UCHAMBUZI WA KITABU I Can, I Must, I Will: The Spirit of Success (Naweza, Nalazimika, Nitafanya: Msukumo/shauku ya mafanikio)


Habari yako mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri.

Ni matumaini yangu kuwa unaendelea kupambana kwa ajili ya ukamilisho wa maisha yako. Leo hii nakuletea uchambuzi wa kitabu cha mpendwa wetu Marehemu Dr. Reginald Mengi cha I Can, I Must, I Will. Kitabu hiki nilikinunua kwa TSHS 35,000/= mnamo mwezi Machi, 2019 kwenye duka moja la Vitabu Mkoani Morogoro. Niliomba sana kupunguziwa bei lakini bahati mbaya muuzaji kwanza hakuwa na lugha nzuri kwa wateja hivyo ilinibidi tu ninunue kwa kuwa nilishazunguka kwenye duka jingine na kuambiwa kuwa walikuwa wameishiwa.

Ninachohitaji kukushirikisha hapa wala si bei niliyonunulia wala tabia ya muuzaji wa duka bali ni ile nia ya dhati niliyokuwa ya kupata kitabu hiki ambacho niliamini kitaniwezesha kujifunza mengi kutoka kwa mwanamafanikio nguli wa Kitanzania aliyeanzia chini kabisa na kufanikiwa kuwa miongoni mwa matajiri ndani ya ardhi ya Tanzania na hata Africa kwa ujumla. Bahati mbaya nilipomaliza kusoma kitabu hiki mnamo mwezi Aprili, 2019 nikiwa najiandaa kuwashirikisha wengine nilichojifunza ndani ya kitabu hiki nikawa nimepata ajali ya pikipiki ambayo imenifanya niuguze mguu kwa kipindi cha mwezi hadi sasa bila kufanya chochote. Mungu ni mwema naendelea vizuri kiasi ambacho hata leo nina nguvu za kuendelea kushirikisha mengi ninayojifunza kwenye vitabu mbalimbali.

Nikiwa nimelazwa hospitali baada ya ajali ndipo nikapata habari za kifo cha ghafla cha Dr. Reginald Abraham Mengi, hakika sikuamini taarifa hizo maana ni kama vile nilikuwa naangaza maisha yake yote kupitia kitabu hiki. Kila nilivyokuwa naangaza maisha yake nilimuona Mzee Mengi akiwa anaelekea kwenye mafanikio makubwa zaidi aliyokuwa nayo wakati anaandika kitabu kutokana na misimamo ya hali ya juu niliyojifunza juu yake. Hakika Dr. Mengi umeondoka muda ambao sisi kama vijana tulikuwa bado tuna mengi ya kujifunza kutoka kwako.

Hata hivyo, pamoja na kwamba umeondoka tukiwa bado tunahitaji mengi kutoka kwako kama lilivyo jina lako, hakika tunashukuru kwa zawadi ya urithi wa vizazi na vizazi uliyotuachia kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali za maisha yetu.
Baada ya kukushirikisha hayo machache kuhusiana na masikitiko ya juu ya kifo cha Mpendwa wetu Dr. Reginald Abraham Mengi, karibu nikushirikishe machache niliyojifunza kwenye urithi aliotuachia mimi na wewe. Kwa ujumla kupitia kitabu hiki Dr. Mengi ametushirikisha maisha yake kuanzia akiwa mtoto, akiwa mwanafunzi, wakati anaanzisha biashara yake ya kwanza, namna alivyopanua biashara zake, wajibu aliokuwa nao kwa jamii, misimamo yake kwenye mfumo wa Serikali kwa awamu zote tano, wajibu wake kwenye uhifadhi wa mazingira na matarajio yake kwenye kukuza biashara kwa siku za baadae. Karibu tujifunze machache kati ya mengi yaliyopo kwenye kitabu hiki:-

A.   KUHUSU VIKWAZO VYA KUANZISHA BIASHARA

1.   Hakuna wakati ulio sahihi zaidi kwako kuanzisha biashara.
Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha kuwa kinachoamua ni wakati uanzishe biashara ni dhamira ya kweli kutoka ndani ambayo kila mara inakupa msukumo wa kuchukua hatua dhidi ya fursa iliyopo mikononi mwako. Naamini wengi wetu tumeshindwa kuchukua hatua za kuanzisha biashara kwa vile kila wakati tunaona kuwa wakati sahihi wa kuanzisha biashara bado haujafika aidha kutokana na hali ya kimfumo, mtaji, historia au mazingira. Kumbe tunachofundishwa kupitia kitabu hiki ni kuwa mara zote tunahitaji: kuongozwa na dhamira ya kweli ambayo kila mara inatupa msukumo; kuwa na roho ya kuthubutu; kuwa wabunifu na kutokuogopa hatari (risk) zinazoweza kujitokeza katika biashara husika.

