Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 45 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako uyatumie
kubadilisha kila sekta ya maisha yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio
yangu kuwa muda ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada
mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako.
Hata hivyo, mtandao huu unahitaji
maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako (tuma
maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “How To Think Like Leonardo da Vinci” kutoka kwa mwandishi Michael
J. Gelb. Mwandishi anatumia kitabu hiki kwa ajili ya kutushirikisha kanuni
ambazo Leonardo da Vinci alizitumia katika maisha yake. Leonardo da Vinci
alikuwa ni Muitalino ambaye aliishi miaka 67 kati ya mwaka 1452 hadi 1519.
Katika kipindi cha umri wake Leonardo aliishi maisha ya mafanikio ambayo
yalijengwa juu misingi na kanuni mbalimbali.
Kanuni
hizi zilimfanya da Vinci kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa kwenye fani
mbalimbali kama vile uvumbuzi, uchoraji, uchongaji, usanifu, sayansi, muziki,
hisabati, uhandisi, fasihi, jeolojia, sayansi ya anga, botani, fasihi,
historia, na ramani.
Mara
nyingi da Vinci amekuwa akijulikana kama baba wa teknolojia na usanifu na kama
mmoja wa wachoraji na mtu mwenye akili sana wa wakati wote. Wakati mwingine
hujulikana kutokana na uvumbuzi wa parachute, helikopita na tanki.
Karibu
tujifunze machache kutoka kwa da Vinci kati ya mengi ambayo tumeshirikishwa
katika kitabu hiki:
1. Ubongo wako una akili/uwezo wa
hali ya juu kuliko unavyodhania. Mwandishi anatushirikisha kuwa kumekuwepo na
upotoshaji mkubwa wa aina mbili juu ya akili ya mwanadamu. Upotoshaji wa kwanza
ni ule unaodai kuwa akili ya mwanadamu inategemea jeni (genes) wakati wa
kuzaliana na akili hiyo haiwezi kuongezeka katika umri wa mwanada. Mwandishi
anatushirikisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa jeni zinachangia asilimia 48 tu ya
akili na asilimia 52 iliyobaki inapatikana kupitia malezi, elimu na mazingira
ambayo mwanadamu anapitia kipindi chote cha maisha yake.
2. Upotoshaji wa pili ni ile dhana
ya kwamba ujuzi wa hoja za hisabati na uwezo wa lugha kuwa unaweza kupimwa kwa
kipimo cha IQ (kipimo cha akili). Tafiti zinaonesha kuwa kila mmoja wetu ana
angalau uwezo wa akili ambao umegawanyika katika sehemu tofauti saba. Na kila
mmoja anaweza kufanikiwa katika sehemu zote hizo saba na zaidi kama ambavyo da
Vinci alifanikiwa. Sehemu hizo na mifano ya watu waliofanikiwa ni pamoja na;
Mantiki (logic) – uwezo wa hisabati, mfano, Isaac
Newton, Marie Curie;
Lugha (verbal) – uwezo wa lugha, mfano, William
Shakespeare;
Makenika – mfano, Buckerminster Fuller;
Muziki;
Mwili – uwezo wa matumizi ya viungo vya mwili,
mfano, Mohamed Ali;
Uwezo kujali wengine kwenye matendo ya kijamii –
mfano, Nelson Mandela; na
Uwezo wa binafsi – mfano, Mother Teresa.
3. Siyo kweli kwamba mtu akizeeka
na ubongo wake ndivyo unazeeka. Mwandishi anatushirikisha kuwa ubongo wa
kawaida unakuwa bora zaidi kadri umri unavyoongezeka kama endapo mhusika
ameweka jitihada za kuendeleza ubongo wake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
ubongo una nuroni (neurons) ambazo zina uwezo wa kutengeneza muunganiko wa vitu
vipya au mazingira mapya katika kipindi chote cha mwanadamu.
4. Kama
ambavyo makinda ya ndege anaiga mbinu za kukabiliana na maisha kutoka kwa mama
yao, binadamu pia anao uwezo wa kuiga mambo mazuri katika maisha yake.
Kufanikiwa katika kila sekta ya maisha yako unahitaji kuwa na walimu kwenye
sekta hizo ambao kwa namna moja au nyingine walifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa
maana nyingine unahitaji kuwa na ‘role
models’. Mfano, kama unahitaji kuwa kiongozi bora huna bora kujifunza
kutoka viongozi maarufu kama J.K Nyerere, Nelson Mandela na Winston Churchill.
Kama unahitaji kufanikiwa kwenye uvumbuzi huna budi kujifunza kutoka kwa
Leonardo da Vinci, Albert Einsten na wengineo.
