Hongera Rafiki Yangu kwa Kujiunga Chuo Kikuu Lakini Katika Safari Yako ya Masomo Tekeleza Haya: Barua ya Wazi Kwa Wanachuo wa Mwaka wa Kwanza Kwa Vyuo Vikuu Vyote

Habari ya leo rafiki yangu na msomaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa una afya njema na mapambano yanaendelea kwa ajili ya kuifanya kesho yako iwe bora zaidi ya leo. Leo hii katika makala za kila wiki nakuletea makala maalumu kwa ajili yakufikisha nasaha zangu kwa wanafunzi wote waliojiunga na vyuo mbalimbali kwa ajili ya masomo yao ya elimu ya juu. Wewe kama unafuatilia mtandao huu na sio mlengwa wa makala hii naomba tu unisaidie kuisambaza kwa walengwa kwa kadri unavyoweza.

Kabla ya kuanza barua yangu ningependa nianze kwa kujitambulisha ili ifahamike kuwa anayeandika makala hii ni nani. Kwa majina anaitwa Augustine Mathias Bilondwa, ni mwajiriwa na mjasiliamali, ambaye alihitimu elimu yake ya uzamili (Masters Degree) katika Chuo Kikuu cha Sokoine mwaka 2015 ambako pia alihitimu elimu yake ya digrii ya kwanza mwaka 2011 katika fani ya sayansi ya misitu.

Baada ya kumfahamu japo kidogo nina ni huyu anayekuandikia barua hii ya wazi sasa angependa akushirikishe machache ambayo roho yake inamsukuma afikishe ujumbe huu kwako kwa ajili ya kupanua ufahamu wako katika safari yako yote uwapo unaitafuta elimu ya juu.

Nianze kwa kuweka wazi kuwa barua hii ya wazi haitoi mwongozo wa namna gani unatakiwa kuhishi kwa ajili ya kufaulu masomo ya elimu yako la hasha. Lengo la barua hii ni kukuongoza namna gani unatakiwa kuishi kwa ajili ya kufanikiwa kimaisha nyakati zote ukiwa Chuoni na hata maisha baada yachuo.

Kwa  ufupi nahitaji utambue kuwa namna unatavyoishi kwa mafanikio kwenye haya nitakayo kushirikisha ndivyo utakuwa umeweka msingi imara wa maisha yako na hata baada ya kumaliza chuo msingi huu hautayumbishwa na mawimbi ya aina yoyote ile katika maisha yako yote. 

Rafiki kazana na masomo yako ambayo umejiunga nayo lakini nisaidie kutekeleza haya kwa ajili ya ufanisi wa maisha yako na jamii kwa ujumla:­-

Moja, wekeza sana kuitafuta elimu ambayo inalenga kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii yetuRafiki, uwapo Chuoni utakutana na mazingira ambayo yatakufanya usome kwa ajili ya kujibia mitihani badala ya kusoma kuelewa. Nakusihi sana kila unachojifunza jitahidi kujiuliza ni namna gani unaweza kutumia elimu yake kwenye mazingira ya jamii inayo kuzunguka. Katika kufanya hivyo unahitaji kuwa na picha ya familia yako ambayo umeiacha nyumbani pamoja na picha ya changamoto zilizopo kwenye jamii yako. Picha hiyo iwe chachu ya kujifunza na kuelewa na hatimaye kutafsiri elimu husika kwa vitendo. Tumia elimu hiyo kwa ajili ya kutatua changamoto za umasikini, maradhi na magonjwa, tumia elimu hiyo kwa ajili ya kuboresha mbinu za uzalishaji na hata kuboresha mbinu za mawasiliano. Kwa ujumla jamii inahitaji kupata kitu cha ziada kutoka kwako hivyo huna budi kuwa mfano bora kupitia yale unayojifunza na  kuyatafsiri kwa vitendo.

