Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 42 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako uyatumie
kubadilisha kila sekta ya maisha yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio
yangu kuwa muda ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada
mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako.
Hata hivyo, mtandao huu unahitaji
maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako au namna
ambavyo unahitaji makala hizi ziboreshwe zaidi (tuma maoni/ushauri/ushuhuda
wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Kama bado haujajiunga na mtandao huu, BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu. Kwa
kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Teach Your Child How To Think” kutoka kwa mwandishi Dr. Edward
De Bono. Edward De Bono ni mkufunzi na mwandishi mashuhuri ambaye ameandika
vitabu vingi vyenye nia ya kuelimisha watu kwenye sekta mbalimbali za maisha
yao. Mwandishi huyu ameandika vitabu vingi vya mbinu za kufikiri na baadhi ya
vitabu hivi ni ‘Lateral Thinking’, ‘Six Thinking Hats’ na ‘Teach Yourself To Think’. Sifa kubwa ya
mwandishi huyu ni kwamba ana uzoefu wa kufanya kazi katika vyuo mbalimbali na
sehemu tofauti kwenye nchi zaidi ya 45.
Dr.
de Bono anatushirikisha hamasa kubwa ya kuandika kitabu hiki ni kuona angalau
katika ulimwengu huu kuna vijana wachache ambao wanaweza kusema “mimi ni mfikiriaji mzuri na ninafurahi
tasnia hii ya kufikiri vyema”. Kufikiri vyema kunaweza kufanywa na kila mtu
pasipo kujali taaluma, IQ, umri au mazingira. Hivyo kila mmoja anaweza
kujifunza mbinu za kufikiri na hatimaye akazitumia mbinu hizi kufikia viwango bora
vya kufikiri kwenye maisha yake ya kila siku. Na kadri siku zinavyozidi kwenda
ndivyo mbinu hizi zinahitaji kutumika kwa ajili ya kuwa na ufanisi kwenye
sehemu ya kazi, biashara, uongozi au kijamii.
Kitabu
hiki hakitakufaha kama unaamini kuwa;
1. Watu
wenye akili sana ndo wafikiriaji wazuri na watu wenye akili za wastani hawana
uwezo wa kufikiri – uzoefu unaonesha kinyume chake;
2. Mbinu
za kurifikiri zinafundishwa mashuleni na tayari ulishafundishwa enzi hizo ukiwa
shuleni – ukweli ni kwamba walimu mashuleni hawafundishi hata chembe moja ya
mbinu za kufikiri;
3. Uwezo
wa kufikiri haufundishwi bali unakuja wenyewe kwa kutegemea hali unayopitia –
ukweli ni kwamba mbinu za kufikiri zinafundishwa sawa na mbinu za sayansi
yoyote ile zinavyofundishwa.
Katika
mfumo wa ufundishaji ambao unatumiwa na wengi ni ule ambao umejikita kwenye
taarifa. Mfumo huu ni rahisi kuufundisha na ni rahisi kuujaribisha. Hii ndio
sababu kubwa ya kuona kuwa elimu ya sasa imejikita kwenye mfumo huu, lakini
tunahitaji kufahamu kuwa kufikiri sio mbadala wa mfumo wa taarifa bali mfumo wa
taarifa unaweza kuwa sehemu ya mbinu za kufikiri. Endapo taarifa zote zingekuwa
ni sahihi na zinajitosheleza kwa maana hiyo kusingekuwa na umuhimu wa kufikiri
bali tungejikita kwenye ukweli wa taarifa zilizopo. Ukweli ni kwamba tunaishi
katika dunia ambayo taarifa hazijitoshelezi na ukweli wake ni wa mashaka hivyo
hatuwezi kukwepa kufikiri.
Mbinu
za kufikiri hazikwepeki kutokana na ukweli kwamba tunaishi katika mazingira
ambayo hatujui kesho itakuwaje (mipango ya baadae), tunahitaji ubunifu wa vitu
vipya, tunahitaji kuboresha taarifa zilizopo, tunahitaji kufanikisha
biashara/kazi zetu. Kutokana na uhalisia huu, hakuna namna tunaweza kukwepa
mbinu za kufikiri kwenye maisha yetu hapa duniani.
