Habari ya leo rafiki na msomaji wa
mtandao wa fikra za kitajiri.
Kwanza niombe radhi kwa kushindwa
kukushirikisha usomaji wa kitabu kwa takribani wiki 2 zilizopita kutokana na
sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.
Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Karibu tena katika mtandao wa
FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya uchambuzi wa kitabu cha wiki hii. Leo hii ikiwa
ni wiki ya 11 katika kipindi cha mwaka 2018 naendelea kukushirikisha uchambuzi
wa vitabu vyenye mafundisho tofauti katika kila sekta ya maisha yako.
Kama ambavyo, makala hizi za uchambuzi
wa vitabu zimekuwa zikikufikia kila wiki kwa kadri ambavyo napata muda wa
kukushirikisha kile ninachojifunza kutoka kwenye vitabu hivi. Ni matarajio
yangu kuwa muda ninaotumia kukushirikisha uchambuzi wa vitabu umekuwa wa msaada
mkubwa kwako katika kubadilisha maisha yako.
Unaweza kujiunga na mtandao huu, KWA KUBONYEZA BONYEZA HAPA
na
kujaza fomu kisha bofya “jiunge/subscribe” utakuwa umejiunga na mtandao huu.
Kwa kujiunga na mtandao huu utapata makala zinazochapishwa humu moja kwa moja
kwenye barua pepe yako bila malipo yoyote.
Kitabu
cha wiki hii ni “Se Habla Dinero ~ Pesa
zinaongea” kutoka kwa mwandishi Lynn Jimenez.
Neno
“FEDHA” limekuwa ni kitendawili ambacho kila mtu anatoa majibu kulingana na
mazoea yake kwenye ulimwengu wa fedha. Wapo wanaosema fedha kamwe haiwezi
kutosha, fedha hazitunziki, fedha hazitakiwi kuongelewa au fedha zipo chache na
kwa watu wachache ambao ni wateule. Ni kutokana na mtazamo huu watu wengi
linapokuja suala la kuwa na uhuru wa kifedha maswali mengi yanakuwa; nitaweza
vipi kutengeneza pesa? Naweza vipi kuitunza pesa isipotee? Nawezaje kuifurahia
pesa yangu kwa sasa huku nikiendelea kutengeneza pesa kwa ajili ya siku zijazo?
Mwandishi
katika kitabu hiki anatushirikisha mbinu muhimu za kufanikiwa kifedha na
hatimaye kuwa na uhuru wa kifedha. Hii ni pamoja na mbinu za uwekezaji, namna
ya kukopa kwa mafanikio na jinsi ya kudhibiti matumizi ya fedha zako. Hivyo,
kupitia kitabu hiki tunapata majibu ya namna ya kutengeneza pesa, kutumia pesa
na kuiwekeza kwa ajili ya kupata fedha zaidi.
Karibu
tujifunze machache kati ya mengi ambayo mwandishi anatushirikisha katika kitabu
hiki:
1. Mafanikio kwenye kitu chochote
kile ni matokeo ya imani ulijiwekea. Katika sekta ya fedha kila mtu ana imani
yake, wapo wanao amini kuwa pesa ni mbaya au nzuri. Mwandishi anatushirikisha
kuwa pesa ni nyenzo tu kwa ajili ya kufanikisha baadhi ya majukumu tulionao.
Ubaya au uzuri wa pesa unategemea na namna tunavyoitumia katika kukamilisha
hayo majukumu. Endapo imetumiwa vyema fedha itakusaidia kukamilisha majukumu
yote muhimu katika maisha yako ya kila siku.
2. Endapo fedha itatumiwa vibaya
itamfanya mhusika kukosa uhuru wa kuwa karibu na watu wake wa karibu na hata
kukosa mahitaji muhimu ya maisha. Pia, fedha inapotumiwa vibaya mhusika anaweza
kuingia kwenye madeni makubwa ikiwa ni pamoja na kukosa uhuru wa maisha yake.
Jambo muhimu la kujifunza ni kwamba unatakiwa kuidhibiti fedha na usipofanya
hivyo itakudhibiti yenyewe. Njia bora ya kudhibiti pesa yako ni kuwa na
vipaumbele vya namna ya kuitumia kutekeleza matakwa yako muhimu bila kupoteza
utu wako.
