UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Njia 4 Zitakazo Kuwezesha Kupata Mtaji

NENO LA SIKU_APRILI 16/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Njia 4 Zitakazo Kuwezesha Kupata Mtaji.

Hongera rafiki kwa kuendelea kufuatilia masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri. Ni siku nyingine ambayo naamini imekuwa miongoni mwa siku bora hasa kwa kuzingatia kuwa umeitumia kutekeleza vipaumbele muhimu vya maisha yako. 

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu tena katika makala ya leo ambapo nitakushirikisha njia nne za kupata mtaji wakati wa kuanzisha biashara ya ndoto yako.

Katika makala ya jana tuliona kuwa asilimia kubwa ya watu wanashindwa kuanzisha biashara kutokana na sababu za kukosa mtaji.

Tuliona kuwa pamoja na wengi kuelezea mtaji kama kikwazo nambari moja wakati wa kuanzisha biashara, ukweli ni kwamba wengi wanashindwa kuanzisha biashara kwa sababu hawana mawazo sahihi pamoja na maarifa sahihi kuhusu biashara wanazotamani kuanzisha.

Kama ni mara yako ya kwanza kusoma makala hizi nashauri usome mfululizo wa makala zote kupitia wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.

SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Kikwazo Ambacho Hukwamisha Wengi Kuanzisha Biashara

Kama una kiu ya kuanzisha biashara karibu ujifunze njia nne ambazo zitakuwezesha kupata mtaji.

Nikumbushe kuwa katika tafsiri ya biashara, tunaposema mtaji tunamaanisha uwezo wa kukuwezesha kuanzisha, kusimamia au kukuza biashara.

Uwezo huu tunaweza kuugawa makundi matatu ambayo ni: nguvu kazi, rasilimali fedha na ujuzi au maarifa.

Nguvu kazi inajumuisha uwezo uliopo ndani mwako ikiwa unaweza kufanya kazi zinazohusiana na usimamizi au uendeshaji wa biashara utakayo anzisha. Pia, nguvu kazi hujumuisha uwezo ulionao kupitia mahusiano yako na watu wanao kuzunguka.

Rasilimali fedha hujumuisha uwezo ulionao wa kifedha kupitia fedha taslimu au mali unazomiliki ambazo zinaweza kubadilishwa kuwa fedha kwa ajili ya ya kuanzisha biashara unayotamani.

Ujuzi au maarifa hujumuisha uwezo ulionao ambao unaweza kutumika kuzalisha fedha zaidi.

Kupitia makundi haya tunapata njia nne za kukusanya mtaji wa kuanzisha biashara kama ilivyo elezwa hapa chini;-

Kupitia mahusiano ya ndugu au marafiki. Hii ni njia ya kupata mtaji ambayo hutegemea uhusiano pamoja na uwezo wa ndugu au marafiki wako wa karibu.

Njia hii inaweza kuhusisha kupata mtaji kupitia mirathi, kufanya kazi kwa ndugu au rafiki kwa makubaliano maalum au kukopeshwa mtaji kwa masharti nafuu ikitegemeana na uaminifu wako kwa ndugu au rafiki mwenye uwezo wa kifedha.

Jambo la kuzingatia, njia hii ya kupata mtaji haipo wazi kwa kila mtu maana hutegemea hali ya kifedha na utayari wa ndugu au marafiki katika kukuwezesha kimtaji.

Kupitia akiba binafsi. Ni njia ya kupata mtaji ambayo hutokana hazina yako ya pesa taslimu au mali unazomiliki ambazo zinaweza kugeuzwa kwenye fedha taslimu kwa urahisi.

Njia hii inakutaka uwe na akiba ambayo ambayo umeikusanya kwa muda mrefu kwa ajili ya kukuza mtaji.

Katika makala zilizopita tuliona kuwa njia rahisi ya kukuza akiba yako ni kupitia njia ya kujilipa kwanza ambapo unakuwa na nidhamu ya kutenga kiasi cha pesa kwa ajili ya akiba na uwekezaji.

SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Tumia Siri Hii Kukuza Utajiri Wako

Pia, kwa njia hii unaweza kupata mtaji kupitia mali unazomiliki kama vile mifugo, ardhi, mitambo, hisa, nyumba, gari au mali nyinginezo ambazo unamiliki zinazoweza kubadilishwa kwenye fedha taslimu kwa urahisi.

