Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 44 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako uyatumie
kubadilisha kila sekta ya maisha yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio
yangu kuwa muda ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada
mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako.
Hata hivyo, mtandao huu unahitaji
maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako au namna
ambavyo unahitaji makala hizi ziboreshwe zaidi (tuma maoni/ushauri/ushuhuda
wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Kama bado haujajiunga na mtandao huu, BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa
kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “TED Talks” kutoka kwa mwandishi Chris Anderson. Chris ana
taaluma ya uhandishi wa habari kutoka Chuo Kikuu cha Oxford. Baada ya kuhitimu
masomo yake Chris alifanikiwa kuanzisha majarida zaidi ya 100 yenye mafundisho
na taarifa mbalimbali kwa jamii. TED ni Shirika lisilo la kiserikali ambalo
lilianzishwa mwaka 1984 kwa ajili ya kujihusisha na vyombo vya habari. TED
linajihusisha na uwekaji wa taarifa hasa mazungumzo kwenye mitandao na
mazungumzo hayo yanapatikana bila malipo yoyote. Chris amekuwa Rais wa TED toka
mwaka 2001 mpaka wakati anaandika kitabu hiki. Shirika hili linaongozwa na
kauli mbiu “Ideas Worth Spreading = Thamani ya Uenezaji wa Mawazo”.
Linapokuja
suala la kujieleza mbele za watu, watu wengi wanashindwa kufanya hivyo kutokana
na hofu ya umati unaowazunguka. Ni kutokana na hali hii watu wengi wanaweza
kujieleza kwa maandishi lakini wengi wao wanashindwa kuongea kile
walichoandika. Mwandishi Chris anatumia kitabu hiki kutushirikisha mbinu za kutoa
mada/ujumbe mbele za watu na ukaeleweka kile ulichokusudia kuwasilisha.
Karibu
tujifunze machache niliyojifunza kwenye kitabu hiki:
1. Mara zote unapoongea mbele za
watu jitahidi kuwa wewe. Hii ina maana kuwa usiogope umati unaokuzunguka kwa
kuhisi kuwa labda kuna watu wenye elimu/uelewa mkubwa zaidi yako. Ni kawaida
kuwa na hofu wakati unajiandaa kuwasilisha mada, mwandishi anatushirikisha kuwa
kabla ya kusimama mbele za watu unahitaji kutumia hofu yako kwa ajili ya
kujiandaa vyema. Hali hii itakufanya uwe na uelewa mpana kwenye mada yako na
matokeo yake utajiamini zaidi.
2. Kama mtoa mada una jukumu kubwa
la kuhakikisha unawasilisha ujumbe wenye thamani kubwa ndani ya nafsi yako
pamoja na wale wanaokusikiliza. Hapa unahitaji kujikita kwenye kutoa wazo la
thamani ambalo lipo ndani ya nafsi yako na linaweza kuwa na thamani hiyo hiyo
kwa wasikilizaji. Wazo hilo liwe na sifa ya kujenga picha katika akili za
wasikilizaji na linaweza kuishi ndani ya nafsi zao kutokana na thamani yake.
3. Kila mwenye wazo lenye mashiko
au thamani anao uwezo wa kushirikisha hilo kwa wengine. Haijalishi kiwango cha
kujiamini ulichonacho, uwezo wako wa kuongea kwa haraka au uwezo wa kumudu
hadhira yako. Silaha muhimu ambayo unatakiwa kuwa nayo ni wazo ambalo lenye
thamani au maana kwa wanaokusikiliza. Na wazo sio lazima liwe gumu bali ni
chochote ambacho kinaweza kubalidilisha mtazamo wa watu kwa ajili ya hatua moja
mbele kwenye mazingira yanayowazunguka.
4. Wapo
watu wengi ambao wanasema kuwa hawana wazo lolote la kuwashirikisha wengine
lakini mwandishi anatuambia kuwa kila mtu ana wazo la kipekee ambalo linaweza
kuwa somo kwa wengine. Wazo hili si jingine bali ni ule uzoefu wa maisha yako.
Maisha yako ni hadithi yenye mafundisho tosha kwa wengine.
5. Watu
wengi wanashindwa kufahamu thamani waliyonayo kwa vile muda wote wameishi
maisha ya kujihisi kutokuweza kwenye kila jambo au hali. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kama wewe ni mmoja wa watu hawa unachotakiwa kufanya ni
kuwauliza watu wako wa karibu ili wakushirikishe vitu vya kipekee wanavyoviona kutoka
kwako.
