Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 41 katika kipindi cha mwaka 2017 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kukupa maarifa ambayo ni wajibu wako uyatumie
kubadilisha kila sekta ya maisha yako.
Makala hizi za uchambuzi wa vitabu
zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa kukushirikisha
kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu vya maarifa mbalimbali. Ni matarajio
yangu kuwa muda ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada
mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako. Hata hivyo, mtandao huu bado
unahitaji maoni/ushauri au shuhuda kwa namna ambavyo umekuwa wa msaada kwako au
namna ambavyo unahitaji makala hizi ziboreshwe zaidi (tuma
maoni/ushauri/ushuhuda wako kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com).
Ili uendelee kunufaika na makala za
mtandao huu BONYEZA HAPA na
ujaze fomu kisha bonyeza “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “I Declare 31 Promisies To Speak Over Your Life” kutoka
kwa mwandishi na mzungumzaji mahiri Joel Osteen. Joel ni Mchungaji Mkuu wa
Kanisa la Lakewood Church lililopo Huston, Texas nchini Marekani. Amekuwa muhubiri,
mwandishi, kiongozi na mhamasishaji kwa watu wa rika mbalimbali kupitia kazi
zake. Kupitia kanisa lake pekee kwa wiki linapata wahumini wasiopungua 45,000.
Joel Osteen ana video za mafundisho mbalimbali ambazo unaweza kuzipata bure
kabisa kupitia mtandao wa Youtube.
Kupitia
kitabu hiki Joel anatushirikisha ahadi 31 za matamko dhidi ya maisha yako
ambazo amezigawa kwa muundo wa siku. Ahadi hizi unaweza kuzinena dhidi ya nafsi
yako katika kipindi cha mwezi mmoja na hatimaye ukafanikiwa kubadilisha matamko
ambayo yamekuwa kandamizi katika hisitoria ya maisha yako. Mara nyingi tumekuwa
tukisikia msemo “maneno uumba” na ndicho mwandishi anachotushirikisha kupitia
zawadi ya kitabu hiki.
Kadri
tunavyoongea kauli nzuri au mbaya ndivyo tunaumba kile ambacho tumenena na hii ni
kutokana na ukweli kwamba maneno yana nguvu katika kuumba. Watu wengi wanaongea
kauli mbaya dhidi ya nafsi zao, dhidi ya familia zao au dhidi ya maisha yao ya
baadae pasipokugundua nguvu ya kauli hizo katika maisha yao. Hizi ni baadhi ya kauli
ambazo zinaongelewa na wengi wetu katika jamii zinazotuzunguka; mfano kauli
kama (a) mie ndo niwe tajiri! (b) mtoto huyu hana akili sawa na ndugu zake (c)
ugonjwa huu sidhani utaniacha salama (d) biashara ni ngumu siwezi kukabiliana
na changamoto zake; na kauli nyinginezo nyingi. Maneno matakatifu yanasema kuwa
“tutakula matunda ya maneno yetu” ikiwa na maana kuwa tutapata kulingana na
kile ambacho tumekuwa tunajiongelea katika maisha yetu ya kila siku.
Kwa
ujumla kama mwongozo wa maisha yako unatakiwa uhakikishe maneno ya kinywa chako
yanatolewa katika hali ambayo unahitaji maisha yako yaonekane – maisha yenye
msingi wa uchanya kwenye kila hali/tukio unalokabiliana nalo. Tambua kuwa kamwe
hauwezi kupata mafanikio wakati mara zote unajiongelea kauli za kushindwa, mara
zote hauwezi kushiba wakati wewe mara zote unajinenea kauli za njaa au hauwezi
kupata watoto wema wakati mara zote unanena maneno mabaya dhidi yao. Kupitia
vinywa vyetu tunaweza kubariki au kulaani maisha yetu ya baadae na hivyo kila
mmoja wetu anahitaji kulinda sana maneno ya kinywa chake.