Hii ni njia ambayo inakutaka uwe na nidhamu ya kutosha hasa katika kutenga fedha kwa kipindi cha muda mrefu kwa ajili ya akiba na uwekezaji.

Kwa kukosa nidhamu binafsi, wengi hushindwa kutenga akiba au hujikuta wametumia kiasi kilichotengwa kwenye matumizi mengine kinyume na malengo ya awali.

Kupitia njia ya mikopo (OPM). Hii ni njia ambayo unatumia pesa za watu wengine (using other people’s money - OPM) kukuza mtaji wako.

Ni njia ya uhakika ya kupata mtaji ikiwa unakopesheka au una wazo la biashara ambalo linauzika.

Hata hivyo, njia hii huwa ni ngumu hasa kwa wale wanao anzisha biashara kutokana na kutokuwa na dhamana ambazo hutakiwa na wakopeshaji kama vile taasisi za fedha (benki, SACCOS/VICOBA, microfinance au watu binafsi).

Pia, mara nyingi taasisi za kifedha huwa zinatoa pesa kwenye biashara ambazo tayari zina uhakika wa uendelevu.

Pamoja na changamoto za upatikanaji wa mikopo, njia hii inaweza kutumika kukuza mtaji wako kupitia mikopo ya benki, SACCOS/VICOBA, Microfinance au mikopo ya serikali kwa makundi maalum.

Kupitia SACCOS/VICOBA unaweza kukopa ikiwa hata hivyo wewe ni mwana ushirika (SACCOS) wenye malengo ya kukopesha wanachama wake kulingana na hisa wanazomiliki kwenye SACCOS/VICOBA husika.

Kupitia njia ya mikopo ya benki, kama tulivyoona masharti yake huwa ni magumu hasa kwa biashara ambazo hazina uhakika wa kurejesha kiasi unachohitaji.

Hata hivyo, kama ni mwajiriwa unaweza kutumia ajira yako kama dhamana ya kukopa na kupata mtaji wa kuanzisha biashara badala ya kununua gari au kujenga nyumba.

Kupitia njia ya kukopa kwenye ‘Microfinance’ au watu binafsi, mikopo hii hupatikana kwa masharti rahisi lakini huwa na riba kubwa wakati wa kurejesha.

Hali inaweza kusababisha kushindwa kukuza biashara yako kutokana riba unayotakiwa kurejesha kuzidi faida inayozalishwa kwenye biashara husika.

Kupitia mikopo maalum ya Serikali, mikopo hii hutolewa kwa makundi maalum kwenye jamii kama vile vijana, akina mama au watu wenye ulemavu.

Kupata mikopo hii, ikiwa upo kwenye makundi yaliyotajwa inabidi uwe kwenye kikundi kilichosajiliwa na kupitia kikundi chenu mnaomba mkopo huo ambao hutolewa na Serikali za Mitaa, baadhi ya taasisi za Serikali kama vile SIDO au baadhi ya miradi ya Serikali inayofadhiliwa na Mashirika.

Kupitia njia ya kuuza ujuzi, maarifa au kipaji. Njia hii inahusisha kubadilishana ujuzi, maarifa au kipaji na fedha.

Ni njia ambayo inaweza kutumika kukuza mtaji ikiwa una nidhamu na pesa unazopata kutoka kwenye mauzo ya ujuzi, maarifa au kipaji.

Pia, wakati mwingine msingi wa biashara unaweza kujengwa kupitia kutumia ujuzi, maarifa au kipaji chako.

Kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, katika karne hii ni rahisi kukuza mtaji kwa kuwa unaweza kuuza ujuzi, maarifa au kipaji chako kwa urahisi tena bila kizuizi cha mipaka ya nchi.

Mfano, tunaona jinsi ambavyo mmiliki wa mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp anavyo tengeneza pesa nyingi kutokana na ‘software’ ya mawasiliano aliyoianzisha kupitia ujuzi mifumo ya kompyuta.

Na wewe katika eneo lako, unaweza kuuza kipaji, ujuzi au maarifa na kukusanya pesa kwa ajili ya kukuza mtaji wako.

