Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa
ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa ni wiki ya 20 katika
kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi wa vitabu nikiwa na
lengo kubwa la kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako kuyatumia ili ubadilishe
kila sekta ya maisha yako.
Uamzi wa kubadilisha maisha yako upo
mikononi mwako na hivyo kama mpaka sasa haujajifunza kitu chochote katika
makala hizi nakushauri husiendelee kupoteza muda wako na badala yake ufanye
mambo ambayo umeyazoea.
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu utakuwa umejiunga na mtandao wa fikra za kitajiri. Kwa kujiunga na
mtandao huu utapata makala zinazochapishwa na mtandao wa fikra za kitajiri moja
kwa moja kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Little Red Book Of Selling” kutoka
kwa mwandishi Jeffrey Gitommer’s. Mwandishi ni mzungumzaji/mhamasishaji
mashuhuri kwenye masuala ya biashara hasa upande wa mauzo na amefanikiwa
kuandika vitabu vingi vya mauzo na mafanikio kwa ujumla.
Kwa
ujumla katika kitabu hiki anatushirikisha mambo muhimu katika tasnia ya mauzo
ambayo analenga kuboresha ujuzi wetu katika kupata, kulinda na kuridhisha
wateja wetu katika sehemu ya soko tuliyopo. Katika kitabu hiki tunaongozwa na ujumbe
kuwa kama wateja “watakupenda,
watakuamini, wana na tumaini na wewe na hatimaye wakawa na uhakika na wewe”
kwa vyovyote vile ni uwezekano wa kuendelea kununua biadhaa/huduma zako. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba pindi wateja wanapokupenda inapelekea wawe na
uaminifu kwako na uaminifu unapelekea wanunue kutoka kwako na wanaponunua
kutoka kwako kwa pamoja mnakuwa na mahusiano ambayo yanapelekea mzunguko wa
mauzo.
Ujumbe
mwingine ambao mwandishi anatupa kama angalizo kwenye tasnia ya mauzo ni kwamba
wateja hawataki kuuzwa kwa maana ya kutapeliwa bali wanahitaji kununua. Hapa ndipo
kila muuzaji ni lazima kwanza apate jibu la kwa nini watu wananunua? Hili ni swali
muhimu la kuzingatia kabla ya kuanza kuweka malengo ya mauzo japo wauzaji wengi
huwa wanakosea na kujiuliza ni kwa jinsi gani nitauza? Hauwezi kufanikiwa
katika jibu la swali la pili kwa maana ni kwa jinsi gani nitauza kama haujapata
jibu la kwa nini watu wananunua. Hivyo msingi mkubwa wa mauzo yenye mafanikio
ni kufahamu kwa nini watu huwa wananunua.
Mwandishi
anatushirikisha majibu ya swali kwa nini watu wananunua ambayo ameyapata baada
ya kuwahoji watu kwa muda mrefu:-
i. Watu
wananunua kwa vile wanampenda muuzaji;
ii. Wananunua
kwa vile wanafahamu kile wanachotaka kununua;
iii. Wanaona
utofauti wa muuzaji/kampuni ikilinganishwa na wauzaji wengine;
iv. Wanaona
thamani katika bidhaa/huduma wanayonunua;
v. Wanamuamini,
wanatumaini na kuwa na uhakika na muuzaji;
vi. Wanajisikia
kuwa huru pindi wanaponunua;
vii.
Wanajisikia bidhaa/huduma zinakidhi mahitaji
yao;
viii.
Bei ni ya kawaida japo sio lazima iwe bei ya
chini;
ix. Wana
uhakika kuwa bidhaa/huduma itaongeza uzalishaji wao;
x. Wana
uhakika kuwa bidhaa/huduma itaongeza faida yao; na
xi. Wana
uhakika kuwa muuzaji anawasaidia kufikia malengo yao huku nae akifikia mahitaji
yake.
Hapo
unaweza kuona kuwa wengi wetu tumekuwa tukikosea kwa kumfikiria mteja upande
mmoja tu wa bei kumbe mteja naye ana mahitaji yake zaidi ya kuangalia bei. Mwandishi
anatushirikisha kuwa hiyo ndo misingi muhimu ambayo kila muuzaji anatakiwa kuwa
nayo kwa ajili ya kuboresha mauzo ya huduma/bidhaa zake. Ukiwa na misingi hii
utafanikiwa kuwa muuza bora kipindi cha maisha yako yote.
