Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 39 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako
kuyatumia ili ubadilishe kila sekta ya maisha yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio
yangu kuwa muda ninaotumia kushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada
mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, mtandao huu bado
unahitaji maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako au
namna ambavyo unahitaji makala hizi ziboreshwe zaidi (tuma
maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu cha wiki hii ni “Primary Greatness” kutoka
kwa mwandishi mahiri Stephen R. Covey. Stephen Covey ni mwandishi, kiongozi,
mshauri, mwalimu na kocha wa mafanikio mahiri katika ngazi ya kimataifa.
Mwandishi ameandika vitabu vingi ambavyo vimekuwa vikifanya vyema kwenye soko
na mojawapo ya vitabu hivi ni The Seven
Habits of Highly Effective People. Kitabu hiki kimetajwa kama kitabu namba
moja katika kuhamasisha watu kwenye karne hii ya 21.
Mwandishi
anatushirikisha kuwa kuna njia mbili za kuishi; njia ya kwanza ni maisha
yaliyojikita kwenye mafanikio ya misingi halisi ya nafsi yako (Primary
greatness). Misingi hii ni ya kipekee kwa kila mtu na inajumuisha tabia,
uaminifu, uadilifu, shauku na matamanio yako ambavyo vyote hivi vinaanzia ndani
mwako. Njia ya pili ni mfumo wa maisha yanayotokana na mafanikio yako ambayo
hasa yamejikita kwenye misingi ya kidunia (Secondary greatness). Maisha haya
yanatokana na mafanikio yako kupitia kwenye cheo chako, jina lako, umaarufu
wako pamoja na heshima uliyonayo kwenye jamii inayokuzunguka.
Mwandishi
anatushirikisha kuwa kama unahitaji maisha ya mafanikio makubwa ni lazima
uzingatie njia ya kwanza kwa maana ya kuishi misingi halisi ya nafsi yako.
Unapoishi misingi halisi ya nafsi yako ni rahisi kufanikiwa katika njia ya pili
ya mfumo wa maisha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba misingi halisi ya nafsi yako ina tabia ya kumzawadia kila mmoja anayeiishi kwa kadri inavyotakiwa.
Zawadi
zinazotolewa na mfumo wa maisha unaozingatia misingi ya nafsi yako ni pamoja na
kuwa na amani ya roho, hekima, busara, furaha, kujiamini, kusaidia wengine
pamoja na mahusiano mema dhidi ya watu wako wa karibu. Zawadi hizi zote kwa
pamoja ni zaidi ya zawadi zinazotolewa na aina ya pili ya mfumo wa maisha kama
vile vyeo, fedha, umaarufu, hanasa pamoja na ubinafsi.
Katika
maisha mafanikio ambayo yamejikita kwenye aina ya pili ya mfumo wa maisha ni
sawa na nyumba ambayo imejengwa juu ya mchanga ambayo ni wazi kamwe haiwezi kudumu ni lazima
itaporomoka tu.
Karibu
tujifunze namna ya kuishi maisha yaliyojikita kwenye misingi ya nafsi zetu:
1. Kila mtu anaishi katika pande
tatu za maisha; upande wa kwanza ni maisha ya wazi dhidi ya jamii
inayokuzunguka (public life), upande wa pili ni maisha binafsi (private) na
upande wa tatu ni maisha ya siri (secret life). Maisha ya siri ndipo roho yako
ilipo na ni kupitia maisha haya unaweza kugundua/kujiuliza shauku/matamanio ya
maisha yako. Maisha haya ya siri kwa ujumla ni ufunguo wa kuishi maisha yenye
mafanikio ya misingi halisi ya nafsi yako (primary greatness). Hata hivyo, ili
kufikia misingi halisi ya maisha yako ni lazima uwe tayari kujikana kutoka kwenye
mitazamo ya jamii inayokuzunguka.