Karibu
tujifunze machache niliyojifunza kwenye kitabu hiki:
1. Imani ya kwamba kuwa na akili
nyingi ni sawa na kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri imepelekea utoshaji wa aina
mbili. Kwanza, jamii kuamini kuwa wanafunzi wenye akili nyingi hawaitaji
kujisumbua juu ya lolote kwa kuwa kitendo cha kuwa na akili nyingi tayari wana
uwezo mkubwa wa kufikiri. Pili, watu wasio na akili hawahitaji kujisumbua
badala yake wakazane kwa ajili ya kuwa na akili nyingi vinginevyo kamwe
hawawezi kuwa na uwezo mkubwa wakufikiri. Mwandishi anatushirikisha kuwa huu ni
upotoshaji mkubwa kwani kuwa na akili nyingi ni sawa na gari zuri endapo linaendeshwa
na dereva mbaya. Akili nyingi ni lazima ziongozwe na uwezo wa kufikiri kwa
ajili ya kuona, kuchambua na kung’amua
(judge) mambo kwa mapana yake.
2. Upotoshaji mwingine ni juu ya
akili dhidi ya hekima. Jamii imeaminisha kwamba hekima inakuja yenyewe kwa
kadri mtu anavyozidi kuongezeka umri. Kutokana na upotoshaji huu jamii inaweka mkazo
wa kuwafundisha watoto kuwa na akili kuliko wanavyowekeza kuwafundisha kuwa na
hekima. Ukweli ni kwamba hekima haiji yenyewe kama ambavyo tumepotoshwa bali
misingi ya hekima inahitaji kufundishwa kama ilivyo misingi ya ukuaji wa akili.
3. Kufikiri kwa mwitikio wa jambo/hali flani (reactive
thinking) dhidi ya kufikiri kinadharia/dadisi (pro active thinking). Mwandishi
anatushikirisha kuwa mfumo wa shule nyingi umejengwa kwa ajili ya kumfanya
mwanafunzi muda wote afikiri kwa ajili ya kuitikia kujibu maswali (quiz, test,
exams) badala ya kumfanya afikirie kubuni vitu vipya nje ya darasa/mazingira
yake. Bahati mbaya maisha yanahitaji utumie udadisi wa hali ya juu kwa ajili
kufanikiwa katika sekta zote za maisha. Kwa maana nyingine kufanikiwa katika
maisha kunahitaji muhusika afikirie kwa mapana nje ya boksi. Ni rahisi kula
chakula ambacho tayari kimepikwa lakini kuandaa chakula husika kunahitaji hatua
za ziada.
4. Upotoshaji
mwingine kwa jamii ni ile nadharia ya kwamba ukishajua inakuwa rahisi kufanya.
Mifumo ya elimu inamuandaa mtoto kwenye kujua ujuzi katika sekta mbalimbali
lakini mtoto huyu haandaliwi kivitendo zaidi. Motokeo yake mtoto anakuwa na
ujuzi ambao hajui utatumika vipi katika maisha yake. Kutoka kwenye kujua hadi
kufanya kuna michakato mingi katika maisha ya kila siku ambayo yote kwa pamoja
inahitaji mhusika awe na mbinu za kufikiri na kung’amua mambo. Mtoto anahitaji
kufundishwa umuhimu wa kuthamini mawazo ya wengine, vipaumbele, malengo,
kufanya maamuzi, utatuzi wa migogoro, ubunifu pamoja na mambo mengine. Haya
yote hayafundishwi katika mfumo wa elimu ya sasa ambayo imejikita kwenye
kufikiri kimwitikio zaidi (reactive thinking).
5. Kufikiri
kwa mapana (critical thinking) ni sehemu tu ya kufikiri ambayo kama hakuna
mbinu za kufikiri kwa ajili ya uumbaji au ubunifu wa vitu, dhana ya kufikiri
kwa mapana inakuwa haina tija dani yake. Shule/vyuo vinahamasisha kufikiri kwa
mapana ambako ukitazama kwa undani wake wakufunzi wanalenga kuwafundisha
wanafunzi wao kuepuka makosa. Hii ni hatari sana kwani mtu ambaye amefundishwa
kwa ajili ya kuepuka makosa muda mwingi anajikita kwenye yale anayofahamu. Hali
hii inapelekea uwepo wa nafasi pana ya kuwa na kundi kubwa la vijana ambao
hawapo tayari kujaribu kufanya mambo mapya.
6. Watu
wengi ndani ya nafsi zao hawataki kushindwa juu ya mada iliyopo mbele yao na
hivyo wapo tayari kutetea kile wanachoamini kwa namna yoyote ile. Hali hii pia
ni matokeo ya mfumo wa elimu yetu. Mfumo huu unalenga kutoa wanafunzi
wanaofanya vyema na kuwaona wasiofanya vyema kana kwamba hawawezi lolote katika
maisha. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili uwe bora kwenye kufikiri ni lazima
uruhusu kupata taarifa mpya kutoka kwa wengine. Hii itakuongezea ujuzi kutoka
wanaokuzunguka.