Karibu
tujifunze machache niliyojifunza kwenye kitabu hiki:
1. SIKU YA 1: AHADI. Maajabu ya Mungu na baraka zake
zilizo kuu kuliko zote zitanishukia katika maisha yangu. Nitaona mlipuko wa
mapenzi ya Mwenyezi Mungu dhidi ya nafsi yangu. Wema wa Mungu wenye kunitakia ongezeko katika
kila hali kupitia neema zake kuu. Mungu ataniinua kuliko nilivyowahi kuota juu
ya mema yake katika historia ya maisha yangu kwani baraka zake nyingi zipo
katika njia zangu. Hii ndio ahadi yangu siku ya leo. Mwandishi anatushirikisha
kuwa ahadi hii inalenga kukupa tumaini jipya katika maisha yako. Yawezekana
umekuwa katika nyakati ngumu kiasi ambacho umekata tamaa na kuona kuwa hakuna
nuru tena mbele yako. Maandiko matakatifu (Waefeso 2:7) yanatupa tumaini kuwa
Mungu ni mwingi wa neema na wema wake kwetu hauna kiasi.
2. SIKU YA 2: AHADI. Nahadi nitanufahaika na
uaminifu wa Mungu, sitakuwa na wasiwasi wal hofu huu ya uaminifu wake kwa waja
wake. Uaminifu wangu utakuwa ndani yake muda wote nikiamini kuwa kamwe
hataniacha. Nitatumia kila zawadi ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka ndani yangu na
nitaishi kwa kadri ya mapenzi yake. Nitatimiza kusudi la maisha yangu katika
kila nifanyalo. Hii ndio ahadi yangu siku ya leo. Kila mmoja wetu ana ahadi
ambazo Mungu ameziweka juu yake. Yawezekana umetumia muda mrefu ukisubiri ahadi
hizi zitimie katika maisha yako bila mafanikio lakini mwandishi anatushirikisha
kuwa hii haimaainishi kuwa Mungu amekusahau. Watu wengi wanashindwa kuona ahadi
hizi zikitimia katika maisha yao kwa vile wanakata tamaa mapema. Kupitia ahadi
unapaswa kutambua kuwa ahadi zake Mwenyezi Mungu dhidi ya nafsi yako zipo hai
na zitatimia katika maisha yako endapo utaendelea kupambana kupitia vipaji
ulivyopewa. Timiza wajibu wako na mkono wake wa kuume upo juu yako mara zote
(Waebrania 13).
3. SIKU
YA 3: AHADI. Natambua
kuwa siku ya leo kuna neema nyingi dhidi ya nafsi yangu. Nina nguvu, ukakamavu,
ujasiri na uelewa dhidi ya maamuzi na matendo yangu. Hakuna kikwazo chochote
ambacho kitanizuia kukamilisha kile ambacho nimekusuduia kufanya katika
kutimiza mapenzi yake Mwenyezi Mungu. Natambua kuwa kila changamoto katika
maisha yangu ni kwa ajili ya kunijenga zaidi ili nikomae kuliko nilivyokuwa
kabla ya changamoto husika. Mimi ni mshindi na hivyo nitashinda kila
kikwazo/changamoto. Hii ndio ahadi yangu siku ya leo. Kama vile Waislaeli walivyopewa ‘manna’
kila siku ndivyo ilivyo kwetu, kila siku tunapewa neema mpya katika maisha
yetu. Kila siku tunapewa neema ya hekima, neema ya busara, neema ya amani,
neema ya kupendana na neema ya kusameheana. Hivyo ni wajibu wetu kila siku
kuhakikisha tunatumia neema hizi kwa ajili ya kuboresha kila sekta ya maisha
yetu.
4. SIKU YA 4: AHADI. Naahidi
kuwa bado sijachelewa kutumia Baraka nilizojaliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili
ya kukamilisha kila kitu ambacho Mungu amekusudia katika maisha yangu. Mlango
kwa ajili ya fursa bado upo wazi kwa ajili yangu. Mungu ana makusudi mema na
mimi na kila wakati anaendelea kuniandaa kwa ajili ya kutimiza ndoto zangu. Huu
ndio wakati sahihi, nipo tayari kutimiza ndoto zangu. Hii ndio ahadi yangu.