3. Kama mzazi unahitaji
kuwafundisha watoto wako kuhusu fedha wakiwa bado wadogo na njia rahisi ya
kufanya hivyo ni kuruhusu wote kuongelea fedha. Hii ni pamoja na kuongelea
mapato na matumizi ya fedha za familia kila mara na namna fedha hizo jinsi
zinavyopatikana kutoka kwenye mifereji mliyonayo.
4. Unapokuwa
na hela ambayo unahitaji kuiwekeza kwa ajili ya baadaye ni muhimu kuhakikisha
fedha hizo inawekezwa sehemu salama. Kwenye kuifadhi fedha kila mtu ana sehemu
anazohifadhia fedha zake. Wapo ambao wanahifadhi benki, wapo wanaohifadhi chini
ya godoro au kwenye kibuyu. Mwandishi anatushirikisha kuwa unapohifadhi fedha
ni muhimu kujihakikishia juu ya usalama wa fedha hizo dhidi ya wezi, wadudu/panya
au majanga ya moto. Pia, ni muhimu kuhifadhi sehemu ambayo fedha inaongezeka
kwa siku za baadae kupitia ongezeko la riba (compounding interest).
5. Fahamu
umuhimu wa ongezeko la riba katika kuwekeza pesa zako. Unapowekeza fedha kwenye
benki ambayo ongezeko la riba mfano ni 5% kwa mwaka ina maana kuwa baada ya
mwaka mmoja fedha hizo zitaongezeka kwa 5% na baada ya mwaka wa pili ongezeko
litakuwa ni 5% ya kiasi kilichokuwepo baada ya ongezeko la mwaka wa kwanza.
Hivyo, hivyo mpaka miaka kumi na kuendelea na hivyo ndivyo fedha zako
zinatengeneza fedha zaidi wakati wewe ukiwa umepumzika.
6. Kama
huhitaji kutumia fedha zako ndani ya muda mfupi unaweza kuwekeza fedha hizo
kwenye ‘fixed account’ ambapo utafanikiwa kupata ongezeko la riba kulingana na
utaratibu wa benki uliweka fedha zako. Pia, mwandishi anatushauri kufungua
akaunti ya uwekezaji (saving account) badala ya akaunti ya kutunzia fedha
(deposite account). Katika akaunti ya uwekezaji, pesa inayowekezwa inaongezeka
kila mwaka kwa kutegemea riba inayotolewa na benki.
7. Mifumo
ya kuweka au kutoa pesa kwenye akaunti yako ya benki siku hizi imerahisishwa
kwa kutumia mfumo wa mtandao. Siku hizi unaweza kufanya huduma zote za kibenki
ukiwa kwenye umekaa Ofisini au nyumbani kwako kwa kutumia simu yako au kompyuta
mpakato. Hata hivyo, mwandishi anatukumbusha umuhimu wa kuhakikisha mifumo hii hisiwe
sehemu ya kurahisisha matumizi ya hovyo ya fedha zako.
8. Kipindi
cha muda unaotakiwa ili pesa inayowekezwa itumike kwa siku za baadae ndicho
kinaamua njia ipi ya uwekezaji itumike kwa ajili ya kuwekeza peza zako. Hii ina
maana kwamba kama unategemea pesa unayowekeza uitumie ndani ya wiki mbili
zijazo au mwezi hauwezi kuiweka kwenye akaunti ya akiba ukitegemea kufaidika
kupitia ongezeko la riba. Lakini kama pesa hiyo ipo kwenye mipango ya mwaka
mmoja na kuendelea huna budi kuiwekeza kwenye sehemu ambayo fedha itaongezeka
kupitia ongezeko la riba au kupitia gawio.
9. Watu
wengi wanashindwa kutenga fedha kwa ajili ya uwekezaji ili kukidhi mahitaji ya
fedha kwa siku za baadae lakini kamwe hawajahi kukosa fedha kwa ajili vitu
visivyo vya lazima kama vile kununua kila toleo la nguo zinazoingia au fedha za
vocha kwa ajili ya vifurushi. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili kuwa na uhuru
wa kifedha ni lazima mhusika awe tayari kwa ajili ya kujibana kwenye matumizi
yasiyo ya lazima na fedha hizo zitengwe kwa ajili ya uwekezaji.