7. Uchambuzi/tathimini
na usanifu ni vitu ambavyo ni muhimu kuunganishwa kwa ajili ya kukabiliana na
hali/changamoto tulizonazo. Hata hivyo mitaala ya elimu zetu inazingatia sana
kwenye upande wa kufikiri kwa uchambuzi/tathimini (analytical thinking) kuliko
upande wa kufikiri kwa usanifu. Usanifu imeachwa kwa watu wanaosomea uhandisi
na mitindo. Hali hii inapelekea kushindwa kutatua changamoto zilizopo na
matokeo yake ni changamoto hizo kujirudia mara kwa mara.
8. Misingi
mikuu ya kufikiri vyema ni mtazamo na hisia. Mara nyingi mkazo umewekwa kwenye
kufikiri kwa mantiki na kusahau umuhimu wa hisia na mtazamo. Ukweli ni kwamba
mantiki ni muhimu katika kufikiri lakini bila ya kuhusisha mtazamo na hisia
hatuwezi kuja na fikra bora.
9. Je
ni nyakati na sehemu zipi tunatakiwa kutumia mbinu za kufikiri? Mwandishi
anatushirikisha kuwa kufikiri kunatakiwa kufanyika kila wakati na kila sehemu
ya maisha yetu. Tunahitaji kujifunza kufikiri vyema kwa ajili ya kuboresha au
kutatua changamoto za kimahusiano, kiuchumi, kiroho, kijamii pamoja na
kifamilia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ni kupitia kufikiri tunaweza
kufanya vitu vyenye ubora na utofauti. Hata hivyo kwa vile vitu ambavyo tayari
vimekuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku hatuna haja ya kupoteza nguvu
nyingi kwa ajili ya kufikiria juu yake.
10.
Tunaweza kufaninisha mtiririko wa
kufikiri na mtiririko wa matukio ya fundi selemara katika kutenegeneza thamani.
Fundi selemara ana kazi kubwa tatu ambazo ni kukata mbao kwa vipimo
vinavyotakiwa, kuunga vipande vya mbao na mwisho ni kutoa umbo la kifaa kinachotakiwa. Katika mtiririko wa kufikiri, hatua ya kwanza
ya fundi selemara ni sawa na kuchimba kwa kina, kuchambua, kujikita kwenye
lengo/taarifa na kukusanya tahadhari zote juu ya taarifa inayokuhitaji
kufikiria kwa kina, ubunifu na mantiki.
Hatua ya kuunga
vipande vya mbao ni sawa na kutafuta muunganiko wa mawazo, uhusiano, kuchambua
nadharia na kuanza kusanifu kile ambacho unahisi ni suluhisho la changamoto
iliyopo mbele yako.
Hatua ya kutoa umbo
la mwisho kwenye kufikiri ni sawa na kuhukumu, kuoanisha, kulinganisha,
kuthaminisha na kuamua juu ya hatua za kuchukua.
11. Kama fundi selemara anavyoongozwa na
kanuni, taratibu/tabia, mbinu na muundo au mpangilio wa sehemu ya kufanyia kazi
ndivyo pia ilivyo kwenye mbinu za kufikiri. Hii ina maana kwamba kufikiri vyema
kunaongozwa na kanuni ambazo ni lazima kila mmoja awe tayari kuzifuata; tabia –
zipo tabia ambazo kila mmoja mwenye kuhitaji kuwa bora katika kufikiri
anatakiwa ajijengee. Hii ni pamoja na kuwa na mtazamo chanya kwenye suala zima
la kufikiri; na muundo – huu unajumuhisha mazingira yanayomzunguka kila mmoja
kwa ajili ya kuwa bora katika kufikiri.
12. Unaweza kujenga mtazamo bora wa
kufikiri kwa kuhakikisha mara zote unakuwa uhuru kupokea mawazo kutoka kwa
wengine. Mwandishi anatushirikisha kuwa kizuizi kikubwa kwa watu kufikia
viwango bora vya kufikiri ni tabia ya kuona kuwa mawazo yao ni sahihi kuliko
mawazo ya wengine. Muhimu ni kuhakikisha kuwa mawazo yako hauyafanyi kuwa
sheria wala msaafu na hivyo yanaweza kuboreshwa kupitia kuwasilikiliza wengine.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba kazi ya kufikiri sio kulinda mawazo yako ili
mara zote uonekane upo sahihi bali lengo kuu la kufikiri ni kupata mawazo
mapya.