Kila mmoja wetu Mungu ameweka vitu vya kipekee ndani mwake. Hata hivyo,
tumeshindwa kutumia upekee huu kutokana na tabia za kusema tupo bize sana,
nilijaribu nikashindwa hivyo siwezikuridia tena, mimi sina kipaji hicho –
siwezi na nyinginezo nyingi. Hata kama umeenda nje ya ndoto za maisha yako
habari njema ni kwamba Mungu aliye hai kamwe hatokuacha endapo utasimama katika
nafasi yako ili kukamilisha ndoto za maisha yako (2Timotheo 1:6).
5. SIKU YA 5: AHADI. Najivunia
nafasi ya Mwenyezi Mungu na kila jambo ambalo ameniwezesha kwenye maisha yangu.
Kamwe sitabweteka na watu, fursa na upendo wake bali kila siku nitaendelea
kutafuta watu wapya, fursa pamoja na kuvutia mapenzi yake zaidi. Nitaendelea
kutenda yaliyo mema badala kutenda mabaya. Nitaendelea kumshukuru kwa jinsi
nilivyo na yale niliyonayo badala ya kuendelea kulalamikia yale ambayo
nimekosa. Kila siku nitaichukulia kama zawadi katika maisha yangu na hivyo roho
yangu itajawa na sifa na utukufu kwa ajili ya upendo wake mkuu. Hii ndio ahadi
yangu. Mwandishi anatushirikisha kuwa maisha yetu hayana uhakika wa kuwa siku
kama ya leo mwaka ujao tutakuwepo katika dunia hii. Ni kutokana na ukweli huu
tunatakiwa kila siku tuishi kana kwamba ndo siku yetu ya mwisho katika maisha
ya ulimwengu huu. Ni kutokana na ukweli huu hatupaswi kuishi maisha ya
malalamiko, machukizo, uchoyo, wivu na msengenyo bali kila dakika katika maisha
yetu itumike kufanikisha kusudi la uwepo wetu hapa duniani.
6. SIKU YA 6: AHADI. Naahidi
kuacha urithi wa imani thabiti kama alama ya maisha yangu kwa vizazi vijavyo.
Maisha yangu yatakuwa yenye ubora na uaminifu. Kwa vile napanda hatua kiimani
na kutenda matendo mema ni matarajio yangu kuwa watu wengi watanifuata kwa
ajili ya utimilifu wa utukufu wa Mwenyezi Mungu. Hii ndio ahadi yangu. Mwandishi
anatushirikisha kuwa kadri unavyotenda wema na kuishi misingi ya imani ndivyo Baraka
zake Mwenyezi zitamiminika katika maisha yako na hivyo kushibishwa katika kila
sekta ya maisha yako. Shibe hii ni pamoja na amani ya roho, afya njema pamoja
na wema kutoka kwa jamii inayokuzunguka.
7. SIKU YA 7: AHADI. Natambuwa kuwa Mungu ana mipango
mikubwa kwa ajili ya maisha yangu. Anaongoza hatua zangu hata kama yawezekana
sijui ni kwa jinsi gani miujiza yake inatendeka katika maisha yangu lakini bado
natambua kuwa Mungu hashangazwi na tabia yangu hiyo. Mungu ni mwingi wa rehema,
upendo na uvumilivu hata nyakati ambazo naenda kinyume na mapenzi yake. Hata
hivyo natambua kuwa katika nyakati ambazo yeye amekusudia kutenda miujiza yake
katika maisha yangu, kila kitu kitakwenda sawa. Hii ndio ahadi yangu. Ahadi
inatokana na ukweli kwamba maandiko yanatuambia kuwa kila mmoja siku za maisha
zimeandikwa katika kitabu cha Mwenyezi Mungu kuanzia mwanzo wa maisha yako hadi
mwisho wake. Hivyo Mungu anatutambua mafanikio na changamoto tunazopitia katika
kila siku ya maisha yetu.
8. SIKU YA 8: AHADI. Natambua
kuwa mipango ya Mwenyezi Mungu dhidi ya maisha yangu ipo karibu kutimia.
Mipango hii haitasimamishwa na mwanadamu wala changamoto ya aina yoyote ile.
