Hii Hapa Kauli Mbiu Ambayo Nakusihi iwe Mwongozo wako kipindi chote cha mwaka 2017


Tunapoelekea kuumaliza mwaka 2016 na kuuanza mwaka 2017 ni matumaini yangu kuwa rafiki unaendelea vizuri. Ni jambo la heri na la kujivunia kuona mpaka sasa tu wazima wa afya kwani wapo wengi ambao walitamani kufikia siku kama ya leo lakini hawakufanikiwa. Hivyo mimi na wewe ni akina nani hasa mpaka tumefanikiwa kufikia muda kama huu? Shukrani za pekee ni kwake muumba kwani ndiye anaejua makusudi ya uwepo wetu hapa duniani.

Karibu tena katika makala yangu ya leo ambapo leo hii nitakushirikisha kauli mbiu muhimu ambayo inatakiwa kuwa dira ya mafanikio yako katika kipindi chote cha mwaka 2017. Kabla ya kufahamu kauli mbiu hii, ningependa nikukumbushe kuwa nimekuwa nikijitahidi kuhakikisha kila makala ninayoandika inakuwa na hamasa ya kukutaka wewe rafiki yangu uwe na mtazamo wa kuona kuwa kila aina ya mafanikio unayoyataka yanaanzia ndani mwako na wala si kwingineko. Kwa maana hii leo hii jinsi ulivyo ni matokeo ya mambo ambayo umekuwa ukiyachagua katika maisha yako ya kila siku.

Miaka itakuja na kupita kama ambavyo majuzi tulisherekea mwaka 2016 ndivyo ilivyo hata kesho tutasherekea mwaka 2017 hali kadhalika 2018. Jambo moja la kujiuliza kila tunaposherekea mwaka mpya ni je tupo kwenye njia sahihi ya kuzielekea ndoto zetu? Bila kufanya hivyo tutaendelea kusherekea sherehe za mwaka mpya enzi na enzi mpaka pale ambapo maisha yetu yatafikia ukomo kwenye sayari hii huku tukizikwa na ndoto zetu.

Rafiki yangu leo hii unaposherekea mwaka mpya 2017 naomba nikupe kauli mbiu ambayo itakuwa mwongozo wako katika kipindi chote cha mwaka 2017. Kauli mbiu hii si nyingine bali ni KUWAZA CHANYA (POSITIVE THINKING) katika kila hali/tukio.

Nini Maana ya Kauli Mbiu Hii?
Kuwaza Chanya maana yake ni kwamba unaifundisha akili (ubongo) yako muda wote ifikilie katika hali ya uchanya pasipo kutoa nafasi kwa mawazo hasi. Kwa maana hii ni kwamba kila tukio unalokutana nalo unatakiwa ufahamu kuwa tukio hilo lina sura mbili (Chanya au Hasi) na hivyo wajibu wako mkubwa ni kutafuta hali ya uchanya kwenye tukio husika.


Ukiwa unawaza katika hali chanya kamwe wewe haupaswi kuwa mtu wa kunungunika, kulalamika, kukasirika, kuwa na hofu, kuwa mmbea, kuwa na visingizio, kukata tamaa, kuhahirisha mambo n.k. bali unatakiwa matukio yote unayokutana nayo unayachambua ili upate upande chanya wa hayo matukio. Mfano, umepanga kukutana na mtu sehemu flani na umejitahidi ukafika muda ule ule mliokubaliana lakini kwa bahati mbaya yeye amechelewa kufika kwa muda wa nusu saa. Kwenye tukio kama hili unachoweza kufanya ni kuangalia kwa muda huo unaomsubiria ni kitu gani unaweza kufanya ili akiendelea kuchelewa husipoteze muda wako bure, unaweza ukasoma kitabu/makala kama unacho kwenye simu (softcopy), unaweza ukasikiliza nyimbo ambazo huwa ukisikiliza zinakupa hamasa au faraja au ukasikiliza sauti za vitabu vilivyosomwa (audio books).

Je nini unatakiwa kufanya ili uwaze chanya muda wote?
Ili uwaze chanya kwenye kila aina ya tukio fanya mambo yafuatayo;

Fikiri kama mtoto. Watoto huwa wana mfumo wa mawazo ambao mtu mzima ukifanikiwa kuuhishi mfumo huu kamwe hauwezi kuwa na mawazo hasi. Mfano, watoto muda wote wana furaha, hawana hofu na matukio ya baadae au yaliyopita (wanaishi maisha ya sasa), hawakati tamaa pale wanapokutana na jambo jipya na hawafikirii kuhusu sheria zinasemaje. Kwa hali kama hii watoto wanawaza mambo mema kwenye kila hali wanayokutana nayo kwani hawajui mabaya yaliyopo kwenye ulimwengu huu.
Kama mtu mzima unaweza kuwaza kama mtoto pale ambapo unafanya jambo jipya. Husifikirie kushindwa kwenye kila jambo unalofanya bali fahamu ya kuwa una mfumo wa mawazo ambao unaweza kutekeleza kila jambo endapo umetumiwa ipasavyo. Pia, tumia njia hivyo kujiepusha hofu ambayo imekuwa ikuzuia kutekeleza malengo yako.
Tumia lugha ya mwili (Body language). Mwaka 2017 hakikisha kuwa mwonekano wako wa nje unaonyesha kile unachokiwaza ndani mwako. Mara nyingi kwenye jamii inayotuzunguka tumezoea kusikia kauli kama kijana yule anaonekana kuwa na tabia nzuri, yule mzee huwa ana busara sana… Unaweza ukajua mawazo ya mtu hata kabla hajaongea ila kwa kuangalia mwonekano wake wa nje. Hivyo ndivyo na wewe unatakiwa uwe kama kweli unawaza chanya ili jamii inayokuzunguka ione vitu vya tofauti kutoka kwako. Tambua kuwa tupo jinsi tulivyo kutokana na yale tunayoyawaza muda mwingi.

