Uchambuzi wa Kitabu cha The One Thing: Mwongozo wa kufanikiwa kimaisha kwa kujikita kwenye jambo moja baada ya jingine.
Habari rafiki yangu mpendwa, hongera kwa kuendelea kujifunza kupitia Makala za uchambuzi wa vitabu ambazo nimekuwa nashirikisha jamii kupitia mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha leo ambacho ni cha 8 kati ya vitabu 30 ambavyo nimejiwekea lengo kuvisoma katika kipindi cha mwaka huu 2020.
Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali JIUNGE SASA.
Kitabu ninachokushirikisha kupitia makala hii ni “The One Thing” kutoka kwa mwandishi Garry Keller. Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha mbinu mbalimbali kwa ajili ya kuepuka kugusa gusa mambo mengi katika Maisha ili kuhakikisha kila mara tunafanikisha jambo mojo baada ya jingine. Kuna msemo wa Warusi kuwa “ukifukuza sungura wawili kwa wakati mmoja utajikuta umeshindwa kumkamata hata mmoja wao”. Tafsiri yake ni kwamba, tunafanikiwa kimaisha pale tunapokuwa na utaratibu wa kufanikisha jambo moja baada ya jingine.
Tunafanikiwa kwa kuchagua kitu kimoja na kuhakikisha tunaweka jitihada kubwa za kuhakikisha kitu hiko kinafanikishwa katika nyakati husika. Hivyo, mafanikio makubwa yanapatikana kwa kuweka nguvu ya pamoja kwenye jambo moja kwa wakati husika. Unapofanya mambo mengi kwa wakati mmoja unatawanya nguvu na rasilimali ambazo zingetumika kufanikisha jambo moja kwa muda mfupi. Kutokana na mtawanyiko huo wa nguvu na rasilimali, mara nyingi huwa ni mwanzo wa kukata tamaa kwa kuwa hakuna tija kwenye yale unayofanya.
Watu wote tuna muda sawa lakini tunatofautiana kimaendeleo, wapo wanaofanya kazi nyingi kwa ufanisi, wapo wanaopata zaidi, wapo wanaingiza pesa nyingi na wapo wanaoangaika kimaisha. Kama kipimo cha muda ni sawa kwa wote kwa nini pawepo tofauti hizo? Mwandishi anatushirikisha kuwa wale wenye mafanikio katika Maisha wamejifunza mbinu ya kufanya jambo moja baada ya jingine kwa wakati husika. Ni kupitia siri hii, watu wenye mafanikio wanatekeleza majukumu yao kulingana na orodha ya vipaumbele. Ni kupitia siri hii, watu wenye mafanikio wanatambua kuwa mafanikio makubwa katika Maisha yanapatikana kwa kufanya vitu vichache kwa ufanisi mkubwa. Kumbe, mafanikio yanapatikana kwa kufanya vitu vichache vyenye athari chanya badala ya kufanya vitu vingi vyenye athari hasi.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
UTANGULIZI
1. Kulingana na gunduzi za kisayansi, kitu kidogo katika mpangilio wa vitu vyenye mfanano wa mapana hila urefu tofauti kina uwezo wa kusababisha mwendo ambao utaharibu utulivu wa vitu vyote kwa mfuatano hadi kufikia kiwango cha mshindo mkubwa. Kwa maneno rahisi ni kwamba, jambo dogo ambalo limetekelezwa kwa ufanisi lina uwezo wa kusababisha matokeo makubwa katika Maisha. Ili ufanikishe matamanio au ndoto ulizonazo ni lazima utambue ni ‘vitu vipi vidogo ambavyo utajitoa kuvifanyia kazi kila siku kwa ajili ya ufanisi mkubwa katika kipindi cha muda maalumu’. Mafanikio kwenye jambo dogo yanazaa mafanikio zaidi na kadri unavyoendelea kufanikiwa ndivyo mafanikio yanaongezeka zaidi na zaidi.
2. Makampuni na biashara nyingi zinatambua umuhimu wa kujikita kwenye jambo moja, ndiyo maana tunashuhudia kampuni zinazofahamika kwa kuzalisha aina moja ya bidhaa au kutoa huduma moja kwa wateja. Kadri unavyojikita kwenye jambo moja ndivyo unajitangaza kupitia jambo hilo na hatimaye kila mmoja atakufahamu, na hivyo ndivyo mafanikio yanavyopatikana. Hivyo, ili ufanikiwe hauna budi kuchagua bidhaa au huduma moja na kuhakikisha kila siku unatekeleza majukumu yanayolenga kuiboresha bidhaa/huduma hiyo.