6. Teknolojia
ya lugha ni uvumbuzi wa kipekee katika hisitoria ya mwanadamu ambao umewezesha
mtu mmoja kushirikisha wengine mawazo aliyonayo. Hata hivyo, lugha hii
inawezesha ujumbe kufika kwa wengine kwa kutegemea umaridadi wa mhusika katika
kuchambua mtiririko wa maneno ili ulete sentensi zenye maana, msisimko au
thamani na mahitaji halisi ya msikilizaji.
7. Yafanye
maongezi au wasilisho lako kuwa na sifa ya safari kwa msikilizaji. Msikilizaji
ajione yupo kwenye safari yenye kila aina ya vitu vipya na uzoefu wa kila aina
ambao hajawai kuupata katika maisha yake. Maongezi yako yawe na sawa na filamu
au kitabu cha simulizi ambacho kila mara kinakuhamasisha kusoma ukurasa
unaofuata. Hali hii itamfanya msikilizaji ajenge picha katika akili yake na
hivyo kuwa na hamasa ya kuendelea kukusikiliza. Mfanye msikilizaji ahusishe
milango yake yote ya fahamu kadiri unavyoongea.
8. Unapowasilisha
mada epuka makosa haya manne katika maongezi yenye ubunifu; Moja, epuka maongezi yenye mlengo wa
kutangaza sifa zako kana kwamba unatangaza bidhaa kwa ajili ya kununuliwa.
Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanafanya makosa kiasi ambacho pale
wanapoongea wanaishia kueleza sifa walizonazo au mafanikio yao. Kumbe
wanachotakiwa kufanya ni kuwasilisha wazo au mada kwa ufasaha ili kupitia
wasilisho hilo wafanikiwe kujenga heshima au uaminifu au mtazamo chanya kutoka
kwa wasikilizaji wao. Mara zote lenga kumpatia msikilizaji kitu kipya badala
kufikiria utapata nini kutoka kwake.
9. Mbili, epuka
maongezi yasiyo na dira. Hii inajumuisha makosa ambayo mtoa mada anazama
kueleza vitu ambavyo vipo nje kusudio la mada anayowasilisha. Matokeo yake ni
mtoa mada kueleza vitu vingi ambavyo havina uhusiano na mada aliyokusudia
kuwasilisha. Hali hii inafanya wasikilizaji wakose hamasa ya kuendelea
kukusikiliza. Kumbuka kuwa watu wanakupa dakika chache katika maisha yao kwa
ajili ya kusikiliza vitu vya kipekee au vipya hivyo huna budi kuhakikisha
unalenga kwenye pointi ulizokusudia.
10. Tatu, epuka
kuzama kwenye kuelezea zaidi kampuni yako au taasisi unayofanyia kazi bali
jikite kwenye upekee uliopo kwenye wazo au mada ya kibunifu unayowasilisha.
Mwandishi anatushirikisha kuwa mara zote kampuni au taasisi unayomiliki au
kufanyia kazi inaweza ionekane bora katika macho yako lakini kwa wengine
ikaonekana haina ubora au upekee wa aina yoyote ile.
11. Nne,
epuka hamasa iliopitiliza. Kulenga kuhamasisha wasikilizaji ni mojawapo ya
viungo vya maongezi lakini pale inapopitiliza inaweza kuwa ni kikwazo kwa mtoa
mada kueleweka kwa hadhira yake. Ni kawaida kila mtoa mada kuhitaji mrejesho
mara baada ya kumaliza kuwasilisha au wakati anaendelea kuwasilisha kwani
mrejesho huo ni ishara ya kueleweka. Mrejesho huo unaweza kuwa wa makofi au
mpasho kama ambavyo tumezoea katika mazingira yetu. Mwandishi anatuhadharisha
kuwa hakuna sababu ya kulazimisha kupewa mrejesho huo wakati unawasilisha kwani
inaweza kupelekea upoteze umakini wa hadhira kwenye mada yako.
12. Hakikisha maneno au sentensi zako zina
muunganiko au uhusiano na zote kwa pamoja zinafikisha ujumbe wa mada yako.
Maneno yako ni lazima yote yajikite kwenye lengo mahususi la mada au ujumbe
wako. Ili uendane na muda ni lazima uhakikishe maneno yako yanakuwa na “maneno
viunganishi” ambayo yanabeba ujumbe wa mada yako. Mada yako unatakiwa
kuipangalia katika muundo maalumu ili iwe rahisi kwa wasikilizaji kuelewa.