Kuwa na muda wa kuongea na nafsi yako. Unapoishi kwenye kauli mbiu ya uchanya, mwaka 2017 hakikisha unakuwa na muda wa kuongea na nafsi yako. Kuongea na nafsi yako ni pale ambapo unakuwa na maneno ya kujiongelea mwenyewe na mara nyingi inafaa uwe sehemu yenye utulivu kwa ajili ya kuepuka mwingiliano na kalele nyingine ambazo zinaweza kukuhamisha.
Unapoongea na nafsi yako hakikisha unajisemea maneno chanya ambayo yanakuhamasisha kuchukuwa hatua za ushindi. Epuka sentensi kama “Kila ninalogusa linaniendea kinyume, Siwezi kukamilisha kazi hii kwa muda, Siwezi kufanya biashara, Siwezi kufaulu somo hili, n.k”. Maneno chanya ambayo unaweza kujisemea ni;
  • Kila ninalogusa lazima nifanikiwe;
  • Sijawahi kushindwa, hivyo lazima niishinde changamoto hii;
  • Naweza kufanya jambo lolote ninalodhamiria;
  • Najiamini katika huduma ninazotoa hivyo lazima nipate wateja;
  • Mimi ni bingwa katika tasnia hii;
  • Mimi ni hodari; n.k

Kuwa mtu wa kutathmini mawazo yako. Zoezi la kuwaza chanya ni gumu kama ulikuwa hujazoea kufanya hivyo. Kwa vyovyote vile lazima utajikuta unaanza kutawaliwa na mawazo hasi. Ili kukabiliana na mawazo hasi lazima uwe na muda wa kujiuliza mara kwa mara juu ya lile unalowaza kama lina mchango kwenye mafanikio yako na pale unapotambua kuwa upo katikati ya mawazo hasi achana nayo mara moja.

Chagua marafiki na makundi ya kujumuika nayo. Kuna msemo maarufu usemao kuwa ndege wenye manyoa yanayofanana huruka pamoja. Kama ulikuwa na marafiki ambao mmekuwa mnatumia muda mwingi kufanya mambo yasiyo na tija katika mafanikio yako kwa sasa unatakiwa kuchagua marafiki wapya ambao watapelekea ufanikiwe kuiishi kauli mbiu ya uchanya. Epuka marafiki ambao muda mwingi wanautumia kulalamika, kusengenya, kubeza yaw engine, kukatishana tamaa n.k

Pia, Katika ulimwengu wa sasa ambao umetawaliwa na mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano husipokuwa makini kwenye makundi (magroup) ambayo umeunganishwa nayo itakuwa vigumu sana kwako kuwaza chanya kwani mara nyingi makundi haya yametawaliwa na mzaha mwingi ambao kwako hauna tija. Mwaka 2017 hakikisha makundi ambayo hayana tija unajiondoa mara moja na kujiunga na makundi mapya ambayo yatakupa mawazo, ushauri pamoja na changamoto katika kutekeleza malengo yako.

Tenga muda wa kusoma vitabu au makala za hamasa. Kama unataka kufanikiwa ni lazima uwe mtu wa kusoma vitabu au makala zinazoendana na yale unayoyahitaji katika maisha yako. Dunia kwa sasa imekuwa ni kijiji kwani unaweza kusoma kitabu chochote kile kwa kutumia simu yako. Tatizo letu tumekuwa wavivu sana katika kujisomea vitabu/makala za namna hii lakini cha kushangaza utakuta mtu muda wote yupo bize na kusoma posti za watu au magazeti ya udaku kwenye mtandao hila ukimuambia tumia saa moja kila siku kujisomea kitabu/makala atakuambia kuwa makala/kitabu kina kurasa nyingi sana.
Mpendwa rafiki yangu naomba mwaka 2017 utambue kuwa hakuna mafanikio yoyote ambayo yatakuja kwa njia ya mkato lazima uwe tayari kuwekeza nguvu, muda pamoja na rasilimali ili hatimaye ufanikiwe. Anza kuwekeza sasa kwa ulisha ubongo wako na maarifa mbalimbali kutoka kwa waliofanikiwa.

Kuwa Mtu wa Vitendo.  Mwaka 2017 unapoongozwa na kauli mbiu ya uchanya hakikisha yale unayoyawaza unayaweka katika mfumo wa vitendo mara moja pasipo kuhairisha au kusubiria. Wanafalsafa wanatuambia kuwa kila kitu kinaumbwa kutokana na mfumo wa mawazo na kupitia mfumo huu kila mtu ana uwezo wa kuumba chochote anachokiwaza. Tatizo kubwa ambalo limekuwa linatutofautisha kwenye uumbaji wa vitu ni pale ambapo wengi wetu tumeruhusu visingizio kukutawala na hivyo kuishia kutofanya lolote. Wengi mtakuwa mashahidi kuwa unaweza kuwa na wazo zuri hila kutokana na mazoea ya kuwaza pasipo kutenda inafikia kipindi mpaka unalisahau wazo lako halafu ghafla ukiwa unatembea mtaani unashangaa kuna mtu ameanzisha biashara au anatoa huduma sawa na lile wazo lako. Hapa kinachokutofautisha wewe na yeye ni kwamba mwenzio alikuwa na wazo na akalitafsiri kwenye vitendo. Mwaka 2017 hakikisha unakuwa mtu wa vitendo badala ya kuishia kuwaza tu.

Mwisho naomba nikutakie sherehe njema za mwaka mpya. Rafiki yangu unaposherekea mwaka mpya hakikisha unauanza mwaka mpya kwa kuwaza chanya kwani nakuhakikishia kuwa miezi 12 ni muda mfupi sana ukiwa unaishi kwenye malengo yako. Ulimwengu wa sasa ni ulimwengu wa teknolojia ya mawasiliano hivyo kama rafiki naomba uendelee kusambaza jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadirisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. HERI YA MWAKA MPYA 2017.
Karibuni kwenye fikra tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com



Tunaposherekea Siku Kuu ya Christmas Karibu Nikushirikishe Stori Hii – Jinsi Wazazi/Walezi Wanavyoharibu Vipaji vya Watoto Wao!

Ni matumaini yangu kuwa rafiki unaendelea vizuri na mapambano kwa ajili ya kufanikisha ndoto zako. Huu ni wakati mwingine ambao Mwenyezi Mungu ametujalia kwa ajili ya kuyafanya maisha yetu kuwa bora kiafya, kiimani, kiuchumi na kijamii pia. Ni wakati ambao Wakristu wote duniani tunaungana kwa ajili ya kushangilia kuzaliwa kwa mwokozi wetu Yesu Kristu tukiwa tunafakari ukombozi wetu. Ni jambo la heri kuona sisi tulio hai tunafikia siku kama ya leo tukiwa na nguvu za kutosha kwa ajili ya kufanikisha shughuli zetu za kila siku. Hongera sana rafiki kwa zawadi hii muhimu.

Nakupa hongera kwa sababu naamini kuwa ukiwa na uhai na nguvu ni zawadi tosha kwako wewe rafiki yangu ambae unatamani siku moja ufikie ndoto zako. Leo hii ningependa nikushirikishe stori muhimu katika maisha yangu ambayo ilitokea siku kama ya leo (24, Desemba). Karibu tuwe pamoja ili tujifunze kitu kutoka kwenye stori hii.

