Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 4 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha
yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio yangu kuwa muda
ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada mkubwa kwako
katika kubadilisha maisha yako.
Hata hivyo, mtandao huu unahitaji
maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako (tuma
maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kijitabu
cha wiki hii ni “How To Write a Marketing Plam” kutoka kwa mwandishi John
Westwood. Katika kitabu hiki tunashirikishwa namna ya bora ya kuongeza mauzo ya
biashara kupitia kwenye mpango wa masoko.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi Robert Kiyosaki
anatushirikisha katika kitabu hiki:
1. Biashara ili iwe ya mafanikio
ni lazima iwe na mpango. Mpango huu katika sehemu zake ni lazima uwe na mpango
wa masoko. Mpango wa masoko unaelezea juu ya namna ambavyo kampuni itapenya
kwenye soko kwa kuonesha mbinu zitakazotumika pamoja na kiwango kinachokusudiwa
kuingizwa kwenye soko na asilimia soko inayolengwa. Mpango huu ni nyenzo ya
mawasiliano ndani ya kampuni kwani unaelezea mpango wa kampuni katika kuingia
kwenye soko pamoja na namna kuendelea kulinda soko husika.
2. Katika kuandaa mpango wa masoko
ni lazima kwanza utambue kuwa ili kampuni iweze kuzalisha faida ni lazima
ifanikishe mauzo ya bidhaa au huduma zake kwenye soko. Hivyo, ili kampuni
ifanikishe mauzo ni lazima iangalie uwezo ilionao katika kuzalisha biadhaa au
kutoa huduma. Hapa ndipo mpango wa mauzo unahitaji kuzingatia mahitaji ya
wateja kwani bila kuzingatia hilo kampuni haitaweza kuongeza mauzo yake. Kutokana
na hilo, mpango wa mauzo ni lazima uzingatie sehemu tatu ambazo ni (a) uwezo wa
kampuni kwenye kuzalisha bidhaa au kutoa huduma (b) mahitaji ya wateja kwenye
soko husika na (c) mazingira ya soko husika.
3. Mpango
wa mauzo katika kufikia mahitaji ya soko ni lazima ujikite kwenye sehemu kuu
nne juu ya bidhaa/huduma zake. Sehemu hizi ni (a) aina ya bidhaa/huduma
inayouzwa (b) sera ya mauzo kwa maana ya bei (c) namna ya kutangaza
bidhaa/huduma zake na (d) njia za kusambaza bidhaa/huduma husika.
4. Usambazaji
na utangazaji wa bidhaa/huduma vinahitajika hasa pale unapoingia kwenye soko
jipya wakati bidhaa/huduma pamoja na bei vinalenga kwenye namna ya kuendelea
kumridhisha mteja.
5. Mpango
wa masoko unaandaliwa kwa kutumia taarifa za soko ambalo kampuni inalenga kuuza
bidhaa/huduma zake. Hii ni maana kwamba kabla ya kuandaa mpango wa mauzo ni
lazima ufanye ukaguzi wa soko husika kwa ajili ya kutafiti taarifa muhimu za
soko na uzalishaji wa bidhaa za kampuni. Na mara nyingi inahusisha utafiti juu
ya bidhaa, bei yake, njia sahihi za kutangaza bidhaa na njia sahihi ya
kusambaza bidhaa husika.
6. Katika
utafiti wa soko ni muhimu kuzingatia taarifa muhimu kama vile namna ambavyo
soko linabadirika mara kwa mara, ukubwa wa soko, mchanganuo wa wapinzani wako
wa karibu, hali ya soko, bidhaa zipi zinapendwa sana sokoni hasa zile ambazo
zinaendana na bidhaa zako, taarifa muhimu za Serikali, kisiasa na kijamii.
7. Mpango
wa masoko ni lazima uweze kutofautisha mahitaji tofauti ya wateja katika soko
husika. Mwandishi anatushirikisha kuwa sio wateja wote katika soko watahitaji
aina moja au radha moja ya bidhaa zako. Ndio maana katika soko la vinjwaji
mfano, kampuni ya Pepsi au Cocacola utakutana na radha zote. Hii ni pamoja na
kuzingatia vifungashio vyenye ujazo tofauti kwa ajili ya kutofautisha bei ya
bidhaa husika. Hali hii inamfanya mteja apate machaguo anayohitaji.
8. Unapoandaa
mpango wa masoko ni lazima ufanye tathimini ya uwezo wako (strength), madhaifu
ya kampuni yako (weakness), fursa zilizopo (opportunity) na hali hatarishi
zilizopo (threat). Tathmini hii itakuwezesha kufahamu sehemu muhimu za
kuboresha, kuchangamkia au hatua za kuchukua dhidi ya changamoto.
9. Mpango
wa masoko ni lazima uwe na malengo ya mauzo na malengo haya ni lazima yawe na
mikakati/njia zitakazotumika kutimiza malengo. Malengo haya ni lazima yajikite
kwenye bidhaa/huduma inayotolewa kwenye soko husika wakati mikakati/njia
inapaswa kujikita kwenye bei ya bidhaa/huduma, njia za usambazaji pamoja na mbinu
za kujitangaza. Mikakati ya kufikia malengo ni lazima itengenezewe malengo
pamoja na mikakati ya kufikia kusudio lengwa.