Mbili, jilipe kwanza kwenye kila shilingi inayoingia mikononi mwako kupitia  ‘Boom’ au chanzo chochote halali. Hapa namaanisha uwekezaji kwa kila shilingi inayoingia mikononi mwako. Husikubali kutumia hela yote unayopata bila kutenga asilimia yake kwa ajili ya uwekezaji. Kwa bahati mbaya sana elimu hii ya uwekezaji kwa maana ya elimu ya pesa pengine hujawahi kufundishwa mahali popote na ni mategemeo yangu kuwa hata katika masomo uliyo chagua hakuna sehemu ambayo utafundishwa elimu hii kwa ufasaha. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mitahala ya elimu yetu na hata nchi nyingi haijaweza kufundisha elimu hii kama inavyotakiwa. Kutokana na elimu hii kutofundishwa kwa ufasaha tumekuwa tukifanya maamuzi yenye makosa katika suala zima la utawala wa fedha (financial management) na hivyo kuendelea kuwa kwenye mzunguko wa umasikini pasipo kujali kiwango cha elimu tulichonacho.

Rafiki yangu katika kujilipa kwanza nahitaji uwe na utamaduni wa kutenga asilimia 10 au 20% ya kila fedha inayoingia mikononi mwaka kwa ajili ya uwekezaji wa muda mfupi na muda mrefu. Unaweza ukafungua akaunti maalumu benki kwa ajili ya kuwekeza fedha hizo au ukanunua hisa za makampuni yanayofanya vizuri kwenye soko au ukafungua akaunti ya Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (Mf. Mfuko wa Umoja) au ukanunua Dhamana za Serikali (Government Bonds). Kumbuka, katika yote hakikisha unawekeza fedha zako sehemu ambapo zitaongezeka kwa muda kupitia ongezeko la riba.

Rafiki kama maneno haya yamekuwa magumu kwako jitahidi sana kuyapa nafasi katika muda wako wa ziada ili kuhakikisha unachimba kwa undani ili uyafahamu kwa kina. Kumbuka ni kupitia uwekezaji utafanikiwa kuwa na maisha yenye uhuru wa kifedha (financial freedom) ambao naamini kuwa ndio ndoto yako kubwa.

Tatu, husikubali kuwa mtumwa wa teknolojia ya mawasiliano. Rafiki bahati nzuri sana umeingia Chuoni wakati ambao mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano yapo kwenye kilele chake na pengine bado uvumbuzi wa teknolojia hii unakuja zaidi ya sasa. Rafiki natambua kuwa ni katika kipindi hiki utahitaji kumiliki simu janja hata kama hukuwahi kuimiliki hapo nyuma. Nakuomba sana rafiki ufahamu kuwa simu janja hizi zimewafanya watu wengi kuwa watumwa kiuchumi, kiakili, kifikra na hata kiutamaduni. Rafiki fahamu kuwa watu hawa wamekuwa watumwa bila ya wao kutambua kuwa ni watumwa.

Utumwa huu unatokana na mitandao ya kijamii waliojiunga nayo kwenye simu zao. Mitandao hii kwa kutaja tu michache ni kama WhatsApp, Facebook, Insta na mingineyo. Rafiki ni katika mitandao hii unakuta watu hawa wana makundi zaidi ya kumi na yote hakuna hata moja ambalo linajadiri mambo ya maana hisipokuwa ni udaku tu. Rafiki kuwa unapokuwa na simu janja chagua makundi yanayoendana na vipaumbele vya maisha yako na sio tu kujiunga na makundi ya umbea na kusambaza picha na video sizizo kuwa na maana.

Rafiki kumbuka kuwa makundi haya si tu yanakupotezea muda kutokana na kushabikia meseji zisizokuwa na maana bali yanasababisha kuwa na bajeti kubwa ya mawasiliano na mtandao. Hii inatokana na ukweli kwamba kadri unavyofungua video au ujumbe wenye mb 200 ndivyo na kifurushi chako ulichojiunga kupitia simu yako kinavyopungua mb 200 hizo hizo.

Soma: BARUA YANGU YA WAZI KWA WAHITIMU WA VYUO

Nne, kuwa na vipaumbele vyako husikubali kupelekeshwa na makundi ya marafiki wapya. Rafiki nimekuwa Chuoni kwa muda wa miaka mitano na katika kipindi hicho chote nimeona vijana wengi wanaokuja wakiwa vijana wazuri na wapenda dini kulingana na imani zao. Hata hivyo, baada ya miezi michache vijana hawa waliangukia kwenye mikono ya Dunia hisiyo mizuri kwa vile walishindwa kuchagua marafiki wema. Rafiki kumbuka kuwa sasa wewe ni mtu mzima kwa maana sasa unajua ni kipi bora na kipi sio bora katika maisha yako na hapa ndipo tunasema kuwa tayari unajitambua. Rafiki kama bado hauna vipaumbele vya maisha yako nachelea kusema kuwa bado hujafikia hatua ya kuwa mtu mzima.