Stori yangu inaanzia hapa “Ilikuwa mwaka 1999 siku kama ya leo kipindi hicho nikiwa mwanafunzi wa darasa la tano, tukiwa tunajiandaa kusherekea Sikuu ya Christmas niliamua kwenda kukusanya kuni za biashara ili ninaposherekea Siku Kuu niwe na fedha kwa ajili ya kufurahi nikiwa na watoto wenzangu. Asubuhi na mapema baada ya kuamka niliipanga vizuri ratiba yangu kwa kuanza na kukusanya mzigo wa kwanza kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na baadae ndo nikaendea mzigo wa kuni za kuuza.
Baada ya kupangilia vizuri ratiba yangu nilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani siku hiyo niliweza kukusanya mizigo miwili ya kuni moja kwa ajili matumizi ya nyumbani na mwingine kwa ajili ya kuuza. Biashara ilienda vizuri kwani nilifanikiwa kupata fedha yangu shilingi 500 za kitanzania kama malipo yangu na ndipo nikarudi nyumbani nikiwa na tabasamu la kutosha kutokana na mafanikio ya siku hiyo na matarajio ya siku inayofuata kwani tayari uhakika wa kusherekea vizuri ulikuwepo.

Baada ya kufika nyumbani nilikuta nasubiliwa na mama mzazi (Mwenyezi Mungu amurehemu) kwa hasira sana kwa kile ambacho ilisemekana kuwa niliondoka bila kuaga na kibaya zaidi nilipoulizwa nilikuwa wapi ndo nikajibu kuwa nilienda kukusanya kuni za biashara. Ilinibidi nipokee kipigo cha hali ya juu kutokana na makosa hayo na kuonywa kuwa kwamwe hisije ikajirudia na kibaya zaidi nikanyanganywa ile shilingi 500 kwa kile ambacho ilisemekana mimi kama mtoto ni tabia mbaya kujizoesha pesa”.

Kwanini nimekushirikisha stori hii iliyonitokea mimi?
Rafiki leo hii nilipokumbuka mkasa huu nikaona nikushirikishe wewe ambae najua kwa sasa yawezekana ni baba/mama wa familia na tayari una watoto au kama bado haujaingia kwenye maisha ya ndoa ni matarajio yangu kuwa siku moja unatamani kuingia kwenye maisha haya. Ukiwa mzazi/mlezi natarajia kuwa wewe kama baba/mama unajua wajibu wako mkubwa wa kuhakikisha unakuwa kiongozi wa wanao katika kuwakuza kwenye misingi ya kiroho, kijamii na kiuchumi. Ni wazi kuwa kizazi kilichokuzwa vyema kwa kuzingatia misingi hii lazime kiwe kizazi chenye kila aina ya mafanikio.

Yamkini wazazi walio wengi wamekuwa wakiegemea kwenye makuzi ya kiroho na kijamii na kusahau msingi mkuu mwingine wa kumkuza mtoto kiuchumi. Katika msingi huu wazazi/walezi wengi badala ya kuwaendeleza watoto kiuchumi wamekuwa wakiua vipaji vya watoto wao na hivyo watoto kuendelea kuwa wategemezi siku hadi siku. Mbaya zaidi ni kwamba watoto hawa wanaendelea kuamini kauli za wazazi wao ambazo zilichangia kuua vipaji/ndoto zao na hatimaye tunakuwa na vizazi vyenye fikra hasi kwenye mafanikio ya kiuchumi. Mfano fikiria kama kauli hiyo iliyonitokea ya kuwa mimi kama mtoto sipaswi kujizoesha pesa kwani kwa kufanya hivyo ningekuwa mwizi. Naamini kauli kama hii imekuwa ikitumiwa na wazazi/walezi walio wengi kwa watoto wanaowalea na hivyo kupelekea watoto wengi kuamini kuwa ukipenda pesa sana utakuwa mwizi!! Matokeo yake ni watoto kubadiri fikra/mitazamo yao kuhusu pesa.

Mfano mzuri ni mimi baada ya kupigwa kutokana na makosa hayo ilinibidi niache kabisa kujihusisha na aina yoyote ile ya biashara kipindi chote cha utoto wangu na hata nilipokuwa katika elimu ya sekondari sikuweza kufanya biashara yoyote ambayo ingeenda kinyume na matakwa ya wazazi wangu. Matokeo yake ilinibidi nibadirishe kabisa fikra zangu na kufikiria masomo tu huku nikiamini kuwa masomo ndo mkombozi wa maisha yangu na hivyo kupelekea kuwa mtegemezi kwa wazazi wangu kipindi chote cha masomo yangu.
Rafiki yangu mpendwa kama mzazi/mlezi naomba utambue kuwa wewe una wajibu mkubwa wa kuhakikisha unamuongoza mwanao ili aweze kuendeleza vipaji alivyonavyo hasa linapokuja suala zima la vipaji vya kujikomboa kiuchumi. Fikiria kama bilionea Bill Gates angekatishwa tamaa na wazazi leo hii angekuwaje? Wapo wakina Bill Gates wengi ambao ndoto zao zimekatishwa kutokana na mazingira ya malezi yao hivyo kama mzazi unatakiwa kulitambua hilo na kusimama imara.

Rafiki yangu naomba pia utambue kuwa wanamafanikio walio wengi ni wale ambao wamefanya vitu wanavyovipenda kutoka rohoni mwao na si wale ambao wamekalilishwa kuwa mwanangu nenda shule soma kwa bidii ili upate kazi nzuri itakayokuwezesha kulipwa vizuri na hatimaye uweze kutusaidia wazazi wako. Ndio maana wanamafanikio wengi ni wale ambao mwanzo walikataliwa na jamii kutoka na yale wanayofanya kuonekana yanaenda kinyume na mazoea ya jamii. Kutokana na ukweli huu ni wazi kuwa vizazi hadi vizazi vinapita pasipo kuwa na misingi imara ya elimu fedha na hivyo kuzalisha vizazi ambavyo ni tegemezi kwa kuwa jamii inapenda kuishi kwa mazoea. Rafiki yangu naomba wewe kama mzazi/mlezi mtarajiwa hepuka sana kumlea mwanao kwa mazoea ya jamii bali hakikisha unaendelea kujifunza vipaji alivyonavyo ili umsaidie kuviendeleza. 


Mpendwa rafiki yangu naomba utambue kuwa kutokana na wengi wetu kukosa misingi ya elimu ya fedha tumeendelea kuadhibiwa na dunia kwenye upande wa elimu hii na hivyo kuwa masikini kizazi hadi kizazi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa tumekuwa tukiishi kwenye mazoea ya jamii ambayo yanaenda kinyume na kanuni za mafanikio ya fedha. Matokeo yake ni kurudia makosa yaleyale ambayo yalifanywa na mababu zetu na hivyo kujikuta hatusogei kokote mpaka tunaishia kuimba nyimbo zilezile….hoo familia yetu hatujawahi kuwa matajiri hivyo na mimi siwezi kuwa tajiri!, sina fedha za kutosha kuanzisha biashara!, Serikali imekaza hivyo hatuwezi kutimiza ndoto zetu… na nyimbo nyingine nyingi.