Karibu
tujifunze wote machache niliyojifunza kutoka kitabu hiki:
1. Kinachowatoutisha
watu au taasisi katika viwango vya mauzo ni namna ambavyo wanatumia mbinu za
mauzo. Mbinu za mauzo ni nyingi lakini ni vyema kila muuzaji akafahamu kuwa ili
uwe muuzaji bora ni lazima uzingatie mbinu hizi hapa (a) Kwanza kabisa ujiamini
kuwa unaweza (b) Andaa mazingira ya kukuwezesha kuwa muuzaji bora ikiwa ni
pamoja na kuchagua kundi la marafiki wanaokufaha (c) Pata muda kujifunza na
kuhakikisha siku yako unaipangilia vizuri (d) Kuwa na majibu ambayo unahisi
wateja watakuuliza maswali (e) Kuwa mtu mwenye thamani huku ukitafuta fursa
mpya mara kwa mara (f) Kuwa mtu wa vitendo na mara sote husiogope kushindwa (g)
Chunga sana matumizi yako ikilinganishwa na uwekezaji au akiba yako (h) Jenga
tabia njema na muda wote kuwa macho kwa ajili kuliteka soko; na (i) Wapuuze
watu wanaokubeza.
2. Tenga
muda maalum kwa ajili ya kupitia malengo yako ya mauzo kwa kila siku. Mwandishi
anatushirikisha kuwa ni vyema kila siku uwe na muda kuangalia namna ambavyo
siku yako itakwenda na muda huu ni vyema ukawa ni wa asubuhi na mapema kabla
watu hawajaamka kwa ajili ya utulivu. Pia kila siku unatakiwa kutenga muda kwa
ajili ya kufanya tathimini namna ambavyo umefanikisha malengo ya siku husika. Hapa
unatakiwa kuongozwa na nidhamu ya hali ya juu yenye chimbuko la hamasa kutoka
ndani mwako pasipo kusubiria kusukumwa na mwajiri wako au mtu yeyote. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba hakuna mtu ambaye atakuja kukutunuku digrii ya
mafanikio, digirii ya mafanikio unajitunuku mwenyewe kwa kuongozwa na bidii
katika kazi. Ndiyo bidii katika kazi ndo nyenzo ambayo itakufanya jamii
inayokuzunguka ione kuwa wewe ni mtu mwenye bahati. Bahati inatafutwa hivyo
hakikisha unaitafuta bahati yako.
3. Anza
kwa kujilaumu mwenyewe kutokana na kiwango cha mauzo yako badala ya kulaumu mfumo
au serikali, mazingira au watu wanaokuzunguka. Mwandishi anatushirikisha kuwa
watu wengi wanafikia hatua ya kulaumu waajiri wao, serikali, watu wao wa karibu
au hata pengine wateja kabla ya kujiuliza wao wanahusika vipi kwenye kiwango
cha mauzo yao. Kwa ujumla kiwango cha mauzo yako kinategemea na (a) Imani yako –
Je unajiamini kuwa unaweza kuuza kwa kiwango kile unachokusudia? (b) Mazoea ya
kazi yako – Je unaenda kazini ukiwa umechelewa na unafunga mapema jioni lakini
bado unategemea kuwa na kiwango kikubwa cha mauzo? (c) Hisia mbaya juu yako –
Je unahisia mbaya juu ya bidhaa/huduma au una wasiwasi wa bei zako? (d) Tabia
mbaya kama ulevi/utaji wa sigara ukiwa kazini (e) Hautimizi ahadi kwa wateja au
pengine unatimiza kinyume na makubaliano. Hizi baadhi ya sehemu muhimu ambazo
unatakiwa kujitathimini kwa ajili ya kuboresha kiwango cha mauzo yako.
4. Siku
mbaya au nzuri unaiandaa mwenyewe kila unapoamka asubuhi. Ni kawaida kusikia
mtu anakuambia kuwa leo sina mudi ya kufanya au leo siku yangu imekwenda
vibaya. Mwandishi anatushirikisha kuwa ukifanya tathimini siku ambayo unadai
kuwa imekwendea vibaya utagundua kuwa kwa asilimia kubwa ubaya wa siku hiyo
wewe ndo umechangia kwa kiasi kikubwa hasa kutokana na fikra/mtazamo wako kwa
siku husika. Mfano, ni kawaida kwa watu walio wengi kuwa na uzalishaji mdogo
kwenye siku za jumatatu na ijumaa kutokana na mitazamo yao juu ya siku husika.