3. Ili ufanikiwe unatakiwa kutambua MTU MMOJA ambaye ndiye anashikiria mafanikio yako. Katika historia ya Maisha yako fikiria mafanikio ambayo umewahi kupata kwa asilimia kubwa yalichangiwa na nani? Jiulize ndoto/matamanio ya mafanikio katika Maisha uliyonayo kwa sasa unahitakiji kupata mtu wa aina gani kwa ajili ya kufikia matamanio/ndoto hazo. Hakuna mtu mwenye mafanikio ambaye amefikia mafanikio hayo pasipo kushikwa mkono na watu wengine kwa namna moja au nyingine. Mtu huyo mmoja anaweza kuwa mzazi, mwenza wako, rafiki, bosi, ndugu au mtu awaye yeyote katika jamii kwa kuwa ulimwengu wa sasa umeunganishwa kuwa kitu kimoja. Hivyo, tambua kuwa hakuna anayefanikiwa peke yake.
4. Ili ufanikiwe unatakiwa kutambua na kuendeleza KIPAJI au UJUZI maalum. Mwandishi anatushirikisha kuwa mafanikio yanahusisha kutumia vipaji tulivyozaliwa navyo au ujuzi ambao tunao kwa ajili ya kuzalisha bidhaa au kutoa huduma kwa jamii. Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kimaisha kwa kuwa wameshindwa kutambua ubora wao upo wapi. Mafanikio yanakutaka ujitambue mwenyewe kwanza ikiwa ni pamoja na kufahamu Maisha yako ni kwa ajili ya kufanikisha nini Duniani hapa.
SEHEMU YA KWANZA: AINA ZA UONGO 6 AMBAO TUMEAMINISHWA KUWA KWELI
5. Uongo #1: Kila kitu kina umuhimu sawa (everything matters equally). Usawa ni uongo ambao dunia imeubadilisha uonekane kuwa ukweli. Katika hali yoyote chini ya maamuzi ya mwanadamu Duniani hakuna usawa. Tulipokuwa Watoto tulijukuta katika hali ya utegemezi kwenye kila tulichohitaji kufanya katika Maisha yetu. Kipaumbele namba moja katika umri huo ilikuwa ni kucheza michezo ya kila aina na yeyote ambaye alikusudia kututoa kwenye kipaumbele hicho kwetu alionekana mtu mbaya. Kadri miaka ilivyopita ndivyo tulijikuta tunabadilika kutoka kwenye hali ya utegemezi na kuanza kutakiwa kujitegemea wenyewe na pengine kuanza kutegemewa. Katika kipindi hiki cha Maisha ya kujitegemea na kutegemewa ni lazima uwe tayari kufanya maamuzi sahihi. Maisha yetu ni matokeo ya maamuzi tunayofanya kila siku kwenye kila sekta. Katika kufanya maamuzi haya ndipo tunatakiwa kutambua kuwa hakuna usawa Duniani, hivyo, chochote unachofanya hakikisha umeongozwa na mfumo wako wa maamuzi.
6. Watu wenye mafanikio wana utaratibu wa kutekeleza majukumu yao kulingana na umuhimu na vipaumbele vya majukumu husika. Hapa ndipo dhana ya kuwa “hakuna usawa Duniani” unapotakiwa kuitumia katika majukumu yako kwa kuwa hata majukumu yetu ya kila siku yana umuhimu na vipaumbele tofauti. Hata hivyo, ili ufanikiwe unatakiwa kuwa na vipaumbele vyenye mwendelezo katika kila siku ya Maisha yako. Badala ya kuandaa orodha ya majukumu ya siku unatakiwa kuondaa orodha ya vitu unavyohitaji kufanikisha katika Maisha yako na kila siku kuhakikisha unapiga hatua kuelekea kwenye ukamilisho wa orodha hiyo.