2. Maisha ya siri yanajengwa
kupitia tathimini binafsi ya nafsi yako. Tathimini hii ni lazima ijikite kwenye
uthibitisho wa nafsi. Sifa kuu za uthibitisho wa maisha ambazo
zinaweza kutumika kama mwongozo ni:
v Ni lazima uwe uthibitisho huo uwe chimbuko la nafsi
yako kwa maana ya kwamba sio wa kuiga kutoka kwa wengine;
v Ni lazima uwe katika hali ya
uchanya badala ya kuwa hasi. Kwa maana ya kwamba ni lazima unene yaliyo mema
badala ya mabaya juu ya nafsi yako;
v Ni lazima ujengwe katika hali
ya usasa au wakati uliopo kwa maana hisitoria ya maisha yako haina nafasi
katika maisha yako ya sasa na ya nyakati zijazo;
v Ni lazima uwe na maono, kwa maana
unaweza kuutafsiri kwa picha katika mfumo wako wa milango ya fahamu; na
v Ni lazima uwe na hisia, kwa
maana ni lazima uwe na muunganiko mkubwa wa kihisia.
3. Tabia yako kwa maana ya jinsi
ulivyo ni muhimu kuliko uwezo ulionao kwa maana ya uwezo wako kiutendaji. Hii
ina maana kwamba kama unahitaji kuboresha uwezo wako kiutendaji ni lazima
kwanza uwe tayari kubadilisha tabia zako ili ziendane na shauku/matamanio yako ya kiutendaji. Kwa maana nyingine, tabia ni msingi wa kufanikisha kila kitu katika
maisha yako. Hata hivyo, msingi huu unajengwa na ujasiri, uvumilivu pamoja na
staha. Vyote hivi kwa pamoja vinapelekea ukuaji wa kihisia (emotional maturity)
kwa muhusika ambavyo pia ni msingi wa maamuzi yote ikiwa ni pamoja na mahusiano yako.
4. Kwa asili kila kiumbe au kila mwanadamu ni lazima
aongozwe na kanuni au sheria za asili. Kutokana na ukweli huu kila mwanadamu ni
lazima awe tayari kuishi kulingana na kanuni au sheria za asili kwenye kila
sekta ya maisha yake. Kanuni au sheria hizi za asili hazibadiliki mara kwa mara
au kutoka sehemu moja hadi nyingine (there are universal). Pia kanuni/sheria hizi
zimekuwepo vizazi na vizazi hivyo zinauongoza ulimwengu kwa ujumla wake na
hivyo kwenda kinyume na sheria hizi ni sawa na kupoteza muda wako.
Unachotakiwa kujifunza hapa ni kwamba hauwezi kuishi maisha yenye
mafanikio ya nafsi yako halisi kama hauna kanuni au sheria zinazokuongoza.
Unahitaji kujiwekea kanuni binafsi ili ziwe mwongozo wa maisha yako ya kila
siku. Hii ni pamoja na kuainisha yapi lazima yafanywe na wewe na yapi hautakiwi
kufanya. Haya kwa pamoja ndiyo yataamua tabia zako na hivyo kuboresha utendaji
wako wa kazi.
5. Binadamu
wote tumepewa zawadi kuu nne ambazo ni kujitambua (self awareness), uwezo wa
kutambua jema na baya (conscience), utashi wa kujitegemea (independent will)
na mawazo ya ubunifu (creative imagination).
Kupitia zawadi
ya kujitambua kila mwanadamu anaweza kutathimini dhana/misingi yake
kwenye ulimwengu unaomzunguka na hivyo anaweza kurudi kwenye misingi ya nafsi
yake katika ulimwengu huu kupitia zawadi hii.
Kupitia uwezo
wa kutambua mema na mabaya tunapata muunganiko wa nafsi zetu dhidi ya
mazingira ya nje kwa maana ulimwengu unaotuzunguka. Na hapa ndipo utagundua
kuwa daima nafsi zetu zinatuvuta kwenye matendo mema wakati ulimwengu unavutia
kwenye matendo ya ulimwengu ambayo yanakinzana na nafsi.
