Ni matumaini yangu kuwa rafiki unaendelea vizuri na
mapambano kwa ajili ya kufanikisha ndoto zako. Huu ni wakati mwingine ambao Mwenyezi
Mungu ametujalia kwa ajili ya kuyafanya maisha yetu kuwa bora kiafya, kiimani,
kiuchumi na kijamii pia. Ni wakati ambao Wakristu wote duniani tunaungana kwa
ajili ya kushangilia kuzaliwa kwa mwokozi wetu Yesu Kristu tukiwa tunafakari
ukombozi wetu. Ni jambo la heri kuona sisi tulio hai tunafikia siku kama ya leo
tukiwa na nguvu za kutosha kwa ajili ya kufanikisha shughuli zetu za kila siku.
Hongera sana rafiki kwa zawadi hii muhimu.
Nakupa hongera kwa sababu naamini kuwa ukiwa na uhai na
nguvu ni zawadi tosha kwako wewe rafiki yangu ambae unatamani siku moja ufikie
ndoto zako. Leo hii ningependa nikushirikishe stori muhimu katika maisha yangu
ambayo ilitokea siku kama ya leo (24, Desemba). Karibu tuwe pamoja ili
tujifunze kitu kutoka kwenye stori hii.
Stori yangu inaanzia hapa “Ilikuwa mwaka 1999 siku kama
ya leo kipindi hicho nikiwa mwanafunzi wa darasa la tano, tukiwa tunajiandaa
kusherekea Sikuu ya Christmas niliamua kwenda kukusanya kuni za biashara ili
ninaposherekea Siku Kuu niwe na fedha kwa ajili ya kufurahi nikiwa na watoto
wenzangu. Asubuhi na mapema baada ya kuamka niliipanga vizuri ratiba yangu kwa
kuanza na kukusanya mzigo wa kwanza kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na baadae
ndo nikaendea mzigo wa kuni za kuuza.
Baada ya kupangilia vizuri ratiba yangu nilifanikiwa kwa
kiasi kikubwa kwani siku hiyo niliweza kukusanya mizigo miwili ya kuni moja kwa
ajili matumizi ya nyumbani na mwingine kwa ajili ya kuuza. Biashara ilienda
vizuri kwani nilifanikiwa kupata fedha yangu shilingi 500 za kitanzania kama
malipo yangu na ndipo nikarudi nyumbani nikiwa na tabasamu la kutosha kutokana
na mafanikio ya siku hiyo na matarajio ya siku inayofuata kwani tayari uhakika
wa kusherekea vizuri ulikuwepo.
Baada ya kufika nyumbani nilikuta nasubiliwa na mama
mzazi (Mwenyezi Mungu amurehemu) kwa hasira sana kwa kile ambacho ilisemekana kuwa
niliondoka bila kuaga na kibaya zaidi nilipoulizwa nilikuwa wapi ndo nikajibu
kuwa nilienda kukusanya kuni za biashara. Ilinibidi nipokee kipigo cha hali ya
juu kutokana na makosa hayo na kuonywa kuwa kwamwe hisije ikajirudia na kibaya
zaidi nikanyanganywa ile shilingi 500 kwa kile ambacho ilisemekana mimi kama mtoto
ni tabia mbaya kujizoesha pesa”.
Kwanini
nimekushirikisha stori hii iliyonitokea mimi?
Rafiki leo hii nilipokumbuka mkasa huu nikaona
nikushirikishe wewe ambae najua kwa sasa yawezekana ni baba/mama wa familia na
tayari una watoto au kama bado haujaingia kwenye maisha ya ndoa ni matarajio yangu
kuwa siku moja unatamani kuingia kwenye maisha haya. Ukiwa mzazi/mlezi
natarajia kuwa wewe kama baba/mama unajua wajibu wako mkubwa wa kuhakikisha
unakuwa kiongozi wa wanao katika kuwakuza kwenye misingi ya kiroho, kijamii na
kiuchumi. Ni wazi kuwa kizazi kilichokuzwa vyema kwa kuzingatia misingi hii
lazime kiwe kizazi chenye kila aina ya mafanikio.
Yamkini wazazi walio wengi wamekuwa wakiegemea kwenye
makuzi ya kiroho na kijamii na kusahau msingi mkuu mwingine wa kumkuza mtoto kiuchumi.
Katika msingi huu wazazi/walezi wengi badala ya kuwaendeleza watoto kiuchumi
wamekuwa wakiua vipaji vya watoto wao na hivyo watoto kuendelea kuwa
wategemezi siku hadi siku. Mbaya zaidi ni kwamba watoto hawa wanaendelea kuamini
kauli za wazazi wao ambazo zilichangia kuua vipaji/ndoto zao na hatimaye
tunakuwa na vizazi vyenye fikra hasi kwenye mafanikio ya kiuchumi. Mfano fikiria
kama kauli hiyo iliyonitokea ya kuwa mimi kama mtoto sipaswi kujizoesha pesa
kwani kwa kufanya hivyo ningekuwa mwizi. Naamini kauli kama hii imekuwa ikitumiwa
na wazazi/walezi walio wengi kwa watoto wanaowalea na hivyo kupelekea watoto
wengi kuamini kuwa ukipenda pesa sana utakuwa mwizi!! Matokeo yake ni watoto
kubadiri fikra/mitazamo yao kuhusu pesa.