7. Andaa vipaumbele vya kutekeleza katika siku husika kulingana na tija yake katika kukamilisha orodha ya vitu unavyohitaji kufanikisha. Kumbuka Duniani hakuna usawa, vivyo hivyo, majukumu yako katika siku yana tija tofauti kwenye uzalishaji wa matokeo. Hapa ndipo unatakiwa kuifahamu na kuitumia kanuni ya Vilfredo Pareto mwanauchumi muitaliano ambaye katika karne ya 19 aligundua kuwa “takribani asilimia 80 ya ardhi yote (au uchumi) ilikuwa mikononi mwa asilimia 20 pekee ya idadi ya watu”. Baadaye kanuni iligundulika kuwa inafanya kazi katika sehemu nyingi za Maisha. Mfano, asilimia ya 20 ya pembejeo inazalisha 80% ya mazao; 20% pekee ya wafanyakazi wanazalisha 80% ya matokeo; 20% ya wateja wanaleta 80% ya mapato na zaidi na zaidi. Kwa ujumla unatakiwa kupanga vipaumbele vyako kulingana na tija ya uzalishaji wa matokeo kwenye orodha ya vipaumbele vya mafanikio yako. Kumbe, ufanikiwe unatakiwa kujikita kwenye 20% ya kazi ambazo zinaingiza pato la 80% ya matokeo yote. Asilimia 80 ya kazi zinazobakia inabidi utafute watu wa kuifanya kwa ajili yako. Matokeo makubwa (80) unayohitaji yanatokana na vitu vidogo (20) unavyovifanya kwenye majukumu yako ya kila siku. Na pengine husiishie kwenye asilimilia 20 unaweza kutumia kanuni hii kwa kupunguza vipaumbele kutoka asilimia 100 kuja 20 na kutoka asilimia 20 kuja mpaka asilimia 1.
8. Uongo #2: Kufanya kazi zaidi ya moja kwa wakati mmoja (Multitasking). Kufanya majukumu mawili kwa wakati mmoja ni uongo kwa kuwa kati ya majukumu yote hakuna ambalo litafanyika kwa viwango vinavyotakiwa. Maamuzi ya busara ni kukamilisha kazi moja baada ya nyingine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ubongo wa mwanadamu umeumbwa katika mfumo ambao unawezesha kufanya kazi moja kwa ufasaha na siyo kufanya kazi zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Unaweza kuongea na kutembea au kunywa na kuandika lakini kutambua kuwa matokeo yanayopatikana yanakuwa hayana au ubora ule ule ikilinganishwa kama ungefanya kazi moja baada ya nyingine. Dunia ya sasa imejaa visumbufu (distractions) vya kila aina ambavyo vinapoteza utulivu wa akili kwenye kazi iliyopo mezani. Kuna usumbufu unaotokana na watu wa karibu yako (Ofisini au nyumbani), milio ya simu kutoka kwenye simu janja, mitandao ya kijamii, barua pepe na kila aina ya visumbufu ambavyo vinazuia ufanisi wa majukumu ya siku husika. Ufanisi katika unapatikana kwa kutuliza akili kwenye jukumu moja baada ya jingine.
9. Ubongo wa mwanadamu umesukwa katika hali ambayo inawezesha kufanya kazi zaidi ya moja japo katika kazi hizo mhusika hawezi kutuliza akili kwenye kazi zote hizo. Unaweza kusikiliza mziki huku unasoma au unaweza kutembea ukiwa unaongea lakini kati ya vyote hivyo ni lazima ukubali moja lipate kipaumbele mbele ya jingine. Unaweza kuweka utulivu wa akili kwenye matukio zaidi ya moja lakini tafsiri yake ni kwamba akili umeigawa (divided mind) kushughulikia tukio zaidi ya moja na matokeo yake ni ufanisi mdogo katika unayofanya. Kumbe pale tunapofanya jambo zaidi ya moja ni lazima tuwe tayari kulipa gharama kwenye ufanisi/ubora wa matokeo pamoja na muda au athari zinazoweza kujitokeza kama vile ajali. Kazi ambayo ingefanyika kwa muda mfupi itatakiwa kufanyika kwa muda mrefu ili kupata ubora unaohitajika. Watafiti wameonesha kuwa, takribani asilimia 28 ya muda wa kazi katika siku unapotea kutokana na kukosa utulivu kwenye kazi moja. Tafiti zinaonesha pia kuwa zaidi ya asilimia 16 ya ajali za barabarani zinatokana na madereva au watumiaji wa barabara kushindwa kutuliza akili kwenye jambo moja.