13. Muundo wa maongezi yako ni lazima
uzingatie kwenye kujibu maswali matatu; (a) nini? – hapa mtoa mada ni lazima
jikite kwenye kuelezea maelezo ya awali/utangaulizi juu ya kile anachotaka
kuwasilisha (b) Kwa ajili ya nini? – mtoa mada aelezee juu ya umuhimu wa mada
yake na misingi inayomfanya aone mada hiyo ni muhimu; na (c) Sasa nini? – mtoa mada
aelezee juu ya hatua muhimu zinazotakiwa kuchukuliwa kwa ajili ya kukabiliana
na changamoto iliyopo au kunufaika na mada yake. Hii inafuatiwa na hitimisho na
mapendekezo kwa ufupi.
14. Wakati unawasilisha mada yako hakikisha
kuna muunganiko kati yako na hadhira (wasikilizaji) yako. Hiki ndicho kinatofautisha
ujumbe unaowasilishwa kwa maandishi na ule unaowasilishwa kwa maongezi. Hizi ni
baadhi ya njia ambazo mwandishi anatushirikisha kwa ajili ya kuwa na muunganiko
na hadhira yako; i) hakikisha macho yako yanawatazama wasikilizaji toka mwanzo
wa unawasilisha mada yako – hakikisha muda wote unakuwa na tabasamu la asili bila
kuonesha uso wenye hofu wakati wote unapowatazama, ii) Onesha mguso kwenye mada
unayowasilisha – hali hii inawafanya wasikilizaji wapate muunganiko wa kihisia
kwa kile unachowasilisha, na iii) wafanye wasikilizaji wako wacheke lakini si kwa
kiasi kilichopitiliza – kicheko kinaonesha kuwa pale wawili mnapocheka wote mpo
kwenye hisia zinazofanana kwa wakati huo.
15. Kuwa na uwezo wa kuwasilisha kwa mfumo
wa hadithi. Mwandishi anatushirikisha kuwa tafiti kati ya vizazi na vizazi
inaonyesha kuwa kwa asili mwanadamu anapenda hadithi. Pale unapoongea unaweza
kutumia mwanya wa tafiti hizi kuvuta hisia za watu kwa kutumia hadithi ambayo
inaendane na mada yako unayowasilisha. Muhimu; hakikisha hadithi yako ipo sawa
kwenye misingi ya maadili, imani na tamaduni za sehemu husika.
16. Kuwa na uwezo wa kuelezea mada yako kwa
ufasaha na umahili wa aina yake. Kadri unavyojieleza unatakiwa uamshe hisia za
msikilizaji juu ya kile unachowasilisha. Pia, unahitaji kuhakikisha kuwa kuna
muunganiko wa maelezo ya maneno katika mada yako. Hii ina maana kwamba maneno unavyoyaeleza
yalete muunganiko kutoka neno linaloanza na linalofuata. Vivyo hivyo sentensi
pia ziwe na muunganiko wa kimantiki.
17. Kuwa na uwezo wa kushawishi. Hii ni
hazina kubwa unayotakiwa kuitumia kwa ajili ya kubadilisha mtazamo wa
wasikilizaji wako walionao juu ya ulimwengu huu na hatimaye ufanikiwe kuwapeleka
kwenye mtazamo wa maono ya mada yako. Ili ufanikiwe katika sehemu hii ni lazima
maongezi yako yajikite kwenye mantiki ambazo zina msingi wa kweli na mada yako
iwasilishe kwa mfumo ambao unamfanya msikilizaji hasichoke kukusikiliza.
18. Kuwa na uwezo wa kuwapa wasikilizaji
wako ufunuo mpya katika maarifa/uzoefu wao. Hapa katika mawasilisho yako
unaweza kuweka picha za miradi yako mipya ambayo imetokana na ubunifu wako
ambao pengine ni mpya kwenye uelewa wa wasikilizaji wako.
19. Tumia nguvu ya matumizi ya lugha ya
mwili kwa ajili ya kufikisha ujumbe. Mwandishi anatushirikisha kuwa kupitia
matumizi ya lugha ya mwili unaweza kuwasilisha mada yako kwa maneno machache na
ukaeleweka zaidi. Hii pia njia kuunganisha na watazamaji wako ikiwa ni pamoja
na kuamsha hisia za watazamaji wako.
20. Kama unatumia vifaa vya teknolojia ya
mwanga kama vile “projector” hakikisha unaandaa walisho lako katika mfumo ambao
unaonekana vizuri. Hii ni pamoja na kuepuka kutumia maneno mengi kwenye ‘slides’
zako badala yake tumia picha au vibonzo kwa ajili ya kuvuta utayari wa
wasikilizaji kwenye kile unachowasilisha. Hata hivyo, mwonekano wa mtoa mada
unatakiwa kwenda sambamba na kile ambacho kinaonekana kwenye wasilisho lake.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com