Mpendwa rafiki yangu tambua kuwa kutokana na kuishi kwa mazoea tumebadirishwa fikra zetu na jamii na hivyo kuaminishwa kuwa mafanikio ya kifedha ni kwa wateule wachache. Jambo hili limepelekea kuamini kuwa wewe kamwe hauwezi kuwa kati ya hao wachache kitu ambacho si kweli. Kama mzazi naomba utambue kuwa una wajibu mkubwa wa kumuandaa mwanao ili aweze kuwa na misingi imara ya elimu ya fedha na hatimaye tufanikiwe kuwa na kizazi chenye kila aina ya ubunifu katika kujitengenezea kipato hivyo kuondoa utegemezi unaotuandama kwa sasa. Badala ya kuendelea kuilalamikia Serikali naomba ujiulize wewe kama wewe wajibu wako ni upi katika kufanikisha maendeleo ya taifa hili hasa ukianzia na wajibu wako katika kukuza vipaji vya watoto wako kiroho, kijamii na kiuchumi.

Mwisho naomba nikutakie sherehe njema za Siku Kuu ya Christmas hapo kesho nikiamini kuwa kesho itakuwa siku yako nzuri ya kukaa pamoja na familia yako na kutafakari mambo makuu Mwenyezi Mungu aliyokujalia kupitia familia hii. Mpendwa rafiki yangu niendelee kukuomba kusambaza jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadirisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi.
Karibuni kwenye ulimwengu wa elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com


Fahamu Sababu Zilizosababisha Ushindwe Kufikia Malengo Yako Mwaka 2016

Rafiki yangu mpendwa ni matumani yangu kuwa haujambao na unaendelea na mapambano ya kufanikisha ndoto zako. Rafiki mpendwa nimekuwa nikikusisitizia umuhimu wa kuandaa kesho yako kwa kuahakkikisha unatumia muda vizuri ulionao kwa sasa ili kupitia yale unayoyafanya sasa yawe msingi wa ushindi ndoto zako hapo baadae. Kupitia kanuni hii ni wazi kuwa hakuna kesho bora pasipo kuwa na leo bora.


Baada ya utangulizi huu unaolenga kukupa hamasa na kutambua wajibu wako katika kufikia ndoto zako, leo hii ningependa tusafiri wote katika safari ambayo kituo chetu cha kwanza kinaitwa Januari Mosi, 2016 na mwisho wa safari yetu ni 31 Desemba, 2016. Mpendwa rafiki ni matumaini yangu kuwa kama una ndoto na ungependa kuzitimiza siku moja ni lazima unapoanza mwaka mpya huwa unaweka malengo ambayo hadi mwisho wa mwaka unahitaji yawe yamekamilika. Naamini rafiki yangu kuwa wewe ni tofauti na wale wengine ambao wamekuwa wakihitaji siku moja kuwa na mafanikio makubwa pasipokuweka jitihada zozote bali wakisubiria muujiza utokee. Kama unataka mwaka 2017 ufikie malengo yako tofauti na mwaka huu endelea kusoma makala hii hadi mwisho ili ufahamu siri kubwa ambazo zimekuwa zikikukwamisha mwaka hadi mwaka. Karibu ujifunze hapa chini;

Siri ya kwanza; Mwaka 2016 umekuwa mtu wa kulalamika; hakuna sumu kubwa ambayo imekuwa ikiua ndoto za walio wengi kama malalamiko. Watu wengi wamekuwa wakitafuta sababu za kuhalalisha kushindwa kwao kuonekane kuwa wameshindwa kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao. Mfano, mwaka 2016 watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imesababisha maisha kuwa magumu kwa misingi kuwa hali ya kifedha si shwari. Leo hii jiulize kama hali ya kifedha ilikuwa shwari katika Serikali ya Awamu ya Nne wewe kama wewe imekusaidia vipi kutimiza ndoto zako? Ili upate mafanikio unayoyataka ni lazima ufahamu kuwa Serikali haiwezi kukutimizia ndoto zako kwani hata yenyewe imeshindwa kutatua matatizo iliyonayo. Fahamu pia kuwa katika hali yoyote ile wewe mwenyewe ndo unajua kile unachohitaji au vile unavyotaka uwe hivyo ni wajibu wako kuanza kufanyia kazi ndoto yako sasa.

Muhimu: Aanza Januari, 2017 kwa kujitwisha msalaba wa maisha yako ukitambua kuwa wewe ni muhusika namba moja wa maisha yako na pale ambapo utashindwa kutimiza ndoto zako fahamu kuwa wa kulaumiwa ni wewe mwenyewe na wala si Serikali, familia, mwajiri wako wala mazingira yoyote yale.

Bonyeza kiunganishi hiki kusoma makala ya wewe ni mshindi huna sababu ya kushindwa: http://fikrazakitajiri.blogspot.com/2016/12/wewe-ni-mshindi-huna-sababu-ya-kushindwa.html

Siri ya pili; Mwaka 2016 uliruhusu hofu ya kushindwa ikutawale badala ya kuruhusu hamu ya mafanikio: Mpendwa rafiki yangu wanasaikolojia wanatuambia kuwa sisi ni zao la kile ambacho tunawaza mara kwa mara. Kwa maana hii sisi ni waumbaji wa maisha yetu ya baadae “we are the creator of our own destiny”. Kwa ukweli huu ni wazi kuwa mwaka 2016 kama uliruhusu hofu ya kushindwa kuliko hamu ya kushinda maana yake ni kwamba wewe mwenyewe ulijijengea msingi wa kushindwa kuliko kushinda na hivyo matokeo yake umehindwa kutimiza malengo yako.

Muhimu: Katika kipindi chote cha mwaka 2017, hakikisha hauruhusu hofu kuyatawala maisha yako. Iambie nafsi yako kuwa mimi ni mshindi na nimeumbwa kwa ajili ya kushinda bila kujali ni mazingira yapi napitia kwa sasa na kwa mtazamo huu nitashinda chochote kile ambacho nitadhamiria kufanya. 

