NENO LA SIKU_APRILI 16/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Njia 4 Zitakazo Kuwezesha Kupata Mtaji.
Hongera rafiki kwa kuendelea kufuatilia masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri. Ni siku nyingine ambayo naamini imekuwa miongoni mwa siku bora hasa kwa kuzingatia kuwa umeitumia kutekeleza vipaumbele muhimu vya maisha yako.
Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA
Karibu tena katika makala ya leo ambapo nitakushirikisha njia nne za kupata mtaji wakati wa kuanzisha biashara ya ndoto yako.
Katika makala ya jana tuliona kuwa asilimia kubwa ya watu wanashindwa kuanzisha biashara kutokana na sababu za kukosa mtaji.
Tuliona kuwa pamoja na wengi kuelezea mtaji kama kikwazo nambari moja wakati wa kuanzisha biashara, ukweli ni kwamba wengi wanashindwa kuanzisha biashara kwa sababu hawana mawazo sahihi pamoja na maarifa sahihi kuhusu biashara wanazotamani kuanzisha.
Kama ni mara yako ya kwanza kusoma makala hizi nashauri usome mfululizo wa makala zote kupitia wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.
SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Kikwazo Ambacho Hukwamisha Wengi Kuanzisha Biashara
Kama una kiu ya kuanzisha biashara karibu ujifunze njia nne ambazo zitakuwezesha kupata mtaji.
Nikumbushe kuwa katika tafsiri ya biashara, tunaposema mtaji tunamaanisha uwezo wa kukuwezesha kuanzisha, kusimamia au kukuza biashara.
Uwezo huu tunaweza kuugawa makundi matatu ambayo ni: nguvu kazi, rasilimali fedha na ujuzi au maarifa.
Nguvu kazi inajumuisha uwezo uliopo ndani mwako ikiwa unaweza kufanya kazi zinazohusiana na usimamizi au uendeshaji wa biashara utakayo anzisha. Pia, nguvu kazi hujumuisha uwezo ulionao kupitia mahusiano yako na watu wanao kuzunguka.
Rasilimali fedha hujumuisha uwezo ulionao wa kifedha kupitia fedha taslimu au mali unazomiliki ambazo zinaweza kubadilishwa kuwa fedha kwa ajili ya ya kuanzisha biashara unayotamani.
Ujuzi au maarifa hujumuisha uwezo ulionao ambao unaweza kutumika kuzalisha fedha zaidi.
Kupitia makundi haya tunapata njia nne za kukusanya mtaji wa kuanzisha biashara kama ilivyo elezwa hapa chini;-
Kupitia mahusiano ya ndugu au marafiki. Hii ni njia ya kupata mtaji ambayo hutegemea uhusiano pamoja na uwezo wa ndugu au marafiki wako wa karibu.
Njia hii inaweza kuhusisha kupata mtaji kupitia mirathi, kufanya kazi kwa ndugu au rafiki kwa makubaliano maalum au kukopeshwa mtaji kwa masharti nafuu ikitegemeana na uaminifu wako kwa ndugu au rafiki mwenye uwezo wa kifedha.
Jambo la kuzingatia, njia hii ya kupata mtaji haipo wazi kwa kila mtu maana hutegemea hali ya kifedha na utayari wa ndugu au marafiki katika kukuwezesha kimtaji.
Kupitia akiba binafsi. Ni njia ya kupata mtaji ambayo hutokana hazina yako ya pesa taslimu au mali unazomiliki ambazo zinaweza kugeuzwa kwenye fedha taslimu kwa urahisi.
Njia hii inakutaka uwe na akiba ambayo ambayo umeikusanya kwa muda mrefu kwa ajili ya kukuza mtaji.
Katika makala zilizopita tuliona kuwa njia rahisi ya kukuza akiba yako ni kupitia njia ya kujilipa kwanza ambapo unakuwa na nidhamu ya kutenga kiasi cha pesa kwa ajili ya akiba na uwekezaji.
SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Tumia Siri Hii Kukuza Utajiri Wako
Pia, kwa njia hii unaweza kupata mtaji kupitia mali unazomiliki kama vile mifugo, ardhi, mitambo, hisa, nyumba, gari au mali nyinginezo ambazo unamiliki zinazoweza kubadilishwa kwenye fedha taslimu kwa urahisi.
Hii ni njia ambayo inakutaka uwe na nidhamu ya kutosha hasa katika kutenga fedha kwa kipindi cha muda mrefu kwa ajili ya akiba na uwekezaji.