Hitimisho. Moja ya changamoto kubwa ambayo wajasiriamali wanakabiliana nayo ni kutafuta pesa kwa ajili ya kuanzisha, kuendesha au kufanikisha ukuaji wa biashara.

Mtaji umeendelea kuwa kikwazo nambari moja ambacho hukwamisha watu katika kuelekea kwenye ukamilisho wa ndoto zao.

Hata hivyo, watu ambao wamedhamiria kuishi ndoto zao wamefanikiwa kukuza mtaji kupitia njia ambazo nimekushirikisha kupitia makala hii.


NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.


WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.


UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Kikwazo Ambacho Hukwamisha Wengi Kuanzisha Biashara.

NENO LA SIKU_MACHI 28/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Kikwazo Ambacho Hukwamisha Wengi Kuanzisha Biashara.

Hongera rafiki yangu na mfuatiliaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa siku hii ya leo. Ni siku nyingine ambapo naamini umebahatika kuwa na siku bora, siku ambayo imekuwa ngazi ya kufikia kilele cha mafanikio unayotamani. 

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu tena katika makala ambazo zinalenga kukufunulia mbinu mbalimbali za kukuza pato lako.

Imekuwa ni takribani wiki tatu tangu nilipoandika makala ya mwisho ambayo ilihitimisha makundi ya biashara ambayo unaweza kuchagua kabla ya kuanzisha biashara yako.

Ikiwa hukufanikiwa kusoma mwendelezo wa makala zilizotangulia nashauri utembelee wavuti FIKRA ZA KITAJIRI ili kusoma makala zote.

SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya tano.

Katika makala ya leo tutaangalia kikwazo ambacho hukwamisha watu wengi kuanzisha biashara wanazotamani. Naamini wote tunakubaliana kuwa “asilimia kubwa ya watu katika jamii wana ndoto za kuanzisha biashara”.

Iwe ni wasomi au wasiyo wasomi, wengi wanatamani kumiliki biashara kama njia mbadala ya kuingiza kipato nje ya shughuli wanazofanya.

Mwajiriwa anatamani kumiliki biashara ili awe huru kwenye kukidhi mahitaji ya kipesa.

Vivyo hivyo, mkulima au mfugaji anatamani amiliki biashara kama njia ya kujiongezea kipato nje ya shughuli zake za kilimo au ufugaji.

Ikiwa kumiliki biashara ni kiu ya watu wengi, kwa nini wengi huwa wanashindwa kuanzisha biashara?

Watu wengi wanashindwa kuanzisha biashara kwa kuendekeza kikwazo cha “kutokuwa na au uhaba wa mtaji” kama kigezo namba moja wakati wa kuanzisha biashara.

Ukiachagua watu 10 ambao wamewahi kuwa na dhamira ya kuanzisha biashara na kuwauliza kwa nini hawakufanikiwa kuanzisha biashara, watu nane wanaweza kukupatia jibu la kukosa mtaji kama kikwazo kikuu huku wengine waliobakia wakitaja vikwazo vingine nje ya mtaji.

Tafsiri yake ni kwamba, asilimia kubwa ya watu ambao wameshindwa kuanzisha biashara za ndoto zao hutanguliza mtaji kama hitaji nambari moja wakati wa kuanzisha biashara.

Hivi ni kweli kuwa mtaji ni hitaji pekee wakati wa kuanzisha biashara?

Kujibu swali hili tunatakiwa kwanza kuelewa maana ya mtaji katika mantiki ya uanzishwaji na usimamizi wa biashara.

Katika mtazamo wa biashara tunaweza kuelezea mtaji kama: “uwezo (kifedha, nguvukazi, au ujuzi) wa kuanzisha biashara, kufadhili fursa za ukuaji wa biashara, au kuzindua bidhaa mpya sokoni.”

Jambo la msingi la kuzingatia katika maana hii ya mtaji ni; tunapozungumzia mtaji hatumaanishi uwezo wa kipesa pekee!

Siyo biashara zote ambazo ni lazima uanze na kigezo cha kukosa mtaji wa kifedha, kuna biashara ambazo unaweza kuanzisha kwa kutumia nguvu kazi au ujuzi na maarifa uliyonayo.