Siri ya tatu; Mwaka 2016 umekuwa mtu wa kuhairisha mambo. Huu ni ugonjwa ambao umeangamiza ndoto nyingi na umekuwa ukisababishwa na watu wengi kuona kuwa muda upo wa kutosha. Watu wengi wametawaliwa na kauli za nitafanya badala ya kauli za ninafanya. Ulipoanza mwezi wa kwanza 2016 uliona kuwa mwaka ni mrefu na hivyo kusogeza kile ambacho ulikuwa umepanga kukamilisha kwenye miezi ya baadae hadi ukajikuta robo ya kwanza imekatika, nusu ikapita, hadi robo ya tatu na mwisho wake ukakata tamaa na kujisemea kuwa mwaka huu mambo yangu yamenibana ngoja nijipange kwa ajili ya mwakani.

Muhimu: Mwaka 2017 tambua kuwa hakuna siku hata moja ambayo hautabanwa na mambo yako na hivyo hakikisha unafanya mara moja kile ambacho umelenga kukamilisha. Haijalishi unaanza kwa kiasi kidogo sana cha msingi wewe anzisha ukiwa na picha kubwa unayotaka kuifikia.

Siri ya nne; Mwaka 2016 ulitumia kiasi chote ulichokipata pasipo kujiwekea akiba: Imekuwa ni kawaida ya watu walio wengi kutumia kiasi chote wanachopata pasipo kujiwekea akiba kwa ajili ya baadae. Binafsi nilikuwa kwenye kundi hili lakini siku moja katika kujisomea vitabu vya kanuni/siri za mafanikio nikakutana na kanuni ya “Kujilipa Kwanza”. Kanuni hii ni rahisi sana na unachotakiwa kukifanya kupitia kanuni hii ni kuhakikisha unajiwekea sheria ya kwamba kila shilingi inayoingia mkononi mwako lazima ikatwe asilimia fulani kwa ajili ya akiba yako ya baadae. Binafsi nimekuwa nawekeza asilimia kumi ya kila shilingi inayoingia mikononi wangu. Nitafute kwa watsapp kupitia namba 0786 881 155 kwa ajili ya kufundishwa zaidi namna gani unaweza kujilipa kwanza kwa muda mrefu ukiongozwa na nidhamu ya hali ya juu pasipo kushawishika kutumia hiyo akiba yako. Ni aibu sana mwajiriwa au mtu yeyeto mwenye uhakika wa kupata kipato hata kama ni kidogo kiasi gani kufikia mwisho wa mwaka ukiwa hauna hata shilingi uliyoiweka kwa ajili ya akiba yako ya baadae.

Muhimu: Mwaka 2017 tumia kauli ya hata mbuyu ulianza kama mchicha kuhakikisha kuwa unaanza kujiwekea akiba hata kama ni kidogo kiasi gani cha msingi uongozwe na nidhamu binafsi ya hali ya juu.

Siri ya tano; Mwaka 2016 hukuwa na orodha ya malengo yako iliyoandikwa: Ukiwa na malengo kichwani mwako pasipo kuyaandika sehemu ni moja ya sababu nyingine inayowakwamisha walio wengi hii ni kutokana na ukweli kuwa kadri utakavyokuwa unayosoma mara kwa mara ndivyo utakavyokuwa na hamasa ya kupigana kuyatimiza. Kuna sababu kuu nne za kwanini unapaswa kuyaandika malengo yako kwenye karatasi au compyuta yako:
a)    Ni rashisi kuyarejea na hivyo unaweza kuyakumbuka pindi unapoyatekeleza;
b)   Yanapimika. Ni rahisi kujua kuwa unatekeleza lipi kwa muda gani;
c)    Yanajieleza vizuri tofauti na kuwa nayo kichwani mwako; na
d)   Ni rahisi kuyahuisha (review) ili kuendana na hali halisi ya wakati huo.

Muhimu: Mwaka 2017 nunua kijitabu kidogo (diary) kwa ajili ya kuandika malengo yako na mambo mengine muhimu na hakikisha kijitabu hicho unasafiri nacho kila sehemu na hakikisha unayasoma kila siku.

Siri ya sita; Mwaka 2016 uliruhusu muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii na malumbano yasiyo na tija kuliko kwenye mambo yako binafsi: Mpendwa rafiki yangu hakuna kitu kibaya ambacho kwa sasa kinaharibu vijana kama kukua kwa teknolojia ya mawasiliano. Vijana wengi kwa sasa wanashinda kwenye mitandao ya kijamii wakisubiria kupost na kuchangia kwenye mada mbalimbali. Kumbuka kile unachokiwaza/kufanya muda mwingi ndicho kinakutambulisha jinsi ulivyo, kwa ukweli huu ni wazi kwamba kadri unavyoshinda kwenye mitandao ya kijamii ndivyo unapoteza muda ambao ungeutumia kuwaza au kufanya vitu vya maana kwa ajili ya kutimiza malengo yako.

Muhimu: Mwaka 2017 aanza kwa kupunguza makundi yote ambayo hayana mchango wa maana kwenye kutimiza ndoto zako. Jiepushe na makundi au marafiki ambao walishakata tamaa ya mafanikio na hakikisha unajiunga na marafiki wapya wenye mtazamo kama wako.

Siri ya saba; Mwaka 2016 umeishi maisha ya kuigiza: Rafiki mpendwa kamwe hauwezi kufanikiwa kama hauishi vile unavyotaka wewe badala yake umekuwa mtu wa kuiridhisha jamii au watu wako wa karibu. Katika dunia ya sasa imekuwa ni kawaida watu kuishi kulingana na matakwa ya jamii au ndugu zao na hivyo kujikuta hawana vipaumbele vya maisha yao. Rafiki yangu naomba ujifunze kusema HAPANA pale unapoona maisha unayoishi hayaendani na matakwa yako. Pia, jifunze ukweli kuwa sio kila unaloambia hapana ni hapana kwani jamii tunayoishi kwa sasa ina kila sababu ya kukuonesha kuwa hauwezi kufanikiwa na hivyo kukukatisha tamaa.

Muhimu: Mwaka 2017 hakikisha unaishi misingi ya maisha yako vile unavyotaka wewe na si jinsi gani jamii ilivyozoea. Hakikisha unaishi kwa kufanya vitu kwa hali tofauti ya mazoea ya jamii.

Mpendwa rafiki yangu nimekushirikisha siri saba ambazo zimekukwamisha mwaka 2016. Ni matumaini yangu kuwa makala hii itakusaidia kutimiza malengo yako kwa mwaka 2017. Mpendwa rafiki yangu kama umejifunza kitu kwenye makala hii naomba uisambaze kwa kadri uwezavyo ili siri hizi ziwafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadirisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Karibuni kwenye ulimwengu wa elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com




Dunia Inabadilika kwa Kasi Sana; Je Umeijenga Safina Yako?

Mpendwa rafiki yangu kwenye ukurasa huu wa facebook naamini kuwa upo vizuri na unaendelea kupambana ili kuhakikisha kuwa kesho yako inakuwa bora kwani naamini unatambua kuwa hakuna kesho bora ambayo haikundaliwa. 