13. Kusikiliza na kujifunza ni viungo
muhimu kwa ajili ya kufikia viwango bora vya kufikiria. Na hapa ndipo unahitaji
kuwa mpole kwani kiburi ni alama ya watu wasio na uwezo mzuri wa kufikiri. Hii inaweza
kuwa kazi ngumu kwako kutokana na ukweli kwamba tunazungukwa na watu wenye
uelewa tofauti na yale tunayofahamu lakini hatuna budi kuifundisha akili yetu
muda ione mema kutoka kwa watu hao au mazingira yanayotuzunguka.
14. Punguza kufanya vitu vingi kwa wakati
mmoja; mara nyingi katika kufikiri tunachanganya vitu vingi kwa wakati mmoja na
matokeo yake ni ufanisi finyu. Mwandishi anatushirikisha mbinu za kuwa na ufanisi
katika kufikiri kwa kutumia hatua sita ambazo amezipa jina la kofia sita za
kufikiri. Unahitaji kuvaa kofia moja baada ya nyingine ili ukamilishe mzunguko
wa wazo ambalo unafikiria kwa wakati husika na hatimaye mchanganyiko wa kofia
zote ulete ukamilifu ya fikra zako kwa wakati mmoja.
Kofia
nyeupe, hii ni kofia ya kwanza kuvaliwa na unahitaji kutumia
kofia hii kwa ajili ya kukusanya ukweli, takwimu na taarifa juu ya kile
unachofikiria. Jiulize je ni taarifa zipi zilizopo ikinganishwa na kile
ninachohitaji. Je ni taarifa zipi hazipo?
Kofia
nyekundu, unapovaa kofia hii unahitaji kujiuliza juu ya hisia,
mguso na imani/uelewa wako juu ya mada unayofikiri. Jiulize je kwa sasa nina
hisia zipi juu ya mada hii ninayowaza.
Kofia
nyeusi, kofia hii inakukumbusha kuchukua tahadhari kwa ajili ya
kuhakikisha taarifa ulizonazo ni sahihi. Jiulize je hii inaendena na ukweli? Je
itafanya kazi? Je ni salama? Je inatekelezeka?
Kofia
ya njano, kofia hii inakukumbusha ujiulize juu ya umuhimu na faida
za kile unachofikiria. Jiulize je kuna umuhimu wa kufanya hivyo? Je kuna faida?
Kwani nini kiwe na umuhimu au faida?
Kofia
ya kijani, katika kofia hii sasa unahitaji kufanya uchambuzi,
mapendekezo, kutafuta mawazo mapya na hatimaye kuja na mbadala. Jiulize je kuna
mawazo au njia mbadala?
Kofia
ya bluu, kofia hii inakufanya ufikiri juu ya kile unachofikiri
kwa maana ya kwamba ni hatua muhimu kwa ajili ya kuhakikisha unaendelea kubaki
njia kuu ya fikira zako bila kuchepuka. Na hapa ndipo unakufikiria juu ya hatua
inayofuata.
15. Tumia mfumo wa dakika tano kwa ajili ya
kupitia kwenye mzunguko mzima wa kufikiria. Katika dakika hizi fanya haya;
Dakika
ya kwanza; hakikisha umekamilisha lengo la kile unachofikiria,
kuwa wazi juu ya mapana ya kile unachofikilia, kuwa wazi juu ya matokeo
tarajiwa na kuwa wazi juu ya hali/mazingira yaliyipo kwenye mada husika. Kama taarifa
husika hazipo unaweza unaweza ukadhania (assume) na kuendelea na dakika
inayofuatia.
Dakika
ya pili na tatu; fanya uchambuzi wa mada husika kwa
kutegemea uzoefu wako na taarifa zilizopo juu ya mada husika na hatimaye uwe na
mwanga juu ya mada hiyo. Tumia mwanga huo kwa ajili ya kutengeneza mapendekezo
kadhaa ambayo yanaweza kuwa hatua za kuchukua au suluhisho la changamoto
husika.
Dakika
ya nne; hii ni hatua ya kuchagua ni pendekezo lipi lifanyiwe
kazi kati ya mapendekezo mengi uliyonayo. Je ni pendekezo lipi ambalo linatekelezeka
kwa urahisi, ambalo linaendana na utashi/vipaumbele vyangu au mazingira
yaliyopo.
Dakika
ya tano; kama tayari umefikia hitimisho la kuchagua pendekezo
husika sasa unahitaji kulinganisha pendekezo hilo na njia mbadala zilizopo. Hii
ni pamoja na kuainisha changamoto ambazo unaweza kukutana nazo katika
kutekeleza pendekezo lako.