Mfano mzuri ni mimi baada ya kupigwa kutokana na makosa
hayo ilinibidi niache kabisa kujihusisha na aina yoyote ile ya biashara kipindi
chote cha utoto wangu na hata nilipokuwa katika elimu ya sekondari sikuweza
kufanya biashara yoyote ambayo ingeenda kinyume na matakwa ya wazazi wangu. Matokeo
yake ilinibidi nibadirishe kabisa fikra zangu na kufikiria masomo tu huku
nikiamini kuwa masomo ndo mkombozi wa maisha yangu na hivyo kupelekea kuwa
mtegemezi kwa wazazi wangu kipindi chote cha masomo yangu.
Rafiki yangu mpendwa kama mzazi/mlezi naomba utambue
kuwa wewe una wajibu mkubwa wa kuhakikisha unamuongoza mwanao ili aweze
kuendeleza vipaji alivyonavyo hasa linapokuja suala zima la vipaji vya
kujikomboa kiuchumi. Fikiria kama bilionea Bill Gates angekatishwa tamaa na
wazazi leo hii angekuwaje? Wapo wakina Bill Gates wengi ambao ndoto zao
zimekatishwa kutokana na mazingira ya malezi yao hivyo kama mzazi unatakiwa kulitambua
hilo na kusimama imara.
Rafiki yangu naomba pia utambue kuwa wanamafanikio walio
wengi ni wale ambao wamefanya vitu wanavyovipenda kutoka rohoni mwao na si wale
ambao wamekalilishwa kuwa mwanangu nenda shule soma kwa bidii ili upate kazi
nzuri itakayokuwezesha kulipwa vizuri na hatimaye uweze kutusaidia wazazi wako.
Ndio maana wanamafanikio wengi ni wale ambao mwanzo walikataliwa na jamii
kutoka na yale wanayofanya kuonekana yanaenda kinyume na mazoea ya jamii. Kutokana
na ukweli huu ni wazi kuwa vizazi hadi vizazi vinapita pasipo kuwa na misingi
imara ya elimu fedha na hivyo kuzalisha vizazi ambavyo ni tegemezi kwa kuwa
jamii inapenda kuishi kwa mazoea. Rafiki yangu naomba wewe kama mzazi/mlezi
mtarajiwa hepuka sana kumlea mwanao kwa mazoea ya jamii bali hakikisha
unaendelea kujifunza vipaji alivyonavyo ili umsaidie kuviendeleza.
Mpendwa rafiki yangu naomba utambue kuwa kutokana na
wengi wetu kukosa misingi ya elimu ya fedha tumeendelea kuadhibiwa na dunia
kwenye upande wa elimu hii na hivyo kuwa masikini kizazi hadi kizazi. Hii ni
kutokana na ukweli kuwa tumekuwa tukiishi kwenye mazoea ya jamii ambayo
yanaenda kinyume na kanuni za mafanikio ya fedha. Matokeo yake ni kurudia
makosa yaleyale ambayo yalifanywa na mababu zetu na hivyo kujikuta hatusogei
kokote mpaka tunaishia kuimba nyimbo zilezile….hoo familia yetu hatujawahi kuwa
matajiri hivyo na mimi siwezi kuwa tajiri!, sina fedha za kutosha kuanzisha
biashara!, Serikali imekaza hivyo hatuwezi kutimiza ndoto zetu… na nyimbo
nyingine nyingi.
Mpendwa rafiki yangu tambua kuwa kutokana na kuishi kwa
mazoea tumebadirishwa fikra zetu na jamii na hivyo kuaminishwa kuwa mafanikio
ya kifedha ni kwa wateule wachache. Jambo hili limepelekea kuamini kuwa wewe
kamwe hauwezi kuwa kati ya hao wachache kitu ambacho si kweli. Kama mzazi
naomba utambue kuwa una wajibu mkubwa wa kumuandaa mwanao ili aweze kuwa na misingi
imara ya elimu ya fedha na hatimaye tufanikiwe kuwa na kizazi chenye kila aina
ya ubunifu katika kujitengenezea kipato hivyo kuondoa utegemezi unaotuandama
kwa sasa. Badala ya kuendelea kuilalamikia Serikali naomba ujiulize wewe kama
wewe wajibu wako ni upi katika kufanikisha maendeleo ya taifa hili hasa ukianzia
na wajibu wako katika kukuza vipaji vya watoto wako kiroho, kijamii na
kiuchumi.
Mwisho naomba nikutakie sherehe njema za Siku Kuu ya
Christmas hapo kesho nikiamini kuwa kesho itakuwa siku yako nzuri ya kukaa
pamoja na familia yako na kutafakari mambo makuu Mwenyezi Mungu aliyokujalia
kupitia familia hii. Mpendwa rafiki yangu niendelee kukuomba kusambaza jumbe
hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye
tufanikiwe kuibadirisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi.
Karibuni kwenye ulimwengu wa elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com
0786881155
bilondwam@yahoo.com