5. Historia
ya mwanadamu imepitia kwenye mabadiliko mbalimbali ambayo kila kizazi
kinachoingia kinakuja na maboresha ya namna ya kurahisisha utendaji kazi pamoja
na kuboresha njia bora za mawasiliano. Mabadiliko haya ni lazima yawe na athari
chanya/hasi kwa kila binadamu ambaye bado anaishi pasipo kujali utashi wake.
Kiwango cha athari chanya/hasi kitategemea na jinsi mwanadamu ambavyo
amejiandaa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko yanayotokea. Uwezo wa
mwanadamu katika kujifunza na kukabiliana na mabadiliko kwa kutumia mfumo wa
fikra huru ni nyenzo pekee ya kumuokoa dhidi ya mabadiliko ya kila aina.
Leonardo aliishi kwenye matazamo wa namna hii na alitabiri juu ya mabadiliko
haya katika historia ya mwanadamu.
6. Kwa
ufupi historia ya maisha ya Leonardo da Vinci inaonesha kuwa mama yake alikuwa
mkulima wa kawaida na alimzaa kwa baba ambaye alikuwa hajafunga nae ndoa. Baba
yake alikuwa ni mhasibu, hata hivyo, kwa vile Leonardo alikuwa ni mtoto wa nje
ya ndoa alilelewa na babu yake mpaka pale ambapo alifikia umri wa kujitegemea.
Pamoja na changamoto zote hizo bado hazikuwa kikwazo kwa da Vinci kufikia
mafanikio makubwa kimaisha na kitaaluma. Mpaka anakufa katika umri wa miaka 67
bado da Vinci alikuwa na uwezo wa kuendelea kujifunza na aliomba msamaha kwa
“Mungu na wanadamu” kutokana na kuacha kazi nyingi ambazo zilikuwa hazikamilika
wakati umauti unamfikia.
Kanuni saba za
Leonardo da Vinci (Seven da Vincian Principles)
7. Kanuni ya kwanza: Udadisi. Kanuni
hii da Vinci aliitumia kwa ajili ya kuwa na kiu ya kujifunza mara zote katika
maisha yake. Kanuni hii ilisimama kama kanuni namba moja katika maisha yake kwa
kuwa hamu ya kufahamu, kujifunza au kukua inatakiwa kuwa kipaumbele namba moja
kwa ajili ya kuwa na maisha yenye ujuzi, hekima na ubunifu kwenye kila sekta.
Leonardo tokea akiwa mtoto alikuwa na kiu ya kujifunza mambo mengi zaidi ya
yale aliyofundishwa na walimu wake. Katika kujifunza huko mara zote hakuwa
tayari kukubali neno NDIYO au HAPANA kama jibu la kujitosheleza.
8. Akili
kubwa ni lazima mara zote iulize maswali makubwa. Maswali haya ni lazima
yahusishe mfumo mzima wa fikra na yajikite kwenye mazingira yanayotuzunguka
pamoja na uzoefu tulionao kwenye kila sekta ya maisha yetu. Hapa unahitaji kuwa
na fikra huru kwa ajili ya kuuchunguza ulimwengu huu na hatimaye kuweza kupanua
uelewa wako dhidi ya watu na vitu vinavyo kunzunguka. Kufanikisha zoezi hili ni
lazima kwanza ujenge tabia ya kutembea na kijitabu kidogo kwa ajili ya
kuhifadhi fikra zinazokujia pamoja na kuwa na muda wa kutafakari mawazo/fursa mbalimbali.
9. Kanuni ya pili: Vitendo. Kanuni hii ni maalamu kwa
ajili ya kutafsili ujuzi unaojifunza kwenye vitendo kwa kutumia uzoefu,
uvumilivu na utayari wa kujifunza kutokana na makosa. Hakuna sababu ya
kujifunza vitu ambavyo havitumiki katika maisha yako. Ni kutokana na msingi huu
da Vinci mara zote alitafsili kila alichojifunza kwenye vitendo bila kujali
kama ujuzi huo unaenda kinyume na mazoea au mtazamo wa watu kwa nyakati hizo. Hivyo,
mara zote da Vinci aliamini kuwa makosa ni sehemu ya kujifunza na hii ilimfanya
aamini kuwa uzoefu una nafasi kubwa katika mafanikio ya mwanadamu.