Kwa kukosa nidhamu binafsi, wengi hushindwa kutenga akiba au hujikuta wametumia kiasi kilichotengwa kwenye matumizi mengine kinyume na malengo ya awali.
Kupitia njia ya mikopo (OPM). Hii ni njia ambayo unatumia pesa za watu wengine (using other people’s money - OPM) kukuza mtaji wako.
Ni njia ya uhakika ya kupata mtaji ikiwa unakopesheka au una wazo la biashara ambalo linauzika.
Hata hivyo, njia hii huwa ni ngumu hasa kwa wale wanao anzisha biashara kutokana na kutokuwa na dhamana ambazo hutakiwa na wakopeshaji kama vile taasisi za fedha (benki, SACCOS/VICOBA, microfinance au watu binafsi).
Pia, mara nyingi taasisi za kifedha huwa zinatoa pesa kwenye biashara ambazo tayari zina uhakika wa uendelevu.
Pamoja na changamoto za upatikanaji wa mikopo, njia hii inaweza kutumika kukuza mtaji wako kupitia mikopo ya benki, SACCOS/VICOBA, Microfinance au mikopo ya serikali kwa makundi maalum.
Kupitia SACCOS/VICOBA unaweza kukopa ikiwa hata hivyo wewe ni mwana ushirika (SACCOS) wenye malengo ya kukopesha wanachama wake kulingana na hisa wanazomiliki kwenye SACCOS/VICOBA husika.
Kupitia njia ya mikopo ya benki, kama tulivyoona masharti yake huwa ni magumu hasa kwa biashara ambazo hazina uhakika wa kurejesha kiasi unachohitaji.
Hata hivyo, kama ni mwajiriwa unaweza kutumia ajira yako kama dhamana ya kukopa na kupata mtaji wa kuanzisha biashara badala ya kununua gari au kujenga nyumba.
Kupitia njia ya kukopa kwenye ‘Microfinance’ au watu binafsi, mikopo hii hupatikana kwa masharti rahisi lakini huwa na riba kubwa wakati wa kurejesha.
Hali inaweza kusababisha kushindwa kukuza biashara yako kutokana riba unayotakiwa kurejesha kuzidi faida inayozalishwa kwenye biashara husika.
Kupitia mikopo maalum ya Serikali, mikopo hii hutolewa kwa makundi maalum kwenye jamii kama vile vijana, akina mama au watu wenye ulemavu.
Kupata mikopo hii, ikiwa upo kwenye makundi yaliyotajwa inabidi uwe kwenye kikundi kilichosajiliwa na kupitia kikundi chenu mnaomba mkopo huo ambao hutolewa na Serikali za Mitaa, baadhi ya taasisi za Serikali kama vile SIDO au baadhi ya miradi ya Serikali inayofadhiliwa na Mashirika.
Kupitia njia ya kuuza ujuzi, maarifa au kipaji. Njia hii inahusisha kubadilishana ujuzi, maarifa au kipaji na fedha.
Ni njia ambayo inaweza kutumika kukuza mtaji ikiwa una nidhamu na pesa unazopata kutoka kwenye mauzo ya ujuzi, maarifa au kipaji.
Pia, wakati mwingine msingi wa biashara unaweza kujengwa kupitia kutumia ujuzi, maarifa au kipaji chako.
Kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, katika karne hii ni rahisi kukuza mtaji kwa kuwa unaweza kuuza ujuzi, maarifa au kipaji chako kwa urahisi tena bila kizuizi cha mipaka ya nchi.
Mfano, tunaona jinsi ambavyo mmiliki wa mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp anavyo tengeneza pesa nyingi kutokana na ‘software’ ya mawasiliano aliyoianzisha kupitia ujuzi mifumo ya kompyuta.
Na wewe katika eneo lako, unaweza kuuza kipaji, ujuzi au maarifa na kukusanya pesa kwa ajili ya kukuza mtaji wako.
Hitimisho. Moja ya changamoto kubwa ambayo wajasiriamali wanakabiliana nayo ni kutafuta pesa kwa ajili ya kuanzisha, kuendesha au kufanikisha ukuaji wa biashara.
Mtaji umeendelea kuwa kikwazo nambari moja ambacho hukwamisha watu katika kuelekea kwenye ukamilisho wa ndoto zao.
Hata hivyo, watu ambao wamedhamiria kuishi ndoto zao wamefanikiwa kukuza mtaji kupitia njia ambazo nimekushirikisha kupitia makala hii.
NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.
WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.
Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.