Kwanza kabisa napenda nianze barua yangu kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwako wewe rafiki mpendwa kwa kufanikiwa kuhitimu elimu yako ambayo kwangu Mimi nafahamu kuwa umepitia katika milima na mabonde lakini kwa jitihada na malengo hatimaye umefanikiwa kupata cheti chako. Hongera sana.
Nakupa hongera kwa sababu ambazo zinanipa tumaini la kwamba wewe ni kati ya watu wachache waliofanikiwa kufikia hatua hiyo ya elimu ya juu, diploma au cheti. Hongera zangu za dhati nazitoa kwako pia kwa vile naliona tumaini katika wewe kuwa wewe ni moja kati ya watu ambao wanaweza kujiwekea malengo na hatimaye kuyafanikisha pasipo kukatishwa tamaa zozote zinazowakumba njiani.
Pamoja na pongezi zangu Mpendwa rafiki muhitimu wa chuo naomba nikupe wosia wangu kupitia barua hii ya wazi kwako. Wosia huu naomba uwe mwongozo katika maisha yako mapya unayoenda kuishi kwa sasa mara baada ya kumaliza masomo yako. Kupitia wosia huu nakupa angalizo sita ambazo unatakiwa kuzifikilia katika maisha yako mapya. Karibu uzipitie angalizo hizo na kuzitafakari kwa kina.
1. KUHITIMU CHUO SI LESENI YA KUFANIKIWA MAISHANI MWAKO: Ndugu mpendwa muhitimu nafahamu kuwa pindi ukiwa chuo ulikuwa na matumaini makubwa sana kuwa baada ya kuhitimu elimu yako utapata kazi nzuri ambayo itakuwa ni ufunguo wako katika kutekeleza ndoto ulizo nazo lakini napenda ufahamu fika kuwa ukweli ni kwamba elimu ya darasani na mafanikio yako kimaisha ni vitu viwili tofauti. Mtaani wapo wasomi wengi ambayo tena wamesoma wakawa wataalam wabobezi katika fani zao lakini mpaka sasa wanaangaika kimapato. Vipato vyao haviendani na elimu walizonazo, kila siku nyimbo zao ni sina hela ya kutosha, nafanya kazi hii kwa sababu nisipoifanya familia itakufa njàa, siwezi kuacha kazi kwa sababu nikiacha kazi nitapoteza mafao yangu ya uzeeni pamoja na kiinua mgongo, naenda kuongeza elimu ili niweze kupandishwa cheo kazini na nyinginezo nyingi. Haya yote ni ishara kuwa kama kusoma kungekuwa leseni ya kufanikiwa kimaisha basi wasomi ndo wangekuwa ni watu waliofanikiwa sana katika jamii zetu lakini kumbe ni wasomi hawa hawa ambao madenii yao kwenye maduka ya mangi hayaishi. Ni wasomi hawa ambao akaunti zao za benki zinanusa harufu ya fedha mwishoni mwa mwezi na baada ya hapo wamiliki wanasahau njia iendayo ATM za NMB mpaka mwishoni mwa mwezi ili wakapange msururu ambao unalenga kwenda kujenga jina la uhaminifu kwa mangi na wengine kwenye wamiliki wa baa. Hali iko hivyo ndg muhitimu hivyo jitafakali upyaaa.,...
2. UMEHITIMU ELIMU YA DARASANI SASA UNATAKIWA KUANZA DARASA LA AWALI KWENYE ELIMU YA MAFANIKIO: Waswahili tuna msemo unaosema kuwa elimu haina mwisho lakini Mimi nakuambia kuwa elimu uliyohitimu ina mwisho wake na ñdio maana siku uliyohitimu ulivaa joho na ukafurahia sana hadi kututumia picha kwenye mitandao ya kijamii. Leo hii napenda nikuambie kuwa sasa unapaswa kuanza elimu mpya ambayo aina mwisho na elimu hii sio nyingine bali ni elimu ya kimafanikio. Mafanikio haya yajumuisha kila sehemu ya maisha yako kuanzia ngazi ya familia, jamii, kifedha, kiroho, kikazi n.k...Mpendwa rafiki naomba ufahamu kuwa elimu hii ni tofauti na hiyo uliyohitimu kwani katika elimu hii wewe ndo mwalimu na wewe ndo mwanafunzi, somo unajipa mwenyewe na kujitathimini mwenyewe pia, mtihani unajipa mwenyewe na kujisahihisha mwenyewe. Vivyo hivyo kushindwa kufaulu mtihani katika elimu hii ni msingi wa baadae kitu ambacho ni kinyume na elimu uliyohitimu. Kwa maana nyingine ni kwamba elimu hii haiwaachi wale wenye vipaji vidogo (slow learners) bali inawapa nafasi kila kukicha ili hatimaye wafanikiwe. Ni ELIMU hii ambayo Mada za kujifunza haziishi bali kila siku kuna somo jipya na kamwe mwanafunzi hakuna siku atasema sasa nafahamu kila kitu bali kila kukicha mwanafunzi anajiona hajui chochote na hivyo kufungua nafasi ya kujifunza mambo mapya. Karibu sana katika ulimwengu wa elimu hii.
