Fahamu Sababu Zilizosababisha Ushindwe Kufikia Malengo Yako Mwaka 2016

Rafiki yangu mpendwa ni matumani yangu kuwa haujambao na unaendelea na mapambano ya kufanikisha ndoto zako. Rafiki mpendwa nimekuwa nikikusisitizia umuhimu wa kuandaa kesho yako kwa kuahakkikisha unatumia muda vizuri ulionao kwa sasa ili kupitia yale unayoyafanya sasa yawe msingi wa ushindi ndoto zako hapo baadae. Kupitia kanuni hii ni wazi kuwa hakuna kesho bora pasipo kuwa na leo bora.


Baada ya utangulizi huu unaolenga kukupa hamasa na kutambua wajibu wako katika kufikia ndoto zako, leo hii ningependa tusafiri wote katika safari ambayo kituo chetu cha kwanza kinaitwa Januari Mosi, 2016 na mwisho wa safari yetu ni 31 Desemba, 2016. Mpendwa rafiki ni matumaini yangu kuwa kama una ndoto na ungependa kuzitimiza siku moja ni lazima unapoanza mwaka mpya huwa unaweka malengo ambayo hadi mwisho wa mwaka unahitaji yawe yamekamilika. Naamini rafiki yangu kuwa wewe ni tofauti na wale wengine ambao wamekuwa wakihitaji siku moja kuwa na mafanikio makubwa pasipokuweka jitihada zozote bali wakisubiria muujiza utokee. Kama unataka mwaka 2017 ufikie malengo yako tofauti na mwaka huu endelea kusoma makala hii hadi mwisho ili ufahamu siri kubwa ambazo zimekuwa zikikukwamisha mwaka hadi mwaka. Karibu ujifunze hapa chini;

Siri ya kwanza; Mwaka 2016 umekuwa mtu wa kulalamika; hakuna sumu kubwa ambayo imekuwa ikiua ndoto za walio wengi kama malalamiko. Watu wengi wamekuwa wakitafuta sababu za kuhalalisha kushindwa kwao kuonekane kuwa wameshindwa kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao. Mfano, mwaka 2016 watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imesababisha maisha kuwa magumu kwa misingi kuwa hali ya kifedha si shwari. Leo hii jiulize kama hali ya kifedha ilikuwa shwari katika Serikali ya Awamu ya Nne wewe kama wewe imekusaidia vipi kutimiza ndoto zako? Ili upate mafanikio unayoyataka ni lazima ufahamu kuwa Serikali haiwezi kukutimizia ndoto zako kwani hata yenyewe imeshindwa kutatua matatizo iliyonayo. Fahamu pia kuwa katika hali yoyote ile wewe mwenyewe ndo unajua kile unachohitaji au vile unavyotaka uwe hivyo ni wajibu wako kuanza kufanyia kazi ndoto yako sasa.

Muhimu: Aanza Januari, 2017 kwa kujitwisha msalaba wa maisha yako ukitambua kuwa wewe ni muhusika namba moja wa maisha yako na pale ambapo utashindwa kutimiza ndoto zako fahamu kuwa wa kulaumiwa ni wewe mwenyewe na wala si Serikali, familia, mwajiri wako wala mazingira yoyote yale.

Bonyeza kiunganishi hiki kusoma makala ya wewe ni mshindi huna sababu ya kushindwa: http://fikrazakitajiri.blogspot.com/2016/12/wewe-ni-mshindi-huna-sababu-ya-kushindwa.html

Siri ya pili; Mwaka 2016 uliruhusu hofu ya kushindwa ikutawale badala ya kuruhusu hamu ya mafanikio: Mpendwa rafiki yangu wanasaikolojia wanatuambia kuwa sisi ni zao la kile ambacho tunawaza mara kwa mara. Kwa maana hii sisi ni waumbaji wa maisha yetu ya baadae “we are the creator of our own destiny”. Kwa ukweli huu ni wazi kuwa mwaka 2016 kama uliruhusu hofu ya kushindwa kuliko hamu ya kushinda maana yake ni kwamba wewe mwenyewe ulijijengea msingi wa kushindwa kuliko kushinda na hivyo matokeo yake umehindwa kutimiza malengo yako.

Muhimu: Katika kipindi chote cha mwaka 2017, hakikisha hauruhusu hofu kuyatawala maisha yako. Iambie nafsi yako kuwa mimi ni mshindi na nimeumbwa kwa ajili ya kushinda bila kujali ni mazingira yapi napitia kwa sasa na kwa mtazamo huu nitashinda chochote kile ambacho nitadhamiria kufanya. 

Siri ya tatu; Mwaka 2016 umekuwa mtu wa kuhairisha mambo. Huu ni ugonjwa ambao umeangamiza ndoto nyingi na umekuwa ukisababishwa na watu wengi kuona kuwa muda upo wa kutosha. Watu wengi wametawaliwa na kauli za nitafanya badala ya kauli za ninafanya. Ulipoanza mwezi wa kwanza 2016 uliona kuwa mwaka ni mrefu na hivyo kusogeza kile ambacho ulikuwa umepanga kukamilisha kwenye miezi ya baadae hadi ukajikuta robo ya kwanza imekatika, nusu ikapita, hadi robo ya tatu na mwisho wake ukakata tamaa na kujisemea kuwa mwaka huu mambo yangu yamenibana ngoja nijipange kwa ajili ya mwakani.

Muhimu: Mwaka 2017 tambua kuwa hakuna siku hata moja ambayo hautabanwa na mambo yako na hivyo hakikisha unafanya mara moja kile ambacho umelenga kukamilisha. Haijalishi unaanza kwa kiasi kidogo sana cha msingi wewe anzisha ukiwa na picha kubwa unayotaka kuifikia.

