Habari
ya leo mpenzi msomaji wa makala hizi katika ukurasa huu wa Facebook. Ni
matumaini yangu kuwa upo vizuri na unaendelea
kupambana ili kuifanya kesho yako kuwa bora zaidi ya leo yako. Nasema hivyo kwa
matumaini ya kwamba mpendwa rafiki yangu unafahamu kuwa hakuna kesho bora
ambayo haijaandaliwa kwa jana yake. Hivyo naomba uendelee kukazana kila iitwapo
leo kwa ajili ya mafanikio makubwa ya baadae.
Karibu tujifunze wote ambapo leo
hii nimelenga nikuoneshe nguvu ya ajabu iliyopo ndani mwako ambayo ipo toka
siku uliyoumbwa na ni nguvu hii ambayo imekuwa ikiwatengeneza mabillionaire na
mamilionea kila kukicha ikitegemea na jitihada zao katika kutumia nguvu hii.
Kama unataka kujifunza zaidi juu ya nguvu karibu tujifunze wote.
Kabla ya kuanza ningependa utafakali sehemu hii ya
sura ya biblia takatifu Mwanzo 1:26, nanukuu “Mungu akasema, Na tumfanye mtu
kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa
angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu
ya nchi”. Baada ya kutafakari sehemu hii ya maandiko matakatifu karibu
nikushirikishe mambo makuu matano ambayo hujawai kufikilia mchango wake katika
mafanikio yako.
MOJA:
TUMEPEWA NGUVU YA KUUMBA KITU CHOCHOTE TUNACHOTAKA: Sehemu ya
maandiko matakatifu tuliyosoma hapo juu inatukumbusha kuwa tumeumbwa kwa mfano
wa Mwenyezi Mungu na tukapewa nguvu ya kutawala vitu vyote vilivyopo duniani
humu. Hata hivyo tunatakiwa kufahamu kuwa kwa kuumbwa kwa mfano wake tumepewa
nguvu ya kuwa waumbaji katika mazingira yetu yanayotuzunguka kwa kutumia vitu
ambavyo tuna mamlaka ya kuvitawala. Pointi muhimu ambayo nataka uondoke nayo ni
kwamba chochote kile ambacho utaweka dhamira kiasi kwamba kikawa ni sehemu ya
fikra zako za kila muda basi hakuna muhujiza wa kukuzuia kupata kitu hicho.
Watu wengi waliofanikiwa ambao nimefuatilia historia zao wametumia siri hii
kupata mafanikio ya hali ya juu. Mfano, mgunduzi wa magari ya V8 HENRY FORD,
alitumia siri hii kufanikiwa kutengeneza kwa mara ya kwanza gari la kifahari
lenye silinda (cylinder) nane ndani ya injini moja. Mwanzoni alipotoa wazo hili
kwa wafanyakazi wake alipewa jibu kuwa haiwezekani kutengeneza gari lenye
silinda nane ndani ya injini moja lakini jibu alilowapa lilikuwa endelea mpaka
mfanikiwe kwani nahitaji gari la modeling hiyo. Aliporudi kuwauliza mara ya
pili alipewa jibu sawa na lile la kwanza lakini akawaambia ni lazima nipate
gari hilo endelea kulifanyia kazi. Hali iliendelea hivyo mpaka mara nne. Lakini
hatimae leo hii tunatembelea magari ya kifahari ya V8 kutokana na nguvu ya
uumbaji aliyokuwa nayo Henry Ford.
MUHIMU: Tafakari kwa
kina juu ya nguvu uliyonayo katika kuumba vitu kimawazo na kivitendo na kisha
iambie nafsi yako kuwa nitaumba vitu vingi kwa kadri niwezavyo pasipo
kukatishwa tamaa na maneno ya watu.
MBILI: KILA
KILICHOPO DUNIANI HUMU NI KWA AJILI YA USHINDI WAKO: Kila mahali
ulipo kuna fursa ambayo inakusubilia wewe uitumie na kuiendeleza ipasavyo. Kuna
msemo usemao kuwa “kila mahali kuna dhahabu japo watu wengi hawajui jinsi ya
kuitafuta”. Naamini unakubaliana na msemo huu, binafsi nimekuwa nikiutumia kila
siku na kila sehemu ninapokuwa hasa sehemu zinazokimbiwa na watu kwa kuonekana
hazifai kitu. Mpendwa rafiki yangu fungua macho na kutazama ipasavyo mazingira
yanayokuzunguka na kila kukicha hakikisha unatumia fursa zilizopo kwa kadri
uwezavyo.
MUHIMU: Fahamu ya
kuwa kila sehemu ulipo kuna dhahabu hivyo jukumu lako kubwa ni kujifunza jinsi
gani wengine wamefanikiwa kuchimba dhahabu hiyo kwa mafanikio makubwa sana.
TATU: WEWE
NI KIUMBE PEKEE CHENYE UWEZO WA KUCHAGUA JEMA NA BAYA. Kila
mwanadamu amepewa uwezo wa hali ya juu wa kuchagua kati ya jema na baya. Ubongo
wa mwanadamu ni sehemu yenye mfumo wa hali ya juu unaowezesha kila
linalofanyika kupitia kwenye mfumo huu. Ubongo huu umegawanyika kiasi kwamba
kila sehemu ina jukumu lake ambalo inalifanyia kazi. Linalofanywa au kutamkwa
lazima lipitie kwenye sehemu ya ubongo inayojihusisha na fikra na ndipo
muhusika anafanya kile kilichofanyiwa kazi kwenye ubongo. Kwa maana nyingine ni
kwamba ubongo ndo kompyuta ya asili ya binadamu ambayo jukumu lake kubwa ni
kuchakata taarifa zote zinazoingizwa na hatimaye kutoa matokeo. Kwa maana hiyo
matokeo yatakayotoka yatategemea taarifa zinazoingizwa (garbage in garbage
out). Ukiujaza ubongo wako taarifa za uovu, hofu, chuki, kusengenya, kukata
tamaa na kushindwa vivyo hivyo utegemee matokeo yanayoendana na hayo.