10. Uongo #3: Maisha yenye nidhamu. Kuna uongo uliogeuzwa kuwa ukweli kwamba mtu mwenye mafanikio ni lazima awe na nidhamu. Huu ni uongo mwingine ambao tumeaminishwa. Ukweli ni kwamba hatuhitaji nidhamu zaidi ya hii tuliyonayo ili kufikia mafanikio tunayotamani bali tunatakiwa kuwa na mwongozo na usimamizi wa nidhamu tuliyonayo ili kufikia mafanikio tunayotaka. Mafanikio siyo sawa na mbio za marathoni ambazo ukipoteza nidhamu kidogo unaondolewa kwenye mbio na washindani wenzako. Mafanikio yanahusisha utekelezaji wa yale ambayo huyatekelezi wakati unafahamu yana mchango chanya katika kufikia matamanio yako. Hivyo, kwa lugha rahisi tunaweza kusema kuwa mafanikio yanahusisha kujifunza tabia mpya na tabia hizo zikishakuwa sehemu ya Maisha yako (daily routine) huna haja ya kuwa mtumwa kupitia uongo wa nidhamu. Pointi muhimu ambayo mwandishi anatushirikisha ni kwamba, “mafanikio yanapatikana kwa kufanya vitu vilivyo sahihi na siyo kufanya kila kitu kwa usahihi (success is about doing the right thing and not about doing everything right)”
11. Tabia na nidhamu ni ambayo watu wengi hawataki kuyasikia kutokana na ukweli kwamba yanaminya uhuru katika Maisha. Maneno haya yanategemeana na pengine yametumika kumaanisha maana moja. Ukweli ni kwamba katika Maisha unahitaji kuwa na nidhamu kwa ajili ya kujenga tabia mpya. Hivyo, tabia zikishakuwa sehemu ya Maisha hazihitaji nguvu za ziada kuendelea kuziishi. Baada ya kuwa na mkusanyiko wa tabia mpya ndipo mhusika anaonekana kuwa mtu mwenye nidhamu (disciplined person). Kwa tafsiri hii, hautaji kuwa na nidhamu ya kuishi vitendo vya kukuwezesha kufanikiwa bali unatakiwa uwe na nidhamu ya kujifunza tabia mpya ambazo zinawezesha vitendo hivyo kuwa sehemu ya Maisha. Tafiti zinaonesha kuwa inachukua angalau siku 66 mhusika kujenga tabia mpya. Na mhusika hawezi kujenga tabia mpya zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Na kadri mhusika anavyojenga tabia nyingi zenye kumwezesha kufanya vitu nje ya mazoea yake ndivyo anaonekana mwenye mafanikio na nidhamu.
12. Uongo #4: Nguvu ya utashi mara zote ni nguvu ya wito. Mwandishi anatushirikisha kuwa msemo wa “kwenye utashi/nia mara zote kuna njia” umewapotosha watu wengi ikilinganishwa na jinsi ulivyowasaidia. Msemo huu ukitafsiriwa katika upande mmoja unatoa nafasi kwa mhusika kuwa na hamasa ya kufanikisha hitaji lake. Hata hivyo, msemo huu unaacha kigezo cha umuhimu wa muda katika kufikia hitaji lako. Ukweli ni kwamba ni vigumu kwa binadamu wa kawaida kuwa na nia/utashi wa kufanikisha hitaji lake kila siku. Kuna siku ambazo anakuwa kwenye viwango vya juu vya utashi wa kutekeleza kwa vitendo hitaji lake na zipo nyakati ambazo hajisikii kabisa kujihusisha na lolote. Nguvu ya utashi kwa binadamu pamoja na kwamba inaweza kuhuishwa (renewable) inapatikana kwa uchache (scarcity supply) kila siku. Kutokana na ukweli huu, kama unahitaji kuwa na ufanisi mzuri huna budi kuhakikisha nguvu hiyo inatumiwa kutekeleza vitu vya muhimu katika vipaumbele vya siku husika.