Unaweza kutumia nguvu na maarifa au ujuzi wako kukuza uwezo wa kifedha ambao utakuwezesha kupanua biashara unayofanya katika kuelekea kwenye biashara ya ndoto yako.

Kwa mtazamo huu, tunaweza kuona kuwa watu wengi wanashindwa kuanzisha biashara kwa kutafsiri mtaji katika upande mmoja wa uwezo wa kifedha.

Tafsiri hii hupelekea wengi kushindwa kuona uwezo walionao (nguvu, maarifa au ujuzi) katika kuelekea kwenye biashara wanazotaka kuanzisha.

Pia, asilimia kubwa ya watu wanaoendekeza kiwazo cha mtaji wa kifedha, wakiulizwa swali ni kiasi gani cha mtaji wanataka na kiasi hicho kitatumika vipi katika kuanzisha biashara wanazotamani, utashangaa kuona siyo wote wanaojua kiasi kamili cha mtaji na mtiririko wa matumizi ya kiasi hiko wakati wa kuanzisha biashara.

Hali hii inatoa picha kuwa, asilimia kubwa ya watu wanashindwa kuanzisha biashara kutokana na kikwazo cha kukosa wazo na maarifa sahihi kuhusu biashara badala ya mtaji kama inavyodhaniwa.

Kwa kukosa wazo na maarifa sahihi, hupelekea wengi wawe na mtazamo wa kuanzisha biashara yenye kuhitaji mtaji mkubwa wa kipesa kabla ya kufikiria kwanza biashara ambazo mtaji wake upo ndani ya uwezo wao.

Kumbe, unapofikiria kuanzisha biashara kabla ya kusema sina mtaji ni vyema ujitathimini una uwezo gani ambao ni mtaji wa kukuwezesha kukuza mtaji zaidi wa kipesa.

Jiulize unamiliki rasilimali zipi ambazo unaweza kuzibadilisha katika mtaji wa kifedha! Jiulize una ujuzi au maarifa yapi ambayo yanaweza kutumika kukuza mtaji unaotaka!

Jiulize ni biashara ipi ambayo unaweza kuifanya kulingana na uwezo wako wa sasa! Jiulize unaweza kutumia vipi mahusiano na watu wako wa karibu katika kukuza mtaji wa biashara unayotamani.

Hitimisho. Kuna msemo kuwa "Watu hawana mpango wa kushindwa, wanashindwa kutokana na kukosa kupanga."

Unapofikiria kuanzisha biashara unatakiwa uweke mpango mzuri ambao utakuwezesha kutumia uwezo ulionao kwa sasa kama mtaji nambari moja wa kuanzisha na kukuza biashara yako.

Husiogope kuanza kidogo badala yake ogopa kutokuanzisha kile ambacho kipo ndani ya uwezo wako.


NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.


WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki kipatikana kwa bei ya punguzo ya Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.


UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya tano.

NENO LA SIKU_MACHI 23/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya tano.

Rafiki na mfuatiliaji wa masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri, hongera kwa kuwa na siku bora katika maisha yako. Siku ya leo naamini imekuwa siku muhimu ya kukusogeza kwenye kilele cha mafanikio unayotamani katika kipindi cha uhai wako.

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika mwendelezo wa makala zinazokufunulia mbinu za jinsi gani unaweza kuwa tajiri kuanzia ngazi ya chini kabisa. Makala ya leo ni mwendelezo wa makundi ya biashara ambayo unaweza kuchagua kundi moja wapo na kuanzisha biashara ambayo itakuwezesha kukuza pato lako.

Ikiwa ni mara yako ya kwanza kufuatilia masomo haya nashauri usome makala zilizotangulia kupitia wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.  

SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Nne

Tuhitimishe kujifunza makundi ya biashara kwa kuangazia kundi la mwisho la Biashara mtandaoni (online or electronic business).

Hili ni kundi la mwisho kuelezewa siyo kwa umuhimu wake bali kutokana na makundi yote tuliyojifunza yanaweza kuhusisha biashara mtandao kama njia ya kufungua masoko mapya au kuongeza mauzo.

Biashara ya “Kielektroniki” au “Mtandaoni" ni aina yoyote ya shughuli za kibiashara inayohusisha ubadilishaji wa taarifa za biashara kwa njia ya mtandao.