Mungu atanipatia majibu ya matatizo au changamoto zote ambazo nitakutana nazo
katika kutimiza ndoto za maisha yangu. Watu wema na mapito sahihi yananisubilia
kwa ajili ya kutimiza ndoto hizi. Nipo tayari kutimiza wajibu wangu kwa ajili
ya ndoto hizi. Hii ndio ahadi yangu. Mwandishi anatushirikisha kuwa Mwenyezi
Mungu anajua ni nyakati zipi atatimiza mipango yake kwetu hata kama nyakati
ambazo sisi kama wanadamu hataturajii miujiza yake. Maandiko yanatukumbusha kuwa
Mungu ni mwaminifu naye si sawa na mwanadamu kwani akiahidi anatimiza.
9. SIKU YA 9: AHADI. Natambua
kuwa miujiza isiyotarajiwa inakuja katika maisha yangu. Muda si mrefu nitatoka
katika hali ya kuwa na uchache na kuingia kwenye hali ya kutosheka kwa kila hali/tukio
katika kila sekta ya maisha yangu. Wajibu wangu ni kusimama imara kwa ajili ya
kupokea Baraka hizi na kuziishi katika maisha yangu ya kila siku. Naye Mwenyezi
Mungu atafungua milango yake ya asili kwa ajili ya mafanikio yangu (Waefeso
3:20). Hii ndio ahadi yangu. Maandiko yanasema kuwa ukiwa na imani katika mambo
madogo naye Mwenye Mungu atakuzawadia kwa mambo makubwa (Mathayo 25:21).
10. SIKU
YA 10: AHADI. Natambua kuwa Mungu ataharakisha mipango
yake dhidi yangu katika maisha yangu kwa kadri ninavyoendelea kumwamini.
Nitatimiza ndoto zangu ndani ya muda mfupi kuliko ambavyo nimewahi kufikiria.
Haitakuchukua mwaka kumaliza madeni yangu au kukutana na watu wema katika
maisha yangu. Mungu anatenda miujiza kwa kasi kuliko ilivyowahi kutokea na
hivyo atanipa ushindi muda si mrefu tofauti na nidhaniavyo. Hii ndio ahadi
yangu. Mwandishi anatushirikisha kuwa kama ambavyo Yesu aliweza kutengeneza
muujiza wa kugeuza maji kuwa mvinyo bora ndani ya dakika chache ndivyo pia
atafanikisha miujiza katika maisha yako ndani ya siku chache. Ili miujiza hii
iweze kufanyika ni lazima kwanza uamini kuwa Mungu anaweza kukutendea maajabu
kwa maana ya kwamba ni lazima uwe tayari kutekeleza wajibu wako.
11. SIKU
YA 11: AHADI. Kwa kuwa
namwabudu na kumuheshimu Mwenyezi Mungu natambua kuwa atanishibisha na
kunitosheleza katika kila sekta ya maisha yangu. Mungu atatenda kwa wingi na
ziada nazo Baraka zake zitapita kiasi katika maisha yangu. Natambua kuwa ili
haya yote yatimie ni lazima niwe sehemu sahihi na kwa wakati sahihi. Watu wote
watakuwa wema kwangu kwa ajili ya kukamilisha miujiza ya maisha yangu. Nami
nimezungukwa na wema wa Mungu. Hii ndio ahadi yangu. Mungu anawapenda wale wote
wanaotii sheria zake na hivyo uwazidishia katika kila hali kwenye maisha yao.
Unachotakiwa kufanya ni kuishi sheria zake na matokeo yake ni kupendwa na kila
mtu na hatimaye utapata mafanikio kwenye kila sekta ya maisha yako (biashara au
kazini kwako).
12. SIKU
YA 12: AHADI. Mimi ni wa kipekee na wa ajabu na wala sio
mtu wa kawaida hivyo nastahili kupata matokeo yasiyo ya kawaida. Kati viumbe
vyote vilivyoumbwa, Mungu muumba anajivunia kwa kuniumba. Mimi ni sawa na kito
cha thamani kwake. Nami sitamwangusha bali nitaendelea kumwabudu na kumtukuza
kwani mimi ni mtoto wake na nimeumbwa kwa sura yake. Hii ndio ahadi yangu. Tunaishi
katika jamii ambayo inaweza kututazama kwa jicho tofauti na Mungu
anavyotutazama. Jamii inaweza kutuona kuwa sisi si chochote na hatimaye kama ni
wepesi wa kukubali tutazama kwenye mtazamo wa jamii. Matokeo yake ni kuishi
maisha ya kawaida ambayo si makusudi ya Mungu (Waefeso 10:2).