5. Je unaongozwa
na falsafa zipi? Falsafa zinazaa mtazamo, mtazamo unaleta vitendo na vitendo
vinaleta matokeo na hatimaye matokeo yanaleta mtindo wa maisha yako. Kama haupendi
mtindo wa maisha yako ni lazima kwanza unagalie falsafa zinazokuongoza na
hatimaye uzibadilishe falsafa hizo kwa ajili ya kufikia mtindo mpya wa maisha. Watu
wa mauzo mara nyingi wanafanya kosa kubwa la kutazama sehemu ya vitendo kabla
ya kuangalia kwanza falsafa zinazowaongoza. Kwa kifupi falsafa ni vile vitu
ambavyo una imani juu yake na katika maisha yako umeviweka kama mwongozo wako
kwenye kila sekta ya maisha yako. Kwa maana hii falsa zinatofautiana kati ya
mtu mmoja na mwingine.
6. Kuwa
na mtazamo wa NDIYO. Mwandishi anatushirikisha kuwa mtazamo wa ndiyo ni nyenzo
muhimu ya kukabiliana na kila aina ya mazingira au tukio kwa muuzaji yeyeto
yule. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ukiwana mtazamo wa ndiyo utakuwa tayari
kufanya kazi hata kwenye mazingira ambayo wenzako wanaona kuwa hayawezekani. Mtazamo
huu unakufanya ujione kuwa kila kitu au tukio linaanza na NDIYO hata kama ni
HAPANA hivyo kukujengea msingi imara wa kuona kuwa kila jambo linaweza kutekelezwa
endapo utaweka jitihada.
7. Kazi
ya kesho inaandaliwa usiku wa leo. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama unataka
kuwa muuzaji bora ni lazima uwe tayari kuindaa siku yako wakati watu wengine
wamelala au wanaangalia TV usiku. Husikubali kupoteza muda wako kwa kuangalia
michezo au filamu ambazo hazikuongezei kitu katika tasnia ya kazi yako na
badala yake tumia muda huo kupangilia vyema kazi zako kwa ajili ya siku
inayofuatia. Hapa unatakiwa kufahamu kuwa kadri unavyoharibu muda wako kwenye
TV au siku hizi kwenye mitandao ya kijamii ndivyo unakubali kutumiwa na watu
wengine kutimiza malengo yao ya mauzo.
8. Je wewe
ni mshindi au mlalamikaji? Mwandishi anatushirikisha kuwa kama kweli unataka
kuwa msshindi katika kazi zako za mauzo ni lazima kwanza uepuke tabia ya kuwa
mlalamikaji. Hakikisha jukumu la ushindi unaliweka chini ya mamlaka yako ili
hata pale unaposhindwa ujiulize wewe mwenyewe kwa nini umeshindwa na sio
kulalamikia wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba dhana ya ulalamikaji
inakufanya ujitoe kwenye uhusika wa jambo au tukio na badala yake unamuachia
mtu mwingine kama ndo amesababisha. Pia, unatakiwa kukumbuka kuwa hakuna mtu
anayejitambua atapenda kukaa na mtu mlalamikaji. Kwa maana hivyo kadri
unavyokuwa mlalamikaji unazidi kujiwekea mbali na watu wenye mchango chanya
katika maendeleo ya kazi yako.
9. Utambulisho
wako (self branding) ni nyenzo muhimu kwa wateja wako. Kadri watu wanavyokufahamu
zaidi ndivyo watavutiwa kufanya biashara na wewe. Mwandishi anatushirikisha
kuwa watu wengi kwenye tasnia ya mauzo wanafanya makosa ya kupigania
utambulisho wa bidhaa/huduma zao kuliko wanavyoweka jitihada za kutambulisha
majina yao wenyewe. Ili kuachana na makosa haya unahitaji kujitambulisha kwanza
ili ufahamike kwa wateja wako na kadri wateja wanavyofahamu utambulisho wako ni
rahisi kuvutiwa na yale unayofanya ikiwa ni pamoja na kampuni, bidhaa au huduma
zako. Katika kujitambulisha unahitaji kujipambanua kama mtu mwenye kupigania
kutatua matatizo ya wanajamii inayokuzunguka, unahitaji kujenga picha ya
tofauti kwa wateja wako, unahitaji kujenga imani kwa wateja wako na unahitaji
kuonekana mbunifu kupitia yale unayofanya. Muhimu tambua kuwa katika tasnia ya
mauzo ni lazima utambue kuwa “si yule unayemfahamu bali ni yupi anakufahamu”
hivyo unahitaji kujitangaza kwa hali na mali.