2.   Kamwe historia haina nafasi ya kuamua mafanikio ya mtu.
Kupitia kitabu hiki Mwandishi anatushirikisha kuwa pamoja na kwamba familia ya mzee wake ilikuwa familia masikini kiasi ambacho alikuwa akienda shuleni peku, lakini historia hiyo ya maisha haikuwa kikwazo kwake yeye au kaka yake aitwaye Elitira Mengi kufikia mafanikio waliyofikia. Kupitia kitabu hiki anatushirikisha namna ambavyo kaka huyo alianzia biashara ya chini kabisa ikiwa ni pamoja na kuuza mayai mpaka akafikia hatua tajiri Mkubwa Mkoani Kilimanjaro mwenye asili ya Tanzania na hata kujenga nyumba ya ghorofa katika kipindi cha utawala wa Rais JK Nyerere. Hapa tunahitaji kujifunza kuwa mlango wa mafanikio upo wazi kila mmoja wetu bila kujali historia ya maisha yake. Muhimu ni kutambua nini unataka katika maisha yako na kuangalia fursa zilizopo ili fursa hizo zibadilishwe kutoka kwenye changamoto na kuwa biashara.

3.   Mfumo wa Serikali si kigezo cha kushindwa kufikia mafanikio.
Hapa mwandishi anatushirikisha namna ambavyo baada ya kurudi kutoka Scotland ambako alisomea uhasibu na kufanya kazi alikutana na Tanzania mpya ambayo kipindi hicho Sera ya Ujamaa ilikuwa ndo misingi ya utawala wa Mwalimu JK Nyerere. Sekta nyingi za uzalishaji mali zilikuwa chini ya Serikali na baadhi ya Wafanyabiashara wenye asili ya India pamoja na wazawa akiwemo kaka yake Elitira walinyanganywa mali zao na mali hizo kuwa mali za Serikali. Hata hivyo, hali hii haikuwa kigezo kwa Dr. Mengi kutulia na kuacha kutafuta fursa. Ni katika kipindi hiki mwishoni mwa utawala wa Mwalimu JK Nyerere, Dr. Mengi alianzisha kiwanda chake cha kwanza cha kalamu chini ya Kampuni ya Tanzania Kalamu Company Limited. Somo kubwa hapa, tujiulize ni mara ngapi tunalalamikia mifumo iliyopo kama kikwazo cha kupata mafanikio zaidi.

4.   Mafanikio kwenye taaluma yako yasiwe kikwazo cha kutokuchukua hatua za kiabiashara.
Mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya kurejea kutoka Scotland aliendelea kufanya kazi na Taasisi isiyokuwa ya Serikali iliyojulikana kwa jina la Cooper and Lybrand (C&L) jambo lilomfanya aonekane kuwa sio mzalendo kwa nchi yake ikizingatiwa kuwa kipindi hicho nchi ilikuwa kwenye Sera ya Ujamaa. Hata hivyo, Dr. Mengi hakuvunjika moyo aliendelea kutimiza majukumu yake kiasi ambacho hata wakuu walianza kutambua mchango wake. Katika kipindi hicho cha kilele cha mafanikio katika kazi yake alianza kupata teuzi za kitaifa kama vile kuteuliwa na Mwalimu Nyerere kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA). Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo Dr. Mengi aliona bado ana ombwe kubwa ndani yake nalo ni kuhakikisha anatumia kwa kadri awezavyo: vipaji alivyonavyo, uwezo, akili na nguvu ili kufikia mafanikio makubwa zaidi. Somo kubwa hapa ni kwamba hatupaswi kuridhika na mafanikio ya muda mfupi badala yake kila hatua tunahitaji kuwa na mpango wa kusonga hatua ya zaida.