13. SIKU
YA 13: AHADI. Natambua kuwa Mungu analeta siku ya
mafanikio na ukuaji kwenye kila sekta ya maisha yangu. Nami sipo tayari
kukwamishwa na vizuizi vya ulimwengu huu kwani nipo tayari kubadilika kwa ajili
ya kupokea mafanikio na ukuaji huu. Milango mipya ya fursa, mahusiano mapya,
baraka mpya na upendo wa kila hali upo mbele yangu. Hii ndio ahadi yangu. Mungu
anaongoza hatua zako na yupo tayari kufungua milango ya asili kwa ajili ya
mafanikio yako. Hapa unahitaji kukumbuka kuwa kila changamoto unayopitia ni
sehemu ya kukufanya ukue zaidi kwa ajili ya maisha yako ya baadae.
14. SIKU
YA 14: AHADI. Naahidi
kutumia maneno ya kinywa changu kwa ajili ya kuwabariki watu badala ya
kuwalaani. Nitaongelea wema na ushindi badala ya kuongelea ubaya dhidi ya
familia yangu, marafiki na jamii inayonizunguka. Maneno kama wewe ni mzuri, una
kipaji cha hali ya juu, wewe ni wa pekee, najivunia kuwa karibu na wewe na
utakuwa mtu mkubwa katika maisha yako yatakuwa sehemu ya maongezi yangu ya kila
siku dhidi ya watu ninaokutana nao. Hii ndio ahadi yangu. Maneno haya ya
ushindi yana nguvu kubwa ya kubadilisha watu na hivyo kupitia maneno hayo
unakamilisha uumbaji wa Mwenyezi Mungu kwa watu wake.
15. SIKU
YA 15: AHADI. Natambukuwa naianza siku hii nikiwa na
akili timamu zenye uchu wa kushinda kuliko kushindwa kwenye jambo lolote lile.
Kwa imani nipo vizuri kiuwezo, nimetiwa mafuta, nina vifaa vyote vya ushindi na
nina nguvu za ushindi. Mawazo yangu yanaongozwa na neno la Mungu wala hakuna
kikwazo ambacho kitanishinda kwa kuwa akili yangu imewekewa ushindi. Hii ndio
ahadi yangu. Ahadi za Mungu zipo katika wakati timilifu uliopita na zinaonesha
kuwa tayari zipo ndani mwako, wajibu wako ni kuzifanya ahadi hizi ziwe timilifu
katika maisha yako. Hii haijalishi nyakati unazopitia kwa sasa iwe kimahusiano,
kiuchumi, kikazi au kijamii bali wajibu wako unahitaji kujisema kuwa Mungu ana
makusudi mema na mimi naye ahadi zake sio za uongo. Kupata baraka hizi
unahitaji kuongea, kutembea, kutenda, kufikiri, kufurahi na kuvaa kama
mbarikiwa wa Mungu.
16. SIKU
YA 16: AHADI. Nitaishi maisha ya uponyaji nikiguswa sana
na mahitaji ya wengine wanaonizunguka. Nitawainua walioanguka, nitawahuisha
waliovunjika moyo na kuwapa hamasa waliokata tamaa. Nitatimiza haya yote kwa
wema na huruma. Sitasubulia miujiza itokee bali nitakuwa sehemu ya kutimiza
miujiza hii kwa kuonesha upendo wa Mungu kila sehemu ninapoenda. Hii ndio ahadi
yangu. Kazi kubwa tuliyopewa katika maisha haya nikufuta machozi watu walio
kwenye maisha ya huzuni. Sasa kila mmoja anatakiwa kujitazama upya kama kweli
amakuwa sehemu ya kuwafariji watu au amekuwa sababu ya kuwaumiza watu.