Kupitia utashi wa kujitegemea ndipo tunapata uwezo wa kutenda. Ni kupitia uwezo huu
kila mwanadamu anaweza kuamua hatima ya maisha yake kwa kuamua ni matendo yapi anaweza kufanya ambayo awali hakutarajia kama anaweza kuyafanikisha.
Kupitia mawazo
ya ubinifu kila mwanadamu amepewa mamlaka ya kushinda historia ya
utumwa wa maisha yake. Hii ina maana kwamba kupitia zawadi hii mwanadamu
anaweza kuwa na maono makubwa juu ya nafsi yake na hivyo anaweza kupanga
mipango mikubwa kwa ajili ya mafanikio ya kila sekta ya maisha yake.
6. Unahitaji
daima kuishi kwenye misingi ya nafsi yako halisi ili ufanikishe matamanio ya
maisha yako. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanashindwa kufikia
kusudi la maisha yao kwa vile wanayumbishwa na mawimbi pindi wanapokuwa njiani.
Baadhi ya mawimbi ambayo ni hatari kwa kila mtu ni tamaduni – kadri mtu
anavyohama kutoka sehemu moja hadi nyingine ndivyo mabadiliko ya tamaduni
yanavyotokea na hivyo kupelekea kuyumba kwa muhusika kwenye misingi ya nafsi
yake. Pia, hisia kali ni wimbi jingine ambalo linahatarisha mtu kuishi misingi
ya nafsi yake – daima unahitaji kuzishinda hisia zako kwenye maamuzi au
mazingira unayopitia kwenye kila hatua ya maisha yako.
7. Imani
tulizonazo juu ya ulimwengu na vyote vilivyomo ndizo zinatufanya tuonekana
jinsi tulivyo. Imani hizi ndizo zinatufanya tuonekane wafungwa wa akili kiasi
kwamba zinatuzuia kuishi misingi halisi ya nafsi zetu na hivyo kushidwa kuishi
maisha yanayoongozwa na kanuni maalumu. Kutokana na kufungwa na imani hizi
tunashindwa kuona mwanga na tumaini jipya katika maisha yetu. Hali hii
inasababishwa na vikwazo vikuu ambavyo ni pamoja na (a) utumwa wa hisia
(emotional imprisonment) – hisia hizi zinatufanya kujiona wema ukilinganisha na
wale wanaotuzunguka; (b) ugonjwa wa kutafuta makosa pekee – ni kawaida kwa watu
wengi kutafuta makosa badala ya kutafuta yaliyo mema kutoka kwa wengine. Kabla
kuangalia makosa (kibanzi) ya wengine unahitaji kwanza kuondoa vibanzi
vilivyopo ndani mwako; (c) utumwa wa mara zote kuona uachache (scarcity) katika
kila hali/tukio au rasilimali – ukiwa na mtazamo wa uchache daima utaendelea
kuamini kuwa hauwezi kufanikisha matamanio yako kwa sababu ya uchache huo.
Kukabiliana na hali hii unahitaji kuwa na mtazamo wa ushindi kwa pande zote –
win win situation; (d) kushindwa kulinganisha majukumu yetu – hii ni kanuni ya
asili ambayo inatutaka kuhakikisha tunakamilisha majukumu yetu kwa uwiano. Kwa
maana ya kwamba usizame kwenye jukumu moja na kusahau mengine.
NYENZO 12 ZA MAFANIKIO
8. Nyenzo ya kwanza: Uadilifu.
Uadilifu ni hali ya kuishi kwa kufuata na kulinda misingi ya kanuni
ulizojiwekea katika maisha yako. Uadilifu ni hatua ya kwanza ya kuishi maisha
yenye misingi ya nafsi yako (primary greatness) na mtu anayeishi pasipokuwa na
kanuni zozote zinazoongoza maisha yake ni sawa na kwamba tayari ameyapoteza. Maisha
yenye uadilifu kwa ujumla wake ni maisha yanayozingatia maadili mema katika
jamii na maisha haya yanazingatia vitu kwa ujumla wake. Hii ina maana kwamba
hautakiwi kuchagua kuwa na maadili mema katika sehemu moja na kuacha sehemu
nyingine bali kila sekta ya maisha yako inatakiwa iongozwe na uadalifu. Watu
ambao wamepoteza uadilifu wanaishi maisha ya kuigiza huku wakiogopa mtazamo wa
jamii kuliko kuogopa kwenda kinyume na kanuni halisi za nafsi zao.