Kama ndo hivyo ni jambo la kujivunia kwa hatua hiyo katika safari uliyoianzisha. Safari hii ni ndefu na tofauti na safari nyingine yenyewe haina mwisho badala yake imejaa milima na mabonde. Ni katika safari hii unatambua kuwa kadri unavyomaliza hatua moja ndivyo unavyojifunza kuwa kuna hatua zaidi mbele. Nelson Mandela alilielezea hili vizuri; nanukuu tafsiri ya Kiswahili “Baada ya kupanda kilima na kufika kileleni ndipo nilipojifunza kuwa kuna vilima vingi ambavyo napaswa kuvipanda”

Hivyo mpendwa rafiki yangu hakikisha kuwa kila iitwapo leo unafanya jambo ambalo ni ushindi wa kukufikisha kwenye kilele cha mafanikio huku ukitambua kuwa ushindi mmoja unaanzisha safari nyingine.

Kama ambavyo tumeona kuwa maisha ni safari ambayo haina mwisho endapo upo duniani humu ndivyo ilivyo kwenye elimu. Leo hii ningependa rafiki yangu nikuletee makala inayohusu jinsi gani dunia inavyobadirika kwa kasi na namna ambavyo unatakiwa kujilinda dhidi ya mabadiriko haya, kwa maana nyingine unatakiwa kuijenga safina yako. Karibu tujifunze wote na baada ya mafundisho haya ujiulize je umeijenga safina yako??

Kabla ya kuanza somo la leo ningependa tujikumbushe kidogo kwenye kwenye historia ya binadamu na ugunduzi wa teknolojia. Tuliopita shule tunakumbuka kuwa binadamu amepitia kwenye mifumo ya ugunduzi wa teknolojia tokea kipindi cha zama za mawe, kikafuatiwa na kipindi za zama za chuma, kilichofuatiwa na mapinduzi ya viwanda na baadae ndipo zama za taarifa (information era).

Katika mapinduzi haya ujifunze yafuatayo; Moja, Mabadiriko ya teknolojia yanalenga kuongeza tija ya utendaji kazi pamoja kuongeza/kuboresha uzalishaji mali. Kwa maana ya kwamba binadamu amekuwa na ugunduzi wa teknolojia ambayo moja kwa moja unalenga katika kurahisisha utendaji kazi. Mfano, katika zama za mawe mwanadamu alitegemea zaidi matumizi ya vifaa vya mawe ambavyo utendaji na uzalishaji wake ulikuwa duni ilikilinganishwa zama za mapinduzi ya viwanda.

Pili, kila umbuzi wa teknolojia unalenga kuimaliza kabisa teknolojia iliyokuwepo mwanzo au kuiboresha kwa ajili ya ufanisi zaidi. Mfano, ugunduzi wa teknolojia ya habari/mawasiliano umepelekea kuboresha utendaji kazi wa sekta ya viwanda. Sote ni mashahidi kuwa kwa sasa dunia imekuwa ni familia moja ambayo kila linatokea sehemu yoyote linaweza kumfikia mtu yeyote cha msingi awe ameunganishwa na ulimwengu mpya kwa maana ya mtandao wa intaneti. Kwa maana hiyo ni rahisi mtu kutangaza bidhaa zake na kuuza popote apendako kwa urahisi zaidi ata kama yeye hajawahi kufika huko.

Tatu, kila ugunduzi wa teknolojia upo kwa ajili ya mafanikio yako. Tumeona ni jinsi gani mwanadamu aliweza kuboresha hali ya maisha yake kipindi cha zama za chuma ikilinganishwa na zama za mawe. Pia, baada ya mapinduzi ya viwanda ukisoma historia utaona kuwa ndipo mfumo wa upebapari ulipoibuka kwa kasi. Kwa hisitoria utagundua kuwa katika kipindi hicho ndipo mataifa mengi yalikuwa na mitaji ya kutosha na ndipo wakaanza kutafuta sehemu za uwekezajaji nje ya mipaka yao.

Ninachotaka ujifunze hapa ni kuwa katika kipindi cha ubepari au kipindi cha mapinduzi ya viwanda ndipo matajiri wengi wa historia waliweza kufanikiwa kiuchumi, mifano michache ni kama Andrew Carnegie ambaye alikuwa tajiri kupitia kiwanda cha kutengeneza vyuma (steel industry) na bilionea mwingine ni John D. Rockefeller ambaye alifanikiwa kupitia biashara ya mafuta. Lakini pia, angalia kipindi hiki cha mapinduzi ya habari/teknolojia ya mawasiliano ambacho mtu anaweza kulala masikini na akaamka tajiri. Katika kipindi hiki jarida la Marekani la Forbes linakuambia kuwa ni kipindi ambacho kimetengeneza mabilionea wengi kuliko kipindi chochote kile, mifano michache ni kama Bill Gates kupitia ugunduzi wake wa Microsoft na Mark Zuckerberg mmiliki wa facebook na wengineo wengi.. swali la kujiuliza ni je umeijenga safina yako katika kipindi hiki cha mapinduzi ya mawasiliano???

Nne, kila uvumbuzi wa teknolojia unasababisha mifumo ya maisha ya mwanadamu kubadirika. Hapa ndipo patamu, kama hujagundua kuwa dunia inabadirika na inakutaka kwa lazima ubadirike utateseka sana kwa vile utaendelea kuishi katika mfumo ambao umepitwa na wakati. Mfano mzuri enzi za babu zetu na baba zetu ilikuwa ni kawaida kutuambia kuwa nenda shule mwanangu na ujifunze kwa bidii ili uje upate ajira nzuri kwa ajili ya kutusaidia wazazi wako….. lakini leo hii kizazi chetu ni mashahidi kuwa wapo wasomi wengi wanaoendelea kuhangaika mitaani kwa ajili ya ajira pasipo mafanikio. Dunia imebadirika lazima tubadirike na kufikilia zaidi kuwasomesha watoto wetu kwa ajili ya wao kuzalisha ajira nasi kutegemea ajira. Kama mzazi hakikisha unaanza kuzalisha ajira leo hii kwa kadri uwezavyo ili kesho na kesho kutwa mwanao ukamwajiri kipindi anaanza maisha yake.