10. Thamani ya bidhaa zako pamoja na
mahusiano yako na wateja ni sifa mbili muhimu za kuongeza kiwango cha mauzo
yako na wala sio bei ya bidhaa/huduma zako. Watu wengi wanachanganya maana ya thamani
kwa mteja kuwa ni kama vile punguzo la bei, bidhaa za bure zinazoambatana na
kitu unachonunua, nyongeza n.k. Ukweli ni kwamba thamani kwa mteja ni vile vitu
vinavyofanyika kwa mteja au mteja mtarajiwa kwa ajili ya faida yake
pasipokutegemea wewe utafaidika na nini. Kwa maana hii ni lazima kwanza
utangulize thamani kwa mteja wako na hatimaye faida itakufuata yenyewe. Hii ni
pamoja na kutoa elimisho juu ya bidhaa au biashara yako kupitia makala, mitandao
ya kijamii au semina za bure huku ukiacha namba zako za mawasiliano kwa ajili
ya wateja watarajiwa. Kutokana na ukweli huu watu hawangalii bei bali
wanaangalia thamani yako na huduma zako kwani kadri thamani inavyozidi kuwa
kubwa ndivyo na wateja hawangalii kiwango cha bei.
11. Acha kuwa na fikra za kuwa biashara yako
ni kuuza bidhaa/huduma kwa wateja na badala yake fikiria kuwa biashara yako ni
kuuza thamani kwa wateja wako. Kumbuka kuwa unapouza thamani bei inakuwa sio
kipimo cha mauzo yako na badala yake kinachoamua kiwango cha mauzo ni thamani
unayotoa. Pia, kumbuka kuwa sio wateja wote watanunua kwa kuangalia thamani
kwani tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 30 – 40 ya wateja wananunua kwa
kuangalia bei ya chini ikilinganishwa na asilimia 60 – 70 ya wateja
wanaotangulizwa thamani kwanza.
12. Kiwango cha mauzo yako kina uhusiano
mkubwa na jitihada unazoweka kwenye kujenga mtandao na wateja wako. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba kadri unavyozidi kuwa na mtandao mkubwa ndivyo
unaongeza idadi ya marafiki na idadi ya marafiki ina mchango chanya kwenye
kiwango cha mauzo yako. Hapa unahitaji kutumia majukwaa au matukio mbalimbali
kwa ajili kupanua mtandao wako. Unaweza kutumia mitandao ya kijamii, maonyesho
mbalimbali kama maonyesho ya biashara, nanenane, mkusanyiko wa watu kwa ajili
ya michezo na matukio mengineyo.
13. Kiwango cha mauzo yako kinategemea na idadi
ya wateja au wateja tarajiwa ambao unaweza kuwashawishi. Mwandishi anatushirikisha
kuwa kuna uhusiano mkubwa katika ya mauzo na uwezo wa kushawishi wateja wako. Pia,
unapofanya ushawishi ni lazima utambue kuwa ni kundi lipi katika jamii
unalilenga kwa ajili ya kufanya biashara na wewe. Mfano, itakuwa haina maana
kumshawishi mtoto wakati unajua kuwa mtoa maamzi ni baba au mama. Itakuwa haina
maana kumshawishi mwajiriwa wa kampuni kwa ajili ya bidhaa au huduma zako wakati
unajua kabisa kuwa mtoa maamuzi ni bosi wake.
14. Kufanikiwa katika kuwashawishi wateja
kunategemea na namna ambavyo unauliza au kujibu maswali pindi unapokutana na
wateja watarajiwa. Mwandishi anatushirikisha kuwa kabla ya kufanya ushawishi na
wateja ni lazima kwanza upangilie vyema maswali na majibu ili vyote kwa pamoja
vimushawishi mtu kufanya biashara na wewe. Muda wote uliza maswali ambayo
yatakutifautisha na wapinzani wako wa kibiashara, uliza maswali ambayo
yatamfanya mteja aone thamani katika bidhaa/huduma yako, uliza maswali ambayo
yatamfa mteja aone fursa mpya katika biashara zake au maswali ambayo yanampa shauku
ya kuendelea kukusikiliza. Kumbuka kuwa kama mteja mtarajiwa hajashawishika ni
kwa sababu na wewe haukuwa na ushawishi hivyo endelea kujifunza mbinu za
kushawishi.
