Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 33 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Ni matarajio yangu kuwa makala hizi
zimekuwa na msaada mkubwa kwako kwa kadri ambavyo umekuwa ukichukua hatua za
kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, makala hizi haziwezi kubadilisha chochote
kama umekuwa mtu wa kusoma na kutokufanyia kazi yale unayojifunza.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao wa
fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa
humu moja kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “The Warren Buffet
Way”
kutoka
kwa mwandishi Robert G. Hagstrom. Kitabu hiki nit oleo la pili na kimeandikwa
kuelezea maisha ya bilionea Warren Buffett. Mwandishi anatumia kitabu hiki
kutushirikisha mbinu ambazo mwekezaji bilionea Warren Buffet amekuwa akizitumia
kukuza utajiri wake. Kwa kifupi kama ni mara yako ya kwanza kusikia jina la
Warren Buffet unachotakiwa kufahamu ni kwamba bilionea huyu ni mwekezaji ambaye
amewahi kuwa tajiri namba moja wa dunia kwa kipindi kirefu na amekuwa kati ya
matajiri watano wanaoongoza kwa muda sasa.
Warren
Buffet amekuwa tajiri kupitia uwekezaji katika kampuni yake ya Berkshire Hathaway
ambayo inajihusisha na uwekezaji kwenye biashara tofauti. Mwandishi anatumia
uzoefu aliopata kupitia ripoti mbalimbali juu ya kampuni ya Berkshire Hathaway
na maongezi na watu wa karibu na Warren Buffet kutushirikisha mbinu ambazo
zimekuwa zikutumiwa na Warren Buffett kupata mafanikio kiuwekezaji. Kwa ufupi
ni kwamba Warren Buffet amekuwa ni mtu ambaye anachukua hatua mapema kama
tahadhari dhidi ya nyakati zinazokuja na hivyo nyakati hizo (mbaya au nzuri)
zinapowadia zinamkuta ameshajiandaa kiuwekezaji.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye hiki:
1. Tofauti
na mabilionea wengine Warrant Buffet ni bilionea ambaye amepata utajiri wake
kupitia kwenye uwekezaji wa hisa na uwekezaji kwenye makampuni ya bima. Mabilionea
wengine katika orodha ya matajiri wakubwa duniani wametengeneza utajiri wao
kupitia teknolojia ya computa pamoja na teknolojia ya mtandao. Mfano, wa matajiri
hawa ni kama Bill Gates na Mark Zuckerberg.
Kupitia kitabu hiki tutajifunza mambo mengi muhimu kuhusu uwekezaji wa hisa. Warren
Buffet tunaambiwa kuwa baba yake alikuwa ni dalali wa hisa (stock broker) na
huu ulikuwa msingi kwa Warren kuhamasika kwenye uwekezaji wa hisa. Hamasa yake
iliongezeka zaidi baada ya kusoma kitabu cha The Intelligent Investor cha Benjamin Graham kiasi ambacho
alishawishika kuomba kozi katika Chuo ambacho Profesa Graham alikuwa anafundisha
ili aweze kujifunza mengi kutoka kwake. Hii inatufundisha kuwa kama unahitaji
kufanikiwa katika sekta uliochagua husichoke kujifunza maarifa mapya kwa njia
yoyote ile.
2. Katika
kununua hisa za kampuni, Warren Buffett amekuwa akinunua kwa bei ya chini hisa
za kampuni ambazo ni rahisi kukadiria ukuaji wa uchumi wake kwa siku zinajazo. Kwa
kufanya hivi imekuwa rahisi kwake kununua hisa za kampuni kwa bei ya chini na
baada ya muda hisa hizo zinaongezeka thamani na hatimaye anapata faida kutokana
na hisa anazomiliki kwenye kampuni husika. Sifa nyingine aliyonayo Buffet
katika uwekezaji ni kwamba kamwe hawekezi kwenye biashara ambayo hana uzoefu
nayo au haifahamu kwa undani.
3. Uwekezaji
wenye tija ni ule ambao kupitia tathimini ya kina unaridhisha uhakika wa
mwendelezo wa mtaji/kianzio na uhakika wa faida inayoridhisha. Huu ni maana ya uwekezaji kutoka kwa Benjamin
Graham ambayo Warren Buffett amekuwa akiitumia kuchagua biashara za kuwekeza. Maana
hii ina sehemu kuu mbili ambazo katika sehemu ya kwanza unatakiwa kufanya
tathimini ya kina dhidi ya kampuni ambayo unahitaji kuwekeza fedha zako – kwa maana
unatahiji kuwa na taarifa sahihi za kampuni husika. Sehemu ya pili inakutahadharisha
kuwa kabla ya kufanya uwekezaji wowote unatakiwa kujiridhisha kuwa sehemu
unayotaka kuwekeza itakuwa salama dhidi ya kianzio/mtaji wako na uhakika wa
faida kwa ajili ya kuongeza thamani kile ulichowekeza.