10. Katika uwekezaji unahitaji kutenga
fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu kwenye uzee wako au fedha kwa ajili ya
kustaafu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kama kiumbe hai kila siku
unaongezeka umri na kadri unavyoongezeka umri ndivyo uwezo wa kufanya kazi
unavyozidi kupungua. Matokeo yake kuna kipindi ambacho hautakuwa na uwezo wa
kufanya kazi wakati mahitaji ya fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji muhimu ya
maisha yatakuwa yako palepale.
11. Ili uwe uhuru wa kifedha ni lazima
utumize hatua mbili ambazo ni kudhibiti matumizi ya fedha na kuhakikisha
unajilipa kwanza. Hatua hizi zinategemeana kutokana na ukweli kwamba
unapodhibiti matumizi ya fedha unaokoa fedha ambazo unatakiwa kuziwekeza kwa
ajili ya kukuza fedha zako (kujilipa kwanza). Hii ndio siri ya kuwa tajiri na
ili ufanikishe siri hii unatakiwa kuanza sasa kwa kuhakikisha kila mara unapopata
fedha utenge fedha kwa ajili ya kuwekeza kabla kufanya matumizi mengine. Kwa
maana uwekezaji uwe kipaumbele namna moja.
12. Katika kudhibiti matumizi ya hovyo
unahitaji kuwa na bajeti ya fedha zako na bajeti hii inatakiwa kuwa mwongozo
katika manunuzi/matumizi ya kila mara. Bajeti hii inatakiwa kuwa mahitaji yote
muhimu ambayo yanatakiwa katika maisha yako ya kila siku bila kusahau fedha za
uwekezaji. Hii ni pamoja na fedha ambazo huwa unatoa kama msaada kwa ndugu na
jamaa pamoja na gharama za afya, sadaka, mavazi, chakula na vinywaji.
13. Siri nyingine ambayo mwandishi
anatushirikisha katika kitabu hiki ni kuhakikisha matumizi yanakuwa kidogo
ukilinganisha na mapato. Hii inakuafanya ujibane kwa ajili ya kuishi maisha ya
hadhi yako. Watu wengi katika maisha wanaishi maisha ya maigizo na matokeo yake
matumizi yao yanakuwa makubwa kuliko mapato walinayo jambo linalopelekea maisha
ya kuunga kuunga. Mfano, mtu analazimika kula kwenye hoteli kila siku wakati
ana uwezo wa kununua chakula na kupika chakula ambacho ni bei nafuu ukilinganisha
na cha hotelini.
14. Punguza/epuka madeni yasiyo ya lazima
kwa ajili ya kuokoa fedha ambazo utawekeza kwa matumizi ya baadae. Mwandishi anatushirikisha
kuwa watu wengi wanakandamizwa na madeni ambayo mara nyingi yanalipwa na riba
juu. Na madeni yaliyo mengi wakopaji wanachukua mkopo kabla kufanya tathimini
ya namna mkopo husika unatakiwa kutumika kuzalisha faida kama sehemu ya kulipia
riba ya mkopo na faida. Mkopo mzuri ni ule ambao unakopa kwa ajili ya kupanua
biashara ambayo tayari unafahamu changamoto zake. Epuka mkopo kwa ajili ya
kununua gari, kujenga jina baa na kununua vyakula.
15. Kuna tofauti kubwa kati ya kuwa tajiri
na kuonekana tajiri. Watu wengi wanakazana kwa ajili ya kuonekana matajiri na
hivyo wanaishi maisha ya kuigiza mifumo ya maisha ya matajiri na matokeo yake
wanashindwa kuufikia utajiri wa kweli (uhuru wa kifedha). Mfano, mtu anataka
aonekane anaendesha gari kali wakati hata uwezo wa kulihudumia kwake ni tatizo.
Ili uwe tajiri ni lazima ukazane kununua vitu ambavyo thamani yake inaongezeka
kadri siku zinavyoongezeka.
16. Husikazane kwa ajili ya kumiliki gari
kubwa au nyumba kubwa ambayo ipo nje ya uwezo wako. Watu wengi wanapambana kwa
ajili ya vitu ambavyo vinahitaji gharama kubwa na matokeo yake wanashindwa
kukamilisha miradi hiyo au hata pale wanapokamilisha wanakuwa kwenye madeni
makubwa. Pigania kile ambacho ukamilishwaji wake hautakuchia pengo kubwa
kiuchumi.