3. WEWE NI MWAJIRI HUSIYEJITAMBUA: Nafahamu kuwa baada ya kumaliza elimu yako tayari unajiandaa kubeba baasha kwa ajili ya kutafuta ajira lakini rafiki yangu naomba kabla ya kufanya hivyo fanya zoezi la kila siku kutenga dakika tano za kutafakari nini ambacho wewe unaweza kufanya kwa muda huu ambacho kinaweza kukuingizia kipato na hivyo kuwa ajira yako kwa muda huu. Ukifanikiwa kupata wazo hilo kila siku jipe dakika za kutafakali ni jinsi gani unaweza kulikuza wazo lako na hatimaye ikawa ni ajira inayoweza kuajiri watu wengine hata kama ni wachache sana au wa elimu ya chini kabisa lakini wewe husikate tamaa bali endelea kuwa çhanya ukiamini ipo siku biashara hiyo itakua kulingana na jitihada zako. Simaanishi kuwa watu wote wajiari wenyewe la hasha, ninachokupa hapa ni kutokana na uzoefu wangu wa kwamba kuna watu mitahani mwaka wa sita sasa tokea wamalize elimu yao mpaka sasa wapo mitaani wakitembea na baasha kwa ajili ya kutafuta ajira bila mafanikio sanasana wanachoambulia kutoka kwa waajiri ni kukatishwa tamaa hadi wanajiona walikosea kusoma. Rafiki muhitimu naomba husiwe kama wao bali angaika kujiari kwanza wakati unaendelea kutafuta ajira kwani pengine unaweza kufikia maamuzi ya kutoajiriwa tena kutokana na nini unafanya kwa wakati huo.
4. WEWE NI RUBANI NAMBA MOJA WA MAISHA YAKO: Ndugu yangu mpendwa naomba unapoyaanza maisha mapya uje na falsa ya kuwa hakuna wa kumlaumu pale ambapo mambo hayataenda kama ulivyotarajia bali unatakiwa kujilaumu mwenyewe. Wewe ndo muhusika mkuu wa maisha yako na wala sio serikali, mzazi, Ndugu wala marafiki. Wewe ndo una uamuzi wa jinsi gani unataka maisha yako yawe. Kumbuka kuwa kila jambo utakalolifanya katika kila siku ya maisha yako lina mchango mkubwa katika mafanikio yako ya baadae hivyo nakusihi saana mpendwa muhitimu wa chuo uwe makini na maamuzi yako kwani ndo yameshikilia Mafanikio ya maisha yako ya baadae.
5. KUWA MAKINI SANA NA MAWIMBI YA DUNIA: Kwa sasa tunaishi kwenye dunia yenye kila aina ya mawimbi, yapo mawimbi yanayoonekana kuwa na kasi kubwa kiasi kwamba rafiki yangu muhitimu jahazi lako haliwezi kuvuka salama. Lakini pia yako mawimbi yenye kasi hisiyo na madhara kwa jahazi lako. Nakusihi sana kabla hujaingiza jahazi lako angalia kasi ya wimbi linalokuja mbele yako. Namaanisha kuwa mtaani mtakutana na mengi ambayo dunia imewaandalia na pengine dunia ilishawatengea mafungu yenu kila mmoja hata mkiwa bado masomoni, ushauri wangu ni kwamba kadri mnavyoanza maisha mapya fahamu kuwa mpo katika jamii tofauti na ile mliyoizoea hivyo kuna mengi mnayafahamu lakini wao hawayafahamu hivyo ni muda mzuri kwenu nyinyi kuhakikisha mnatumia fursa hizo kuwa mtaji kwenu. Kuweni tayari kutengwa na jamii pale ambapo unalolisimamia ni jipya katika jamii husika kwa maana jamii imezoea kufanya vitu kwa mazoea nakusihi sana rafiki yangu chochote utakochokifanya kifanyeni kwa hatua ya ziada ambayo imeongeza ubora tofauti na mazoea ya jamii inayokuzunguka. Epuka kabisa makundi yasiyo na maana katika maisha mapya unayoyaendea bali jumuika na makundi unayoona yanaendana na falsa zako.
6. JALI SANA MUDA WAKO: Ndugu yangu mpendwa muhitimu naomba nimalizie kwa kukupa angalizo juu ya muda wako. Naomba ufahamu kuwa muda ni Mali kama ambavyo tumezoea kusema pasipo kufahamu tafsiri yake sahihi. Fahamu kuwa watu wote tunapewa zawadi sawa kwa siku yaani masaa 24 lakini kinachotutofautisha kimafanikio ni jinsi gani kila mmoja anatumia sekunde ya muda wake. Anza maisha mapya kwa kuhakikisha kuwa kila dakika ya muda wako unaitumia kutekeleza kile ulichopanga kukamilisha kwa siku husika. Epuka sana kukaa kwenye mitandao ya kijamii kuchart mambo yasiyo na maana huku ukibadilisha mtandao wa kijamii mmoja hadi mwingine kumbuka kuwa hayo yanakupotezea muda wako na kibaya zaidi yanakuharibia mfumo wa fikra zako kwani badala ya kuwaza mambo ya maana unaishia kuwaza mambo ya kijinga. Nakusihi sana rafiki yangu uhakikishe kila dakika unajiukiza juu ya lile unalolifanya kama lina mchango kwenye Mafanikio yako ya baadae.
Naomba uyapokee hayo na kuhakikisha kuwa unayatafakari na kuyafanyia kazi. Kama umejifunza kitu katika barua hii naomba uisambaze kwa kushare kwa kadri uwezavyo ili elimu hii iwafikie wengi na hatimaye kwa pamoja tuweze kuibadirisha dunia hii na kuwa mahala pazuri pa kuishi. Karibuni kwenye elimu hisiyokuwa na mwisho.
A.M. Bilondwa
0786881155
bilondwam@yahoo.com