16. Kuna njia mbili za kufikiria juu ya
mada; njia ya kwanza ni njia ya kufikiria moja kwa moja (forward thinking) na
njia ya pili ni kufikiria sambamba (pararell thinking). Ufikiria kwa njia ya
moja kwa moja pale ambapo fikra zako zinalenga kwenye jambo moja. Kwa maana
nyingine ni kwamba mawazo yanajikta kutoka kutoka kwenye tukio moja hadi
jingine na tukio moja linapelekea kuanza kwa tukio linalofuatia. Kwa upande wa
fikra sambamba, unakuwa na njia/matukio kadhaa ya kuchagua na matukio hayo
hayana uhusiano kati ya tukio moja na jingine. Kwa maana nyingine kukamilika
kwa tukio moja hakupelekei kuanza kwa tukio jingine. Kwa upande wa mfumo
sambamba wa kufikiri unahitaji kujiuliza maswali kama vile ni lipi/kipi
kinafuata?, mbadala upi uliopo, mawazo yapo yaliyopo n.k. Katika mfumo wa moja
kwa moja, maswali ya kujiuliza ni kama vile baada ya hili ni lipi linafuatia? Mifumo
hii yote ni muhimu, mfano, mfumo sambamba unasaidia kukusanya taarifa au njia mbadala
juu ya mada husika. Na mfumo wa moja kwa moja unatumika kwa ajili ya kufikia
hitimisho juu ya njia mbadala ulizonazo.
17. Mara nyingi tunazungukwa na mawazo
ambayo yanakuwa katika upana wake ni kupitia kufikiri mawazo haya yanatakiwa
kuchujwa mpaka kufikia kiwango cha maelezo ya kina. Kupitia zoezi hili kila
wazo linalokuja katika akili yako linatakiwa kuchambuliwa kwa kina hatimaye
kuja na ubunifu katika kuboresha mazingira yanayotuzunguka. Hivyo, katika kila
wazo pana linalokujia unahitaji kujiuliza ni kipi unaweza kufanya kwa ajili ya
kutumia wazo husika kuboresha mazingira yako.
18. Mbinu nyingine ya kuboresha ujuzi wa
kufikiri ni kutumia mbinu ya kufikiri kwa mapana/uwazi (lateral thinking). Ujuzi
huu wa kufikiri kwa mapana unaweza kutumiwa na kila mtu ambaye ameweka jitihada
za kukua katika tasnia ya kufikiri. Mbinu hii inahusisha umuhimu wa mtazamo na
mantiki katika kufikiri kwenye mada husika. Mbinu hii kwa ujumla wake inatumia
kwa ajili ya kutoa mtizamo na mawazo mapya. Hivyo, mbinu hii ni kwa ajili ya
kuepuka mitazamo na mawazo ya zamani ili kuzalisha mtazamo na mawazo mapya kwa
ubunifu zaidi.
19. Kama ambavyo tumeo kuwa kufikiri kunaongozwa
na kanuni kama ilivyo vitu vingine. Kanuni hizo ni pamoja na; 1) mara zote kuwa
mtu mwenye mawazo ya kujenga badala kuwa na mawazo ya kubomoa; 2) fikiri
polepole na mara zote jaribu kufanya vitu kwa urahisi; 3) ondoa nafsi yako aina
ya ‘ego’ kwenye mfumo wako wa kufikiri. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mara
zote ‘ego’ huwa inavutia upande wake na kusahau matakwa ya wengine; 4) kuwa na
muda wa kujihoji juu ya kile unachofikiri kwa wakati huo na mara zote jiulize
je hiki ndicho natakiwa kuwaza kwa sasa; 5) kuwa tayari kubadilisha gia angani –
fahamu ni wakati gani wa kufikiri kwa mantiki na wakati gani unatakiwa kufikiri
kwa ubunifu; 6) Jiulize nini matokeo ya ninachowaza kwa sasa – na matarajio
yangu ni yapi kwa sasa na kwanini nahisi pendekezo langu litafanya kazi; 7)
mguso na hisia ni sehemu muhimu ya kufikiri japo zinatakiwa mara baada ya
kufanya uchunguzi wa mada husika na si vinginevyo; na 8) mara zote tafuta
mbadala, mtazamo na mawazo mapya.
20. Changamoto zinapatikana katika
mazingira yanayotuzunguka na mara zote tunahitaji kulenga kutatua changamoto
hizo kupitia fikra zetu. Njia nzuri ya kutatua changamoto mara zote kufikiri
njia mbadala badala ya kung’ang’ania njia ya awali ambayo imekuingiza kwenye
matatizo.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com