5.   Mtaji si kigezo cha kushindwa kuanzisha biashara
Wengi tumeshindwa kuanzisha biashara kwa kisingizio kuwa hatuna mtaji, kupitia kitabu hiki Dr. Mengi anatupa somo kuwa mtaji wa kwanza ambao upo kwa kila mmoja ni uaminifu. Hapa tunaona Dr. Mengi alivyoanzisha biashara yake ya kwanza kwa kukopeshwa malighafi za kutengenezea Kalamu kwa makubaliano ya kulipa deni hilo ndani ya siku 30. Ili kulinda mtaji wa uaminifu pale alipopata changamoto hasa katika usafirishaji wa mzigo ambao hakumfikia kwa muda aanzishe utengenezaji wa kalamu na kuuza na hatimaye arejeshe pesa ilimbidi atafute njia mbadala ya kupata fedha ili afanikiwe kurejesha ndani ya muda wa makubaliano jambo ambalo alilifanikisha kwa asilimia zote. Wewe na mimi kuna somo kubwa la kujifunza kwenye hili kutokana na ukweli kwamba kwa sasa fursa za upatikanaji wa mikopo ni nyingi ukilinganisha na enzi zake.

6.   Husikubali mtazamo wa watu wanaokuzunguka uwe kikwazo kwako.
Mwandishi anatushirikisha kuwa pamoja na kwamba Uongozi wa Rais ya awamu wa pili uliruhusu raia kufanya biashara au kumiliki uchumi wa nchi bado athari za Uchumi wa Kijamaa ziliendelea kuathiri mitazamo ya wengi sambamba na sekta ya uchumi kwa ujumla. Hali hii ilitokana na mitazamo ya baadhi ya Viongozi ambao walikuwa bado wanaamini kwenye Ujamaa ikizingatiwa kuwa bado Mwalimu Nyerere alikuwa ana nguvu ndani ya Chama cha Mapinduzi kama mwenyekiti wa chama. Hali hii iliendelea kumuathiri Dr. Mengi hata kipindi ambacho alikuwa amefungua kiwanda cha Bonite Bottlers jijini Moshi kwa ajili ya uzalishaji wa vinjwaji baridi vya soda za Coca Cola. Na katika kipindi hicho Mwalimu Nyerere alisimama wazi kupinga uanzishwaji wa viwanda vinavyotegemea malighafi kutoka nje ya nchi akisema kwa mawazo yake havikuwa na msaada katika ukuaji wa uchumi wa nchi. Hata hivyo, yote hayo hayakumvunja moyo Dr. Mengi bali aliendelea kupiga kazi kwa tahadhari na uangalifu mkubwa.

7.   Husiogope upinzani wa kibiashara.
Mwandishi anatushirikisha kuwa wakati anaanzisha kiwanda cha Bonite Bottlers kwa ajili ya uzalishaji wa soda jamii ya Coca Cola alitegemea kukutana na changamoto kwenye soko kwa kuzingatia kuwa kulikuwa na kampuni pinzani ya Fahari Bottlers ikizalisha vinjwaji vya soda jamii ya Pepsi na kwa asilimia kubwa ilikuwa imeteka soko la Tanzania la vinjwaji baridi. Hata hivyo, hii haikuwa sababu ya yeye kutokuanzisha kiwanda cha Bonite Bottlers kwa vile tayari alishaona kuwa fursa ya vinjwaji baridi ipo hasa katika mikoa ya kaskazini mwa Tanzania. Tunahitaji kujiuliza ni mara ngapi tumepoteza fursa za kibiashara kwa kigezo cha uwepo wa washindani wakubwa wa kibiashara kwenye fursa husika.

B.   KUHUSU FURSA, USIMAMIZI NA UKUAJI WA BIASHARA

8.   Kila changamoto katika jamii ni fursa ya kibiashara.
Katika katabu hiki Mwandishi anatushirikisha jinsi alivyoanzisha biashara mbalimbali kwa kuangalia changamoto zilizokuwepo katika jamii katika vvipindi vya nyakati tofauti. Biashara yake ya kwanza ilianzishwa kutokana na uhaba mkubwa wa kalamu nyakati hizo; Bonite Bottlers kwa ajili ya kutengeneza soda za Coca cola na maji ya kunywa ya Kilimanjaro vivyo hivyo ilianzishwa kutokana na uhaba mkubwa wa bidhaa hizo katika ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania. Pia, IPP Group kwa ajili ya huduma za Magazeti, Runinga (ITV) na Redio pia ilianzishwa katika kipindi ambacho kulikuwa na uhitaji mkubwa wa huduma hizo hasa kutokana na uhaba wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na sekta binafsi. Kwa ujumla Dr. Mengi katika kitabu hiki anatushirikisha kuwa katika kipindi cha miaka ya 1983 hadi 1992 alikuwa ameanzisha makampuni mbalimbali kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa nyingi zilizokuwa zinapatikana kwa shida kama vile sabuni, dawa ya meno, cement, ‘toilet paper’, mafuta, chaki na bidhaa nyinginezo. Somo kubwa kwetu hapa ni kujiuliza je jamii tunayoishi kwa sasa hakuna changamoto ambazo zinaweza kugeuzwa kuwa fursa za biashara?