Hivyo, shughuli yoyote inayohusisha ubadilishaji wa bidhaa au huduma kwa malipo kati ya mtu binafsi, kundi la watu au taasisi kupitia mtandao inafaa kutafsiliwa kama biashara mtandao.

Biashara ya kielektroniki inazingatia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuwezesha shughuli za biashara nje ya uhusiano wa ana kwa ana kutokana na kuunganishwa na mtandao.

Biashara ya kielektroniki inatofautiana na makundi mengine ya biashara kutokana na shughuli za kuuza na kununua kukamilishwa kupitia mtandao.

Pia, e-business huwezesha kufanywa michakato yote ya biashara (usafirishaji wa ndani/nje, utengenezaji na uendeshaji, uuzaji na kununua, huduma kwa wateja) ndani ya mnyororo wa thamani kupitia mitandao ya ndani au nje. 

Biashara mtandao ni fursa hai kwa kila mtu katika karne hii ya mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano. Kundi hili la biashara limezalisha na litaendelea kuzalisha mabilionea wengi kutokana na kukua kwa kasi ya watumiaji wa mtandao.

Mfano, mtandao wa First Site Guide unatoa takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2021 takribani “watu bilioni 1.79 walinunua vitu kupitia mtandao.” Katika kipindi hicho 70% ya biashara ndogo hadi za kati ziliwekeza zaidi katika matumizi ya mfumo wa biashara za kidijitali. 

Mifano ya baadhi ya mabilionea ambao wamekuza utajiri wao kupitia matumizi ya biashara mtandao ni: Jeff Bezos, mmiliki wa Kampuni ya Amazon ambayo inajihusisha na kuuza na kununu bidhaa kwa njia ya mtandao; Jack Ma, mmiliki wa Kampuni ya Alibaba inayowezesha kuuuza na kununua kupitia mtandao; Bill Gates, mmiliki wa Kampuni ya Microsoft ambayo inajihusisha na uuzaji wa mifumo ya kompyuta; Mark Zuckerberg, mmiliki wa mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp;  Larry Page, mmiliki wa mtandao wa Google; Pierre Omidyar, mmiliki wa eBay; Garrett Camp, mmiliki wa mtandao wa Uber unaowezesha kuunganisha wateja na vyombo vya usafiri mjini.

Kwa hapa Tanzania, mitandao maarufu inayowezesha biashara mtandao ni pamoja na: KiKuu (uagizaji wa bidhaa kutoka China); Kupatana (mauzo mtandao ya bidhaa mbalimbali); Zoom Tanzania (mauzo ya bidhaa mtandaoni); na Bolt (kuunganisha wateja na usafiri mjini). 

FAIDA ZA BIASHARA MTANDAONI. Kama ambavyo tuliona faida na changamoto za kila kundi la biashara, biashara mtandaoni ina faida zifuatazo:-

Huondoa vikwazo vya eneo na mipaka: Unapofanya biashara kwa njia ya mtandao ni rahisi kuuza kwa wateja nje ya eneo lako maana mtandao unakuunganisha watu kote ulimwenguni.

Pia, mtandao unakuwezesha kueneza taarifa za biashara yako kwa kasi na hupatikanaji wa taarifa hizo muda wote (masaa 24).

Hii ni tofauti na kuuza bidhaa au huduma kwa kuweka biashara yako kwenye pango la biashara.

Kwa mfumo wa kufanya biashara nje ya mtandao, unategemea kupata wateja wanaoweza kulifikia duka au huduma yako katika muda wako wa kazi. 

Hupunguza muda na pesa zinazotumika: Kufanya biashara mtandao kunaondolea kodi za pango la eneo la biashara, umeme, maji na gharama gharama nyingi za uendeshaji.

Mfano, kwa teknolojia ya mtandao mtu mmoja aweza kuhudumia wateja zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja kwa kuunganishwa na teknolojia.

Pia, gharama za mawasiliano na matangazo zinapungua kutokana na teknolojia kuwezesha ujumbe maalumu wa biashara yako kusambazwa kwa watu wengi. 

Huharakisha huduma kwa wateja: Huduma kwa Wateja kupitia mtandao ni rahisi ikilinganishwa na makundi mengine ya biashara.

