NENO LA LEO (NOVEMBA 8, 2020): FAHAMU SHERIA MBILI AMBAZO ZIMESHIKIRIA MAFANIKIO YAKO.
Habari ya asubuhi rafiki yangu na
mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine ambapo tunazawadiwa masaa
24 ambayo hatuna budi kuyatumia kutenda yaliyo mema ili maisha yawe na thamani.
Ni katika asubuhi hii nakukumbusha kuwa maisha yako yanakuwa na thamani pale
ambapo yanatumika kwa faida ya nafsi yako na jamii inayokuzunguka. Basi kila
mmoja wetu aianze siku kwa “kusema hii ndiyo siku bora aliyoifanya Bwana,
nitafurahi, nitamshukuru na kuitumia vyema siku hii kwa ajili ya kuongeza
thamani ya maisha yangu hapa Duniani”.
Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo
tutajifunza kuhusiana sheria mbili ambazo zimeshikilia mafanikio yako kwenye kila
sekta ya maisha yako. Kila siku tunawajibika kutii sheria mbalimbali ziwe za
asili au sheria zilizowekwa na wanadamu. Sheria hizi ndizo zinaongoza maisha yetu
na zinatuwezesha kuishi katika makundi ya kijamii. Katika neno la tafakari ya
leo nitakufunulia sheria mbili ambazo pengine hukuwahi kuzisikia yamkini
zimekuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku. Karibu tujifunze:-
Sheria #1: Kanuni ya dhahabu (the Golden Rule). Sheria ya dhahabu ni moja ya sheria ambayo ina mchango kwenye safari ya mafanikio yako. Ni miongoni mwa sheria zinazopatikana katika dini na tamaduni nyingi. Sheria hii inasema “kila mmoja awatendee wenzake kama ambavyo angetamani wamtendee”. Misingi ya sheria hii ni kutoka katika mafundisho ya Yesu kwa wanafunzi wake kama ilivyonukuliwa hapa: “Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii” (Mathayo 7:12, Luka 6:31 na Walawi 19:18).
Tafsiri yake katika safari ya fedha ni kwamba ikiwa unahitaji kufanikiwa katika maisha, unatakiwa kutenda mema kwa watu wengine kwa kuwa hakuna namna utaweza kufanikiwa kimaisha bila ya uwepo wa watu. Wafanyakazi wenzako ni watu, mwajiri wako ni mtu, wateja wa bidhaa zako ni watu na jamii inayokuzunguka kwa ujumla ni watu. Pia, sheria hii inaweza kutafsiriwa zaidi kuwa: katika ulimwengu wa biashara unatakiwa kutoa thamani kwa unaofanya nao biashara na thamani unayopokea. Husimuuzie mtu bidhaa au huduma ambayo wewe mwenyewe husingeweza kununua kama ungekuwa upande wa mteja.
Sheria #2: Sheria ya Platini (Platinum Rule). Madini ya Platini yana thamani ikilinganishwa na madini ya dhahabu. Hivyo, sheria ya Platini inathamani zaidi ikilinganishwa na sheria ya dhahabu. Sheria ya Platini inasema: “watendee wengine kadri ambavyo wanapenda kutendewa na siyo kadri unavyohitaji kutendewa”. Hii ni sheria nyingine muhimu katika kujumuika na watu wanaokuzunguka, kadri unavyowatendea watu kulingana na mapenzi yao ni rahisi kuaminika kwao. Ili ujenge uaminifu kwa wateja ni lazima uhakikishe unatimiza mahitaji yao kwenye bidhaa/huduma zako. Na kadri unavyotimiza mahitaji ya Wafanyakazi wako ndivyo wataendelea kuwa waaminifu kwako. Vitu vidogo ambavyo unawatendea wateja kulingana na mapenzi yao vina nafasi kubwa ya kukupatia wateja waaminifu kwenye bidhaa/huduma zako.
Mwisho, neno la tafakari ya leo tumejifunza sheria ambazo ni sheria ya Dhahabu na sheria ya Platini. Tumeona jinsi ambavyo tunaweza kutumia sheria hii katika maisha yetu ya kila siku katika kuelekea kwenye mafanikio tunayotamani. Tumia sheria hizi kuboresha mahusiano yako na watu katika jamii unayoishi kwa kuwa hakuna mafanikio bila watu. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629
078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com