10. Kamwe hauwezi kuwa mtu wa vitendo kama
wewe ni mtumwa wa fikra/mtazamo wako. Mwandishi anatushirikisha kuwa sio mitazamo
yote tuliyonayo ni sahihi, Leonardo da Vinci alijaribu fikra/mitazamo yake kwa
vitendo. Pale ambapo aligundua kuwa hakuwa sahihi alikiri makosa na hatimaye
kutumia makosa hayo kama msingi wa kujisahihisha na kuboresha kwenye hatua
zinazofuata. Hapa unahitaji kufanya tathimini juu ya ukweli kwenye fikra,
mtazamo na imani ulizonazo kwenye kila sekta ya maisha yako. Tafuta vyanzo na malengo
ya imani au mitazamo husika katika kipindi chote cha maisha yako.
11. Jifunze kutokana na makosa ya watu
wengine. Mwandishi anatushirikisha kuwa mbinu nyingine ya kujifunza ni kuwa na
“role model” wa uongo. Hii ina maana kuwa unatafuta mtu ambaye amefanya makosa
kwenye kile unachohitaji kufanya na hatimaye unachambua makosa yake kwa ajili
ya kuboresha zaidi.
12. Kanuni
ya tatu: Hisia.
Milango yote ya fahamu ina mchango mkubwa katika uzoefu tulionao kwenye maisha
yetu ya kila siku. Leonardo da Vinci aliamini kuwa siri ya kuwa mtu wa vitendo
inatokana na matumizi ya milango ya fahamu hasa mfumo wa macho. Tunahitaji
kufahamu namna ya kuona vitu/watu wanaotuzunguka. Tunaweza kujifunza mengi kwa
kutumia macho kwani ni kupitia macho haya tunaweza kuhoji maswali mengi juu ya
yale tunayo tazama. Ni kutokana na mtazamo huu da Vinci aliamini kuwa yeyote
anayepoteza uwezo wa kuona anakuwa amepoteza mwonekano wa ulimwengu. Macho
yanabeba uzuri wote wa ulimwengu huu hivyo ni wajibu wetu kuyatumia vyema.
13. Baada ya kuona mlango mwingine wa
fahamu unaofuatia kwa umuhimu kulingana na da Vinci ni kusikia. Hapa ndipo
tunaona kuwa da Vinci pamoja na kuwa mchoraji mzuri (kutumia mlango wa kuona)
alikuwa pia ni mwimbaji mzuri. Hivyo, aliona kuwa muziki una nafasi kubwa
katika kufundisha au kupotosha jamii. Kwa ujumla wake da Vinci aliamini kuwa milango
yote ya fahamu (kuona – macho, kusikia – masikio, kugusa – ngozi, kunusa – pua
na radha/kuongea – ulimi) ina nafasi kubwa ya kumfanya mhusika atambue nafasi
yake na muumba wake kwa maana ya muunganiko wa roho na mwili.
14. Tengeneza uhusiano kati ya mlango wa
fahamu wa kugusa na mfumo wa hisia. Leonardo alishangaa sana kuona kuwa kuna watu
wanagusa vitu pasipo kuwa na hisia juu ya kile wanachogusa. Siri kubwa ya
mlango wa fahamu wa kugusa ni kutambua kuwa unaweza kujifunza kutafsili kila
kitu kwa kutumia mikono na mwili mzima. Chochote unachogusa tengeneza hisia
kana kwamba ndo mara ya kwanza unakigusa.
15. Kanuni
ya nne: Kabiliana na giza. Kanuni hii inalenga kwenye utayari wa
kukabiliana na mazingira, vitendo au hatua zenye utata, utayari wa kutegeua
vitendawili kwenye maisha au utayari wa kuchukua hatua sehemu ambazo huna
uhakika. Kadri unavyoendelea kudadisi na kutenda kwa kutumia uzoefu na milango
yako ya fahamu unatafikia sehemu ambayo uelewi kilichopo mbele yako au ni hatua
zipi unatakiwa kuchukua. Katika hali kama da Vinci alihakikisha anaruhusu fikra
huru katika kichwa chake kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi ambazo wakati
mwingine zinaweza kuwa hatarishi. Kanuni hii inapima ujasiri wetu wa kuchukua
hatua katika mazingira mapya.
16. Kuwa na muda wa kupumzika kwa ajili ya
kutafakari juu ya yale ambayo unaona ni magumu kwako kwa wakati huo. Mwandishi anatushirikisha
kuwa tafiti zinaonesha kuwa watu wengi wanapata majibu ya changamoto
zinazowakabili wakati wa mapumziko. Hivyo, ambapo unaona kuwa kichwa kimegoma
kusonga mbele pata muda kwa ajili ya kupumzika ili utafakari kwa kina.