13. Tumeona kuwa nguvu ya utashi inapatikana kwa uchache (limited supply). Mfano, unapoamka asubuhi unakuwa na kiwango cha juu cha utashi wa kufanya kazi na kadri muda unavyoenda ndivyo molali ya kazi inapungua. Kumbe, kama nguvu ya utashi inapatikana kwa uchache (scarcity) kuna kila sababu ya kuhakikisha nguvu hiyo inatumika ipasavyo. Kumbuka, tunapozungumzia nguvu ya utashi moja kwa moja tunazungumzia uwezo wa akili au ubongo kustahimili kazi iliyopo mbele ya mhusika. Ubongo wa mwanadamu ni takribani 1/50 ya uzito wa mwili wa mwanadamu japo kiungo hiki kinatumia takribani 1/5 ya nishati yote mwilini. Na sehemu ya ubongo yenye matumizi makubwa ya nishati ni ubongo wa mbele (prefrontal cortex) ambayo inahusika na utulivu (focus), kutunza kumbukumbu za muda mfupi, kutatua changamoto na kuhusika na uratibu wa vichocheo ambavyo mwili unatakiwa kuitikia. Kumbe, ili sehemu hii ya ubongo iendelee kufanya kazi ni lazima iwe na nishati ya kutosha kumwezesha mhusika kuwa katika kiwango cha juu cha utashi wa kazi. Hivyo, ili sehemu hii ya ubongo iendelee kufanya kazi kwa ufasaha ni lazima mhusika ajaze tenki lake la nishati kwa kutumia vyakula au vinjwaji ambavyo vinahamsa kiwango cha sukari katika mzunguko wa damu.
14.
Kila siku pasipo
uelewa wetu tunajikuta kwenye kiwango cha chini cha utashi wa kazi pasipo kujua
kuwa sisi wenyewe ndo tumesababisha hali hiyo. Katika nyakati ambazo utashi wa
kufanya kazi upo kwenye kiwango cha juu tunatakiwa kutekeleza majukumu ya
vipaumbele vya muhimu ili kuepuka kupoteza nguvu ambayo ikipotea hairudi tena.
Kumbe, katika majukumu yetu ya kila siku tunapoteza nguvu ya utashi wa kufanya
kazi kutokana na sababu zifuatazo:-
ü Kujaribu
kuishi tabia mpya katika majukumu yetu ya kila siku;
ü Kuchuja
usumbufu unaojitokeza mara kwa mara;
ü Kupambana
na vishawishi vinavyolenga kutuondoa kwenye vipaumbele;
ü Kupambana
na hisia mbaya;
ü Kujaribu
kuwaridhisha wengine;
ü Kutatua
changamoto za mara kwa mara;
ü Kupambana
na hofu;
ü Aina
ya vyakula au vinywaji tunavyokula; au
ü Kujihusisha na kazi ambayo hauipendi kutoka rohoni.
15. Uongo #6: Maisha ya mlinganyo (A balanced life). Hakuna mlinganyo katika Maisha japo ni uongo ambao umeendelea kukubaliwa na wengi kuwa ili ufanikiwe ni lazima uwe na mlinganyo katika Maisha. Maisha yanaundwa na nguzo tatu ambazo ni: Kusudi, Maana na Faida. Ni lazima Maisha yawe na Kusudi maalum, Maisha ni lazima yawe na Maana na Maisha ni lazima yawe na Faida kwa mhusika pamoja na jamii inayomzunguka. Utatu huu hauwezi kuupata kwa kuishi Maisha yenye mlinganyo kama ambavyo inaelezwa na watu wengi. Badala ya kupambana kuishi Maisha ya mlinganyo unatakiwa kuishi Maisha yanayozingatia kutekeleza vitu vya kipaumbele muhimu na si vinginevyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri unavyotumia muda mwingi kwenye majukumu ya kipaumbele ndivyo inakuwa vigumu kuishi Maisha yenye mlinganyo kwa kuwa mambo yasiyo na kipaumbele yananyimwa nafasi.
16. Kuishi Maisha mlinganyo maana yake ni kwamba uwe na uwezo wa kuwa katikatika ya Kazi (majukumu) na Maisha ya kila siku. Maana yake ni kwamba hautakiwi kujikita kwenye kazi zaidi na kusahau Maisha mengine nje ya kazi na kinyume chake ni sahihi. Kama mlinganyo huu ungekuwa unawezekana ingekuwa ni jambo lenye heri lakini ukweli kwamba Maisha ya kila siku yanatulazimisha kutoa nafasi kwa baadhi ya vipaumbele na kuachana na mambo mengine kutokana na uchache wa muda na rasilimali. Matokeo makubwa yanayoonekana kuwa muujiza yanapatikana kwa kutekeleza majukumu ya kipaumbele na kuhakikisha kila mara nguvu kubwa imewekwa kwenye maeneo hayo. Hata hivyo, mwandishi anatushirikisha kuwa pamoja na kufanya kazi kwa kutekeleza majukumu ya kipaumbele tunatakiwa kukumbuka umuhimu wa Maisha nje ya kazi.
