Kwani nini inakupasa kubadili fikra zako ili uwe tajiri?

Karibu msomaji wa makala zangu ambazo zaidi zinajikita katika jinsi gani ambavyo waweza amua kuwa tajiri kwa kubadilisha mtazamo wako. Mpendwa msomaji wangu ni matumaini yangu kuwa uko vizuri na unaendelea na mapambano ya kubadilisha maisha yako kila iitwapo leo. 

Kama ndo hivyo nakupongeza kwa jitihada zako kwani naamini ni kupitia jitihada hizi pamoja tutaibadilisha nchi hii kuwa mahala pazuri pa kuishi badala ya kuishia kulalamikia wanasiasa kuwa wameshindwa kutimiza matarajio yetu.

Ni jambo la kushangaza kulalamikia wanasiasa kuwa wameshindwa kukupa ajira kumbe wewe mwenyewe ni chanzo cha tatizo hilo kwani kila mmoja wetu Mwenyezi Mungu amemuumba na kumkilimia rehema tele za kubadilisha mahala alipo kuwa mahala pazuri pakuishi. Hivyo basi badala ya kulalamikia kukosekana kwa ajira jiulize unafanya nini leo hii ili uweze kuzalisha ajira kwa kizazi cha sasa au kizazi kijacho? You need to be problem solvers rather than problem creators.

Tuachane na hayo ya siasa na badala yake ngoja nijikite kwenye mada yangu ya leo ambao itajikita kwenye jinsi gani ambavyo utapata utajiri kwa kubadilisha fikra zako. Katika makala iliyopita nilielezea kuwa misingi mikuu ya kuwa tajiri ni kupitia (i) Fikra (ii) Malengo (iii) Elimu ya fedha na (iv) Kujali muda.
Leo hii naanza kwa kukuchambulia na kukufunulia siri ambayo huwajahi kuhifikiria kuwa ni muhimili mkuu wa kukufanya uwe tajiri tena tajiri mkubwa zaidi ya wale unaowaona kwenye vyombo vya habari na mitandao mbalimbali. Upo tayari kujua ni siri ipi hiyo?? Kama upo tayari hebu endelea kusoma ili husipitwe na uondo huu ambao utabadilisha maisha yako. 

Kila unalofanya linatokana na fikra zako za kila siku
Kila jambo linalofanyika katika maisha yako ya kila siku lazima lianzie katika mfumo wako wa mawazo. Mfumo huu wa mawazo umetengenezwa kiasi kwamba unafanyia kazi fikra zako ambazo unaziwaza mara kwa mara katika mazingira yako ya kila siku. Kwa maana hiyo kile ambacho unakiwaza sana ndicho mfumo wako wa ndani wa mawazo (subconscious mind) unakifanyia kazi na kukuwezesha wewe kukiweka katika hali ya umbile lake. Hebu tuangalie mfumo huu wa ndani wa mawazo unafanyaje kazi:-

Nguvu ya fikra hasi
Kadri unavyoufanya mfumo wako wa mawazo utawaliwe na fikra hasi ndivyo mfumo wako wa mawazo wa ndani utakavyo tafsiri fikra hizo na kukuletea matokeo hasi. Kinyume chake ni kuwa kama mfumo wako wa mawazo utataliwa na fikra chanya ndivyo mfumo wako wa mawazo wa ndani utakavyo kuletea matokeo katika umbile chanya. Mfano kama wewe unawaza kuwa hauwezi kuwa tajiri moja kwa moja tafsiri ya mfumo wako wa mawazo wa ndani utakuletea matokeo katika maumbile ya kiumaskini. Kumbuka kuwa binadamu tupo jinsi tulivyo kutokana na mitazamo yetu ya ndani (“The outermost of human being is the reflection of his/her innermost”). Kama wewe muda mwingi unawaza kutokukubalika katika jamii vivyo hivyo matokeo yake yatakuwa kutokukubalika. Kama unawaza kushindwa katika yale unayoyafanya matokeo yake yatakuwa kutofanikiwa katika yale unayoyafanya. Kama unawaza kutokupendwa ndivyo hivyo matokeo yake yatakavyokuwa.

Nguvu ya fikra chanya
Kutokana na tulichojifunza hapo juu, yafaa tujifunze kuwa na mawazo ambayo yataumba mambo na vitu tunavyovihitaji pekee na si vile vyenye kutuletea maumbile hasi. Jambo jingine la kushika ni kuwa huwezi kutenda kile usichowaza. Matendo yote ni matokeo ya mawazo. Na kama mtu akisema hutenda pasipo kuwaza, hiyo siyo kweli. Ubongo wa binadamu unazo sehemu kadha wa kadha zinazohusika na kumbukumbu na takwimu mbalimbali na kupitia ubongo huu ndimo kuna mfumo wa mawazo wa ndani wa mtu husika. Kwa mantiki hii kila tunachoamua ni matokeo ya taarifa fulani ambazo zimeshakuwamo katika mfumo wa mawazo wa ndani huko nyuma. Yawezekana hata muhusika hasiwe na habari kuwa taarifa hizo zipo katika mfumo wake wa mawazo wa ndani (subconscious mind), lakini kutofahamu huku hakuzuii taarifa hizo kuendelea kutumika katika maamuzi na maumbile mbalimbali.

Wapo watu ambao hujikuta wanafanya uamuzi wasioupenda ama wanapata matokeo wasiyoyapenda. Tatizo si matokeo, tatizo ni fikra ambazo zinakuja kwa sababu ya taarifa zinazoujaza ubongo wako. Nimesema kuwa ili upate matokeo unayoyataka ni lazima akili yako ijikite katika kutafakari yale tu unayoyataka. Hivyo basi siri kubwa ya kuwa tajiri ni kuufanya mfumo wako wa mawazo wa ndani utafakali juu ya neema za utajiri. Kufikilia juu ya maisha yako ya kitajiri unataka yaweje, kwa maana hiyo ubongo wako unatakiwa uujaze picha ya vitu vya kitajiri ambavyo ni matarajio yako kuvimiliki.

Hitimisho
Nahitimisha kwa kutoa angalizo kuwa kawaida asili ya binadamu inaongozwa na woga/mashaka. Tunakuwa na woga/mashaka kwa vitu vile ambavyo kutokea kwake hatuna nguvu ya kuvizuia ili visitokee. Hivyo, uamuzi mwingi wa binadamu utawaliwa na woga/mashaka kuliko kutawaliwa na kujiamini na matumaini mema. Na kama akili yako isipoona ama kutafakari yale unayoyataka ni vigumu sana kupata matokeo unayoyataka. Kwa maana hiyo siri ninayokuachia leo hii ni kuhakikisha muda wote unawaza yale unayoyataka yatokee katika mazingira chanya na hivyo utokeaji wake uweze kukufanya upige hatua moja kwenda mbele katika kutimiza ndoto zako za kuwa tajiri.

Imeandaliwa na Ndg. Augustine M. Bilondwa
Karibu kwenye fikra za kitajiri  tubadilishane mawazo kupitia mawasiliano yafuatayo:-
Namba ya Simu ya Mkononi                            0786 – 881155/0763 – 745451
Barua pepe                                                    bilondwam@yahoo.com

Blog                                                             fikrazakitajiri.blogspot.com