9. Uadilifu
unajengwa na mihimili miwili ambayo ni unyenyekevu pamoja na ujasiri. Mtu
mnyenyekevu ni lazima aongozwe na misingi ya kanuni au sheria kwa utashi
wake bila kuogopa nguvu za jamii inayomzunguka. Kwa maana hii mtu mnenyekevu
anatambua kuwa kanuni na sheria za asili ndizo zenye mamlaka katika ulimwengu
huu na hivyo anachotakiwa kufanya ni kuishi kwa kufuata kanuni au sheria hizi
kwa faida ya nafsi yako. Muhimili wa pili ni ujasiri, ujasiri ndio unampima mtu
namna anavyokabiliana na maamuzi yake pindi anapokuwa katika hali ya majaribu
au anapokabiliwa na changamoto. Katika kipindi hiki ni muda muafaka wa kumpima
mtu kama atasimama imara kwenye misingi ya kanuni au sheria za asili
zinazomuongoza.
Matunda ya uadilifu
kwa muhusika ni busara na hekima, wingi wa fikra pevu na chanya, uwezo wa
kufanya kazi ukiongozwa na utashi, ushindi kwa kila mwanatimu, na
uaminifu kutoka kwa wote wanaokuzunguka.
10. Nyenzo
ya Pili: Utashi wa kujitoa kwa ajili ya wengine. Maisha
ya mafanikio yenye misingi halisi ya nafsi yako ni lazima yawe na nia thabiti kwa
ajili ya kuwasaidia wengine kupitia vipaji au kalama ambazo umejaliwa. Muda
wote unahitaji kujiuliza ni kipi naweza kuchangia kwa ajili ya kuwanufaisha
wengine badala ya kufikiria kunufaisha tu nafsi yako. Unahitaji kujifunza mara
kwa mara kwa ajili ya kutambua wewe ni nani na umeumbwa kwa ajili ya
kukamilisha kazi ipi katika ulimwengu huu. Muda wote unahitaji kujiuliza
maswali matatu; (a) Je ulimwengu unataka nini kutoka kwangu? (b) Je mimi ni
mzuri katika sekta au kazi ipi? na (c) Je nawezaje kufanya vyema kwenye kazi
nizipendazo katika sehemu yangu ya kazi na hatimaye kufanikisha matakwa ya
wadau wangu?.
11. Kabla ya kufikiria kuwaongoza wengine
unahitaji kwanza kujiongoza mwenyewe. Hii inamaanisha kwamba unahitaji
kubadilisha sehemu zote za maisha yako ambazo zinaenda kinyume na uadilifu
ambao ndio unabeba maadili mema. Jikomboe kwanza kabla ya kufikiria kuwakomboa
wengine, huu ndio msingi wa kujitoa kwa ajili ya wenzako. Hapa unahitaji kwanza
kubeba majukumu ya maisha yako badala ya kutegemea mtu flani atahusika nayo –
hii inaondoa nafasi ya kuwalalamikia wengine bali unapaswa kulaumu mwenyewe
pale unaposhindwa kufikia malengo; pili, ni lazima uwe tayari kulipa gharama
kwa ajili ya kuwa mtu yule unayetamani kuwa (mwadilifu); tatu, unahitaji
kuendelea kuishi misingi ya kanuni za maisha yako kila wakati na kila sehemu;
na nne, unahitaji kuelekeza akili kwa ajili ya kuishi misingi halisi ya nafsi
yako katika kipindi chote cha maisha yako.