17. SIKU
YA 17: AHADI. Naahaidi kuwa nitakuwa imani yangu
itaongozwa na na vitendo kwani imani bila vitendo imekufa. Nitaonesha imani
yangu kwa kuchukua hatua thabiti na za ujasiri ili kudhihirisha kile ambacho
Mungu ameweka ndani ya moyo wangu. Imani yangu haitafichwa bali itaonekana.
Natambua kuwa kadri nitavyoonesha imani yangu ndivyo Mungu atakavyoonekana
katika maisha yangu na kutenda mambo ya kushangaza katika maisha yangu. Hii
ndio ahadi yangu. Mara zote penye nia pana njia hivyo husikubali kukatishwa
tamaa na changamoto za muda kwani kufanya hivyo utajikuta unakimbia ushindi
ambao ulishatayarishwa kwa ajili yako (Marko 2:5).
18. SIKU
YA 18: AHADI. Natambua kuwa mafanikio yanakuja katika
maisha yangu, mpasuko wa ghafla wa wema wa Mungu. Mafuriko ya nguvu za Mungu,
mafuriko ya uponyaji, mafuriko ya hekima, mafuriko ya neema na mafuriko ya
upendo vyote kwa pamoja vinakuja katika maisha yangu. Mimi ni mshindi na
nimeamua kuishi maisha ya ushindi na hivyo natarajia Mungu anizidishie wema
wake na anishangaze kwa huruma yake. Hii ndio ahadi yangu. Umeumbwa na nguvu ya
ajabu ambayo hakuna kinachoweza kuisimamisha. Mungu anaporuhusu mafuriko yake
katika maisha yako hakika hakuna wa kuyazuia mafuriko hayo.
19. SIKU
YA 19: AHADI. Natambua kuwa kuna upako kwa ajili ya
urahisi wa hatua zangu. Mungu yupo upande wangu akinyoosha sehemu zote
zilizopinda kwani kwake mzigo unakuwa mwepesi. Sitaangaika tena, kwani yote
yaliyokuwa magumu sasa yatakuwa mapesi. Neema na baraka zake zimenipa nuru na
kuondoa mafadhahiko yote. Hii ndio ahadi yangu. Mungu anasema nira yake ni
rahisi na mzigo wake ni mwepesi hivyo wote tunakaribishwa kwake kwa ajili ya
kupata makuu yake.
20. SIKU
YA 20: AHADI. Natambua kuwa mimi ni mwenye amani na
mpole na hivyo sitaruhusu watu au hali yoyote kuharibu amani ya roho yangu.
Nitainuka dhidi ya changamoto yoyote ile kwani Mungu amenipa nguvu za kushinda.
Nachagua kuishi maisha ya furaha na amani ili ni mpe nafasi ya Mungu kutenda
kazi yake katika maisha yangu. Hii ndio ahadi yangu. Kadri unavyoruhusu maneno
au matendo ya watu kukuchukiza au kuharibu amani yako ndivyo unaruhusu watu
watawala maisha yako. Watu wana haki ya kuongea au kutendo wanayopenda katika
maisha yao dhidi yako lakini una mamlaka ya kupuuza maneno au matendo yao.
21. SIKU
YA 21: AHADI. Natambua wema wa ajabu wa Mungu katika
maisha yangu. Mungu ataniwezesha kutimiza yale ambayo mimi kama mimi siwezi
kuyatekeleza kwa akili yangu ya ubinadamu. Fursa za ajabu, uponyaji, kuuhishwa
pamoja na mafanikio vyote vipo njia kwa ajili ya utimilifu katika maisha yangu.
Nami nitapata nguvu, afya, hekima na busara. Nitagundua talanta ambazo sikuwahi
kuzigundua kuwa ninazo katika maisha yangu na hatimaye nitatimiza ndoto zangu
nilizojaliwa na Mwenyezi Mungu. Hii ndio ahadi yangu. Je kuna jambo gumu kwa
Mwenyezi Mungu? (Mwanzo 18:14). Je unadhani ndoto zako ni ngumu kwa Mungu?
Maandishi yanasema kuwa endapo mtaondoa vikwazo vyote juu yangu nami
nitashangaza kwa wema wangu (2Wakorintho 9: 8 – 9).
22. SIKU
YA 22: AHADI. Naahaidi kuishi maisha ya ushindi kwani
nimeumbwa kwa sura yake Mwenyezi Mungu na hivyo nina vinasaba (DNA) za ushindi.