MUHIMU: Kuanzia
sasa fahamu kuwa unaweza ukaamua kutenda mema tu na ukafanikiwa kwani wewe ndo
rubani namba moja wa fikra zako. Pia iambie nafsi yako kuwa kuanzia sasa
utaujaza mfumo wako wa ubongo na taarifa za ushindi kwani kwa kufanya hivyo
unajitengenezea mazingira unayotaka kuyaishi.
NNE: WEWE NI
KIUMBE PEKEE MWENYE KUWEZA KUAMUA HATMA YA MUDA WAKO: Wewe ni wa
pekee kwa vile unao uwezo wa kuamua nini kifanyike katika kila sekunde ya
maisha yako. Ushindi wako unatokana na jinsi gani unatumia muda wako.
Kinachotofautisha watu waliofanikiwa katika maisha yao na wale ambao ni watu wa
kawaida ni namna ambavyo makundi haya yanatumia muda wao. Wote tumepewa
sekunde, dakika, Masaa sawa lakini tofauti yetu ni jinsi tunavyotumia zawadi
hii. Wapo wanaotumia zawadi hii kwa kuchart 24/7, wapo wanaotumia kwa kuangalia
luninga 12/7, wapo wanaotumia kubeza wengine, wapo wanaotumia kucheza
kamali….n.k. lakini kumbuka kuwa kila unalolifanya kwenye kila sekunde ya
maisha yako lina mchango mkubwa katika mafanikio yako na hivyo kuamua wewe ni
mtu wa aina gani.
MUHIMU: Kuanzia
sasa fahamu ya kuwa wewe ni mshindi wa maisha yako kama utaamua kutumia vizuri
muda wako. Fahamu ya kuwa jinsi ulivyo ni matokeo ya yale unayoyafanya kwa kila
sekunde ya maisha yako. Chukua hatua sasa ili uwe mshindi.
TANO: NI
WEWE PEKEE MWENYE HAMASA NDANI YAKO: Katika mafanikio hamasa ni ule
msukumo unaokufanya uendelee kufanya kile unachokifanya. Msukumo huu unaweza
kutoka ndani kwa ndani au msukumo wa nje. Mara nyingi msukumu unaotoka nje huwa
ni wa muda ukilinganisha na msukumo unaotoka ndani mwako. Ili upate mafanikio
ni lazima uwe na hamasa ya hali ya juu inayokupa msukumo wa kuendelea kufanya.
Kuna msemo kuwa “unaweza kumpeleka punda kunywa maji lakini hauwezi
kumulazimisha kunywa maji”, hii ina maana kwamba hamasa ya nje haiwezi kukubadilisha
kama wewe mwenyewe haujaamua kubadilika. Jambo jingine la kukumbuka ni kwamba
hamasa ya ndani sio kitu cha siku moja bali inatakiwa iwe sehemu ya maisha yako
ya kila siku sawa na ambavyo kila siku lazima ule hauwezi kusema kuwa leo
nakula chakula cha kutosha siku zote za maisha yangu bali kila siku unatakiwa
upate chakula vivyo hivyo ndivyo ilivyo hamasa ya ndani (self motivation).
Tunaweza kusoma maandiko mbalimbali kuhusu mafanikio ya watu waliofanikiwa
kimaisha na kuhamasika kwa muda lakini kama hatujaamua kufanya hamasa hiyo kuwa
sehemu ya maisha yetu itakuwa sawa na bure. Mfano mzuri ni wewe mwenyewe
umekuwa kila mwanzo wa mwaka unaweka malengo na kujisemea rohoni kuwa mwaka huu
naanza mwaka mpya na mambo mapya kwa maana unaachana na mabaya uliyoyafanya kwa
mwaka unaoisha lakini ghafla kadri mwaka unavyoendelea unajikuta unarudia
makosa yale yale. Kumbe hii inatokana na msukumo wa nje unaoupata kutokana na
jamii kuzoea kufanya hivyo mwaka hadi mwaka.
MUHIMU: Kuanzia
sasa ifundishe nafsi yako kuwa na hamasa ya kudumu inayotoka ndani kwa ndani na
hamasa hii iwe ni sehemu ya maisha yako ya kila siku. Ili kufanikisha hili
tengeneza malengo yako ya muda mfupi na muda mrefu na kuanza kuyafanyia kazi
mara moja.
Mpendwa rafiki yangu nimekushirikisha mambo
matano ya kukuonesha kuwa wewe ni mshindi na hauna sababu ya kushindwa. Naomba
utumie kila siku ya maisha yako kuhakikisha unafanyia kazi yale ambayo
unatamani yawe sehemu ya ushindi wako. Fahamu kuwa hakuna mwaka kama hakuna
sekunde. Vivyo hivyo hakuna mafanikio makubwa pasipo kusherekea ushindi
mdogomdogo. Tengeneza ushindi wako kila iitwapo leo ili ushindi huo uwe sehemu
ya hamasa yako.
Kama umejifunza kitu kwenye makala hii
naomba uisambaze kwa kadri uwezavyo ili somo hili liwafikie wengi na hatimaye
tufanikiwe kuifanya dunia hii kuwa mahali pazuri pakuishi. Karibuni kwenye
elimu hisiyokuwa na mwisho.
A.M. Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com