Rafiki kipindi chote uwapo Chuoni unahitaji kuwa na vipaumbele vya maisha yako na kuhakikisha kila siku unaishi kulingana na vipaumbele hivyo. Rafiki hapa ndipo unahitaji kukubali kuwa tofauti na wenzako ili mradi tu uwe kwenye mstari sahihi. Kamwe husikubali kujiunga kwenye kundi ambalo unaona ni kinyume na vipaumbele vyako kwa vile tu umeshawishiwa na marafiki. Kamwe husikubali kufanya au kushiriki kwenye matukio ya aina yoyote ambayo ni kinyume na vipaumbele vyako kwa vile tu umeona wenzako wanafanya hivyo. Daima kubali kujitofautisha na wenzio hakika rafiki utafika mbali.  

Tano, tenga muda wa kujisomea kwa ajili ya maarifa ya ziada nje ya kozi unayosoma. Rafiki nakusihi sana utenge muda wa kujisomea vitabu vya maarifa mbalimbali. Kama ambavyo nimekusisitiza kwenye umuhimu wa kujitambua, rafiki hauwezi kujitambua kama hauna muda wa kuboresha ubongo wako. Rafiki kumbuka kuwa ubongo wa mwanadamu ni kiungo ambacho kinahitaji kuendelezwa kwa kupata maarifa mbalimbali.
Hivyo, rafiki katika muda wako wa elimu ya juu unahitaji kuwa na muda wa kujisomea vitabu vya maarifa mbalimbali. Hii ni pamoja na kujisoma vitabu kuhusu mwanadamu kwa ujumla wake (mahusiano, kazi na historia), vitabu vya biashara, vitabu vya dini na vitabu falsafa mbalimbali. Hakika kama utafanikiwa kwenye hili utakuwa umeweka msingi imara katika maisha yako na kamwe ubongo wako hautazeeka.

Sita, lenga kuzalisha ajira zaidi kuliko kulenga kujiariwa hata mara baada ya kumaliza masomo. Kujiajiri ni bora zaidi kuliko kuajiliwa kwa vile kujiajiri kunakuweka huru zaidi katika fani ambayo umechagua kufanya. Rafiki najua kwa sasa umeingia Chuoni ukiwa na ndoto kuwa pindi utakapomaliza masomo yako utapata ajira kwa ajili ya kupata mahitaji yako muhimu. Vilevile natambua kuwa umechagua kozi hiyo kwa kujua kuwa kozi hiyo ndo yenye uhakika wa ajira au pengine kozi uliyochagua unajihisi kuwa umekosea unajutia kuwa sehemu ya wanafunzi wanaosoma kozi hiyo. 

Rafiki ukweli ni kwamba ajira kwa sasa zimepungua kwa fani zote ukilinganisha na miaka ya nyuma. Hii ni kutokana na idadi ya vyuo kuongezeka ambayo imepelekea kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaomaliza. Rafiki katika miaka yako yote Chuoni fikiria kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine kwani uzoefu unaonesha kuwa hata waliopo kwenye ajira hawana uhuru wa kifedha.

Rafiki namalizia kwa kukuombea uwe na afya njema katika masomo yako. Pia, nakuombea upate roho wa kukuongoza kusoma barua hii ya wazi mara kwa mara ili kadri unavyoisoma uitafakari kwa macho ya ndani.
Karibuni kwenye Fikra za Kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

PATA UCHAMBUZI WA KITABU CHA THE RULES OF MONEY ( KANUNI ZA PESA)
 
Mwandishi Richard Templar katika kitabu hiki ametushirikisha kanuni 107 ambazo kila mtu anaweza kuzitumia kutengeneza pesa na hatimaye kuwa tajiri. Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Tshs. elfu tano tu (5,000/=). Kanuni zote zimechambuliwa na kuandaliwa kijitabu kidogo chenye kurasa 39 ambazo unaweza kusoma kwenye simu ya mkononi (smart phone) au kwenye kompyuta (pc).

Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-

M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 155 (Majina ni Augustine Mathias)

Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 151 451) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.

UTAJIRI NI HAKI YAKO YA KUZALIWA "BEING RICH IS YOUR BIRTH RIGHT"