Mimi ni kichwa na kamwe sio mkia wala wa kawaida. Nimevishwa kilemba cha
ushindi na mara zote nipo juu wala sio mtu wa chini. Nitaishi maisha yenye
kusudi, shauku, shukrani na utukufu kwani sasa natambua kuwa haya ndio maisha
ambayo niliumbwa kwa ajili ya kuishi. Hii ndio ahadi yangu. Mungu anatuona sisi
kama washindi/wafalme na wala sio watu walioshindwa (Warumi 5:17). Kwa vile
bado una uhai wewe bado ni mtawala na hivyo hupaswi kukata tamaa.
23. SIKU
YA 23: AHADI. Naahaidi kuwa mimi nipo kwa ajili ya
kuwajenga watu. Nitatafuta fursa kwa ajili ya kuwahamasisha wengine ili watumie
vipaji walivyonavyo kwa ajili ya kutimiza ndoto zao. nitaongea maneno ya
ushindi na imani kwa ajili ya kuwahakikishia, kuhidhinisha na kuwawezesha kuwa
wao ni wa thamani kubwa. Nitawaita kwa ajili ya kutambua mbegu ya ukuu iliyopo
ndani mwao ili hatimaye waweze kuishi maisha yenye kusudi la muumba. Hii ndio
ahadi yangu. Kila mmoja anahitaji kuambiwa sifa zake kuu alizonazo ili kupitia
maneno ya wanaomzunguka aweze kukua kutoka hatua moja hadi nyingine. Kuwa mmoja
kati ya watu wanaowabariki watu wanaowazunguka.
24. SIKU
YA 24: AHADI. Nahaidi kuwa nitanena maneno chanya ya
imani na ushindi dhidi ya nafsi yangu, familia yangu pamoja na nyakati zijazo
za maisha yangu. Sitatumia maneno yangu kuelezea hali yangu badala yake
nitatumia maneno yangu kwa ajili ya kubadilisha niliyonayo. Nami nitaita wema,
huruma, upendo, ushindi na uhuishwaji wa nafsi zote kwa ajili sifa na utukufu
kwake Mungu. Sitamwambia Mungu namna matatizo yangu jinsi yalivyo na nguvu bali
nitayaambia matatizo yangu jinsi Mungu wangu alivyo na nguvu kupita vitu vyote.
Hii ndio ahadi yangu. Mara zote ongelea ushindi katika maisha yako badala ya
kujikita kwenye kushindwa au kukata tamaa.
25. SIKU
YA 25: AHADI. Naahaidi kuwa maisha yangu si ya kuishi tu
bali nitaishi maisha ya mafanikio pamoja na changamoto zote ambazo zipo mbele
yangu. Najua kuwa kila kikwazo ni kwa ajili ya kuanza upya na sio muda wa
kudumaa katika kufikia mafanikio ya ndoto zangu. Natambua namna ambavyo hatua
moja inavyoweza kubadilisha kila sekta ya maisha yangu na hivyo nitachukua
hatua muda wote. Hii ndio ahadi yangu. Mungu anaweza kuzidisha muda wako na
kukuwezesha kutimiza kila jambo la muhimu katika maisha yako.
26. SIKU
YA 26: AHADI. Nitachagua imani dhidi ya hofu na hivyo
nitayafikiria yaliyo mema na chanya katika hali ya maisha yangu. Nitatumia
nguvu nilizonazo sio kwa ajili ya kuwa na hofu bali kwa ajili ya kuamini kwani
hofu haina nafasi katika maisha yangu. Sitatoa nafasi ya kudumu kwenye mambo
hasi wala mawazo ya kukatisha tamaa kwani akili yangu imejikita kwa yale ambayo
Mungu ananiwazia. Kwani natambua mpango wake kwa ajili yangu ni wa ushindi,
mafanikio na wingi/shibe kwenye kila sekta ya maisha yangu. Hii ndio ahadi
yangu. Hofu na imani vyote kila kimoja kinamfanya mtu awe na mtazamo kuwa kuna
jambo lisiloonekana litatokea kwa baadae na vyote kwa pamoja vinakinzana. Hii
ina maanisha kuwa ukiamua kuwa na hofu badala ya imani, maisha yako
yatatawaliwa na matendo ya hofu (Ayubu 3:25).