15. Kama unaweza kumchekesha mteja
mtarajiwa kuna uwezekano mkubwa wa kumshawishi anunue kutoka kwako. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mteja unapomgusa hisia zake kiasi cha kuweza kutabasamu au kucheka basi
fahamu kuwa umefanikisha hatua ya kwanza ya mahusiano mazuri kati yako na yeye.
Hivyo katika kutafuta wateja wapya unahitaji kuongozwa na ucheshi wa maneno
pamoja na lugha ya mwili. Hata hivyo ni lazima utambue kuwa mcheshi katika
mauzo inachukua muda ikitegemea na namna mhusika anavyowekeza kwenye kujifunza
kuwa mcheshi.
16. Tumia ubunifu kujitofautisha na wengine
hatimaye kuliteka soko. Kama ambavyo tumeona kuwa watu wapo tayari kulipia
thamani, ni kupitia ubunifu utafanikiwa kutoa thamani kubwa kwa wateja wako. Ubunifu
unategemea na namna ambavyo unatumiwa kichwa chako kwa maana ubongo wako –
unahitaji kujenga tabia ya kufikiri kwa ajili kuwa mbunifu, mtazamo wako –
ukiwa na mtazamo hasi daima hauwezi kuwa mbunifu, namna unavyotazama mazingira
yako – kuna fursa kila sehemu inayokuzunguka na jinsi unavyojitazama mwenyewe –
kama haujiamini kamwe hauwezi kuwa mbunifu. Ili kuwa mbunifu unahitaji kusoma
zaidi kwani kadri unavyosoma makala na vitabu mbalimbali ndivyo unajifunza
ubunifu zaidi.
17. Kama muuzaji unahitaji kuchanganua hali
hatarishi na kuipunguza kabla kufanya biashara na mteja wako. Kadri utavyopunguza
hali hatarishi kwa wateja wako ndivyo itakuwa rahisi kuwavuta watu wengi
kufanya biashara na wewe. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watu wanahitaji
bidhaa/huduma ambazo sio hatarishi (risk free products or services). Hali hatarishi
unahitaji kuzichangunua kwa kuangalia ubora wa bidhaa/huduma zako, thamani
halisi ya huduma zako, ukweli katika kile unachomuhubiria mteja wako, matumizi
au matokeo tarajiwa baada ya kununua bidhaa/huduma zako n.k.
18. Shuhuda wa bidhaa au huduma zako ana
nafasi ya kuwashawishi watu wengi kuliko wewe. Kuna msemo kuwa ukimfukuza mteja
mmoja kutokana na uzembe au uongo wako katika huduma zako unakuwa umefukuza
wateja zaidi ya kumi. Ndicho mwandishi
anachotushirikisha hapa kuwa unatakiwa kuhakikisha kila mteja unayefanya naye
biashara huna budi kumridhisha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri mteja
anavyoridhika na huduma/bidhaa zako ndivyo atavyowaleta wateja wengine wapya.
19. Kuwa macho muda wote kwa ajili ya kufanya
mauzo. Kamwe husikubali kutoka kwenye lengo lako kubwa pasipokujali sehemu
uliyopo, kila sehemu na kila wakati hakikisha upo tayari kwa ajili ushawishi wa
wateja watarajiwa. Hapa muda wote unatakiwa kuongozwa na hamasa tano ambazo ni
(i) hamasa ya ushindi (ii) hamasa ya kujiamini wewe pamoja na bidhaa/huduma
zako (iii) hamasa ya kutegemea matukio chanya kuliko matukio hasi (iv) hamasa
ya kufanikiwa na (v) hamasa ya maamuzi chanya.
20. Jiuzulu nafasi yako kama meneja mkuu wa
ulimwengu. Mwandishi anatushirikisha kuwa mpaka kufikia hapa umepata nyenzo
muhimu za kukusukuma katika tasnia ya mauzo lakini kuna jambo moja la
kuzingatia. Kuna matukio mengi yanatokea na mengine yataendelea kutokea katika
ulimwengu huu lakini kabla ya kuyashabikia jiulize yanachangia nini katika
maisha yako. Kamwe husikubali kutekwa kwenye matukio ya watu wengine, unahitaji
kuandaa matukio yako mwenye ili yaweteke ambao bado hawajajitambua. Sanaa ya
kuuza inahitaji nidhamu ya hali ya juu hasa nidhamu binafsi. Unahitaji kuachana
na ushabiki ambao hauna tija kwako.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com