Zaidi ya hayo, aina hizi za huduma kwa wateja zinazonyumbulika kwa kuwa zinaweza kufanyika zaidi ya saa za kazi za ikilinganishwa na makundi mengine ya biashara.

Pia, ni rahisi kutunza kumbukumbu za malalamiko au maoni ya wateja kuhusu bidhaa au huduma unazouza.

Urahisi wa kuanzisha: Biashara ya mtandao ni rahisi kuanzishwa maana haitaji uwe na mtaji mkubwa. Unaweza kuanzisha biashara hii hata ukiwa nyumbani kwako maana hitaji la msingi ni kifaa kilichounganishwa na mtandao na chenye programu maalumu za kuunganisha na wateja wako.

Ni rahisi kufanya tathimini: Kupitia ‘software’ maalumu za kuwezesha biashara mtandao ni rahisi kuwa na kumbukumbu muhimu za uendeshaji wa biashara yako. Hii nyenzo muhimu ya kufanya tathimini ya mwenendo wa biashara yako.

Mfano, ni rahisi kujua jinsi bidhaa au huduma yako imekuwa na manufaa katika nyakati tofauti kulingana na matukio muhimu katika kipindi cha mwaka mmoja. Kupitia taarifa hizo ni rahisi kujua matakwa ya wateja wa muda mrefu au kugundua ikiwa kuna wateja wapya.

Njia ya kuepuka usumbufu wa gharama za kodi na tozo: Unapofanya biashara yenye pango au eneo maalumu la biashara kuna kodi na tozo nyingi kulingana na kanuni za nchi husika.

Unapofanya biashara mtandao kuna baadhi ya kodi au tozo ambazo utafanikiwa kuzipunguza. Mfano, kupitia biashara mtandao hautoulizwa leseni ya Halmashauri au tozo za usafi n.k.

CHANGAMOTO. Kila kundi la biashara lina changamoto zake, biashara mtandaoni inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

Ukosefu wa muunganiko wa ana kwa ana: Unapofanya biashara mtandao unamnyima mteja fursa ya kukutana na muuzaji, kuchunguza au kuhojiana ana kwa ana kuhusu bidhaa au huduma zako.

Hii ni tofauti na utaratibu wa biashara uliozoeleka ambao humwezesha mteja kuchunguza au kuhoji kuhusu bidhaa au huduma kabla kufanya malipo.

Muda wa kusubiria: Unaponunua bidhaa mtandaoni ni lazima uwe tayari kusubiria kipindi cha muda wa siku kadhaa kabla ya kupokea bidhaa husika.

Hii ni tofauti na makundi mengine ya biashara ambapo mteja hupokea bidhaa yake pale anapokamilisha malipo. 

Usalama na Uaminifu: Mtandaoni kuna wafanyabiashara waaminifu na baadhi wanafanya ulaghai unaopelekea watu kuogopa kufanya biashara kwa mtandao.

Pia, kukua kwa teknolojia kunaweza kupelekea udukuzi wa taarifa binafsi za mteja hali ambayo inatia doa uaminifu wa biashara za mtandaoni.

Baadhi ya wateja bado hawaamini biashara za mtandaoni kwa kutokana na uwepo wa ulaghai wa kila aina kwenye mitandao. 

HITIMISHO. Kwa karne hii ambayo tunashuhudia ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, biashara mtandao ni fursa ambayo kila mfanyabiashara anatakiwa kuifahamu.

Dunia inahama kutoka kwenye mifumo ya kuuza na kununua kwa kutumia pesa taslimu na kuelekea kwenye malipo kwa njia mtandao.

Ni rahisi kufanya biashara mtandaoni maana wakati mwingine siyo lazima uwe na mtaji, siku hizi kuna watu wanaingiza pesa nyingi kwa kutangaza bidhaa za watu wengine (wamiliki wa maduka) na kisha kuuza mtandaoni na kurejesha halali ya mmiliki wa duka.

Pia, ni rahisi kuuza ujuzi au maarifa uliyonayo kupitia njia ya mtandao. Mfano, unaweza kuendesha semina au programu za mafunzo na kuziuza kwa njia ya makundi ya WhatsApp au majukwaa mengine. 

NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.


JIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.