27. SIKU
YA 27: AHADI. Natambua kuwa nina kila aina ya vifaa na
nyenzo kwa ajili ya utimilifu wa kazi nzuri ambazo Mungu amepanga dhidi yangu.
Mimi nipakwa mafuta na kutiwa nguvu na Muumba wa ulimwengu. Kila aina ya
vikwazo na vifungo vimefunguliwa dhidi yangu nami nipo huru na hivyo ni muda
wangu wa kung’aa kama kito cha thamani. Nitainuliwa juu na kushinda vikwazo
vyote kwa ajili ya kushuhudia kila aina ya ufanisi katika maisha yangu. Hii
ndio ahadi yangu.
28. SIKU
YA 28: AHADI. Naahaidi kuwa nitamwomba Mwenyezi Mungu
vitu vikubwa katika maisha yangu. Nitaendesha sara kwa ajili ya kuendelea
kutegemea kupata na kuwa na imani juu ya matokeo makubwa. Nami sitayumbishwa na
mawimbi katika nyakati za changamoto kwenye maisha yangu bali katika nyakati
hizi nitamwomba Mungu kwa ajili ya kuonesha uwepo wake kwani natambua hakuna
linaloshindikana kwake. Hii ndio ahadi yangu. Mara nyingi tunahisi kuwa
hatupaswi kuomba mambo makubwa kutoka kwa Mungu lakini maandiko yanasema kuwa
tunashindwa kupata kwa vile tunashindwa kuomba (Yakobo 4:2 & Zaburi 2:8).
Tunahitaji kuomba tena bila kuchoka tukiongozwa na imani (Marko 11:23).
29. SIKU
YA 29: AHADI. Natambua kuwa Mungu anaweka mambo sawa kwa
ajili ya ufanisi wa maisha yangu. Kupitia yeye natakiwa kuwa na mpango kazi wa
maisha yangu. Hata kama kuna vitu ambavyo kwa sasa sivielewi lakini sitaogopa
kwani ni suala la muda tu. Kwani ipo siku maarifa yote yatafunuliwa kwangu nami
nitaona mpango wa ajabu wa Mungu ukinipeleka sehemu ambazo sikuwa kuziwaza. Hii
ndio ahadi yangu. Haupaswi kushindwa kuwa mvumilivu kwani maisha kwako bado
mpaka pale Mungu atakaposema sasa basi.
30. SIKU YA 30: AHADI. Natambua kuwa Mungu
anaongoza hatua zangu kwa kuhakikisha kuwa mapito yangu yananyoshwa ajili ya
mafanikio yangu. Mpaka sasa tayari ameshaniandalia watu sahihi wa kufanya nao
kazi, fursa sahihi pamoja na majibu ya changamoto zote ambazo nitakutana nazo
katika safari yangu ya mafanikio. Hakuna mtu wala magonywa wala vikwazo ambavyo
vitasimamisha makusudi yake katika maisha yangu kwani yote aliyoahidi katika
maisha yangu yatatimia muda si mrefu. Hii ndio ahadi yangu. Mungu mwenye nguvu
atakupigania kwenye kila hali na hatimaye utashinda (Kutoka 9:1 - 35).
31. SIKU
YA 31: AHADI. Naahaidi kubadilisha kila tabia ambayo
inaenda kinyume na maono ya Mungu katika maisha yangu. Natambua kuwa magonjwa,
shida, ukosefu wa kila hali na ufinyu wa pesa ni vitu ambavyo napitia tu na
muda si mrefu vyote hivi vitakuwa ni historia. Sitaendeshwa tena na yale
ninayoyaona bali nitaendeshwa na yale ninayoyatambua. Mimi ni mshindi kamwe
sitashindwa. Hii ndio ahadi yangu. Hapa mwandishi anatushirikisha umuhimu wa
kuona kuwa hali tunazopitia ni mapito tu na muda si mrefu Mungu atatenda
miujiza yake (2 Wakorintho 4:13).
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi
wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
|
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu hisiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com