inayokuzunguka ione vitu vya
tofauti kutoka kwako. Tambua kuwa tupo jinsi tulivyo kutokana na yale tunayoyawaza
muda mwingi.
Kuwa
na muda wa kuongea na nafsi yako. Unapoishi kwenye kauli mbiu
ya uchanya, mwaka 2017 hakikisha unakuwa na muda wa kuongea na nafsi yako. Kuongea
na nafsi yako ni pale ambapo unakuwa na maneno ya kujiongelea mwenyewe na mara
nyingi inafaa uwe sehemu yenye utulivu kwa ajili ya kuepuka mwingiliano na
kalele nyingine ambazo zinaweza kukuhamisha.
Unapoongea
na nafsi yako hakikisha unajisemea maneno chanya ambayo yanakuhamasisha
kuchukuwa hatua za ushindi. Epuka sentensi kama “Kila ninalogusa linaniendea
kinyume, Siwezi kukamilisha kazi hii kwa muda, Siwezi kufanya biashara, Siwezi
kufaulu somo hili, n.k”. Maneno chanya ambayo unaweza kujisemea ni;
- Kila ninalogusa lazima nifanikiwe;
- Sijawahi kushindwa, hivyo lazima niishinde changamoto hii;
- Naweza kufanya jambo lolote ninalodhamiria;
- Najiamini katika huduma ninazotoa hivyo lazima nipate wateja;
- Mimi ni bingwa katika tasnia hii;
- Mimi ni hodari; n.k
Kuwa
mtu wa kutathmini mawazo yako. Zoezi la kuwaza chanya ni
gumu kama ulikuwa hujazoea kufanya hivyo. Kwa vyovyote vile lazima utajikuta
unaanza kutawaliwa na mawazo hasi. Ili kukabiliana na mawazo hasi lazima uwe na
muda wa kujiuliza mara kwa mara juu ya lile unalowaza kama lina mchango kwenye
mafanikio yako na pale unapotambua kuwa upo katikati ya mawazo hasi achana nayo
mara moja.
Chagua marafiki na makundi ya kujumuika
nayo. Kuna msemo maarufu usemao kuwa ndege wenye manyoa
yanayofanana huruka pamoja. Kama ulikuwa na marafiki ambao mmekuwa mnatumia
muda mwingi kufanya mambo yasiyo na tija katika mafanikio yako kwa sasa unatakiwa
kuchagua marafiki wapya ambao watapelekea ufanikiwe kuiishi kauli mbiu ya
uchanya. Epuka marafiki ambao muda mwingi wanautumia kulalamika, kusengenya,
kubeza yaw engine, kukatishana tamaa n.k
Pia, Katika ulimwengu wa sasa ambao umetawaliwa na
mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano husipokuwa makini kwenye makundi
(magroup) ambayo umeunganishwa nayo itakuwa vigumu sana kwako kuwaza chanya
kwani mara nyingi makundi haya yametawaliwa na mzaha mwingi ambao kwako hauna
tija. Mwaka 2017 hakikisha makundi ambayo hayana tija unajiondoa mara moja na
kujiunga na makundi mapya ambayo yatakupa mawazo, ushauri pamoja na changamoto
katika kutekeleza malengo yako.
Tenga
muda wa kusoma vitabu au makala za hamasa. Kama unataka
kufanikiwa ni lazima uwe mtu wa kusoma vitabu au makala zinazoendana na yale unayoyahitaji
katika maisha yako. Dunia kwa sasa imekuwa ni kijiji kwani unaweza kusoma
kitabu chochote kile kwa kutumia simu yako. Tatizo letu tumekuwa wavivu sana
katika kujisomea vitabu/makala za namna hii lakini cha kushangaza utakuta mtu
muda wote yupo bize na kusoma posti za watu au magazeti ya udaku kwenye mtandao
hila ukimuambia tumia saa moja kila siku kujisomea kitabu/makala atakuambia
kuwa makala/kitabu kina kurasa nyingi sana.
Mpendwa rafiki yangu naomba mwaka 2017 utambue kuwa hakuna
mafanikio yoyote ambayo yatakuja kwa njia ya mkato lazima uwe tayari kuwekeza
nguvu, muda pamoja na rasilimali ili hatimaye ufanikiwe. Anza kuwekeza sasa kwa
ulisha ubongo wako na maarifa mbalimbali kutoka kwa waliofanikiwa.
Kuwa Mtu wa Vitendo.
Mwaka 2017 unapoongozwa na
kauli mbiu ya uchanya hakikisha yale unayoyawaza unayaweka katika mfumo wa vitendo
mara moja pasipo kuhairisha au kusubiria. Wanafalsafa wanatuambia kuwa kila
kitu kinaumbwa kutokana na mfumo wa mawazo na kupitia mfumo huu kila mtu ana
uwezo wa kuumba chochote anachokiwaza. Tatizo kubwa ambalo limekuwa
linatutofautisha kwenye uumbaji wa vitu ni pale ambapo wengi wetu tumeruhusu
visingizio kukutawala na hivyo kuishia kutofanya lolote. Wengi mtakuwa
mashahidi kuwa unaweza kuwa na wazo zuri hila kutokana na mazoea ya kuwaza
pasipo kutenda inafikia kipindi mpaka unalisahau wazo lako halafu ghafla ukiwa
unatembea mtaani unashangaa kuna mtu ameanzisha biashara au anatoa huduma sawa
na lile wazo lako. Hapa kinachokutofautisha wewe na yeye ni kwamba mwenzio
alikuwa na wazo na akalitafsiri kwenye vitendo. Mwaka 2017 hakikisha unakuwa
mtu wa vitendo badala ya kuishia kuwaza tu.
Mwisho naomba nikutakie sherehe njema za mwaka mpya. Rafiki
yangu unaposherekea mwaka mpya hakikisha unauanza mwaka mpya kwa kuwaza chanya
kwani nakuhakikishia kuwa miezi 12 ni muda mfupi sana ukiwa unaishi kwenye
malengo yako. Ulimwengu wa sasa ni ulimwengu wa teknolojia ya mawasiliano hivyo
kama rafiki naomba uendelee kusambaza jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale
unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadirisha dunia hii kuwa
mahali pazuri pa kuishi. HERI YA MWAKA
MPYA 2017.
Karibuni kwenye fikra tajiri ili upate elimu hisiyokuwa
na mwisho.
Born to Win~Dream Big
A.M.
Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com
0786881155
bilondwam@yahoo.com