ZIJUE SHERIA ZA ASILI NA JINSI UNAYOWEZA KUZITUMIA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA SANA - SEHEMU YA PILI

Naamini rafiki yangu unaendelea vizuri katika mapambano yako ya kutimiza ndoto ulizonazo kwani naamini kuwa wewe kama rafiki una ndoto kubwa na nyingi ambazo unatamani kuzifikia. Kama tulivyoona kwenye ujumbe wangu uliopita uliohusu nguvu ya sheria za asili katika kuboresha maisha yetu ya kila siku ambapo tuliona nguvu ya sheria ya asili ya KUPANDA NA KUVUNA, leo hii ningependa tuangalie sheria nyingine ya asili na mchango wake katika maisha yetu ya kila siku.
Kabla ya kuangalia sheria nyingine ningependa kwanza nitangulize shukrani zangu kwa wale waliosoma ujumbe wangu nakuweza kutoa mrejesho. Naamini kuwa hata wale ambao hamkuweza kutoa mrejesho mliweza kutafakari nguvu ya sheria hii ya kupanda na kuvuna katika maisha yenu ya kila siku. Kama mlifanikisha hilo ni jambo la kheri na la kujivunia. Karibu nikushirikishe sheria ya asili hapa chini;
IJUE SHERIA YA ASILI YA KUOTA (The Law of Germination)
Sheri hii ni moja ya sheria ya asili ambayo ina nguvu sana katika kuwatofautisha watu waliofanikiwa sana katika ndoto zao na wale ambao wameshindwa kuzifikia ndoto zao. Kwa ufupi sheria hii inasema kuwa kila mbegu inayopandwa inahitaji muda ili iweze kukomaa na kuzaa matunda. Maana yake ni kwamba kila ndoto uliyonayo kwanza ni lazima upande mbegu (kwa maana ya kuitafsiri ndoto katika mradi) na mbegu hii unatakiwa kuipa muda ili izae matunda.
Katika kutimiza hili wengi wetu tumeshindwa kutimiza sheria hii ya asili kwa kuwa tumekuwa tunahitaji matokeo ya haraka haraka kwa kile tunachokifanya. Mfano, mtu anaanzisha mradi na anataka ndani ya siku chache uwe umetimizia ndoto zake pasipo kukumbuka kuwa mafanikio ni mchakato ambao unafikiwa kwa kufanya vitu vidogo vidogo pasipo kupoteza malengo kwa muda mrefu (Success is created by following simple fundamental principles consistently over time). Kwa maana hiyo ili tuweze kuitumia sheria hii ya asili kwa manufaa yetu tunatakiwa kufahamu kuwa ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunafanya mambo makuu yafuatayo;-
Mosi, kuthamini ushindi mdogo mdogo tunaoupata katika jitihada zetu za kila siku. Tunatakiwa kufahamu kuwa hata hao mabilionea tunaowasikia walianza kama sisi. kuna muda hawakuwa na kitu kama tulivyo sasa lakini kwa kutambua mahitaji ya ndoto zao waliweza kuweka bidiii na hatimaye leo hii wamefanikiwa.
Pili, Hakuna njia ya mkato. Ili kufikia mafanikio makubwa sana tunayoyatamani ni lazima tuwe tayari kujitoa hasa. Ni lazima kutambua ni kipi upo tayari kujitoa sadaka kwa njia halali ili kukuwezesha kutimiza malengo uliyonayo. Lazima uwe tayari kufanya kazi kwa bidii, lazima ujinyime baadhi ya starehe na lazima uwe tayari kuweka akiba kwa kila shiilingi inayoingia mikononi mwako na mengine mengi.
Tatu, Lazima uwe tayari kusoma na kujifunza kutoka wale waliofanikiwa katika kile unachofanya. Elimu haina mwisho hivyo katika safari hii ya kufikia mafanikio makubwa sana ni lazima uwe tayari kujifunza.
Nne na mwisho, tambua kuwa safari hii haitaji kukata tamaa, haijalishi umeanguka mara ngapi, haijalishi utashindwa mara ngapi, haijalishi utasemwa mangapi......katika yote hayo unahitaji kujua mahitaji yako na misingi mikuu inayopelekea kufanya yale unayoyafanya. Na hatimaye uwe tayari kujifunza kutokana na makosa na hatimaye uendelee mbele (The definition of success is how much you can fail faster and learn from the mistakes you make)
Kwa leo naomba niishie kwa haya machache nikiwa naamini kuwa yameongeza kitu kwako katika kufahamu sheria hizi za asali na jinsi tunavyoweza kuzitumia kufikia mafanikio makubwa sana.
Mathias Mugenyi Bilondwa
0786 881 155
onclick='window.open(