17. Muda haumsubirii mtu yeyote. Dunia imejaa watu wengi ambao wanahairisha mambo kwa matarajio kuwa ipo siku watakuwa na muda wa kuyarudia. Mfano, unaweza kupata muda wa kutekeleza majukumu yako ya kila siku na kujikuta unakosa muda wa kukamilisha mahitaji muhimu katika Maisha binafsi. Wafanyakazi au wafanyabiashara wengi wanakosa muda wa kuwa karibu na familia zao kutokana na kubanwa na majukumu yao ya kazi. Mwandishi anatushirikisha kuwa, muda haurudi nyuma wala haumsubiri mtu hivyo kadri unavyopata muda hakikisha unatekeleza mahitaji yako muhimu katika Maisha. Tenga muda kwa ajili ya kukamilisha vipaumbele vyako vya kazi, familia, masuala ya kijamii na
18. Uongo #6: Kubwa ni baya (Big is bad). Huu ni uongo mwingine ambao umezoeleka katika jamii. Ukweli ni kwamba “kikubwa kinaweza kuwa kibaya na kibaya kinaweza kuwa kikubwa bila kusahau kuwa kidogo pua kinaweza kuwa kibaya na kinyume chake ni sahihi”. Kutokana na uongo huo tumeaminishwa kujikita kwenye hatua fupi fupi kwa kuogopa kuwa tukianza na hatua ndefu tutaanguka. Fursa kubwa ni bora kuliko changamoto ndogo na changamoto kubwa ni mbaya kuliko fursa ndogo. Hivyo, ukubwa hauna uhusiano wowote na ubaya maana uzuri au ubaya unategemeana na hali ya tukio husika. Huu ni moja ya uongo kandamizi kwa kuwa kama unaogopa mafanikio makubwa kwa kigezo kuwa mafanikio makubwa ni dhambi (ubaya) kamwe hauwezi kupata mafanikio hayo.
19. Watu wengi ni wahenga (victim) wa kuogopa makubwa kwa kuwa kila panapotajwa matokeo makubwa watu wanayahusisha na ubaya. Mfano, unapotaja neno utajiri kwenye kundi kubwa la watu, watu wengi watakuambia mimi sitaki kuwa tajiri maana utajiri utanifanya nikose muda wa kutosha kupumzika, matajiri ni watu wenye roho mbaya, utajiri utanifanya nikose muda wa kutosha kuwa karibu na familia yangu; na mengine mengine. Unaweza kuona ni jinsi gani uongo huu unaendelea kukandamiza Maisha yetu maana naamini hata wewe mara nyingi umekuwa na hofu kila unafikiria kuanzisha hatua kubwa ambazo zingezaa mafanikio makubwa. Kwa ujumla, kutokana na uongo huu tumekuwa waoga wa matokeo/mafanikio makubwa. Kumbe, badala ya kuwa waoga wa matokeo makubwa kila mara tunatakiwa kufikiria kutatua changamoto kubwa kuhusiana na malengo ya Maisha yetu. Kila mara weka malengo yanayolenga kuongeza mara mbili thamani ya mafanikio yako. Husiridhike na hatua unayofikia maana ili ufikie mafanikio makubwa kila hatua inatakiwa kuwa chanzo cha kufungua hatua kadhaa mbele.
20.
Epuka ukanda wako wa
mazoea (comfort zone), epuka kufanya vitu kwa mazoea kama ambavyo kila mtu anafanya
(acting in a business as usual), fikiria tofauti, kuwa na fikra pana na tekeleza
majukumu yako kwa mapana. Hakuna mwenye kujua ukomo (limit)
wa uwezo wake katika kufikia mafanikio makubwa hivyo hakuna sababu ya kuwa na
fikra finyu ambazo zinaminya uwezo wetu halisi katika kila tunalofanya. Fikra pana
ni chachu ya kufikia mafanikio makubwa kutokana na ukweli kwamba mafanikio ni
vitendo na vitendo ni zao la fikra. Hivyo, mafanikio makubwa (big success) ni
zao la vitendo vya kishindo/tofauti (act big) ambapo ili utende tofauti ni
lazima uwe na fikra pana/tofauti (think big). Watu wote tumepewa muda sawa hila
kinachotofautisha mafanikio yetu ni yale tunayofanya katika muda huo.
Hii ni sehemu ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu hiki. Uchambuzi wa kitabu chote utapatikana kwa gharama ya Tshs. 10,000/=. Jiunge na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa KUBONYEZA HAPA.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate
elimu isiyokuwa na mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Mwalimu Augustine Mathias
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com