17. Kanuni
ya tano: Sanaa/Sayansi. Kanuni hii inalenga kuhakikisha
unakuwa na mlinganyo kati ya sayansi na sanaa au kati ya mantiki na mawazo. Hii
ina maana kwamba unahitaji kushughulisha ubongo wako kwa kuhusisha ujuzi kutoka
pande zote pindi unapofikri. Tafiti zinaonesha kuwa ubongo wa mwanadamu
unagawanyika katika sehemu mbili ambazo ni, sehemu ya kushoto ambayo
inajihusisha na fikra za kichambuzi (analytical thinking) na sehemu ya kulia
ambayo inajihusisha na kufikiri kwa mapana (big picture thinking). Sehemu ya
kushoto inajihusisha na kufikri kwa uchambuzi wa hatua kwa hatua kwa maana
nyingine ni sehemu inayojihusisha na sayansi wakati sehemu ya kulia
inajihusisha na kufikiri kwa mapana juu ya mada husika na hivyo ni sehemu
inayojihusisha na sanaa. Leonardo da Vinci anatufundisha kuwa mara zote tunahitaji
kutumia sehemu zote za ubongo katika kutatua changamoto za maisha yetu ya kila
siku. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ni vigumu kusema kuwa da Vinci alikuwa
msanii kwa maana ya sanaa zake za michoro au kusema alikuwa mwanasayansi kwani
sehemu zote mbili alizitumia katika kazi zake.
18. Kama mzazi au mwajiri unahitaji
kutambua watu wako ambao wanatumia ubongo wa kulia na wale ambao wanatumia
ubongo wa kushoto. Mfano, kama wewe ni mzazi husioneshe kupendelea mtoto ambaye
anafanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi ukilinganisha na yule ambaye
labda anafanya vizuri kwenye masomo ya sanaa. Unahitaji kutambua tofauti
zilizopo katika yao na hivyo kama mzazi hakikisha wote unawapa mlinganyo sawa.
19. Kanuni
ya sita: Ujasiri na utimamu wa mwili. Hapa mwandishi
anatushirikisha kuwa kanuni hii da Vinci aliitumia kwa ajili ya kuwa na afya
bora iliyotokana na mazoezi ya viungo. Hali hii ilimfanya da Vinci kuwa mtu
hodari kwenye kutembea bila kuchoka, kuogelea, kuendesha bike au mazoezi
mengine ya viungo. Leonardo aliamini kuwa kuzeeka kwa kasi ni matokeo ya mwili
kukosa mazoezi ya kutosha na hivyo alihakikisha anatumia viungo vya mwili wake
kwa ajili ya kuwa imara zaidi. Mfano, katika kuchora michoro yake alihakikisha
anatumia mikono yote miwili kama sehemu ya kuimarisha sehemu zote za mwili wake.
20. Jifunze kutunza afya yako. Leonardo
aliamini kuwa tunapaswa kukubali majukumu yetu kama sehemu ya kuimarisha au
ustawi wa afya zetu. Mtazamo wake juu ya ugonjwa ulikuwa ni “ugonjwa
unasababishwa na hali ya kupingana kwa ‘seli’ za mwili ambako usababishwa na
mhusika na hivyo njia ya pekee ya kupona ugonjwa husika ni mhusika kuondoa hali
hiyo katika mwili wake”. Baadhi ya njia ambazo da Vinci alihamasisha kama
sehemu ya kuepuka magonjwa ni mazoezi mepesi, vyakula sahihi, pendelea mboga za
majani, tumia vinjwaji sahihi na usinywe pombe kama haujala kitu, jifunike
vizuri wakati wa usiku, epuka kuwa na hasira/manunguniko, epuka matumizi mengi
ya sukari na chumvi, pendelea vyakula vya asili ambavyo vimepikwa kiasili zaidi
(epuka viungo), kuwa na muda wa kupuzika, nenda chooni mara kwa mara na tafuna
chakula vya kutosha. Binafsi nimezipenda
hizi sijui wewe nipe mrejesho wako……..
21. Kanuni
ya saba: Uhusiano. Kanuni hii da Vinci aliitumia kwa ajili ya
kutambua na kuheshimu uhusiano wa vitu/matukio yote ili kutoa nafasi sawa kwa
pande zote. Kanuni hii inahusisha umuhimu wa kufikiri kimfumo zaidi badala ya
kujikita kwenye kitu/tukio moja na kuacha vitu/matukio mengine. Kila kitu au
kiumbe kwenye mazingira yanayotuzunguka kina umuhimu wake kwa ajili ya ustawi
wa vitu au viumbe wengine. Kila kiungo kwenye mwili wako kina uhusiano mkubwa
na viungo vingine kwenye mwili wako. Hapa ndipo da Vinci alisoma uhusiano wa
viungo vya mwili kama kiungo kimoja au aliheshimu mazingira kutokana na kila
kitu kilichopo ndani yake.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha
dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha
haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com