12. Nyenzo
ya tatu: Kipaumbele.
Kubadilika kutoka katika mafanikio ya kidunia (secondary greatness) kwenda
kwenye mafanikio ya msingi halisi wa nafsi yako (primary greatness) ina maana
kuwa vile vitu ulivyozoea kuvipa kipaumbele cha kwanza sasa vinatakiwa kupewa
nafasi ya mwisho katika mrorongo wa vipaumbele vyako. Katika maisha yenye
msingi halisi wa nafsi yako huna budi kutanguliza vipaumbele kama vile maisha
yako, afya bora, ukuaji wa kiroho, kiakili, mahusiano, familia yako pamoja na ukuaji
wa kiuchumi badala ya kutanguliza vipaumbele ambavyo vimejikita kwenye raha za
muda. Kufanikisha vipaumbele hivi unahitaji kujiuliza vipawa ambavyo umejaliwa
kiasi kwamba kadri unavyotumia vipawa hivyo ndivyo unaishi maisha ya furaha
yenye chimbuko kutoka ndani mwako. Hata hivyo, ni muhimu hakikisha kila
kipaumbele kwenye mtiririko wako kinatekeleza kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na
kutekeleza kila jukumu kwenye mrorongo wa vipaumbele vyako kwa kuzingatia
uharaka wake (keep the first things first).
13. Badilisha mfumo wa kutegemea saa kama
mwongozo wako na badala yake uongozwe na dira (compass). Saa inaweza kuwa na
nafasi yake kama tayari umefanikiwa kuwa na ufanisi katika vipaumbele vyako
lakini kama bado hauwezi kusimamia vipaumbele vyako ni vyema ukatumia mfumo wa
dira. Hii ni kutokana na ukweli kwamba dira ni alama nzuri ya ufanisi kwa vile
muda wote inaonesha mwelekeo – hii katika maisha ya kawaida ni sawa na kusudi,
maono, mtazamo pamoja na usawa. Kama compass (daima haiwezi kupoteza mwelekeo),
uwezo wako wa kutambua mema na mabaya unakuweka kwenye nafasi ya kujibana
kwenye mema tu kila mara unapowaza mabaya. Kutoka kwenye kutumia saa kama
mwongozo hadi kutumia compass unahitaji kuacha kutumia ratiba kama ulivyozoea
na badala yake utumie vipaumbele. Mfano, ratiba inaweza kuonesha kuwa kuna
kikao sehemu flani lakini haiwezi kukuonesha kama kikao hicho ni muhimu kwako.
14. Nyenzo
ya Nne: Jitoe sadaka.
Maisha yenye mafanikio halisi ya nafsi yako yanategemea kufanya kazi kama timu
na wenzako. Maisha haya hapa yanaongozwa na kanuni kuwa kazi inakuwa bora zaidi
pale tunapofanya kazi kama timu kuliko kila mmoja akifanya kivyake. Ni kupitia
shauku ya kujitoa kila mwanadamu anaweza kuunganika na wenzake na muunganiko
huu ni unajengwa na misingi ya mapenzi mema juu ya wengine, fadhira/wema,
unyenyekevu, heshima, uvumilivu na msamaha. Nyenzo ya kujitoa ni muhimu katika
kukuza mahusiano kati ya baba/mama/watoto, ufanisi kazini pamoja na mahusiano
kati ya mteja na mfanyabiashara.
15. Nyenzo
ya Tano: Huduma. Kuwa
tayari kutoa huduma hata kama ni kwa ngazi ya chini kwani katika watu kitu
unachokiona kidogo kwa wengine kinaonekana kikubwa zaidi. Hata hivyo, mzigo
mkubwa ambao unazuia watu kusonga mbele kwenye nyenzo hii ni tabia ya uchoyo.
Katika kutoa huduma unahitaji kuwa tayari kujikana kwa ajili ya wengine pasipo
kujali kama unawafahamu au hawakufahamu. Jukumu lako kubwa ni kutoa thamani kwa
wengine ili hatimaye ubarikiwe kupitia mafanikio ya unaowagusa.