4. Njia
nzuri ya kuitathimini kampuni kwa kina ni kuangalia taarifa za kampuni za
kifedha kwa kipindi kisichopungua miaka mitano. Kama mapato ya kampuni yamekuwa
mara tano au zaidi ya matumizi yote ya mwaka katika kipindi chote cha miaka
mitano basi mwekezaji ana uhakika juu ya usalama wa fedha zake.
5. Kwa
mujibu wa mafundisho ya Benjamin Graham kuhusu uwekezaji kuna sheria mbili;
sheria ya kwanza “kamwe husipoteze”
na sheria ya pili kamwe “husisahau sheria
ya kwanza”. Kwa kifupi ni kwamba wekeza sehemu ambayo una uhakika na
usalama wa fedha zako.
6. Thamani
ya uwekezaji inapatikana kutokana mtiririko wa pesa (net cash flows) unaotegemewa
kuzalishwa katika kipindi chote cha uwekezaji na mtiririko huo wa fedha
ukipunguzwa kwa asilimia ya kiwango cha riba. Hapa kuna vitu viwili vya
kujifunza; moja: umuhimu wa
mtiririko wa fedha ili ya kutambua thamani ya sasa na ya baadae ya kampuni
husika. Kwa upande wa uwekezaji wa hisa njia ya haraka ya kutambua mtiririko wa
fedha wa kampuni husika ni kuangalia kiasi cha gawio kwa wanahisa katika
kipindi kilichopita. Kwa ufupi ni kwamba hisa ni ya thamani kulingana na kiasi cha
gawio ambacho utakipata kwa kila mwaka. Mbili:
umuhimu wa kupunguza kiasi cha mtiririko wa fedha ili kutoa nafasi ya
hatari (risk) ambazo zinawekuikumba kampuni husika.
7. Muda
mzuri wa kununua hisa ni pale wengi wanapouza hisa zao na kuuza pale wengine
wanaponunua. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika soko la hisa nyakati
ambazo kila mtu anauza ni nyakati ambazo hisa zinauzwa kwa bei ya chini kuliko
thamani halisi ya kampuni. Mara nyingi hii huwa inasababishwa na mabadiliko ya
ghafla kwenye uchumi. Nyakati kama hizo kwenye soko la hisa wawekezaji
wanazitumia kununua hisa za kampuni kwa bei ya chini na baadae kuziuza kwa bei
ya juu.
8. Siri
ya mafanikio kibiashara ni rahisi na hii si nyingine bali ni lazima fedha
zinazoingia ziwe nyingi kuliko zinazotoka. Mwandishi anatushirikisha kuwa hii ni
kanuni ambayo ilimwezesha Warren Buffett kufanikiwa kupitia kampuni zake za
bima chini ya umiliki wa kampuni ya Berkshire Hathaway.
9. Biashara
ya bima ni kati ya biashara chache ambazo watu wapo tayari kufanya. Warren
Buffett ametumia nafasi kumiliki makampuni ya bima kiasi ambacho amefanikiwa
kukuza thamani ya kampuni yake Berkshire Hathaway kwenye. Hii inatufundisha
kuwa kama unataka kufanikiwa ni lazima uwe tayari kufanya vitu ambavyo sio kila
mtu anafanya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri unavyofanya vitu vya
kipekee ndivyo unapunguza wapinzani wa bidhaa unayozalisha kwenye soko.
10. Kwake Warren Buffett kununua kampuni au
kununua hisa za kampuni yoyote vyote ni vinachukuliwa kwa nidhamu sawa kwani
kila uamzi unamfanya kuwa mmiliki kamili au sehemu ya wamiliki wa kampuni
husika. Kutokana na msimamo huu, tahadhari anazochukua wakati wa kununua
kampuni ni zile zile wakati wa kununua hisa kwenye kampuni nyingine. Hata hivyo,
kipaumbele chake ni kukunua kampuni pale fursa inapojitokeza ili impe nafasi ya
kudhibiti mtaji wa kampuni husika. Pia, pale ambapo hisa zinajitokeza zikiwa na
thamani nzuri kiuwekezaji Warren Buffett amekuwa akiwekeza kwenye kampuni
zinazomilikiwa na umma kupitia mfumo wa ununuaji wa hisa.