10. Malengo ya mauzo ni lazima yawe yanajieleza,
yanapimika na yanatekelezeka. Malengo haya yanaweza kutengenezwa kwa asilimia
au namba ili iwe rahisi kufanya tathimini ya utekelezaji wake. Hii itasaidia
kutoa mwelekeo wa kampuni kwenye soko husika.
11. Katika mpango wako wa mauzo ni lazima
utambue kuwa bidhaa/huduma yako kwenye soko itapitia hatua kuu sita za mauzo.
Hatua hizi ni; (i) kutambulika sokoni (ii) ukuaji wa mauzo ya awali (iii)
ukuaji wa mauzo wa haraka/ghafla (iv) hatua ya ukomavu – mauzo ya bidhaa/huduma
yamefikia hatua ya juu (v) hatua ya uwepo wa bidhaa/huduma kwa kiwango kikubwa
na (vi) hatua ya kushuka kwa mauzo.
12. Katika kila hatua kampuni inabidi iwe
na mbinu za kuendelea kuongeza mauzo ili iendelee kuteka soko. Mfano, katika
hatua ya sita kampuni inaweza kubadilisha vifungashio au kuongeza ujazo kwa
ajili ya kuendelea kuridhisha wateja.
13. Kadiri unavyoteka soko ndivyo unakuwa
na nguvu kuuza bidhaa/huduma kwa bei unayopenda. Katika kuandaa mpango wa
masoko ni lazima ujikite kwenye kuteka soko kutokana na bidhaa/huduma zako. Hii
ni lazima ianzie kwenye ubora wa bidhaa/huduma unazotoa pamoja na uwezo wako wa
kuzalisha/kutoa huduma husika. Pia, inabidi kukumbuka kuwa ili uteke soko
husika ni lazima mzunguko wa fedha inayoingia kutokana na mauzo uwe juu.
14. Sera ya bei ya kampuni katika kuingia
kwenye soko jipya inaweza kuwa (a) kuuza bidhaa kwa bei ya juu – kadri
unavyouza kwa bei ya juu ndivyo faida inakuwa kubwa lakini idadi ya wateja
inakuwa ndogo au (b) kuuza kwa bei ya chini – kadri unavyoingia kwenye soko
jipya kwa bei chini ndivyo mauzo ya bidhaa/huduma yanavyoongezeka na ndivyo
unavyoongeza uhitaji wa bidhaa/huduma husika kwenye soko.
15. Usambazaji wa bidhaa/huduma kama sehemu
ya mpango wa soko ni lazima ieleze mtawanyiko wa masoko, njia za kusafirisha na
huduma kwa wateja. Muunganiko wa vitu hivi ndivyo unakamilisha mpango wa
usambazi kama sehemu ya mpango wa masoko.
16.Kama kampuni ni lazima kufahamu sehemu
masoko yalipo na ili kutambua njia ya kuwafikia wateja ambayo ni bora katika
kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa/huduma. Hata hivyo, mpango wa
usambazaji ni lazima uunganishwe na utoaji huduma kwa wateja kama sehemu ya
kujitangaza zaidi.
17. Katika sehemu ya mpango wa usambazaji
ni lazima uainishe mfumo wa mauzo ambao utatumika hadi kufikisha bidhaa/huduma
kwenye soko. Je utatumia mfumo wa mauzo wa moja kwa moja au utatumia mfumo
Wauzaji wa jumla na reja reja. Mfumo wa kampuni kuuza bidhaa/huduma zake moja
kwa moja kwenye soko ni mgumu na kiuchumi ni wa gharama kubwa. Hata hivyo
kuamua ni mfumo upi utumike itategemea na aina ya bidhaa/huduma inayotolewa na
kampuni husika.
18. Utekelezaji wa mpango wa masoko ni lazima ndani
yake pawepo mpango wa matangazo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mauzo ya
bidhaa ni matokeo ya uwepo wa taarifa sahihi kwa mteja ambazo zimeambatana na
uwepo wa bidhaa/huduma kwa muda sahihi. Kufanikisha zoezi hili ni lazima
kampuni ianishe mbinu za matangazo zitakazotumika kwa ajili ya kuwafikia
wateja. Je utatumia matangazo ya runinga, redio, magazeti au mitandao.
19. Kwa ajili ya ufanisi wa mpango wa
masoko ni lazima bajeti/gharama za usambazaji pamoja na matangazo zianishwe
kwenye mpango. Hii itasaidia kwenye utekelezaji wa mpango wa usambazaji na
matangazo kama ulivyoainishwa kwenye mpango wa masoko.
20. Mpango wa masoko ni lazima uhuishwe
mara kwa mara kwa ajili ya kuingiza mabadiliko yanayojitokeza. Kutokana na
ukweli huu ni lazima mpango husika uwe unafanyiwa tathimini kwa ajili ya
kujipima utekelezaji wake katika nyakati tofauti.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|