16. Nenzo
ya Sita: Wajibu. Kukubali wajibu wako ni muhimu katika
kufikia mafanikio yenye misingi halisi ya nafsi yako. Ni muhimu kila mmoja
kutekeleza wajibu wake katika hali zote japokuwa changamoto kubwa ni pale
ambapo mambo hayaendi kama inavyotakiwa. Katika nyakati hizo ndipo watu
wanaanza kulaumu wenzao au mazingira yaliyopelekea badala ya kuanza
kujitathimini wao. Katika mafanikio ya maisha halisi ya nafsi yako unahitaji
kutambua kuwa wewe ni muhusika mkuu wa maisha yako kupitia maamuzi yako na wala
sio mzazi, serikali, jamii au mazingira yanayokuzunguka. Nyenzo hii ya wajibu
unatakiwa kuitumia katika kila hali au tukio; unahitaji kujiuliza wajibu wako
ni upi kwenye hali/tukio husika. Hivyo unaweza kutumia nyenzo hii kwa gharama
yoyote ile ili kuponya makovu ya mahusiano yako na watu wanaokuzunguka.
17. Nyenzo
ya Saba: Uaminifu. Watu
wenye mafanikio kwenye maisha ya halisi ya nafsi zao ni waaminifu na mara zote
sio watu wa kusengenya au kuongea uongo dhidi ya wenzao. Mtihani mkubwa kwa
watu walio wengi ni kuwa waaminifu kwa wenzao pindi wanapokuwa hawapo pamoja. Badala
kulalamika kwa mtu ambaye hayupo ni vyema kumfuata au kuwasiliana nae kwa ajili
ya kutatua suala ambalo unaona hajatekelezwa ipasavyo. Kulalamika bila kuchukua
hatua ni sawa na kwamba na wewe umehusika kwenye tatizo lililopo. Hali hii ni
muhimu kwa kila mtu ambaye ana kiu ya kuishi maisha halisi ya nafsi yake kwani
kuwaongea watu vibaya bila ya uwepo wao unatafsiliwa vibaya na jamii
inayokuzunguka. Wengi wanaweza kukuona kama vile unatafuta umaharufu,
unajifanya uonekane bora au unajifurahisha kupitia migongo ya watu wengine.
18. Nyenzo
ya Nane: Usawa (win win situation). Kanuni ya usawa ina
nafasi kubwa katika mafanikio ya maisha yaliyojengwa kwenye misingi halisi ya
nafsi yako kutokana na ukweli kwamba kanuni hii inaeleza kuwa kile unachotoa
kitarudi kwako katika hali nyingine pasipo ufahamu wako. Kutokana na kanuni hii
watu wenye mafanikio katika maisha halisi ya nafsi yao wanaishi katika kauli
mbiu ya kuwa “hakuna mafanikio katika
maisha endapo wengine hawajafanikiwa”. Wale wanaoishi kwa ajili ya
mafanikio ya kidunia kaulimbiu yao kubwa ni “nitapata nini kutokana na kazi hii?” Kanuni hii ni muhimu katika
kila sekta ya maisha yetu kuanzia kwenye mahusiano yetu katika familia, sehemu
za biashara na hata kwenye sehemu ya kazi. Inapotokea kuwa kila mmoja katika
pande mbili akatambua umuhimu wa ushindi kwa mwenzie inakuwa rahisi kufanya
kazi husika kwa roho moja na hivo kila mmoja anaridhika kwa nafasi yake jambo
linalopelekea mafanikio makubwa sana kwa pande zote.