9.   Kadri biashara inavyokua unahitaji kuboresha mazingira ya biashara.
Mwandishi anatushirikisha kuwa alianzisha utengenezaji wa Kalamu ndani ya eneo la nyumba aliyokuwa akiishi. Hata hivyo, kadri biashara ilivyopanuka ilitakiwa kutafuta eneo ambalo lingefaa kuendena na kasi ya ukuaji wa biashara. Hata hivyo, haikuwa rahisi kupata eneo la kupanga kutokana na gharama kubwa za kodi hasa katika maeneo ya viwanda vidogo vidogo kipindi hicho katika eneo la Barabara ya Pugu (sasa barabara ya Nyerere). Hata hivyo, changamoto hii hakumfanya akate tama badala yake ilimbidi kutafuta mbinu mbadala ambayo ilimuwezesha kupata eneo la kukodi kwa gharama nafuu. Somo kubwa ni kwamba kila changamoto ya kibiashara ina suluhisho pale mmiliki wa biashara akiwa amedhamiria kuitatua.

10.  Biashara inahitaji usimamizi wa karibu.
Mwandishi anatushirikisha changamoto iliyokumba nyakati ambazo alihitaji kusimamia biashara zake kwa ukaribu zaidi na wakati huo huo akitakiwa kuendelea kufanya kazi na kampuni ya Cooper and Lybrand (C&L) kama kiongozi kwa tawi la Tanzania. Japo yalikuwa maamuzi magumu kwake kuachana kufanya kazi na kampuni ambayo aliisimia kwa kipindi kirefu lakini yalibakia kuwa maamuzi sahihi kwa ajili ya kupata muda wa kutosha wa kusimamia biashara zake. Na hapa ndipo aliamua kuafuata njia ambayo ni wachache wanaoifuata – njia ya kujiajiri mwenyewe badala ya kuajiriwa. Somo kubwa hapa ni kwamba chochote tunachofanya kwa lengo la kujiongezea kipato uwepo/usimamizi wetu wa karibu ni wa maana sana kwa ajili ya uendelevu na ukuaji wa mradi husika.

Dr. Reginald Abraham Mengi alifanikiwa kufikia mafanikio makubwa na sasa hatunaye katika ulimwengu huu, lakini muhimu ni kutambua hakika Dr. Mengi ataendelea kuishi kupitia urithi huu wa kitabu cha I Can, I must, I will. Kizazi cha sasa na vizazi vijavyo kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa bilionea huyu mwenye asili ya kitanzania na aliyefanikisha utajiri wake ndani ya ardhi ya Tanzania.

Kupata uchambuzi wote wa kitabu hiki changia TSHS. 5,000/= kama sehemu ya kusapoti jitihada zangu za kuendelea kukupatia maarifa mbalimbali kupitia uchambuzi wa vitabu vya mafanikio kwenye kila sekta ya maisha yetu. Tuma mchango wako kupitia namba ya simu +255 763 745451 au +255 786 881155 kisha nitumie ujumbe wa sms kuomba kutumiwa uchambuzi wote wa kitabu.

 xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Pia unaweza kupata uchambuzi wa Kitabu cha Rules of Life (Kanuni za Maisha) kwa kulipia TSHS. 5,000/=. Ndani ya uchambuzi  wa kitabu hiki utapata kanuni (106) ambazo zimechambuliwa kwa lugha rahisi na kuandaliwa kwa mfumo wa pdf. Uchambuzi huu una jumla ya kurasa 40 na ni kitabu ambacho unaweza kusoma kwenye simu yako ya mkononi (smart phone) au kwenye kompyuta mpakato (pc).

Tuma pesa kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: +255 763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: +255 786 881 151 451 (Majina ni Augustine Mathias)

Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Pia unaweza kupata uchambuzi wa Kitabu cha “The Rules of Money” ambacho pia kimeandikwa na Mwandishi Richard Templar.

Uchambuzi wa kina wa Kitabu cha The Rules of Money (Kanuni 107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania (TSHS) elfu tano tu (5,000/=). Uchambuzi wa kanuni zote una jumla ya kurasa 39.

Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 151 451 (Majina ni Augustine Mathias)

Karibu kwenye mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:               0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:            fikrazatajiri@gmail.com