NENO LA LEO (NOVEMBA 02, 2020): TUNAPOELEKEA MWISHO WA MWAKA 2020 JE UMESOMA VITABU VINGAPI?
Habari ya asubuhi rafiki yangu mpendwa na
mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku mpya kati ya siku 60 zilizobakia
kuumaliza mwaka 2020. Ni matumaini yangu kuwa umeamka salama na upo tayari
kuendelea na majukumu yako ya leo. Basi tuianze siku kwa kusema “hii ndiyo
siku bora aliyoifanya Bwana, nitafurahi, nitamshukuru na kuitumia vyema siku
hii kwa ajili ya kuongeza thamani ya maisha yangu hapa Duniani”.
Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo
tutajifunza kwa pamoja tutafakari juu ya umuhimu wa kusoma vitabu. Nilianza kazi
ya kuhamasisha jamii kuhusu usomaji vitabu kwa ajili ya kujiongezea maarifa
mbalimbali tangu mwaka 2016. Katika kipindi hiki cha miaka minne kwenye usomaji wa vitabu
nimegundua kuwa hatuwezi kujijua sisi ni akina nani na tumeumbwa kwa ajili ya
kufanya nini hapa duniani ikiwa hatuna utamaduni wa kusoma vitabu.
Kila mmoja wetu hapa duniani ameumbwa kwa ajili ya kukamilisha kusudi maalumu japo kusudi hilo halipo wazi kwenye maisha yetu ya kila siku. Kupitia usomaji wa vitabu tunaweza kujitambua sisi ni akina nani na tumeumbwa kwa ajili ya kukamilisha kusudi lipi hapa Duniani. Katika kuelezea neno la tafakari ya leo ningependa ninukuu maandiko matakatifu kutoka kwenye Biblia.
Kitabu cha Mithali 4: 13 ambayo yanasema “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike maana yeye ni uzima wako.” Tafsiri yetu walio wengi tunadhania kuwa elimu inayoongelewa hapa ni elimu ya darasani na baada ya kumaliza elimu ya darasani tunakuwa tumehitimisha safari ya kujifunza. Pia, Mithali 1:29 nanukuu “kwa kuwa walichukia maarifa, wala hawakuchagua kumcha Bwana”. Tafsiri yake ikiwa ni kwamba tunapokosa muda wa kujifunza maarifa mapya kupitia usomaji wa vitabu au semina mbalimbali moja kwa moja ni kwamba hatuwezi kumcha Bwana katika kweli na haki kwa kuwa hatuna maarifa ya kutosha kuhusu Mungu na maisha yetu kwa ujumla wake.
Katika kitabu cha Injili ya Yohana, Yohana 8: 32 “tena
mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Ukweli ni kwamba tumeshindwa kuwa huru kiroho,
kimahusiano ya ndoa na familia, kwenye malezi ya Watoto, kiuchumi na kijamii
kwa kuwa tumeshindwa kuijua kweli kupitia usomaji wa vitabu.
Katika kitabu cha Hosea 4:6 nanukuu: “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.” Kila siku tunaangamia kupitia ndimi zetu, tunaangamia kupitia tabia zetu, tunaangamia kupitia uzembe wetu, tunaangamia kupitia upofu wa kutokuona fursa, na tunaangamia kupitia kutokujitambua sisi nani. Majibu ya namna ya kuepukana na maangamizo hayo yanapatikana kupitia usomaji vitabu.
Mwisho, neno la tafakari ya leo ni sehemu ya neno ambalo nililitoa jana katika hafla ya uzinduzi wa vitabu vitabu vitatu ambapo nilialikwa kama Mgeni rasmi wa hafla hiyo. Kubwa ambalo ningependa ujifunze katika neno la tafakari ya leo ni kujiuliza kuwa tunapoelekea mwishoni mwa mwaka 2020 Je umesoma vitabu vingapi? Ikiwa Dunia inabadilika na vyote vilivyomo ndani mwake vinabadilika kila mara, kitu pekee ambacho hakibadiliki ni kazi ya kalamu. Kazi hii inao uwezo wa kudumu vizazi na vizazi kuliko kazi nyinginezo. Hivyo, wajibu ulionao ni kuhakikisha unanufaika na kazi kalamu kutoka kwa waandishi ambao wametoa maisha yao kwa ajili ya kuielimisha jamii. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya
leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na
uwepo wako kwenye kundi hili.
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629
078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com