11. Pamoja na kwamba Warren Buffett amekuwa
akiwekeza kwenye kampuni nyingi kupitia kampuni yake ya Berkshire Hathaway mara
zote vigezo vyake ni vile vile: kuwekeza kwenye biashara rahisi na inayoeleweka,
yenye uhakika wa kutengenaza faida, yenye uwezekano wa kufanya vyema kwenye
soko la hisa, isiyo na madeni makubwa na ambayo tayari uongozi imara unaoendesha
biashara husika. Hizi ini sifa ambazo Warren Buffet anatumia kufanya tathimini kwa
kila kampuni ambayo ipo sokoni. Muda wote Warren Buffett anaamini kuwa haina
maana yoyote kuwekeza kwenye kampuni au kiwanda ambacho haujui uendeshaji wake.
Kwani kwa kufanya hivyo hautaweza kufahamu thamani ya kampuni/kiwanda husika na
hivyo kushindwa kufahamu maenedeleo ya kampuni/kiwanda.
12. Warren Buffett anaamini kuwa biashara
bora ya kumiliki ni ile ambayo kwa muda inaweza kuwekeza mtaji mkubwa na
kusambaa maeneo mengi huku ikizalisha faida kubwa ikilinganishwa na mtaji uliowekezwa.
Ni kutokana na sifa hii, Warren Buffet alishawishika kuwekeza kwa kununua hisa
za kampuni ya vinjwaji vya Coca – cola ambayo mpaka sasa imesambaa katika nchi
zaidi 195.
13. Unapoenda kuwekeza kwenye hisa nenda na
wazo la kumiliki biashara husika. Dhana hii itakufanya kabla ya kuwekeza ufanye
upembuzi yakinifu dhidi ya uendelevu wa kibiashara kwa kampuni ambayo unahitaji
kununua hisa zake. Warren Buffett amekuwa akitumia msingi huu na hivyo kila
kampuni anayonunua hisa zake ni lazima ajione kama yeye ndo mmiliki mkuu wa
kampuni husika na hivyo imani yake ni kwamba kuna muunganiko mkubwa kati ya
mmiliki wa hisa za kampuni na mwenye kampuni.
14. Mtazamo wa Warren Buffett kwenye
mafanikio ya wawekezaji ni “kadri mwekezaji anavyokuwa na taarifa/ufahamu
sahihi kwenye biashara aliyowekeza ndivyo alivyo na nafasi kubwa ya kupata
mafanikio makubwa kwenye uwekezaji husika. Hapa tunafundishwa kuwa kamwe
usikimbilie kuwekeza sehemu ambayo hauna taarifa sahihi au kwenye biashara
ambayo hauna ufahamu wa kutosha jinsi ya invyoendeshwa. Pia, unatakiwa kabla ya
kuwekeza kwenye kampuni ujiridhishe kuwa kampuni husika itaendelea kufanya
vyema kibiashara kwa muda mrefu.
15. Daima husikimbilie kununua hisa au
kampuni ambayo inaonekana kufanya vyema kwa muda mfupi badala yake angalia
uimara wa kampuni kwa siku za baadae. Mwandishi anatushirikisha kuwa Warren
Buffett huwa hanunui hisa/kampuni kwa vile zinafanya vyema kwenye soko kwa
wakati huo bali anaangalia mwenendo wa kampuni kibiashara kupitia taarifa za
kifedha na matarajio ya kukua kwa kampuni kwa siku za baadae. Huu ni msingi ambao unamfanya awe na sifa za
kipekee kwenye uwekezaji kwani watu wengi huwa wanaongozwa na hisia (hasa tamaa
kufanikiwa haraka) kwenye uwekezaji wa hisa. Watu wengi wananunua hisa/kampuni
ambazo zinafanya vyema kwenye soko kwa wakati huo wakidhani kwa kufanya hivyo
watapata mafanikio ya haraka. na tamaa ya kufanikiwa haraka
16. Kabla ya kuwekeza kwenye kampuni kwa
mfumo wa hisa au kununua kampuni husika unahitaji kutathimini umakini wa
watendaji wanaoiendesha kampuni kwa wakati huo. Buffett amekuwa na nidhamu ya
kuhakikisha kila kampuni ambayo anawekeza fedha zake ni lazima iwe na uongozi
imara ambao unatekeleza majukumu yake ipasavyo. Buffet anapenda watendaji ambao
wapo tayari kujiona kama wamiliki wa kampuni badala ya kujiona kama waajiriwa
tu. Kabla ya kuwekeza kwenye kampuni yoyote Buffet huwa anajiuliza maswali
matatu juu uongozi unaoendesha kampuni husika;
i. Je uongozi
uliopo una uadilifu pamoja weledi/uwezo wa kuchanganua mambo haraka? Hasa matawanjo
sahihi wa mtaji kwa ajili uendelevu wa biashara.