Siri ya nne; Mwaka 2016 ulitumia kiasi chote ulichokipata pasipo kujiwekea akiba: Imekuwa ni kawaida ya watu walio wengi kutumia kiasi chote wanachopata pasipo kujiwekea akiba kwa ajili ya baadae. Binafsi nilikuwa kwenye kundi hili lakini siku moja katika kujisomea vitabu vya kanuni/siri za mafanikio nikakutana na kanuni ya “Kujilipa Kwanza”. Kanuni hii ni rahisi sana na unachotakiwa kukifanya kupitia kanuni hii ni kuhakikisha unajiwekea sheria ya kwamba kila shilingi inayoingia mkononi mwako lazima ikatwe asilimia fulani kwa ajili ya akiba yako ya baadae. Binafsi nimekuwa nawekeza asilimia kumi ya kila shilingi inayoingia mikononi wangu. Nitafute kwa watsapp kupitia namba 0786 881 155 kwa ajili ya kufundishwa zaidi namna gani unaweza kujilipa kwanza kwa muda mrefu ukiongozwa na nidhamu ya hali ya juu pasipo kushawishika kutumia hiyo akiba yako. Ni aibu sana mwajiriwa au mtu yeyeto mwenye uhakika wa kupata kipato hata kama ni kidogo kiasi gani kufikia mwisho wa mwaka ukiwa hauna hata shilingi uliyoiweka kwa ajili ya akiba yako ya baadae.

Muhimu: Mwaka 2017 tumia kauli ya hata mbuyu ulianza kama mchicha kuhakikisha kuwa unaanza kujiwekea akiba hata kama ni kidogo kiasi gani cha msingi uongozwe na nidhamu binafsi ya hali ya juu.

Siri ya tano; Mwaka 2016 hukuwa na orodha ya malengo yako iliyoandikwa: Ukiwa na malengo kichwani mwako pasipo kuyaandika sehemu ni moja ya sababu nyingine inayowakwamisha walio wengi hii ni kutokana na ukweli kuwa kadri utakavyokuwa unayosoma mara kwa mara ndivyo utakavyokuwa na hamasa ya kupigana kuyatimiza. Kuna sababu kuu nne za kwanini unapaswa kuyaandika malengo yako kwenye karatasi au compyuta yako:
a)    Ni rashisi kuyarejea na hivyo unaweza kuyakumbuka pindi unapoyatekeleza;
b)   Yanapimika. Ni rahisi kujua kuwa unatekeleza lipi kwa muda gani;
c)    Yanajieleza vizuri tofauti na kuwa nayo kichwani mwako; na
d)   Ni rahisi kuyahuisha (review) ili kuendana na hali halisi ya wakati huo.

Muhimu: Mwaka 2017 nunua kijitabu kidogo (diary) kwa ajili ya kuandika malengo yako na mambo mengine muhimu na hakikisha kijitabu hicho unasafiri nacho kila sehemu na hakikisha unayasoma kila siku.

Siri ya sita; Mwaka 2016 uliruhusu muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii na malumbano yasiyo na tija kuliko kwenye mambo yako binafsi: Mpendwa rafiki yangu hakuna kitu kibaya ambacho kwa sasa kinaharibu vijana kama kukua kwa teknolojia ya mawasiliano. Vijana wengi kwa sasa wanashinda kwenye mitandao ya kijamii wakisubiria kupost na kuchangia kwenye mada mbalimbali. Kumbuka kile unachokiwaza/kufanya muda mwingi ndicho kinakutambulisha jinsi ulivyo, kwa ukweli huu ni wazi kwamba kadri unavyoshinda kwenye mitandao ya kijamii ndivyo unapoteza muda ambao ungeutumia kuwaza au kufanya vitu vya maana kwa ajili ya kutimiza malengo yako.

Muhimu: Mwaka 2017 aanza kwa kupunguza makundi yote ambayo hayana mchango wa maana kwenye kutimiza ndoto zako. Jiepushe na makundi au marafiki ambao walishakata tamaa ya mafanikio na hakikisha unajiunga na marafiki wapya wenye mtazamo kama wako.

Siri ya saba; Mwaka 2016 umeishi maisha ya kuigiza: Rafiki mpendwa kamwe hauwezi kufanikiwa kama hauishi vile unavyotaka wewe badala yake umekuwa mtu wa kuiridhisha jamii au watu wako wa karibu. Katika dunia ya sasa imekuwa ni kawaida watu kuishi kulingana na matakwa ya jamii au ndugu zao na hivyo kujikuta hawana vipaumbele vya maisha yao. Rafiki yangu naomba ujifunze kusema HAPANA pale unapoona maisha unayoishi hayaendani na matakwa yako. Pia, jifunze ukweli kuwa sio kila unaloambia hapana ni hapana kwani jamii tunayoishi kwa sasa ina kila sababu ya kukuonesha kuwa hauwezi kufanikiwa na hivyo kukukatisha tamaa.

Muhimu: Mwaka 2017 hakikisha unaishi misingi ya maisha yako vile unavyotaka wewe na si jinsi gani jamii ilivyozoea. Hakikisha unaishi kwa kufanya vitu kwa hali tofauti ya mazoea ya jamii.

Mpendwa rafiki yangu nimekushirikisha siri saba ambazo zimekukwamisha mwaka 2016. Ni matumaini yangu kuwa makala hii itakusaidia kutimiza malengo yako kwa mwaka 2017. Mpendwa rafiki yangu kama umejifunza kitu kwenye makala hii naomba uisambaze kwa kadri uwezavyo ili siri hizi ziwafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadirisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Karibuni kwenye ulimwengu wa elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com




onclick='window.open(