Dunia imebadirika… zamani ilikuwa ni kawaida mwanafunzi kusomeshwa bure na Serikali kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu, baada ya hapo kikafuatia kizazi cha bodi ya mikopo ya wanafunzi (ambacho ndio kizazi chetu) ambacho tumekopeshwa kabla ya hata kujua tutarudisha vipi hiyo mikopo na leo hii tunaitwa wadaiwa sugu. Pamoja na hayo tutakumbuka kuwa kipindi chetu mikopo hata kama ilikuwa kwa madaraja lakini wanafunzi wengi walipata mikopo. Dunia inabadirika leo hii kupata mikopo ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Sipo kuelezea ugumu wa kupata mikopo kwa sasa la hasha kwani mimi kamwe si mtu wa kulalamikia mfumo bali ninachotaka ujifunze hapa ni kuwa dunia inabadirika kwa kasi sana hivyo ni vyema ukaanza kujenga safina yako kwa ajili ya masomo na ajira ya watoto wako pamoja na ndugu zako kwa kizazi chako na vizazi vyao. Je umeijenga safina?

Mwisho, kadiri dunia inavyobadirika ndivyo inavyowainua watu na kuwaangamiza wengine. Mfano, kuna biashara ambazo enzi zilizopita zilikuwa zinavuma sana na ilikuwa rahisi wamiliki kutengeneza faida kupitia biashara hizo lakini leo hii biashara hizo hazifai kitu tena, mifano michache ni kama biashara ya internet cafรฉ baada ya ugunduzi wa smartphone hazifai kitu tena kwa sababu kila mtu anatembea na intaneti mikononi mwake, mfano mwingine ni biashara ya modem kwa sasa hazifai kitu tena kwani kila mwenye smartphone anaweza kuunganisha intaneti na compyuta yake na mfano mwingine ni ugunduzi wa kutuma pesa kwa njia ya simu kulivyoharibu soko la western union na mengine mengi. Jenga safina yako ukiwa makini kungalia ni biashara hipi inafaa katika kipindi hiki cha mapinduzi ya teknolojia ya habari/mawasiliano.

Mpendwa rafiki yangu nimekushirikisha mambo matano ya kukuonesha kuwa tupo katika dunia ambayo inabadilika kwa kasi. Naomba utumie makala hii kujikumbusha na kujitazama upya kama unacheza ngoma ambayo inachezwa na walimwengu wa sasa hasa katika kufikia ndoto zako. Tengeneza safina yako juu ya msingi imara ili kesho na kesho kutwa hisiyumbishwe na mawinbi ya dunia.

Kama umejifunza kitu kwenye makala hii naomba uisambaze kwa kadri uwezavyo ili somo hili liwafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuifanya dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Karibuni kwenye ulimwengu wa elimu hisiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big


A.M. Bilondwa

0786881155
fikrazakitajiri@gmail.com

Wewe ni Mshindi Huna Sababu ya Kushindwa

Habari ya leo mpenzi msomaji wa makala hizi katika ukurasa huu wa Facebook. Ni matumaini yangu kuwa upo vizuri na unaendelea kupambana ili kuifanya kesho yako kuwa bora zaidi ya leo yako. Nasema hivyo kwa matumaini ya kwamba mpendwa rafiki yangu unafahamu kuwa hakuna kesho bora ambayo haijaandaliwa kwa jana yake. Hivyo naomba uendelee kukazana kila iitwapo leo kwa ajili ya mafanikio makubwa ya baadae. 

Karibu tujifunze wote ambapo leo hii nimelenga nikuoneshe nguvu ya ajabu iliyopo ndani mwako ambayo ipo toka siku uliyoumbwa na ni nguvu hii ambayo imekuwa ikiwatengeneza mabillionaire na mamilionea kila kukicha ikitegemea na jitihada zao katika kutumia nguvu hii. Kama unataka kujifunza zaidi juu ya nguvu karibu tujifunze wote.
Kabla ya kuanza ningependa utafakali sehemu hii ya sura ya biblia takatifu Mwanzo 1:26, nanukuu “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi”. Baada ya kutafakari sehemu hii ya maandiko matakatifu karibu nikushirikishe mambo makuu matano ambayo hujawai kufikilia mchango wake katika mafanikio yako.
MOJA: TUMEPEWA NGUVU YA KUUMBA KITU CHOCHOTE TUNACHOTAKA: Sehemu ya maandiko matakatifu tuliyosoma hapo juu inatukumbusha kuwa tumeumbwa kwa mfano wa Mwenyezi Mungu na tukapewa nguvu ya kutawala vitu vyote vilivyopo duniani humu. Hata hivyo tunatakiwa kufahamu kuwa kwa kuumbwa kwa mfano wake tumepewa nguvu ya kuwa waumbaji katika mazingira yetu yanayotuzunguka kwa kutumia vitu ambavyo tuna mamlaka ya kuvitawala. Pointi muhimu ambayo nataka uondoke nayo ni kwamba chochote kile ambacho utaweka dhamira kiasi kwamba kikawa ni sehemu ya fikra zako za kila muda basi hakuna muhujiza wa kukuzuia kupata kitu hicho. 