17. Hakikisha una uhakika wa kutosha kuhusu
biashara unayokusudia kufanya kabla ya kuchukua mkopo wa biashara. Hii ni
pamoja na kufahamu gharama za uendeshaji wa biashara husika kwa kipindi cha
mwaka. Hata hivyo, mwandishi anatushirikisha kuwa kabla ya kuchukua mkopo
unatakiwa uwe umefanikiwa kuwekeza fedha zako mwenyewe kwa ajili ya gharama
zinazohusiana na uanzishwaji wa biashara. Gharama hizi ni zile zisizo husika
moja kwa moja kwenye utengenezaji wa faida katika biashara unayokusudia
kufanya.
18. Utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu katika
ufanisi wa uendeshaji wa biashara. Takwimu muhimu kama vile bidhaa zinazoingia
na kutoka pamoja na mtiririko wa fedha ni muhimu katika ustawi wa biashara. Takwimu
hizi ndizo zinaonesha kama biashara inakua au imedumaa.
19. Uwekezaji wenye tija ni pale pesa
inapotumika kuzalisha pesa zaidi. Kama mwekezaji unatakiwa kuhakikisha kila
shilingi unayowekeza inatumika kuzalisha pesa kwa ajili ya ukuaji wa fedha
zako. Hapa ndipo unahitaji kufahamu miujiza ya ongezeko la riba kwenye pesa
unayowekeza katika kipindi cha muda maalum. Na ili uwe mwekezaji mwenye
mafanikio ni lazima uwe tayari kutenga asilimia flani ya fedha kwa ajili ya
uwekezaji kutoka kwenye kila shilingi inayoingia kwenye mkono wako.
20. Ili ufanikiwe katika uwekezaji ni
lazima uwe na lengo kubwa la nini hasa unahitaji kufanikisha kupitia uwekezaji
wako. Lengo hili ndilo linatakiwa kuwa chachu kwako kwa ajili ya kuendelea
kutenga fedha kwa ajili ya kufanikisha ndoto zako za uwekezaji. Na hapa ni
lazima uwe tayari kubeba hatari za kiuwekezaji ambazo zinaweza kujitakeza
katika safari yako ya uwekezaji.
21. Katika uwekezaji unatakiwa kufahamu
nguvu ya mfumuko wa bei. Unapowekeza unatakiwa kujiuliza kama kiwango cha ongezeko
la riba kinacholipwa kupitia fedha unazowekeza kama kipo juu ya kasi ya ukuaji
wa mfumuko wa bei. Mfano, kama kiwango cha riba ni asilimia nne kwa kila
shilingi uliyowekeza kwa mwaka na wakati huo huo kasi ya ukuaji wa mfumuko wa
bei ni asilimia nne kwa mwaka, maana yake ni kwamba pamoja na fedha ulizowekeza
zimeongezeka kwa asilimia tatu kwa mwaka lakini ongezeko hilo halina maana
yoyote kwenye soko. Kanuni muhimu katika uwekezaji ni kuhakikisha unawekeza
sehemu ambayo asilimia ya ongezeko la riba ni kubwa kuliko kiwango cha mfumuko
wa bei.
22. Baada ya kufanikiwa kutengeneza utajiri
kupitia uwekezaji mbalimbali sasa unatakiwa kuhakikisha unalinda fedha zako
dhidi ya wezi, wajanja na kodi zisizo za lazima. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba ili uwe tajiri inahitaji miaka kadhaa lakini kupoteza pesa ulizokusanya
kwa kipindi kirefu ni kitendo cha sekunde chache. Hivyo, mwandishi
anatushirikisha umuhimu wa kuwa makini katika kulinda utajiri wako.
Haya ni machache ambayo nimeweza
kukushirikisha kati ya mengi yaliyo kwenye kitabu hiki. Kupata nakala ya kitabu
hiki BONYEZA HAPA na
ujiunge na mtandao wa fikra za kitajiri kisha nitumie ujumbe wa kuomba kitabu
hiki kupitia barua pepe fikrazakitajiri@gmail.com.
Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa
kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe
kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi
hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua
pepe: fikrazatajiri@gmail.com
|