19. Kufanikisha nyenzo hii ya usawa katika
maisha yako mwandishi anatushirikisha baadhi ya mbinu;
v Kwanza
jitathimini na kuwa mkweli juu matakwa na nafsi yako – hapa unahitaji kubadilisha
tabia ambazo zimekuwa zinakufanya uhitaji faida kubwa ikilinga kutoka kwa
wengine. Jiulize kama wewe ndo ungekuwa upande wa pili ungejisikia vipi?;
v Hakikisha
kuna muunganiko mkubwa katika yako na upanda wa pili – muunganiko huu uwe zaidi
ya kile ambacho mnahitaji kutekeleza. Kama ni mteja jenga urafiki zaidi ya
biashara ambayo huwa mnafanya ili mteja aone kuwa unamjali na uelewa wa manufaa
ya bidhaa/huduma yako kuliko yeye;
v Badilishana
ujuzi na taarifa kati ya pande zote mbili; na
v Husisha
matakwa ya wadau wote pasipo kupendelea mdau mmoja katika timu husika.
20. Nyenzo
ya Tisa: Utofauti/Mchanganyiko (diversity). Watu wenye
mafanikio ya chimbuko halisi la nafsi yao muda wote wanahitaji kujichanga na
watu wa aina mbalimbali. Muda wote nia yao ni kujifunza kutoka kwenye kila
kundi la watu kwa ajili ya kuendelea kuboresha uelewa wao na huduma zao pia.
hii ni kutokana na ukweli kwamba pasipo kujichanganya na watu wengine hawawezi
kupata timu/netiweki ya watu na bila mtandao wa watu hakuna kipya wanaweza
kutekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu. Watu wengi wanapenda kujichanganya watu
wanaofahamu jambo linawafanya wanaendelea kuwa na marafiki walewale au uelewa
uleule siku hadi siku.
21. Nyenzo
ya Kumi: Kujifunza (Learning). Mafanikio yenye chimbuko la
nafsi yako halisi muda wote yanahitaji uwe kwenye kujifunza kwa ajili ya
maarifa mapya. Kujifunza ndio njia pekee ambayo itakuwezesha kufahamu makusudi
ya uwepo wako hapa duniani na wajibu wako ni upi katika kuifanya dunia iwe
mahala pazuri kwa kila kiumbe. Mtu ambaye hajifunza ni rahisi kupoteza maisha
yake kwa kuangaikia mambo ya dunia hii ambayo mara nyingi uishia kwenye majuto.
Elimu hii unayoipata inatakiwa kujikita kwenye kila sekta ya maisha yako kwa
ajili ya kukua zaidi ya ulivyo sasa. Unahitaji kujifunza namna ya kuwa mme/mke
bora, baba bora, mfanyakazi/mfanyabiashara bora ikiwa ni pamoja na ukuaji wa
kiroho.
22. Nyenzo
ya Kumi na Moja: Kuuhishwa (Renewal). Kamwe hauwezi kupata mafanikio ya chimbuko la nafsi yako wewe ni mtu wa
kuikataa nafsi yako, afya yako, akili yako, hali yako ya kiroho au hisia zako. Kwa
ujumla unahitaji kwanza uponye makovu yote ambayo yamekuwa yakikuzuia kusonga
mbele kwa ajili ya maisha mapya. Uihishwaji unatakiwa ufanyike kwenye kila
sekta ya maisha yako pasipo kujali historia ya maisha yako. Unahitaji kuponya
historia yako katika masuala ya kiroho, mahusiano, kazi, kijamii na kiuchumi. Kumbuka
kuwa kuanguka sio mwisho wa safari.
23. Nyenzo
ya Kumi na Mbili: Kufundisha. Mpaka sasa umejifunza
nyenzo kumi na moja kwa ajili ya kufanikisha maisha yenye chimbuko la nafsi
yako halisi. Njia rahisi ya kuendelea kukumbuka kitu chochote ulichojifunza ni
kuwafundisha wengine, kwa kadri unavyofundisha wengine ndivyo na wewe unakuwa
bora zaidi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba njia rahisi ya kujifunza kitu
kupitia kufundisha topic husika. Unapofundisha inakusaidia (a) kupata taarifa/maarifa
husika kwa undani (b) kuongeza uelewa wako kwenye maarifa husika; na (c)
kufanikisha ukuaji wa wengine.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com