Watu wengi waliofanikiwa ambao nimefuatilia historia zao wametumia siri hii kupata mafanikio ya hali ya juu. Mfano, mgunduzi wa magari ya V8 HENRY FORD, alitumia siri hii kufanikiwa kutengeneza kwa mara ya kwanza gari la kifahari lenye silinda (cylinder) nane ndani ya injini moja. Mwanzoni alipotoa wazo hili kwa wafanyakazi wake alipewa jibu kuwa haiwezekani kutengeneza gari lenye silinda nane ndani ya injini moja lakini jibu alilowapa lilikuwa endelea mpaka mfanikiwe kwani nahitaji gari la modeling hiyo. Aliporudi kuwauliza mara ya pili alipewa jibu sawa na lile la kwanza lakini akawaambia ni lazima nipate gari hilo endelea kulifanyia kazi. Hali iliendelea hivyo mpaka mara nne. Lakini hatimae leo hii tunatembelea magari ya kifahari ya V8 kutokana na nguvu ya uumbaji aliyokuwa nayo Henry Ford.
MUHIMU: Tafakari kwa kina juu ya nguvu uliyonayo katika kuumba vitu kimawazo na kivitendo na kisha iambie nafsi yako kuwa nitaumba vitu vingi kwa kadri niwezavyo pasipo kukatishwa tamaa na maneno ya watu.
MBILI: KILA KILICHOPO DUNIANI HUMU NI KWA AJILI YA USHINDI WAKO: Kila mahali ulipo kuna fursa ambayo inakusubilia wewe uitumie na kuiendeleza ipasavyo. Kuna msemo usemao kuwa “kila mahali kuna dhahabu japo watu wengi hawajui jinsi ya kuitafuta”. Naamini unakubaliana na msemo huu, binafsi nimekuwa nikiutumia kila siku na kila sehemu ninapokuwa hasa sehemu zinazokimbiwa na watu kwa kuonekana hazifai kitu. Mpendwa rafiki yangu fungua macho na kutazama ipasavyo mazingira yanayokuzunguka na kila kukicha hakikisha unatumia fursa zilizopo kwa kadri uwezavyo.
MUHIMU: Fahamu ya kuwa kila sehemu ulipo kuna dhahabu hivyo jukumu lako kubwa ni kujifunza jinsi gani wengine wamefanikiwa kuchimba dhahabu hiyo kwa mafanikio makubwa sana.
TATU: WEWE NI KIUMBE PEKEE CHENYE UWEZO WA KUCHAGUA JEMA NA BAYA. Kila mwanadamu amepewa uwezo wa hali ya juu wa kuchagua kati ya jema na baya. Ubongo wa mwanadamu ni sehemu yenye mfumo wa hali ya juu unaowezesha kila linalofanyika kupitia kwenye mfumo huu. Ubongo huu umegawanyika kiasi kwamba kila sehemu ina jukumu lake ambalo inalifanyia kazi. Linalofanywa au kutamkwa lazima lipitie kwenye sehemu ya ubongo inayojihusisha na fikra na ndipo muhusika anafanya kile kilichofanyiwa kazi kwenye ubongo. Kwa maana nyingine ni kwamba ubongo ndo kompyuta ya asili ya binadamu ambayo jukumu lake kubwa ni kuchakata taarifa zote zinazoingizwa na hatimaye kutoa matokeo. Kwa maana hiyo matokeo yatakayotoka yatategemea taarifa zinazoingizwa (garbage in garbage out). Ukiujaza ubongo wako taarifa za uovu, hofu, chuki, kusengenya, kukata tamaa na kushindwa vivyo hivyo utegemee matokeo yanayoendana na hayo.
MUHIMU: Kuanzia sasa fahamu kuwa unaweza ukaamua kutenda mema tu na ukafanikiwa kwani wewe ndo rubani namba moja wa fikra zako. Pia iambie nafsi yako kuwa kuanzia sasa utaujaza mfumo wako wa ubongo na taarifa za ushindi kwani kwa kufanya hivyo unajitengenezea mazingira unayotaka kuyaishi.
NNE: WEWE NI KIUMBE PEKEE MWENYE KUWEZA KUAMUA HATMA YA MUDA WAKO: Wewe ni wa pekee kwa vile unao uwezo wa kuamua nini kifanyike katika kila sekunde ya maisha yako. Ushindi wako unatokana na jinsi gani unatumia muda wako. Kinachotofautisha watu waliofanikiwa katika maisha yao na wale ambao ni watu wa kawaida ni namna ambavyo makundi haya yanatumia muda wao. Wote tumepewa sekunde, dakika, Masaa sawa lakini tofauti yetu ni jinsi tunavyotumia zawadi hii. Wapo wanaotumia zawadi hii kwa kuchart 24/7, wapo wanaotumia kwa kuangalia luninga 12/7, wapo wanaotumia kubeza wengine, wapo wanaotumia kucheza kamali….n.k. lakini kumbuka kuwa kila unalolifanya kwenye kila sekunde ya maisha yako lina mchango mkubwa katika mafanikio yako na hivyo kuamua wewe ni mtu wa aina gani.
MUHIMU: Kuanzia sasa fahamu ya kuwa wewe ni mshindi wa maisha yako kama utaamua kutumia vizuri muda wako. Fahamu ya kuwa jinsi ulivyo ni matokeo ya yale unayoyafanya kwa kila sekunde ya maisha yako. Chukua hatua sasa ili uwe mshindi.
TANO: NI WEWE PEKEE MWENYE HAMASA NDANI YAKO: Katika mafanikio hamasa ni ule msukumo unaokufanya uendelee kufanya kile unachokifanya. Msukumo huu unaweza kutoka ndani kwa ndani au msukumo wa nje. Mara nyingi msukumu unaotoka nje huwa ni wa muda ukilinganisha na msukumo unaotoka ndani mwako. Ili upate mafanikio ni lazima uwe na hamasa ya hali ya juu inayokupa msukumo wa kuendelea kufanya. Kuna msemo kuwa “unaweza kumpeleka punda kunywa maji lakini hauwezi kumulazimisha kunywa maji”, hii ina maana kwamba hamasa ya nje haiwezi kukubadilisha kama wewe mwenyewe haujaamua kubadilika. Jambo jingine la kukumbuka ni kwamba hamasa ya ndani sio kitu cha siku moja bali inatakiwa iwe sehemu ya maisha yako ya kila siku sawa na ambavyo kila siku lazima ule hauwezi kusema kuwa leo nakula chakula cha kutosha siku zote za maisha yangu bali kila siku unatakiwa upate chakula vivyo hivyo ndivyo ilivyo hamasa ya ndani (self motivation). 

Tunaweza kusoma maandiko mbalimbali kuhusu mafanikio ya watu waliofanikiwa kimaisha na kuhamasika kwa muda lakini kama hatujaamua kufanya hamasa hiyo kuwa sehemu ya maisha yetu itakuwa sawa na bure. Mfano mzuri ni wewe mwenyewe umekuwa kila mwanzo wa mwaka unaweka malengo na kujisemea rohoni kuwa mwaka huu naanza mwaka mpya na mambo mapya kwa maana unaachana na mabaya uliyoyafanya kwa mwaka unaoisha lakini ghafla kadri mwaka unavyoendelea unajikuta unarudia makosa yale yale. Kumbe hii inatokana na msukumo wa nje unaoupata kutokana na jamii kuzoea kufanya hivyo mwaka hadi mwaka.
MUHIMU: Kuanzia sasa ifundishe nafsi yako kuwa na hamasa ya kudumu inayotoka ndani kwa ndani na hamasa hii iwe ni sehemu ya maisha yako ya kila siku. Ili kufanikisha hili tengeneza malengo yako ya muda mfupi na muda mrefu na kuanza kuyafanyia kazi mara moja.
Mpendwa rafiki yangu nimekushirikisha mambo matano ya kukuonesha kuwa wewe ni mshindi na hauna sababu ya kushindwa. Naomba utumie kila siku ya maisha yako kuhakikisha unafanyia kazi yale ambayo unatamani yawe sehemu ya ushindi wako. Fahamu kuwa hakuna mwaka kama hakuna sekunde. Vivyo hivyo hakuna mafanikio makubwa pasipo kusherekea ushindi mdogomdogo. Tengeneza ushindi wako kila iitwapo leo ili ushindi huo uwe sehemu ya hamasa yako.
Kama umejifunza kitu kwenye makala hii naomba uisambaze kwa kadri uwezavyo ili somo hili liwafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuifanya dunia hii kuwa mahali pazuri pakuishi. Karibuni kwenye elimu hisiyokuwa na mwisho.

A.M. Bilondwa

0786881155
bilondwam@yahoo.com