ii. Je uongozi
una uaminifu dhidi ya kampuni pamoja na wateja wa kampuni? na
iii. Je uongozi
upo tayari kwenda na kasi ya mabadiliko ya soko?
Haya
ni maswali ambayo mwandishi anatushirikisha kwa ajili ya kuyatumia katika
maamuzi tunayofanya kabla ya kuamua kuwekeza kwenye kampuni yoyote.
17. Njia mojawapo ya kufahamu thamani ya
kampuni ni kwa kuangalia mrejesho wa mapato kwa kila hisa uliyowekeza kwenye
kampuni husika. Hapa Warren Buffett anachoangalia ni kiasi ambacho kila
mwekezaji anapata kutoka kwenye kila hisa aliyowekeza kwenye kampuni husika. Ili
kamouni iweze kuwa ni mrejesho wa mapato kwa kila hisa ni lazima kampuni husika
isiwe na madeni mengi. Tunachotakiwa kujifunza hapa ni kwamba sio tu kununua
hisa za kampuni bali tunatakiwa kabla ya kununua tujiridhishe kiasi
kinachotolewa na kampuni husika kama gawio kwa kila hisa inayowekezwa.
18. Uwekezaji mzuri ni ule ambao kila
shilingi inayozalishwa na kampuni inaweza kutasiliwa kwenye angalau thamani ya
shilingi moja kwenye soko. Maana yake ni kwamba kama kila shilingi
inayozalishwa ina thamani ya angalau shilingi moja katika soko tafsili yake ni
kwamba thamani ya kampuni husika katika soko inaongezeka kwa kila shilingi
inayozalishwa. Somo muhimu ni kwamba kama una biashara unapaswa kuhakikisha
kila shilingi ya ziada inayozalishwa na biashara husika ni lazima iwekezwe
sehemu ambapo itazalisha thamani shilingi nyingine au zaidi na matokeo yake ni
kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji wako katika soko. Hakikisha shilingi inazaa
shilingi.
19. Bei ni kile unacholipia na thamani inapatakana
kwenye kile unachopata. Kwa maana nyingine ni kwamba sio mara zote bei
inaonyesha thamani ya kile unachopata. Thamani ya hisa za kampuni zinaweza
kubadilika mara kwa mara kwani zinaongozwa na tamaa au hofu ya watu kwenye soko
la hisa. Kama mwekezaji unahitaji kuangalia thamani ya kampuni na uzalishaji
wake kuliko unavyoangalia thamani ya hisa zake kwenye soko. Watu wa kawaida
wanauza au kununua hisa kwa kuangalia bei na thamani ya hisa za kampuni husika.
Wawekezaji makini kama Buffett wanachoangalia ni kabla ya kununua ni:
i. Kutambua
thamani halisi ya kampuni husika pamoja na uzalishaji wake badala ya kuangalia
thamani ya hisa zake kwenye soko; na
ii. Kununua
pale ambapo biashara inauzwa kwa bei punguzo kuliko thamani yake halisi.
20. Warren Buffet amekuwa akinunua hisa,
dhamana (bonds) au kampuni katika bei ya punguzo na kusubilia mpaka pale bei
inapokuwa imepanda anaziuza kwa faida. Hii imenfanya kuwa mwekezaji mkubwa
kuliko wote katika uso huu wa duniani kwa kipindi kirefu. Hapa tunachojifunza
ni kuhakikisha tunakuwa macho muda wote kwa ajili ya kuchangamkia fursa
zinazojitokeza.
21. Kila mwekezaji ana staili yake ya
uwekezaji kwani wapo ambao wananunua hisa za kila kampuni ambayo inaonekana kufanya
vyema kwenye soko. Warren Buffet staili yake ni kutuliza rasilimali zake kwenye
kampuni chache ambazo zinaonesha kuwa na matarajio ya kudumu kwenye biashara
kwa muda mrefu na zinaendeshwa na watendaji wenye weledi wa kutosha kwenye
tasnia ya biashara na uwekezaji kwa ujumla.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com